KASI YA AHADI ZA AJIRA 2

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

KASI YA AHADI ZA AJIRA 2
…. Inaendelea kutoka Jumapili iliyopita.
Mauritius iliweza. Walifikia kiwango hiki ambacho huwa ni mara chache sana kufikiwa na nchi yoyote duniani. Haikuwa bahati, wala hawakushushiwa neema toka mawinguni ilikuwa ni muunganiko wa mpangilio mzuri wa sera na utawala bora. Siri ya mafanikio yao ilikuwa ni biashara ndogondogo na za kati. Kilichofanyika kikubwa ni serikali kutoa mafunzo kwa vijana na kuwapatia maeneo ya kufanyia biashara ndogondogo hasa biashara ya nyumba ndogondogo kwa ajili ya kulala watalii. Waliwezeshwa kupata mitaji toka benki wakajenga nyumba hizo, serikali ikatangaza utalii kwa nguvu zote. Watalii wengi waliokuwa wakifika Mauritius walilala katika nyumba hizo kwani ziliendeshwa kitaalamu baada ya mafunzo waliyopewa wafanyabiashara na bei zake zilikuwa nafuu. Hii haikupunguza biashara ya hoteli kubwa pia kwa vile idadi ya watalii iliongezeka. Wenye kipato kikubwa waliendelea kulala hoteli kubwa, wenye vipato vidogo walilala katika hizo nyumba ndogo ndogo. Wakaua ndege wengi kwa jiwe moja. Biashara ya utalii ikaongezeka tatizo la ajira likapungua, benki zikazalisha fedha na pato la serikali likaongezeka kupitia kodi, achilia mbali kuweka historia duniani.

Biashara nyingine kama viwanda vidogo vya uchapishaji na nyingine nyingi zilihamasishwa. Mpaka leo uchumi wa nchi hii si mbaya, bidhaa wanazouza Marekani kupitia mpango wa AGOA zimekuwa zikiongezeka kila mwaka. Kuna wenye hoja hafifu kwa hili; watakuambia Mauritius ina idadi ndogo ya watu ndio maana mambo yao ni mazuri, sasa unajiuliza kwa nini China na India zenye watu wengi kuliko nchi nyingine zisiwe na hali mbaya zaidi? Kinyume chake sasa zinatishia hata usalama wa chumi za mataifa makubwa. Wachina wanauza kila mahali hadi sasa Jumuiya ya Ulaya inalalamika. Bidhaa za China zimejaa Ulaya. Siri yao kubwa si kwamba wameanza na vitu vya ajabu. Uzalishaji unafanyika hadi majumbani, elimu yao inawasaidia. Wakihitimu wanaweza kubuni na kuzalisha kitu.

Ni lazima na sisi tuanzie mahali fulani. Kama nilivyosema awali kuna kuchagua. Kwa mfano kufanya kama walivyofanya wenzetu wa Mauritius katika kuhamasisha ujenzi wa nyumba ndogondogo kwa ajili ya watalii wenye kipato cha chini au kukaribisha wawekezaji wachache wakajenga mahoteli makubwa yakazalisha ajira. Unaangalia. Unapima halafu unafanya maamuzi si ya kisiasa bali ya kitaalamu. Tusipoweza kufanya maamuzi ya busara tutakuwa na matatizo mengi sana. Ndio maana baadhi ya wanasiasa hulalamika kuibiwa kura zao wakati wa chaguzi. Watu wanakuwa hawana cha kufanya, wanahudhuria mikutano yote ya kampeni kupoteza muda na kuangalia kama kuna ka-takrima. Matokeo yake kila mgombea anaona kwamba ana washabiki kumbe wapi, ni wapoteza muda tu. Wakati wa kura hawapigi. Ndio sasa wagombea huanza kulia na kusema wameibiwa kura zao.

Tatizo la ukosefu wa ajira lina matokeo mabaya kisiasa, kiusalama, kimaadili na kijamii. Uhalifu tunaolia kwamba umeongezeka ni matokeo ya kukosekana kwa kitu cha kufanya. Kuna kuchagua la kufanya. Ni lazima katika kuamua la kufanya tushirikishe wataalam. Tunapodai kwenda nchi nyingine kujifunza ni lazima tujifunze si kwenda nje ya nchi kununua vitu madukani. Tukirudi tukae chini tutafakari tuliyojifunza na namna ambavyo tunaweza kuiga mazuri yatakayotuletea manufaa badala ya kurudi na kuanza kuhadithia hiki na kile. Ukianza leo kuhesabu idadi ya watanzania ambao wamekwenda nje ya nchi kwa kisingizio cha kuchota uzoefu ni kubwa kweli. Ni kweli tunajifunza?

Changamoto kubwa ya Serikali ijayo ni lazima kwanza kuhakikisha Tanzania inajitosheleza kwa chakula. Anzia hapo zalisha ajira kwa kusisitiza ukulima wa chakula. Ukishajitokeza kwa chakula unaweza kuongea vinginevyo. Kama bado tunaagiza mchele toka Thailand na Vietnam wakati tunaweza kuzalisha chakula cha kutosha ni udhaifu mkubwa. Ajira nyingine zinahitajika tu kujizalishia nyumbani. Tutumie wataalamu wetu wahandisi kutengeneza mashine ndogondogo za kuzalisha bidhaa mbalimbali. Kuna haja kweli ya kuagiza vijiti vya kuchokonolea meno Indonesia? Au pamba za masikio toka Thailand? Kuna haja ya kuagiza wanasesere toka Uchina? Sina uhakika ni namna gani tunavyowatumia vijana wetu wanaohitimu vyuo mbalimbali kusaidia katika juhudi hizi za kuondokana na aibu hii ya kulia ajira wakati tunaagiza vijiti vya kuchokonole meno nje. Huu si wakati wa kupiga kelele za kuendeleza fikra ni wakati wa kuzibadilisha. Badilisha mwelekeo. Mwelekeo wa uzalishaji wa yale tunayoweza kuzalisha hata majumbani kwetu. Tukiona kontena linatoka nje ya nchi tusianze kusema haya vijiti vya kuchokonolea meno vinaingia sasa. Tujue yameleta vifaa na mashine ambazo hatuna uwezo wa kutengeneza.

Lengo la muda mrefu la serikali ya awamu ya nne liwe ni kubadilisha mfumo wa elimu. Elimu ya nadharia sasa ipunguzwe. Vyuo vya ufundi vilenge ubunifu. Wahitimu watoke vyuoni wakiwa wanajua cha kufanya kusaidia katika uzalishaji. Wale vijana wanaosoma shule za vipaji maalum kama Mzumbe, Ilboru, Msalato na Kilalakala, vipaji vyao visiishie shule za sekondari. Hawa ndio waendelee kuendelezwa kwa faida ya taifa letu. Wasiishie kupelekwa bungeni na kupigiwa makofi. Haitoshi vipaji maalum kuishia sekondari. Ni lazima vipaji hivi vitumike zaidi ya hapo. La sivyo shule hizo hazitakuwa na maana yoyote ni afadhali wote wachanganyike katika shule nyingine ili waweze kusaidiana na wenzao wasio na vipaji hivyo.

Haina maana yoyote kusema zitazalishwa ajira milioni moja au milioni mbili. Ajira zipo. Kwani zinazaliwa kutoka wapi? Tunahitaji watu wachache wenye kufikiri na kupanga kwa ajili ya Taifa. Tunawahitaji wataalam kama wale wa Vietnam, waliopendekeza nchi yao kujikwamua katika umaskini kwa kulima mchele. Wataalam hawa walipotoa pendekezo hili kwa mara ya kwanza walionekana kuwa na upungufu wa akili. Waliwataka wakae tena na kufikiri juu ya wazo lao. Wenyewe walisisitiza kilimo cha mchele. Leo hii Vietnam, ni ka ya nchi za kwanza duniani kuuza mchele. Kilimo hiki kinatoa ajira, kilimo hiki kinasaidia uchumi wa nchi ya Vietnam kukua kwa haraka.

Wanaosema watazalisha ajira wana mikakati gani? Mbona hatusikii mapendekezo yoyote? Wanapendekeza Tanzania tufanye nini? Nchi yetu inaweza kufanya mengi, kilimo, utalii, madini nk. Nchi yetu ilivyo kubwa, inaweza kugawanyika kikanda, na kila kanda ikaweka nguvu zote kwa kitu kimoja. Kama Maurtius, Vietnam au Botswana na nchi nyingine masikini zinavyofanya na kufanikiwa kauendelea kwa haraka.. Labda badala ya kusema watazalisha ajira, waseme watahakikisha wataalam wetu tulionao wanawezeshwa kufanya utafiti wa kutosha ili waweze kupendekeza kwa taifa letu ni mambo gani tukazanie kama taifa. Ni maeneo gani wapatiwe wawekezaji wa nje na ni maeneo gani wapewe wawekezaji wa ndani. Wataalam wetu wapendekeze kinachoweza kufanyika kwa kila kanda. Na hapa ni utaalam zaidi ya siasa za kula na kuliuuza taifa. Serikali inayokuja, itoe ahadi ya kuyasimamia maamuzi hayo kwa kufa na kupona.. Ikiwa hivyo, ni lazima ajira zitajileta zenyewe.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment