AJALI ZINAKATISHA MAISHA YA WATANZANIA.

Tarehe 14.1.2012 siku ambayo ajali ya barabarani iliyakatisha maisha ya Mheshimiwa Regia Mtema, mbunge wa viti maalum kupitia chama cha CHADEMA, ilikuwa ni siku ya kukumbuka  kuzaliwa kwangu nikiwa nimefikisha miaka 56. Ndugu, jamaa na marafiki walinitumia salaam za matashi mema, wengine walinipongeza kuvuka wastani wa kuishi wa Mtanzania, tunaambiwa kwamba miaka 43 ndo wastani wa kuishi wa Mtanzania? Mimi na wengine tuliovuka wastani wa kuishi wa Mtanzania tunawajibika kumshukuru Mungu, maana si kwa ubora wetu bali kwa Neema yake; rafiki zangu wa mtandao wa Facebook ndo walitia fora maana hadi leo nilikuwa nimepokea ujumbe wa matashi mema ya “Birthday” kutoka kwa watu mia tatu hamsini. Kati ya hao, rafiki yangu kutoka Tabora alinitumia ujumbe ufuatao: “ Karugendo, hongera kufikisha miaka 56 ya kuzaliwa, kumbuka kadiri miaka inavyoongezeka ndivyo unavyolikaribia kaburi..”
Nami nikamjibu;  “ Asante kwa matashi mema. Zamani tulifikiri kulisogelea kaburi inaendana na umri mkubwa, ila siku hizi mambo ni tofauti. Vijana wanakufa kwa ajali, ukimwi na magonjwa mengine yanayosababishwa na kemikali zinazochanganywa kwenye vyakula, vinywaji na dawa bandia..”

Kabla sijamaliza kusoma salaam zangu za “Birthday” nilipata habari za kushutusha na kusikitisha za kifo cha Mbunge Regia Mtema, kijana ambaye kufuatana na mawazo ya rafiki yangu wa Tabora, umri wake 32? ulikuwa si wa kulikaribia kaburi. Alikuwa bado mdogo, alikuwa ana matumaini ya kuendelea kuishi miaka mingi mbele, wanaomfahamu vizuri wanasema alikuwa amepania mwaka huu uwe ni wa kuwahamasisha vijana kufanya kazi. Alitaka kuwashawishi vijana kuachana na tabia  za kukaa vijiweni na kutegemea miujiza kutoka Mbinguni. Maisha yake yamekatishwa na ajali ya barabarani. Inasikitisha sana Taifa kumpoteza kijana aina ya Regia Mtema, ambaye alionyesha wazi kuwa na hazina kubwa ya kuchangia maendeleo ya taifa letu la Tanzania.
Mbali na kumfahamu Mheshimiwa Regia Mtema, kupitia kwenye vyombo vya habari na kushuhudia mchango wake wa mawazo katika matukio mbali mbali na hata Bungeni, alikuwa rafiki yangu katika mtandao wa “Facebook”. Yeye ni kati ya watu walionitumia ujumbe wa matashi mema wakati wa kukumbuka ya siku  ya kuzaliwa kwangu. Ni imani yangu kwamba ujumbe huo aliuandika muda mfupi kabla ya kuanza safari yake hiyo iliyoyakatisha maisha yake. Aliniombea maisha marefu na kunihakikisha kwamba  vijana wanafuata nyayo zetu sisi wazee katika harakati za kulijenga taifa letu la Tanzania. Wakati nikiusoma ujumbe wa Regia Mtema, kumbe yeye alikuwa akiaga dunia.

Mheshimiwa  Slaa, Katibu mkuu wa Chadema wakati akitoa rambi rambi kwenye vyombo vya habari alisema kifo cha Regia Mtema, kimewasononesha na kuleta huzuni kwa taifa zima, lakini kwa vile ni mpango wa Mungu, hatuwezi kuhoji. Namheshimu sana Dk Slaa, na ninatambua vizuri uwezo wake wa kujenga hoja na kuzisimamia. Ninafahamu vizuri  kwamba yeye ni mwanateolojia aliyebobea. Bahati mbaya ni kwamba theolojia yake hii ya “Kazi ya Mungu haina makosa”, “Bwana ametoa, Bwana ametwaa”, imepitwa na wakati!  Kadiri siku zinavyosonga mbele na mwanadamu anakimbizana na maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia ni lazima tuwe na theolojia inayokwenda na wakati. Najua siku nikikutana na Dkt Slaa  tutabishana juu ya hoja hiii hadi kieleweke!

