WACHUNGAJI WANAWAKE-BUKOBA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2006.

HATIMAYE NA BUKOBA WAMEBARIKI WANAWAKE WACHUNGAJI.

Mwaka 1992, Kanisa La Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) liliamua kuwabariki wanawake wachungaji. Uamuzi huu ulipokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya waumini wa kanisa hili. Utekelezaji wake ulikuwa mgumu kwa baadhi ya diosisi za kanisa hili. Baadhi ya diosisi zilitekeleza uamuzi huu kwa haraka na nyingine zilisita. Msimamo mkali wa kukataa kuwabariki wanawake ulikuwa Kanda ya ziwa, na hasa mkoa wa Kagera. Diosisi za Karagwe na Kagera zilikataa kabisa kukubaliana na uamuzi wa kuwabariki wanawake.

Sababu kubwa zikiwa ni zile zile tulizozizoea kwamba Yesu Kristu hakuwachagua mitume wanawake. Lakini zilikuwepo na sababu nyingine kwa mfano kwamba mwanamke akiwa mja mzito atawezaje kusimama mbele za waumini! Au kwamba mwanamke akiwa kwenye siku zake atawezaje kuendesha ibada. Au kwamba mwanamke akiwa mchungaji ataolewa na nani? Sababu nyingine ni kwamba mchungaji ni kama baba wa familia ya waumini, hivyo mwanamke akiwa mchungaji, ataitwa Baba? Watu wamezoea kusikia Baba Paroko, baba mchungaji – sasa mchungaji mwanamke ataitwa Mama Paroko au mama Mchungaji. Wengine ukisema mama mchungaji, wanaelewa ni mke wa mchungaji. Kuna ambao waliuangalia uchungaji kama kazi ya wanaume.

Mwaka juzi, Askofu Dk. Benson Bagonza, wa diosisi ya Karagwe, aliamua kuuvunja mwiko na kukubali kuwabariki wachungaji wanawake. Hata hivyo haukuwa uamuzi wake, jambo hili liliamuliwa na Diosisi ya Karagwe, kwa kuitikia uamuzi wa KKKT uliofanyika mwaka 1992 kule Morogoro, hata hivyo uamuzi huo ulibaki bila kutekelezwa kwa zaidi ya miaka kumi. Maaskofu wawili waliomtangulia Askofu Bagonza, waliogopa kutekeleza uamuzi huo. Kila mmoja wao hakukubali kuhukumiwa na historia kwa kuwabariki wachungaji wanawake. Askofu Dk.Bagonza, hakuogopa kuhukumiwa na historia.

Askofu Bagonza, alipoamua kutekeleza uamuzi huo, alifanya hivyo kwa kulipatia tukio hilo umuhimu na uzito wa pekee. Aliwabariki wachungaji wawili wanawake bila kuchanganya wachungaji wengine wanaume. Hivyo siku hiyo ilionekana kuwa ya pekee na kubeba ujumbe mzito kwa watu wote wa Karagwe, Kagera, Tanzania, Afrika na dunia nzima. Watu wote waliotoka pande zote za dunia, walikuja wakijua kwamba siku hiyo ilikuwa ni kuwabariki wachungaji wanawake. Walijua ni tukio jipya na la aina yake katika diosisi ya Karagwe. Madhehebu na dini mbalimbali zilialikwa kushuhudia tukio hila la kihistoria.

