KAMA CHADEMA HAWANA “GOOD WILL” MWENYE “GOOD WILL” NI NANI?

Tarehe 10 Novemba wakati Waziri Mkuu Pinda akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa Wabunge, alisema kwamba CHADEMA hawana “Good will”. Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na serikali kumaliza mgogoro wa Arusha:

“Nyie Chadema hicho mnachokifanya huko Arusha hakionyeshi nia njema ya kisiasa ya kumaliza mgogoro huo, huu uwanaharakati wa ‘Peoples Power’ wala hauna tija”.

Waziri Mkuu aliendelea kusisitiza kwamba misuguano ya kisiasa kule Arusha na kwingineko inahitaji “Good will” kwa pande zote. Kwa maana kwamba Serikali iwe na “Good will”, CCM wawe na “Good will” na Chadema wawe na “Good will”. Bahati mbaya alishindwa kuonyesha kwa mifano “Good will” ya upande mwingine zaidi ya kukilaumu chama cha Chadema kwamba hakina  “Good will”. Tungependa na kusikia juu ya “Good will”  ya serikali na ya CCM.

Nimekuwa na heshima kubwa kwa Waziri Mkuu, nimekuwa nikiamini na naendelea kuamini kwamba ni mtu makini. Kwamba sifa anayopewa ya Mtoto wa Mkulima ni kweli, maana hana makuu na wala jina lake halisikiki kwa watu waliohujumu rasilimali za taifa letu. Ni mtu ambaye jina lake halikutajwa huko nyuma kwa watu waliokuwa wakitafuta kuingia madarakani kwa njia zozote zile. Nimekuwa nikimchukulia kuwa mzalendo na mtu mwenye mapenzi makubwa kwa Tanzania na watu wake. Lakini kwa hili la “Good will” amenikwaza! Amenifanya niwe na mashaka kama anafahamu maana ya neno “Good will” kwa lugha yetu “Nia njema”. Najiuliza maswali mengi bila majibu. “Nia njema” ni mtu kuwa mjinga, kukaa kimya na kukubali kila kitu hata kama inamaanisha kupoteza maisha yako, ya familia yako, ya taifa lako na maisha ya vizazi vijavyo? Kupinga malipo ya Dowans, ni kutokuwa na “Good will”, kutaka Demokrasia ya kweli, bila kutumia fedha kununua kura na shahada ni kutokuwa na “Good will”? Kudai rasilimali za nchi hii ziwanufaishe watanzania wote ni kutokuwa na “Good will”? Kutaka watanzania wote kushiriki mjadala wa kuandika katiba mpya ni kutokuwa na “Good will”? Kupinga matumizi mabaya ya fedha za umma na uporwaji wa ardhi unaoendelea katika taifa letu ni kutokuwa na “Good will”?

Mtu mwenye “Good will” ni lazima apende majadiliano na kutafuta muafaka.  Mtu mwenye “Good will” ni lazima atambue kwamba Tanzania ni yetu sote na vyama vyote vya siasa ni sawa. Waziri Mkuu Pinda, anatoa ushuhuda kwamba Chadema, kwa suala la Arusha walikuwa tayari kukaa meza moja na CCM kujadiliana, lakini CCM hawakuona kama kuna jambo la kujadiliana na CHADEMA. Mtu anayeijua hali ya Arusha, atasema hakuna la kujadiliana? Mheshimiwa Waziri Mkuu, alisema hivi Bungeni:
 “Sasa baada ya hapo niliona barua ya CCM kwenda kwa msajili, ambayo wanasema hawaoni kama kuna jambo la kuzungumza na Chadema. Labda kwa wenzetu kama wanaona liko jambo bado la kuzungumza walete taarifa”.

Kwa maelezo haya ya Waziri Mkuu, ambaye ndiye aliyetoa ushauri wa Msajili wa vyama vya siasa kuwakutanisha Chadema na CCM, ili wajadiliane tofauti zao kwenye Umeya wa Arusha, inayonyesha kwamba CCM ndo walikataa kukaa meza moja na Chadema. Hapa nani hana “Good will”, sitaki kuamini kwamba Waziri Mkuu, alitumia neno hili bila kulijua maana yake, au kwamba mapenzi ya chama chake yamemlewesha kiasi cha kutotambua mema na mabaya.

