TANZANIA TUKO NJIA PANDA AU TUMECHANGANYIKIWA?
 
Tarehe 16 na 17 mwezi huu wa Desemba 2011 REDET iliandaa mkutano  wa 18 wa hali ya siasa  Tanzania katika  ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar-es-Salaam. Mara nyingi mikutano hii imekuwa ikiendeshwa kwenye mazingira ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Kufuatana na vurugu, migomo na maandamano, utulivu umepungua kidogo kwenye mazingira ya chuo na REDET iliona si busara kuendesha mkutano huo kwenye mazingira ya chuo maana dalili za kuwa njia panda na kuchanganyikiwa ni hatari! Kuhakikisha mkutano wa Hali ya siasa unaendeshwa kwa amani na utulivu waliamua uendeshwe nje ya mazingira ya chuo.
 
Uamuzi wa kuendesha mkutano huu nje ya chuo ulikuwa mzuri, ingawa baadhi ya washiriki walitamani ungeendeshwa kwenye mazingira ya chuo kikuu kama ilivyokuwa huko nyuma. Hata kama wanafunzi wangeshika mabango, maana mkutano ulifunguliwa na Makamu wa Rais wa Serikali ya Muungano ya Tanzania, ingekuwa vizuri kupima hali ya siasa Tanzania. Ni kujidanganya kutaka kuendesha mkutano wa hali ya siasa nchini kwenye mazingira ya utulivu na amani wakati tumezungukwa na hali tete katika taifa letu. Lakini pia kuendesha Mkutano wa hali ya siasa nje ya chuo kuliwanyima maprofesa na wanafunzi ambao walikuwa wakiendelea na  masomo kushiriki mkutano huo. Huko nyuma maprofesa na wanafunzi wakati wa mapumziko au kama mtu hana vipindi viwili vitatu, walikuwa wakichomoka na kuingia ukumbi wa Nkuruma kushiriki majadiliano. Kwa vile mkutano ulikuwa nje ya chuo nafasi hiyo haikuwepo. Pengo hili lilionekana wazi maana mkutano huu wa 18 wa hali ya siasa Tanzania ulikuwa na ubaridi kidogo.
 
Mada kuu ya mkutano huu ilikuwa Demokrasia Na Mageuzi ya Kijamii Tanzania. Mada hii iligawanywa kwenye mada ndogo tano: Kuielewa Demokrasia na Mageuzi ya Kijamii iliyoandaliwa na Profesa. Athumani J Liviga na kuwasilishwa na Profesa Mallya; Wakala wa Mageuzi ya Kijamii, iliandaliwa na Profesa Frederick J. Kaijage na Bw Bahiru Ally; Demokrasia, Utamaduni na Mageuzi iliyoandaliwa na Profesa Ernest Mallya na kuwasilishwa na Dkt Sansa; Kuzitafakari upya Taasisi za Kisiasa na Kiutawala Tanzania iliyoandaliwa na Dkt Mohamed A.Bakari; Demokrasia na Mageuzi ya Kiuchumi iliyoandaliwa na Prof. Samuel Wangwe na mwisho ni Demokrasia na Mageuzi ya Kijamii Tanzania: Nini kifanyike iliyoandaliwa na Dkt. Benson A.Bana.
 
Mada zote ziliwasilishwa vizuri na kuchambuliwa ipaswavyo. Wadau wa REDET ambao ni wanasiasa, wananchi na wanazuoni walilitumia vizuri jukwaa hili la majadiliano. Tofauti na miaka mingine ambayo watu walikuwa wakichambua na kuongea kwa kuonyesha wazi hisia zao, mwaka huu na hasa kwa upande wa wanazuoni kwa maana ya Maprofesa wa chuo kikuu cha Dar-es-Salaam, hali ilikuwa tofauti kidogo. Waliongea kwa uangalifu mkubwa na kwa umakini wa kutoonyesha hisia  zao. Inawezekana kuna sababu kubwa inayosababisha hali hii kwa nyakati hizi tulizomo, lakini si hoja ya makala hii hivyo nitaijadili huko mbeleni.
 