Tarehe 8.1.2006, Diosisi ya Bukoba, wamefuata nyayo za Askofu Bagonza, na kukubali kuwabariki wachungaji wawili wanawake; Alice Kabigumila na Faith Lugazia Kataraiya. Mbali na kufuata uamuzi wa KKKT uliofanyika 1992, Diosisi ya Bukoba (Kaskazini Magharibi) walifanya uamuzi kwa sauti moja miaka miwili iliyopita kuwabariki wanawake, lakini ikachukua muda kutekeleza. Miaka miwili si haba. Wanawake waliobarikiwa tarehe 8.1.2006,walimaliza masomo yao ya theolojia miaka mingi wakasubiri wanaume kukubali kuwabariki. Mchungaji Alice Kabigumila, ni mwanamke wa kwanza mteolojia Afrika nzima. Alisoma theolojia na kupata phd, lakini alikaa miaka mingi akisubiri kubarikiwa. Tofauti na Karagwe, Bukoba, walijitahidi kupunguza makali ya siku yenyewe. Walibarikiwa wachungaji sita, wanne wanaume na wawili wanawake. Kwa kufanya hivyo walitaka kuonyesha kwamba hili lilikuwa tendo la kawaida la kuwabariki wachungaji. Ingawa ukweli wenyewe ni kwamba hilo halikuwa tendo la kawaida. Na kama wangependa kuwa wa kweli, basi wangefanya kama walivyofanya Karagwe, kwa kuwabariki wanawake peke yao. Na wala hii isingekuwa ubaguzi wa kijinsia, lakini ingeonyesha uzito na ukweli wa mambo kwamba hatua ya kuwabariki wanawake ilifikiwa kwa njia ndefu, kwa kusita, kutafakari na kwa manung’uniko ya moyoni.

Ingawa wakati wa mahubiri Askofu Elisa Bubelwa, Askofu wa Diosisi ya Bukoba , alielezea njia hiyo ndefu, kwamba kufikia uamuzi huo walitembea safari ndefu na mara kwa mara walikaa chini ya kivuli na kupumzika na kutafakari, wakati mwingine walisimama kwenye mto na kunywa maji, waliowashauri vibaya, waliwakatalia maana Bukoba, wana uzoefu wa imani ya Kikristu zaidi ya miaka miamoja! Walitembea pole pole lakini kwa uhakika na hatimaye tarehe 8.1.2006, walihitimisha safari yao na kuwabariki wachungaji wanawake.

Safari hiyo haikuonyeshwa kimatendo wakati wa siku yenyewe. Siku ilifunikwa kwa namna Fulani. Ingawa wanawake walijitahidi kufurukuta wakati wa kusoma risala na kutoa zawadi. Walionyesha jambo hili kwa kuwapatia zawadi wachungaji wanawake na kuwaacha solemba wachungaji wanaume. Mchungaji Alice Kabigumila alipata zawadi ya pikipiki aina ya Yamaha, kutokana na michango ya akina mama wa Diosisi ya Bukoba. Mchungaji Faith Lugazia Kataraiya, kwa vile bado anasomea shahada ya uzamifu kule Marekani, alipata zawadi ya computer ya mkononi (Portable Computer). Tendo hili la akina mama ndio lilionyesha kidogo kwamba kulikuwa na kitu kisichokuwa cha kawaida katika Ibada ya kuwabariki wachungaji tarehe 8.1.2006 kwenye kanisa kuu(Kengele tatu) mjini Bukoba.

Bahati nzuri Mchungaji Alice Kabigumila na Faith Lugazia Kataraiya, wameolewa. Wanaume wao Bwana Kabigumila na Bwana Joeivan Kataraiya, walikuwa wamewasindikiza kwenye Ibada ya kuwabariki. Hivyo swali la nani atawaoa wachungaji wanawake halikujitokeza Bukoba, kama lilivyojitokeza kule Karagwe. Hadi leo hii bado ni swali kubwa kule Karagwe, kuhusu ni nani atawaoa wachungaji wanawake. Ni kweli kwamba wanachapakazi bila kuwa na tofauti na wachungaji wanaume, lakini bado kuna tatizo la wachungaji hawa kupata wanaume. Tatizo jingine ni lile la kuwapanga kwenye sharika wachungaji wanawake na wanaume. Mfano wanapojikuta mchungaji mwanamke na mchungaji mwanaume wamepangwa kwenye usharika mmoja. Kama mchungaji mwanamke ameolewa na mchungani mwanaume ameoa na anaisha na familia yake, tatizo linakuwa si kubwa, ni sawa na yale yaliyo katika jamii ya uhusiano wa familia na familia. Lakini kama mchungaji mwanamke hakuolewa kama hawa wa Karagwe, akajikuta kwenye usharika na mchungaji aliyeoa ,lakini hakai na familia yake kwenye usharika. Wakajikuta mchungaji mwanamke na mchungaji huyo aliyeiacha familia nyumbani na kuishi kwenye usharika, tatizo linakuwa kubwa kidogo. Wachungaji wanaume wa Karagwe, wameanza kulitafakari hili kwa kina. Linahitaji ufumbuzi wa hekima na busara.