Waziri Mkuu anasema: “Labda kwa wenzetu kama wanaona liko jambo bado la kuzungumza walete taarifa”. Kama CCM, hawako tayari kukaa meza moja na CHADEMA kupatanishwa kwa suala la Arusha, hivyo  taarifa anayosema waziri Mkuu ipelekwe wapi na kwa njia zipi? Ndo hivyo inapelekwa kwa njia ya maandamano. Duniani kote, serikali zinazoziba masikio na kuwa na kiburi kupindukia kama ilivyo serikali ya CCM, zinapelekewa ujumbe kwa maandamano na migomo.

Mtu anayeamua kufanya maandamano, au mtu anayeamua kuvaa mabomu na kujilipua, maana yake ni kwamba njia nyingine za kudai haki zake na za wengine zimeshindikana. Uchaguzi wa umeya wa Arusha, ulivurugwa makusudi mazima na CCM kwa kushirikiana na vyombo vya dola. Chadema wangefanya nini zaidi? Wangefanya nini kuonyesha kwamba wana “Good will”? Kukaa kimya na kutulia wakishuhudia haki ikipotea ndiyo kuwa na “Good will”?

Ni nani mwenye “Good will” katika taifa letu la Tanzania? Haya yote tunayoyashuhudia ambayo yamekuwa kama Litania ya EPA, DOWANS, RICHMOND na mengine mengi ndo “Good will”? Thamani ya shilingi inashuka kwa kasi, bei ya mafuta inapanda, bei za  bidhaa nyingine muhimu kama sukari inapanda kwa kasi, mishahara ya watumishi inachelewa…. Hapa kuna “Good will”?

Tumeshuhudia jinsi wabunge wa upinzani walivyo na mchango chanya ndani ya Bunge letu Tukufu. Lakini mara nyingi hoja zao zinatupwa kwa sababu ya wingi wa wabunge wa CCM. “Good will” iko wapi kama wabunge wa CCM, wanazikataa hoja za CHADEMA si kwa kutokuwa na mantiki, bali kwa vile zimetoka upinzani?

Ningependa kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu: Mambo yanapokwenda ovyo serikalini, yeye anajua fika kwamba kuna mambo mengi yanakwenda ovyo. Analikumbuka sakata la Jairo, wapinzani ambao kazi yao kubwa ni kuisahihisha serikali na kuiondoa madarakani (kwa kura) kama haiwezi kutimiza mahitaji ya watanzania ,wafanye nini mambo yanapokwenda ovyo? Wakae kimya ili kuonyesha wana “Good will”?

“Good will” ni kuunga mkono kila kitu hata mambo ya ovyo? Inashangaza kwenye mjadala unaoendelea wa Sheria ya Manunuzi ya Umma, wabunge wa CCM, wanaunga mkono Serikali kununua vitu vichakavu. Kisingizio kwamba hatuwezi kununua vitu vipya, maana hatuna fedha. Ni kweli hatuna fedha?  Nchi yenye dhahabu, almasi, na madini mengine mengi, nchi yenye utajiri mwingine wa mbuga za wanyama, maziwa yenye samaki na ardhi kubwa kwa kilimo, tunasema hatuna fedha? Kama tunakubali kununua vitu vichakavu, basi na viongozi wetu wasitibiwe tena nje ya nchi. Tukubali kwamba sisi ni masikini na hadhi yetu ni vitu chakavu. Viongozi wetu wanazikimbia hospitali zetu na kwenda nchi za nje, kwa vile hospitali zetu ni chakavu. Zingekuwa nzuri na ziko kwenye viwango vizuri wangetibiwa hapa.

“Good will” iko wapi? Watanzania wanalilia katiba mpya. Lakini mswada unaopelekwa Bungeni ni wa marekebisho ya katiba. Kurekebisha katiba na kuandika katiba mpya, ni vitu viwili tofauti. Watu wakiingia barabarani kudai “Katiba mpya” tutasema hawana “Good will”?

Juzi hapa Umoja wa Vijana wa CCM, walikatazwa kufanya mkutano na maandamano, hawakusikia. Wakafanya na hakuna kilichotokea. Chadema, wakijaribu wanakamatwa na kuwekwa ndani. “Good will” iko wapi, kama sheria zinafanya kazi kwa upande mmoja tu wa wapinzani na kukaa kimya kwa upande mwingine wa chama tawala?

Kuna mifano mingi inayoonesha jinsi serikali inavyonyanyasa upinzani na kukipendelea chama tawala. Sina haja ya kutoa mifano maana sote tunaishi Tanzania na tunashuhudia yale yanayotokea kila siku. Kama tuna nia njema na taifa letu, tuondokane na “Kiburi” cha kisiasa, tushirikiane kulijenga taifa letu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.


 

0 comments:

Post a Comment