KADINALI PENGO

MAKALA ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005


NINAKUBALIANA NA MWADHAMA KADINALI PENGO, LAKINI…………

Kuhusu Baba wa taifa marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutangazwa Mwenye Heri na hatimaye mtakatifu, ninakubaliana na Mwadhama Kardinali Pengo, anaposema hivi:

“ Katika Kanisa, mbele ya Mungu na katika utakatifu; hakuna anayetengwa kwa cheo au madaraka, jinsia, umri au kabila… Hivyo, uwezekano wa Mlei kuwa mtakatifu ni ule ule ulio sawa kabisa na ule wa Papa,Kardinali, Askofu, Padri au Mtawa” ( Kiongozi Septemba 17-23,2005).

Huo ndo ukweli na wala hautofautiani na maneno haya:
“ Kwa njia ya imani, ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika kuungana na Kristo. Ninyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, Mtumwa na mtu huru, mwanamke na mwanamme. Nyote ni kitu kimoja katika kuungama na Kristo Yesu (Wagalatia 3: 26 –28).

Ni ukweli ule ule kwamba mbele za Mwenyezi Mungu hakuna matabaka, hakuna walei wala wapakwa mafuta. Lakini Mwadhama Kardinali Pengo, anajua vizuri kwamba pamoja ukweli huu ambao ni mzuri na wenye kuzingatia haki, sivyo tunavyoishi. Kanisa letu lina matabaka na ubaguzi. Walei hawako tabaka moja na mapadri, maaskofu na masista. Ubora wa matabaka haya, “utakatifu” wa matabaka haya, “ukaribu” na Mungu wa matabaka haya uko wazi kabisa. Hili si jambo la kubishania, maana liko wazi. Wapakwa mafuta wana tabaka lao ambalo lina sauti kubwa katika kuliongoza kanisa na kusimamia mambo yote yanayohusiana na uhusiano kati ya Mungu na Muumba. Tofauti iliyopo kati ya walei na wapakwa mafuta ni sawa na tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, au mwanamke na mwanamme!

Padre anaweza kuelewa na kukubali kwamba hata mlei, hata mweusi anaweza kuwa mtakatifu, maana padre amefunzwa theolojia na kupata upeo mkubwa katika imani yake. Anapewa nafasi ambayo mlei wa Tanzania, hajafanikiwa kuipata, hadi kizazi kipya kitakachofuta matabaka na kujenga kanisa la Kristu wa Nazareti. Kanisa lisiokuwa na matabaka. Kwa mlei, ambaye anapata elimu ndogo ya imani yake, maana tabaka lake haliruhusu aelewe mengi zaidi juu ya imani yake, ni vigumu kuamini kwamba mlei mwenzake, ambaye wako pamoja kwenye tabaka la chini katika kanisa anaweza kuwa mtakatifu. Nina imani hata kama angeulizwa Marehemu Mwalimu Nyerere, kwamba yeye na Marehemu Kardinali Rugambwa, ni nani atangulie kuwa mtakatfu, angemtaja Rugambwa! Mwalimu alikuwa na malezi ya walei ya kuabudu “vitakatifu” na kuwaheshimu wahudumu wa vitakatifu!

“Mara kwa mara alishiriki ibada na kupokea Sakramenti ya Ekaristi na Kitubio, akipiga magoti kuonesha heshima na unyenyekevu aliokuwa nao kwa mambo matakatifu tofauti na wengine” (Kiongozi Septemba 17-23,2005).

Mbali na matabaka yaliyopo kati ya wapakwa mafuta na walei, kuna ubaguzi wa wanawake. Kinyume na ilivyokuwa katika makanisa ya mwanzo, sasa hivi wanawake wamewekwa pembeni. Hawapati nafasi ya kushika uongozi wa juu katika kanisa. Bado hatujasikia kanisa katoliki likiongelea kuhusu kuwapadrisha wanawake. Ingawa Mwadhama Kardinali Pengo, anasema kwamba mbele ya Mwenyezi Mungu, hakuna upendeleo, mfumo wa kuwapdrisha wanaume tu kuwa mapadre, unaonyesha aina ya upendeleo. Kama si ubaguzi, basi tunaweza kuupamba vizuri na kuubatiza upendeleo.

Hivyo si jambo la ajabu watu na hasa walei kuhoji mchakato wa kumtangaza Baba wa taifa mwenye heri, kuja kabla wa Marehemu Mwadhama Rugambwa. Si utamaduni wa kanisa katoliki na hasa hapa Tanzania kuwatanguliza walei. Ni kweli Baba wa taifa anastahili kutangazwa mwenye heri na hatimaye Mtakatifu. Ni kweli kwamba Baba wa Taifa hakujilimbikizia mali, aliwatanguliza wengine kabla ya kujifikiria yeye, alikuwa mtu wa sala:

“Hata alipokwenda nchi za nje, kila Jumapili, aliuliza viongozi wenyeji wake kuwa: nitasali wapi… hali hiyo iliwafanya hata marais wenzake wamshangae” ( Kiongozi Septemba 17-23,2005)

Ingawa Mwadhama Kardinali Pengo, anajitahidi kuelezea vizuri juu ya Mwalimu, na bahati nzuri anaelezea yale ambayo kila Mtanzania anayafahamu na kuyakubali, bado kuna dukuduku na wasiwasi. Ni wasi wasi kama ule uliojitokeza baada ya Hotuba ya Mwadhama Kardinali Pengo, kwenye mazishi ya Marehemu Kardinali Rugambwa, kule Kashozi- Bukoba. Hotuba hiyo iliacha maswali mengi zaidi ya majibu.
Hoja yenyewe bado ni ilele ni kwa nini Baba wa Taifa amtangulie Mwadhama Rugambwa? Kwanini mlei amtangulie mpakwa mafuta, katika jamii ambayo utamaduni wake ni kuwatanguliza wapakwa mafuta? Utamaduni wa kuwatanguliza walei, umeanza lini? Ni kwa ajili ya Mwalimu tu, au utaendelea hivyo hivyo?

Mtu pekee anayejulikana kuunda mfumo wa kuwatanguliza walei katika kanisa katoliki la Tanzania, ni marehemu Askofu Christopher Mwoleka, aliyekuwa Askofu wa Kanisa katoliki la Rulenge. Hata kabla ya kifo chake alishaanza kuongelea Utakatifu wa Nyerere. Huyu aliunda jumuiya za kuvunjilia mbali matabaka katika kanisa. Alikazana kuondoa mifumo ya ubaguzi katika kanisa katoliki. Alitaka kujenga kanisa ambalo ni familia moja. Walei walipanda daraja kiasi cha kuleta woga na wasiwasi miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu katika kanisa katoliki la Tanzania. Askofu Mwoleka, alionekana kwenda nje ya mipaka, alizushiwa uongo mwingi ambao ulionyesha anakwenda kinyume na mafundisho ya kanisa katoliki la Roma. Bahati mbaya kwa wengine na bahati nzuri kwa wengine mfumo wa Mwoleka, wa kuwatanguliza walei ulifutiliwa mbali na hivi sasa umezikwa kwenye kaburi lake katika kanisa kuu la Rulenge. Hivyo hata na utakatifu wa Askofu Mwoleka, unaweza kucheleweshwa hadi kizazi kipya chenye mwelekeo wa kujenga kanisa lisilokuwa na matabaka, kanisa alilolenga kujenga Yesu Kristu wa Nazareti!

Anayoeleza Mwadhama Pengo, juu ya mchakato wa kumtanza Marehemu Baba wa Taifa kuwa Mwenye heri, ni ukweli mtupu, lakini sivyo tunavyoishi, na yeye mwenyewe sivyo anavyoishi! Angekuwa mkweli wa nafsi yake, naye angeungana na wale wanahoji ni kwa nini Nyerere, ambaye ni mlei, amtangulie Rugambwa, ambaye mbali na kuwa mpakwa mafuta, alikuwa Kardinali wa kwanza mwafrika kusini mwa jangwa la Sahara. Ni kweli kwamba:
“Hili ni jambo la msingi sana. Mchakato unapoanza ni kumuanika mtu… Hii ni nafasi ya watu kusema uzuri na ubaya wowote katika maisha yake… Nasisitiza kuwa, hakuna atakayelaumiwa au kuchukiwa na Kanisa au kiongozi yeyote wa Kanisa kama atatoa kitu ambacho ni pingamizi. Kama pingamizi zikidhihirika, basi tunanyamaza. Hili sio suala la kificho wala upendeleo wowote. Hatumzibi mtu mdomo; hiki ni kitu cha wazi maana mbele ya Mungu hakuna upendeleo.”( Kiongozi Septemba 17-23, 2005).

Huu uwazi anauongelea Mwadhama Kardinali Pengo, uko wapi katika kanisa Katoliki la Tanzania? Ni nani anaweza kusema wazi na kuyaanika maovu ya kanisa katoliki na asichukiwe? Mimi, nimejitokeza kuandika juu ya kanisa, ili kuonyesha pande zote mbili kwa kukubali kubatizwa kichaa, mkorofi, mhasi, adui wa kanisa, adui wa maaskofu nk, si kweli kwamba mtu anaweza kusema ukweli katika kanisa akabaki salama kiroho. Mchakato wa Mwalimu au watakatifu wengine, utaendeshwa kimyakimya na kwa siri. Huo ndio utamaduni!