Mbali na Dkt Slaa, ukisikiliza ujumbe unaotolewa redioni na kuandikwa kwenye magazeti ni ule ule wa “Kazi ya Mungu, haina makosa”. Hivyo mawazo kama haya ninayoyatoa yanayoelekea kuhoji kazi ya Mungu, ni lazima yatapokelewa na hisia tofauti. Ninalijua hili, lakini ni lazima awepo wa kuanzisha. Na kawaida kuanzisha kitu si kazi nzuri sana, maana kuna kutukanwa mambo yakienda vibaya. Kitulizo ni kwamba kilichoandikwa kimeandikwa. Leo watatukana na kuweka pembeni, lakini kesho na keshokutwa watasoma na kufurahi.

Mambo mengi yanayokatisha maisha ya watu hapa Tanzania, si mpango wa Mungu na wala si kazi ya Mungu, bali ni kazi yetu sisi wenyewe. Jambo hili ni lazima tulieleze bila kuogopa maana kinyume na hapo ni kuendelea kuwapumbaza watu. Ajali kama hii iliyokatisha maisha ya Mheshimiwa Regia Mtema, si mpango wa Mungu. Ni dhambi kubwa kusema kwamba huu ni mpango wa Mungu. Kama barabara ya kutoka Dar-es-Salaam hadi Morogoro, ingekuwa ni ya njia nne, ajali kama hii ya Regia Mtema na nyingine nyingi zinazotokea kila wakati kwenye barabara hii zisingetokea. Wataalamu wanasema kufuatana wingi wa magari yanayotoka na kuingia Dar-es-Salaam kila siku ya Mungu, ni uzembe kuendelea kuwa na aina ya barabara tuliyonayo kwa sasa ya magari kupishana. Tunataka tusitake ni lazima ajali zitaendelea kutokea. Ajali zikitokea, tunasema  Mpango wa Mungu hauna makosa? Na kwamba hatuwezi kuhoji kazi ya Mungu! Theolojia ya aina hii ni ya kuwekwa pembeni kabisa! Mungu anatuumba tuwe na uzima tena tuwe nao tele! Mpango wa Mungu ni uzima  tele, kinyume na hapo ni kutoka kwa yule mwovu!

Tunaachia magari mengi yanaingizwa nchini, bila kuwa na mpango wa kupanua barabara, tunategemea nini? Kama si foleni, basi ni ajali za kila siku. Ni makosa makubwa kusema  foleni na ajali zinazosababishwa na uzembe wetu wa kushindwa kupanua barabara zetu miaka hamsini baada ya uhuru wetu, ni kazi ya Mungu na haina makosa.

Namkumbusha Dkt Slaa, kitu anachokijua mwenyewe. Ni lazima tusimame na kuhoji ni kwa nini maisha ya watanzania yanaendelea kupotea kwenye ajali za barabarani. Tukifanya hivyo, haina maana  imani yetu imekwenda tenge, kuhoji kazi ya Mungu. Ni haki yetu kuhoji tena kwa ukali. Mungu amefanya yote, ameiumba Tanzania ikiwa na rasilimali nyingi, ametupatia akili ya kuzaliwa na kipaji cha kujifunza mambo mapya na kuwa wavumbuzi, ametupatia uwezo wa kuutiisha ulimwengu. Iweje leo hii tunashindwa kuwa na barabara nzuri, kubwa na pana zinazoweza kuruhusu magari kukimbia bila kukutana wala kugusana. Tatizo letu ni kupanga vipaumbele. Tukiyaweka maisha ya watanzania kuwa kipaumbele namba moja, ni lazima ajali za barabarani zitakoma.

Ni lazima tusimame na kuihoji serikali yetu iliyo madarakani: Je maisha ya watanzania ni kipaumbele namba moja? Mtu akifa kwa ajali ni lazima tuhoji kwa ukali kabisa, Albino akichinjwa ni lazima tusimame na kuhoji, hatuwezi kusema kwamba kuyakatisha maisha ya albino kwa imani za kishirikina ni kazi ya Mungu, mtu akifa kwa malaria ni lazima tuhoji kwa ukali, watoto wachanga wakipoteza maisha ni lazima tusimame na kuhoji kwa ukali, mwanamke akipoteza maisha wakati wa kujifungua ni lazima tusimame na kuuliza kwa ukali kabisa. Katika dunia hii ya maendeleo ya sayansi na teknolojia mwanamke kupoteza maisha wakati wa kujifungua si kazi ya Mungu, ni kazi yetu sisi. Ni lazima tuijutie na kupiga magoti kuomba toba kwa muumba wetu.

Tunaachia dawa bandia zinaingizwa nchini. Watu wanazitumia dawa hizi, matokeo yake wanaugua kansa na magonjwa mengine ya hatari. Wakifa, tuseme ni mpango wa Mungu, hauna makosa na haturuhusiwi kuhoji? Baadhi ya vyakula tunavyonunua madukani vimejaa kemikali za hatari. Hatuna mpango imara wa kudhibiti vyakula hivi, ili kuhakikisha ni salama kwa matumizi ya binadamu. Wale wanaohusika na kupima vyakula hivi wakihongwa vijisenti kidogo wanaachia vinapita na kusambaa nchi nzima. Samaki wa mionzi kutoka Japan walifika hadi Morogoro! Kesho na keshokutwa vyakula hivi vikisababisha vifo tuseme ni mpango wa Mungu, kwamba bwana ametoa, na bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe milele! Theolojia hii ni ya kutupwa kabisa na isionekane tena hapa duniani. Sina lengo la kupinga nguvu za Mwenyezi Mungu. Ninafahamu kwamba yeye ni Muumba wa Mbingu na nchi, ambaye anaumba vinavyoonekana na visivyoonekana. Hoja yangu ni kwamba hata yale ambayo  Mungu ameyaweka kwenye himaya yetu, tukishindwa kuyatekeleza kwa uzembe wetu, tunayasukuma kwake.

Tunaruhusu matairi bandia yanaingizwa nchini. Matairi haya yakipasuka, magari yakapinduka na watu wakafa, tuomboleze kwa kusema ni mpango wa Mungu:  Bwana ametoa, bwana ametwaa? Kusema kweli ajali na vifo vingi hapa Tanzania ni vya kujitakia na wala si mpango wa Mungu. Tunamsingizia mungu kwa uzembe wetu na kukwepa wajibu wetu wa kuzipanua barabara zetu. Tunamsingizia Mungu kwa uzembe wetu wa kushindwa kudhibiti bidhaa bandia.

Tunashabikia magari ya mitumba na kununua vitu chakavu. Waheshimiwa wabunge walijadili na kupitisha sheria ya kununua vitu vichakavu. Wanataka tununue magari ya mitumba, meli za mitumba ndege za mitumba. Vitu hivi vichakavu vikileta hatari na kusababisha maisha ya watanzania kupotea, tuseme ni Kazi ya Mungu haina makosa? Ni kukwepa wajibu wetu na kumbebesha Mungu huyu mizigo isiyokuwa ya kwake.

Kifo cha Regia Mtema, kimetusikitisha na kutuletea majonzi makubwa. Kama  alivyosema Mheshimiwa Zitto Kabwe, huyu alikuwa mbunge kijana ambaye ndo ilikuwa mara yake ya kwanza kuingia Bungeni, alikuwa na mpango wa kufanya mambo mengi, lakini maisha yake yamekatishwa kwa ajali ya barabarani. Wale wanaofuatilia mambo ya siasa za Tanzania, watakubalia na mimi kwamba Mheshimiwa Regia Mtema, alikuwa hafungwi na mipaka ya chama chake. Alikuwa ni mbunge aliyekuwa akitetea haki za walemavu, vijana na wanawake wote wa Tanzania, bila kuangalia chama.

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na viongozi wengine wa serikali na vyama vya siasa wamemsifia Marehemu Regia Mtema, kuwa miongoni mwa wa wazalendo wa Tanzania wenye jitihada binafsi za kuleta umoja na mshikamano katika taifa letu. Wazalendo wanaolitanguliza taifa mbele kabla ya kitu chochote kile. Wanatanguliza taifa kabla ya chama chao cha siasa, wanatanguliza taifa kabla ya  tumbo lao na familia zao.

Hivyo wakati tunamlilia Regia Mtema, tuache utamaduni huu wa Kazi ya Mungu haina makosa. Tukubali makosa yetu, tukubali kwamba kwa namna mmoja ama nyingine tumechangia kifo cha Kijana huyu na wengine wanaokufa kwa vifo vinavyoweza kuzuilika. Uchungu tulionao utusukume kuanza kufanya maamuzi ya kulijenga taifa letu lenye viwango. Mungu  amlaze mahali pema peponi ndugu yetu, rafiki yetu, mwanaharakati na mzalendo wa kweli wa Tanzania Mheshimiwa Regia Mtema. Amina.

Na,

Padri Privatus Karugendo 

0 comments:

Post a Comment