MV BUKOBA

UHAKIKI WA KITABU: SITASAHAU MV BUKOBA

1. Rekodi za Kibibliografia.

Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni SITASAHAU MV BUKOBA na kimeandikwa na Nyaisa Simango. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E & D Vision Publishing na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978- 9987- 521- 43- 2. Kimechapishwa mwaka 2009 kikiwa na kurasa 167. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. Utangulizi.

Kitabu hiki ni kumbukumbu ya kupinduka na kuzama kwa meli ya MV Bukoba katika ziwa Victoria mnamo mwaka wa 1996. Hadi leo hii kuna maswali mengi juu ya tukio hili lililochukua roho za watu zaidi ya 800. Je, ni nini hasa kilichosababisha meli ya MV Boboka kuzama? Je, ajali hiyo ingeweza kuzuilika? Watu wamekuwa na mawazo tofauti kuhusu ajali hii. Kuna watu walioamini kuwa kuzama kwa meli hii kulihusiana na uchawi. Hili lilikuwa ni tukio la kwanza katika taifa letu, meli kupinduka na kuzama. Watanzania waliamini sana usafiri wa meli; ulikuwa salama na wa bei nafuu. Lakini baada ya ajali ya MV Bukoba, imani ya watanzania kwa usafiri wa meli iliyumba sana. Kuna baadhi ambao hadi leo hii hawapendi kabisa kusafiri kwa usafiri huu wa meli.

Mwandishi wa kitabu ni mmoja wa abiria wachache walionusurika. Tukio lenyewe la kunusurika lilikuwa la ajabu. Hivyo mwandishi anajaribu kuandika yale aliyoyashuhudia na yale yaliyotangulia kabla ya ajali yenyewe. Inawezekana mwandishi asingeyakumbuka matukio haya yaliyotokea katika meli kama ajali isingetokea. Uwezekano wa kifo ulifanya akili yake kuwa makini kupita kiasi wakati akitafuta njia ya kujiokoa. Anajaribu kuelezea tangu mwanzo wa safari yake toka Dar-es-Salaam kwa treni hadi Mwanza, na kutoka Mwanza kwenda Bukoba, na safari yake ya kurudi kutoka Bukoba na meli hiyohiyo hadi ilipoishia kwa kupinduka na kuzama, kiasi cha maili kumi hivi kabla ya kufika bandarini Mwanza. Amejaribu kuelezea matatizo mbalimbali ya MV Bukoba tangu mwanzo wa safari hadi kuzama kwake, na athari za ajali hii kijamii, kiuchumi na kisiasa. Mwisho anahitimisha kwa kutoa uchambuzi wa majanga kama haya, mapendekezo na ushauri kwa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwa jamii.

Kitabu hiki kinazo sura 15, Mtiririko wa matukio ya Ajali ya Mv Bukoba kama yalivyoripotiwa na vyombo vya habari na picha za kumbukumbu ya ajali hii. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.

III. Mazingira yanayokizunguka kitabu

Ajali ya MV Bukoba, lilikuwa ni janga la kitaifa. Ajali hii ilikuwa ni kati ya changamoto alizozipata Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa; na ni kati ya mambo ambayo hayakupatiwa ufumbuzi wa haraka katika utawala wake.

Ingawa ajali hii lilikuwa ni janga la kitaifa, waliopata pigo kubwa ni kanda ya ziwa na hasa mkoa wa Kagera. Kuna familia iliyopoteza zaidi ya watu 28 katika ajali hii. Lilikuwa pigo kubwa. Watu wa Kagera, wanajulikana kama “Nshomile” (wasomi), la kushangaza ni kwamba “Nshomile” hawa hakuna aliyechukua jukumu la kuandika kumbukumbu ya ajali hii hadi mjukuu wao Nyaisa Simango, alipoamua kufanya kazi hiyo.

Sehemu zilizoiunda MV Bukoba zilitengenezwa Ubelgiji na kuja kuunganishwa mjini Mwanza, mnamo mwaka 1978, na meli hiyo kuanza kazi mnamo mwaka 1979. Kiwango cha abiria ambacho kilitarajiwa kuchukuliwa na meli hiyo kilikuwa ni 400 tu na wafanyakazi 3 na tani 200 za mizigo. Hati ya usalama ya kusafiri baharini (Certificate of Seaworthiness) ambayo meli hiyo ilikuwa nayo iliruhusu abiria 400, wafanyakazi 22 na tani 85 za mizigo. Lakini meli hiyo ilikuwa na abiria mara mbili zaidi ya hao, mbali ya shehena ya mizigo iliyokuwemo ambayo nayo ilikuwa ni zaidi ya mara mbili ya uzito ulioruhusiwa.

Hakuna Kiongozi wa ngazi ya juu aliyewajibishwa kwa ajali hii ambayo kiasi kikubwa ilionyesha uzembe wa hali ya juu. La kushangaza ni kwamba baada ya ajali hii bado kuna ajali nyingine za meli zilifuata kwa uzembe ule ule unaofanana na wa MV Bukoba. Ajali za basi zinaendelea kuyamaliza maisha ya watanzania. Juzi tu ajali tatu zilitokea Nzega, na watu wengi wamepoteza maisha. Hakuna anayewajibishwa. Jitihada za kupunguza ajali zinakwenda kwa mwendo wa kinyonga.

Prof. Haroub Othman, aliyeandika neno la utangulizi katika kitabu cha Sitasahau MV Bukoba, anasema kwamba “Kila kifo kina siku yake”, na kweli Kila kifo kina siku yake! Pamoja na maneno mazuri ya kukitambulisha kwetu kitabu hiki, amekufa kabla kitabu hakijazinduliwa. Mungu, ailaze roho yake mahali pema peponi.

Prof. Haroub Othman, anasema: “ Cha kujiuliza ni; je,
ingekuwa MV Bukoba imefanyiwa matengenezo kwa zile
kasoro zilizojitokeza tangu wakati inaanza kazi…;
Ingekuwa uongozi wa TRC umetekeleza jukumu lake la
uangalizi na usimamizi wa shughuli zote za shirika kwa
uangalifu sana….; Ingekuwa wahusika bandarini Bukoba
na Kemondo Bay walihakikisha kuwa waliopanda melini ni
abiria wanaotakiwa tu na si zaidi, na uzito wa mizigo ni ule
unaoruhusiwa…; Ingekuwa….. Ingekuwa… Lakini
haikuwa hivyo, na ajali ikatokea kwa sababu ya uzembe wa
jinai uliofanywa na binadamu mwenyewe. Sasa cha
kujiuliza tena ni: je, ufanye nini? Cha kufanya sasa ni
kutorejea makosa kama haya, sio tu katika usafiri wa
baharini, angani barabarani na kwenye treni, lakini pia
katika kujenga majumba yetu, shule, hospitali na hata
magereza yetu" (Uk 8).

Nyaisanga G.Simango alizaliwa Wilaya ya Kinondoni,
Dar-es-Salaam. Alisoma Elimu ya Msingi na Sekondari, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kuanzia mwaka 1981 hadi 1991. Alipata Stashahada ya juu ya Ubaharia katika chuo cha Uongozi wa Maendeleo, Mzumbe. Aidha, mwaka 2004 alihitimu shahada ya Uzamili katika Uongozi wa Biashara, mchepuo wa Fedha na Benki Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro. Kwa sasa, Nyaisa Simango ameajiriwa kama Afisa Ugavi, Benki Kuu ya Tanzania. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.

IV. Muhtasari wa Kitabu

Sura ya kwanza, mwandishi anaelezea Meli ya MV Bukoba; wasifu wa meli hiyo na idadi ya watu na mizigo ambayo iliruhusiwa kubeba, ila siku ya ajali ilibeba mara mbili ya uzito uliokuwa ukiruhusiwa.

Sura ya pili ni maandalizi ya Safari ya Mwandishi, kutoka Dar, kuelekea Mwanza. Sura ya tatu ni safari yake kuelekea Mwanza. Sura ya nne ni maelezo juu ya mji wa Mwanza na maandalizi ya safari ya kuelekea Bukoba kwa usafiri wa Mv. Bukoba.

Sura ya tano ni safari ya Mwandishi kuelekea Bukoba, akimsindikiza mfungwa wake aliyetokanaye Dar. Sura ya sita ni maelezo juu ya Bukoba. Sura ya saba ni maelezo juu ya safari ya kurudi kutoka Bukoba kuelekea Mwanza na Mv Bukoba, safari iliyoishia majini! Anaelezea watu walivyokuwa wamejaa, starehe za melini na mengine mengi.

Sura ya nane inaelezea dalili za hali ya hatari kuanza kujitokeza melini. Sura ya tisa ni kupinduka kwa MV Bukoba na yote yaliyofuatia; maji kujaa melini, watu kufa watu kutapatapa huku na kule kutafuta msaada.

Sura ya kumi na kumi na moja zinaelezea jinsi wale waliookoka walivyo panda juu ya mgongo wa MV Bukoba na jinsi walivyoanza kuwa na matumaini ya kuokolewa.

Sura ya kumi na mbili ni maelezo ya kuokolewa na kupelekwa hospitali ya rufaa Bugando. Sura ya kumi na tatu ni maelezo kuhusu kutoka hospitali ya Bugando. Sura ya kumi na nne na kumi na tano na maelezo ya mwandishi kwenda nyumbani kwao Musoma.

Baada ya sura ya kumi na tano inafuata mtiririko wa matukio ya ajali ya MV. Bukoba kama yalivyoripotiwa na vyombo vya habari na mwishoni kabisa ni hitimisho.