Ili watu waweze kumuanika marehemu, ni lazima wawe wamelelewa katika utamaduni wa uwazi, utamaduni wa kusikiliza, kujadiliana, kuhoji, kukosoa na kukosolewa. Je hapa Tanzania mlei anaweza kumkosoa padri, askofu au Kardinali? Si utamaduni wetu! Bado tuko kule kule kwamba “Mkubwa hafanyi makosa”. Kwa mtindo huu hata na mchakato wote wa kumtangaza Mwalimu kuwa Mwenye Heri, utaendeshwa na Mapadri na Maaskofu! Hata hivyo hawa ndio wanaoyajua mambo haya!

Mtu anayekubali kukosolewa, mtu anayekubali udhaifu wake akiwa bado hai ndiye nyota wa utakatifu. Liko wapi jukwaa la kusahihishana, kuanikana, kuhoji, kujadiliana katika kanisa katoliki la Tanzania? Watu wamezoea kufunika mambo, kutohoji, kutowasahihisha viongozi, watu waliozoea unafiki, ili shetani apite, ni vigumu leo hii kuwaambia wanaweza kuwaanika wazi viongozi wao. Ni vigumu kuwaingiza watu kwenye mambo magumu hivi bila maandalizi. Mbali na mambo haya ya utakatifu, yao mambo mengi katika kanisa katoliki yanayohitaji ufafanuzi. Labda tuseme mchakato huu wa utakatifu uwe chanzo cha kuleta mwanga mpya katika kanisa.

Kama Mwadhama Kardinali Pengo, anasisitiza kwamba mbele ya Mwenyezi Mungu, hakuna ubaguzi, ni bora mfano uonekane wazi hapa duniani. Kama anasisitiza uwazi, watu kusema bila woga, basi mifano tuione hapahapa duniani. Kama anasema hakuna matabaka, basi awe wa kwanza kuyavunja. Kinyume na hapo ni kama mchezo wa Luninga!

Katika jamii zenye utamaduni wa uwazi, jamii zenye kuwa na majukwaa ya kujadiliana, kuhoji, kusahihishana, jamii ambazo zimetoa watakatifu wengi, vyombo vya habari kama magazeti, redio, vitabu na Luninga vimekuwa jukwaa la uwazi, la majadiliano, mahojiano, kuanika na kusahihishana.

Katika jamii yetu vyombo vya habari vya kanisa ni Jukwaa la sifa na kufunika mabo ya ndani. Gazeti la Kiongozi, Tumaini letu na majarida mengine ya kanisa yanaadika upande mmoja wa kanisa. Mambo mazuri, mambo ya kusifika. Ingawa kuna ukweli kwamba kuna upande wa pili wa kanisa. Upande wa giza! Yapo mambo yasiyopendeza, mambo ambayo ni bora kama yangebadilika. Haya, ya upande mwingine hayana jukwaa. Yapo, yatabaki hadi mkombozi arudi mara ya pili!

Katika utamaduni huu, wa kuangalia upande mmoja wa shilingi, huwezi kutegemea watu kujitokeza na kusema lolote baya juu ya kiongozi wa dini au wa serikali. Si utamaduni, na watu hawakulelewa hivyo. Kama kweli Mwadhama Kardinali Pengo, ni mkweli, basi aanze na mabadiliko katika vyombo vyake vya habari. Mabadiliko haya, yanaweza kuharakisha mchakato mzima wa Baba wa Taifa, kutangazwa mwenye Heri na kuongeza kasi ya watakatifu wengine kuzaliwa hapa Tanzania.

Hoja zote za Mwadhama Kardinali Pengo, kuhusu kumtanguliza Mwalimu Nyerere, kabla ya Mwadhama Rugambwa, si za msingi. Ni bora Mwadhama Kardinali Pengo, awe wazi kwamba suala hili la watakatifu Tanzania lilikuwa limelala usingizi wa pono. Au akubaliane na usemi wa kihaya usemao “omwatani takweta mushaija” ikiwa na maana kwamba jirani yako hawezi kukusifia. Vinginevyo hana hoja za msingi! Sasa kwa vile tumeamuka, tuendeleze mchakato wa Mwalimu, Mwadhama Rugambwa, Askofu Mwoleka na walei wengine wengi. Sidhani ni dhambi kufanya mchakato wa watakatifu wengi kwa wakati mmoja. Hata hivyo sasa hivi ndio tunaongelea mtakatifu wa kwanza.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

1 comments:

upeothabitiblogspot.com said...

ninapenda makala zako kwa uchambuzi wako yakinifu

Post a Comment