Mkutano huu wa hali ya siasa Tanzania uliibua mengi Mheshimiwa Januari Makamba alionyesha wazi wasi wasi wake wa Tanzania kuwa na idadi kubwa ya vijana ukilinganisha ni nchi nyingine kama Japani; “ Japani ina wazee wengi na vijana ni wachache, vijana hawa wana uhakika wa ajira, tofauti na hapa Tanzania ambapo tuna wazee wachache na vijana wengi ambao hawana uhakika wa ajira na hii ni hatari kubwa kwa taifa letu” Alisema Mheshimiwa Makamba. Mheshimiwa Mnyika, alionyesha wasi wasi wake juu ya mchakato mzima wa kuipata Katiba Mpya: “ Tukikosea mchakato, hatuwezi kupata katiba nzuri ya kuliongoza Taifa letu. Muswada ambao umepitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais, haukujadiliwa na wananchi. Matokeo yake hayawezi kuwa mazuri” Alisisitiza Mheshimiwa Mnyika. Mzee Chipaka, alipinga wazo kwamba tunaandika katiba mpya “Kilichowasilishwa Bungeni ni Kurekebisha katiba, hivyo hapa hakuna hoja ya katiba mpya” Alisema Bwana Chipaka. Naye Bwana Mukama, katibu mkuu wa CCM alisema “ Katiba si muarobaini wa kila kitu. Nchi kama Uingereza haina katiba, lakini mambo yake yanakwenda vizuri. Jambo la msingi si kutunga katiba mpya bali ni taifa kukubaliana linataka kuelekea wapi”. Naye Dkt Benson Bana, mwenyekiti mwenza wa REDET alisema “ Ni lazima katiba mpya ichukue karibia asilimia 80 ya katiba ya sasa. Kwa maana hiyo si kuandika katiba mpya bali ni kufanya marekebisho ya katiba iliyopo sasa”. Na swali ambalo wachangiaji wengi walirudia kila wakati ni: Tanzania tuko njia panda au tumechanganyikiwa? Kufuatana na hali ilivyo sasa hivi; ugumu wa maisha, ufisadi, udhaifu wa uongozi, migomo na maandamano, wizi wa kura wakati uchaguzi, matumizi makubwa ya fedha wakati wa uchaguzi, watu wachache kujitokeza kupiga kura, muswada wa mchakato wa kuandika katiba mpya kupitishwa kinyemela bila kujadiliwa na walio wengi, baadhi ya washiriki wa mkutano huu wa Hali ya siasa Tanzania, walikubali kwamba Tanzania sasa tuko njia panda. Na baadhi walifikiri si njia panda tu bali ni tumechanganyikiwa.
 
Bwana Bashiru Ally, yeye alipinga kwa nguvu zote hoja hii ya kuwa njia panda: “Ili tuseme tuko njia panda, ni lazima tujiulize kama tulikuwa na safari moja” alihoji Bwana Bashiru Ally. Kwa maoni yake ni kwamba ili tupige kelele za kuwa njia panda ni lazima tuonyeshe na dunia ijue kwamba Tanzania tulikuwa tunalenga kumoja. Kwa miaka hamsini tumekuwa tukielekea wapi kama Taifa? Mfumo wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ulifia njiani na baada ya hapo hatujafanikiwa kutengeneza mfumo unaoeleweka, hivyo ni vigumu kusema kwamba tuko njia panda. Labda tuseme tumechanganyikiwa maana tumepotea njia kama taifa.
 
Bi Marie Shaba, muumini mkubwa wa Azimio la Arusha na mwana harakati wa siku nyingi wa kupinga ubeberu na ukoloni mambo leo aliukumbusha mkutano wa 18 wa hali ya siasa Tanzania msimamo wa Mwalimu Nyerere kwamba fedha ni matokeo na wala si msingi wa maendeleo. Wakati akichambua mada iliyoandaliwa na Profesa  Mallya ya Demokrasia, Utamaduni  na Mageuzi ya kijamii alisema “ Tumeabudu fedha na kufikiri kwamba fedha ni msingi wa maendeleo ndo maana tuko njia panda. Tukitanguliza fedha, ni lazima tutangulize faida na ushindani. Kwa njia hii hatuwezi kushughulikia mambo mengine ya msingi ndani ya jamii yetu. Hatari ni kwamba tunaweza kuuza kila kitu hata na kuiuza nchi yetu. Ni muhimu kurudi kwenye misingi ya Azimio la Arusha na kutambua kwamba fedha ni matokeo ya maendeleo na wala si msingi wa maendeleo. Miaka hamsini ya uhuru na hasa ile miaka tulipolizika Azimio la Arusha, imetuonyesha ukweli kwamba fedha si msingi wa maendeleo”.
 