V. TATHMINI YA KITABU

Baada ya kuona muhtasari wa kitabu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Nyaisa Simango.

Ingawa kitabu hiki kimeandikwa zaidi ya miaka kumi baada ya ajali ya MV Bukoba, ni ukweli usiopingika kwamba kazi iliyofanyika ni nzuri sana. Ni lazima tumpongeze mwandishi kwa kazi yake hii ambayo itakuwa na manufaa hata kwa vizazi vijavyo. Mwandishi ametuonyesha umuhimu wa kuandika kumbukumbu ya matukio mbali mbali katika taifa letu. Kama alivyosema Marehemu Prof. Haroub Othman, katika neno la Utangulizi: “ Nyaisa anafaa kushukuriwa kwa kazi hii nzuri na adhimu. Kunusurika kwake kutokana na kifo ndiko kumetuwezesha leo kujua nini kilitokea. Ikiwa wengine waliokuwemo katika meli ile ya MV Bukoba na kubahatika kuwa hai leo hawataelezea kimaandishi au kwa kuhadithia wengine ili yaandikwe, basi polepole janga hili la kitaifa litapotea katika kumbukumbu zetu” (Uk 9).

Hiki ni kitabu cha kwanza kuandikwa juu ya ajali ya MV Bukoba. Hivyo ni vigumu kufanya tathimini juu ya matukio yote yanayoelezwa na Nyaisa. Tunaweza kuwa na mashaka kwamba mwandishi aliwezaje kukumbuka yote hayo katika hali ya kupigania maisha yake. Wakitokea watu wengine baada ya kusoma aliyoyaandika Nyaisa, wakaongezea, wakakosoa na kuboresha zaidi, tunaweza kuwa na kumbukumbu nzuri ya ajali hii ambayo ilichukua roho za watu wengi.

Au labda kama Nyaisa, angefanya juhudi za kutafuta watu waliopona, na kujadiliana nao na kumbushana matukio mbalimbali ndani na nje ya meli, kitabu kingekuwa na sura tofauti. Bukoba, kuna watu wengi waliopona kwenye ajali hii; tungeweza kupata ushuhuda wao pia lingekuwa ni jambo jema na la kudumisha kumbukumbu na historia ya taifa letu.

Katika utangulizi Nyaisa, anasema hivi: “ Nimeelezea kwa ufupi tu baadhi ya matukio niliyoyaona na kushiriki ndani na nje ya MV Bukoba wakati wa safari. Inawezekana nisingeyakumbuka matukio haya yaliyotokea katika meli kama ajali isingetokea, kwani uwezekano wa kifo ulifanya akili yangu kuwa makini kupita kiasi wakati nikitafuta njia za kujiokoa”

Pia Marehemu Prof. Haroub Othman, alisisitiza jambo hili kwenye neno lake la utangulizi: “ Nyaisa hakuwahi kuwa mwandishi, na sidhani kwamba kabla ya ajali hii hata aliwaza kuwa angekuwa mwandishi siku moja. Changamoto, au tishio lolote la nafsi (mtu, jamii, taifa) ni mama wa ubunifu na ujasiri pia. Katika maelezo haya, Nyaisa ametuelezea kwa ufasaha mambo aliyoyaona na kuyapitia katika ajali ile”.

VI. HITIMISHO

Kwa kuhitimisha, ningependa kuwashauri watanzania kukisoma kitabu hiki cha Nyaisa. Pia ni muhimu kwa wale waliopona kwenye ajali hii kukisoma kitabu hiki na kutoa maoni yao.

Mipango ikienda kama ilivyopangwa, kitabu hiki kitazinduliwa hivi karibuni Jijini Dar-es-Salaam na kule Mwanza. Mpango ni kukizindua kitabu hiki tarehe 21.5.2010, kule Mwanza, siku ambayo ni kumbukumbu ya kuzama kwa MV Bukoba. Litakuwa ni jambo zuri kama watu watakusanyika kwa wingi kushuhudia uzinduzi wa kitabu hiki ambacho kinatuletea kumbukumbu ya ajali ya MV. Bukoba.

Shukrani za pekee ziwaendee E&D Vision Publishing, kwa kuona umuhimu wa kukichapa kitabu hiki na kwa kufanya jitihada za pekee kutafuta nyongeza za ziada ambazo ni muhimu sana katika kutunza kumbukumbu ya ajali hii mbaya.

Kila Kifo Kina Siku yake. Prof. Haroub Othman, aliandika neno la utangulizi la kitabu hiki lakini kwa vile kila kifo kina siku yake, ametangulia mbele ya hukumu kabla ya uzinduzi wa kitabu hiki. Baadhi ya wale waliopona kifo kwenye Ajali ya MV Bukoba, ni marehemu, maana Kila kifo kina siku yake!

0 comments:

Post a Comment