Kwakukataa kuwabariki wachungaji wanawake, KKKT, Bukoba, ilikuwa karibu sana na Jimbo Katoliki la Bukoba. Msimamo wao ulijenga uhusiano wa karibu sana na Kanisa Katoliki, maana kanisa hili linapinga kitendo hicho. Sasa kwa vile KKKT, Bukoba, imekubali kuwabariki wanawake, itakuwa imeweka ukuta mkubwa kati ya uhusiano wao. Na hili lilionyeshwa na kutokuwepo mjumbe yeyote kutoka kwenye kanisa hili kwenye sherehe za kuwabariki wachungaji wanawake. Makanisa haya mawili yana utamaduni wa kukaribishana kwenye sherehe mbali mbali. Wakatoliki, walioamua kuwepo kwenye sherehe hizo za kuwabariki wanawake walifanya hivyo kwa uamuzi wao, wakijulikana ni lazima wawe matatani.

Ingawa kulijitokeza tofauti ndogo kati ya kuwabariki wachungaji wanawake wa Karagwe na Bukoba. Kitendo cha kuwabariki ni kile kile, ni ukweli kwamba sasa mkoa wa Kagera una wachungaji wanawake. Ni ukweli kwamba sehemu nyingi za Tanzania, zina wachungaji wanawake. Ni ukweli kwamba wanawake wanaweza. Ni ukweli kwamba wanawake wanaweza kuwa wachungaji, basi wanaweza kuwa mapadri! Na hatimaye maaskofu! Ni fundisho kwa kanisa katoliki. Ni bora viongozi wa Kanisa Katoliki, kuharakisha hatua ya kuwaparisha wanawake, vinginevyo waumini wenyewe wataanza kudai jambo hili. Sasa hivi waumini wana mifano ya kutoa, wameanza kuona jinsi wanawake wanavyoweza kuwa wachungaji. Sasa hivi waumini wa kanisa katoliki wameanza kuona jinsi sababu zilizokuwa zikitolewa si za msingi. Kwamba Yesu, hakuwachagua mitume wanawake si kigezo cha kuwafanya wanawake wasiwe wachungaji. Hata hivyo ukweli kwamba Yesu Kristu, alizaliwa na mwanamke Mama Maria, ukweli kwamba Yesu Kristu, aliambatana na baadhi ya wanawake wakati wa mahubiri yake, ukweli kwamba mtu aliyekuwa karibu na Yesu Kristu ni Mwanamke Maria Magdalena, inatosha kuonyesha kwamba Yesu, hakuwatupa kando wanawake. Hivyo kuwabariki kuwa wachungaji au kuwaparisha si jambo la kumkana au kumsaliti Kristu.

Makala hii imeandikwa kwa lengo la kuwapongeza waumini na viongozi wa kanisa la kiinjili la Kilutheri la Bukoba, kukubali kuwabariki wanawake wachungaji. Na kubwa zaidi kuwapongeza wachungaji wanawake Alice Kabigumila na Faith Lugazia Kataraiya, kwa uvumilivu waliouonyesha katika harakati za kuomba kubarikiwa. Moyo wao wa kutokukata tama, ni ishara na ukomavu mkubwa wa imani. Ukomavu huu waliouonyesha ni chachu kubwa katika utumishi wao. Mungu awalinde na kuwapatia nguvu ili wawe nuru ya kuonyesha kwamba wanawake wanaweza.

Na
Padri Privatus Karugendo.

1 comments:

Doris said...

Makala hii ni kama imeandikwa jana tuu kwa kuwa iko so up to date.
Hata hivyo baadhi ya maswali yanajibiwa na wakati. Pd sasa hivi tunashuhudia wasichana wachungaji wakiolewa baada ya ordination. Kwa Kuwa sasa sio ajabu kuwa mchungaji mwanamke, wanaume wenye kuvutiwa na wasichana wanaofanya kazi ya utume hawaoni shida kuwaposa.
Tena kwa upande mwingine wanaamini kuoa mchungaji sio tuu heshima likini pia uaminifu ni mkubwa zaidi pengine.
Asante kwa makala nzuri Pd.

Post a Comment