Bwana Mangula, Katibu mkuu wa zamani wa CCM, ambaye kusema ukweli alikijengea chama chake heshima kubwa na wakati wake hatukushuhudia mgawanyiko na makundi ya kimtandao kama tunavyoshuhudia hivi leo aliwashambulia wanazuoni kubaki kwenye ngazi ya kitaifa na kimataifa: “ Ninaishi kijijini. Mtu muhimu kwangu ni Mwenyekiti wa Kijiji na mwenyekiti wa kitongoji. Sikumbuki Mkuu wa Wilaya kutembelea kijiji changu au kimwitaji kwa shughuli za siku kwa siku katika kijiji changu. Nimepitia mada zenu zote, naona zinabaki kwenye ngazi ya kitaifa. Mbona hamuelekezi nguvu zenu za utafiti kwenye vijiji na vitongoji. Lakini mbaya zaidi hata marejeo ya mada zenu ni Maprofesa wa Ulaya na Amerika. Hivi hakuna watanzania walioandika juu ya mada hizi mnazoziwasilisha” Alisema Bwana Mangula.
 
Bwana W. Mukama, katibu mkuu wa CCM, alipinga hoja ya kuwa njia panda na kuchanganyikiwa kama taifa. Yeye anaamini Tanzania ina uongozi bora na uchumi wake unakuwa kwa kasi. Ingawa washiriki wengi walimzomea Bwana Mukama kwa mawazo yake hayo yeye aliendelea kujigamba mwamba “ CCM ina ridhaa ya wananchi kuiongoza na kutawala Tanzania” Alisema Bwana Mukama kwa majivuno na kujiamini.
Mawazo ya Bwana Mukama yalipigilia msumari wa nguvu kwenye hoja yetu ya Tanzania kuwa njia panda au kuchanganyikiwa. Maana inashangaza mtu msomi kama Mukama, anaweza vipi kusimama na kusema kwa kujiamini kwamba CCM ina ridhaa ya watanzania? Labda kama angesema kwamba kwa mfumo dhaifu wa demokrasia tulio nao CCM ndicho chama kilichopata kura nyingi. Maana sasa hivi Tanzania tunafikia idadi ya watu milioni 40. Tunaambiwa waliojiandikisha kupiga kura ni milioni 20, na waliojitokeza kupiga kura ni milioni 8 na waliochagua CCM ni kama milioni tao hivi. Kwa takwimu hizi mtu anaweza kupata wapi kiburi cha kusema kwamba CCM ina ridhaa ya watanzania kuongoza?
 
Kuna mshiriki aliyepiga kelele na kusema: “Vyama vya upinzani havikushindwa uchaguzi, ni kwamba havikuwa na fedha za kununua kura”. Katika hali hii ambayo kila mtu anatambua kwamba CCM inashinda chaguzi kwa kununua kura, mtu anaweza vipi kupata kiburi cha kusimama na kusema chama chake kina ridhaa ya kuiongoza Tanzania kama sikuwa njia panda na kuchanganyikiwa? Swali linaweza kuwa je kama CCM ina ridhaa ya kuitawala Tanzania, mbona inatumia fedha nyingi kwenye chaguzi ndogo? Sote tulishuhudia jinsi CCM ilivyotumia fedha nyingi kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga.
 
Wakati baadhi ya watu,wa kitetea uchumi wa Tanzania kukua kwa kasi ya kutisha kwa vigezo vya kiuchumi wananavyovijua wenyewe, watanzania wa kawaida ambao kipato chao ni cha chini wanahoji mambo mengi. Bei ya sukari inakaribia kuwa shilingi elfu tatu. Bei ya petroli na dizeli ina karibia kuwa  elfu mbili na miatano, bei ya mchele na vyakula vingine haishikiki, kodi (pango) ya nyumba inapaa kwa kasi wakati mshahara wa kima cha chini unabaki pale pale.
 
 Tuna watawala ambao wamejilimbikizia mali na wanaendelea kujilimbikizia mali kama tulivyoshuhudia wabunge wakitaka kujiongezea posho; hawaangalii uhai wa taifa letu bali wanaangalia uhai wa matumbo yao na familia zao. Hali kama hii ni lazima ituweke njia panda. Ingawa Bwana Mukama anasema kwamba Katiba si muhimu sana, ni imani ya walio wengi kwamba tukiwa na katiba nzuri na kukubaliana kama taifa tunakotaka kwenda, tutaondoka njia panda na kusonga mbele.
 
Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment