TUNA MENGI YA KUJIFUNZA KUTOKA SUMBAWANGA 2 Makala ya juma lililopita nilipoandika juu ya Sumbawanga, na hasa juu ya vijiji vya Ujamaa ambavyo ni ushuhuda wa kazi kubwa aliyoifanya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, mfumo ambao ni mzuri kwa nchi za Afrika zinazoelekea kwenye maendeleo, baadhi ya watu walinitumia ujumbe wa kunipongeza. Watu wa Sumbawanga, walinishukuru kwa kuiweka Sumbawanga kwenye ramani na kunipongeza kwa kushuhudia ufufuko wa Mwalimu Nyerere katika vijiji vyao vya ujamaa. Mtu mmoja, ninasema mmoja, maana hadi sasa ndiye peke yake anayeonekana kwenda kinyume na wengine, alinipinga vikali sana. Kwa maoni yake, ni kwamba vijiji hivyo vya Sumbawanga si mfumo uliobuniwa na Mwalimu Nyerere, bali ni mfumo uliokuwepo miaka mingi. Bwana huyu alijitambulisha kwa jina la Sixtus Henriko Mwanambuu mzaliwa wa Chala, wilaya ya Nkasi. Kwa vile mimi ninapoandika, situngi misahafu, natoa maoni yangu, nimeonelea niwashirikishe maoni haya ya Bwana Sixtus, jinsi alivyoyaleta kwa njia ya barua pepe, bila kubadilisha chochote. Na mwisho nitawawekea Utetezi wangu. Uwanja uko wazi kwa majadiliano na Kuelimishana. Si kwamba tunashindana, bali tunaelimishana na kuutetea ukweli ili tusipotoshe historia: “…nimesoma makala yako katika gazeti la Tanzania Daima la jana Jumapili Mei 13 (ukurasa wa 14) kwa mshangao, kuhusu Sumbawanga. Mimi ni Mfipa toka kijiji cha Chala wilayani Nkansi. Katika makala yako, umetaja vijiji kadhaa vya Sumbawanga kwamba vijiji hivyo ni matunda ya sera ya Ujamaa ya Mwl Nyerere, ukavivika gamba la ujamaa. Hii ni tofauti kabisa na historia ya vijiji hivyo. “…Kwa taarifa yako, vijiji vingi sana vilikuwapo hata kabla ya mkoloni kufika Ufipa. Historia inaeleza kuwa walipofika Watutsi huku kwetu, waliwakuta Wafipa wakiwa na vijiji vyao. Watu hawa waliingia Ufipa na kwa hila wakaweza kuitawala Ufipa hadi alipofika mkoloni wa kwanza kutoka Ulaya (Mjerumani) kupitia Ujiji, akajistawisha kijiji cha Kasanga, akakibatiza jina la Bismarckville. Wakati wote huo Watutsi walitawala Ufipa kupitia vijiji vyao, kwa watawala wenyeji walioitwa majina mbalimbali kama “Walasi, wenenkandawa” n.k. Mjerumani alifuatiwa na Mwingereza, naye akavikuta vijiji hivyo. “…Kilichofanywa na wakoloni hao ni kunyoosha mistari katika ujenzi wa nyumba za vijiji hivyo, kwa kuzingatia utamaduni wa vile vya huko kwao walikotoka. Lakini vijiji vyenyewe vilibaki vilivyokuwa. Kwa utamaduni wa Kifipa, kila mtu mzima kwa kawaida alikuwa na nyumba mbili; kijijini, na katika shamba lake (Imambi, iliyotumiwa msimu wa kilimo). Desturi ya Wafipa ilikuwa kuishi kijijini kwa pamoja, na kulima mashamba yao binafisi yaliyozunguka kijiji chao, kila mtu na shamba lake. Lakini nyenzo kuu ya uchumi katika Ufipa ilikuwa kushirikiana. Wakati wa kulima walilima kila shamba la mwanakijiji kwa kualikana wakaenda kulima kijiji kizima kwa siku moja katika shamba la mmoja wao (kwa Kifipa ukulimya); wakati wa mavuno walifanya hivyo hivyo, wakavuna shamba moja baada ya jingine mpaka mashamba yote ya kijiji yamevunwa (Ipula, kwa Kifipa). Hii ilihakikisha kila mtu ana chakula, na ndiyo maana wizi wa mazao haukuwepo; na mazao yaliachwa shambani katika ghala ziitwazo “Intanta” ili akina mama waje kuchukua kidogo kidogo na kupeleka kijijini chakula kikihitajika. Kwa kitoweo, walienda kuwinda kwa pamoja katika misitu ya jirani wakitumia mitego ya magogo ya miti (kwa Kifipa inkoka,), na nyavu za katani (Kwa Kifipa amasumbo). Mifugo ilikuwa michache. Kama hukutoka nje ya Ufipa, njia kuu za kupata mifugo zilikuwa mbili: kwa kurithi, na kwa kulipwa kwa kazi ya uchungaji; mfano ng’ombe mmoja kwa kila mwaka wa uchungaji (i ya luti, kwa Kifipa). Kwa kifupi huo ndiyo ujamaa wa jadi wa Mfipa. Wakoloni waliukuta, na vijiji hivyo vilikuwapo. “…Baada ya uhuru, siasa za Mwl Nyerere zilidandia ujamaa huo kwa kutaka kueneza mambo ya Kichina na Kikomunisti. Kuna maeneo siasa hizo zimeimarisha na mahali pengine zikavuruga ujamaa. Utashi ni wako kuamua kama kwa Sumbawanga siasa hizo zimeimarisha au kuvuruga. “…Hivyo ukitegemea Mh. Pinda amsifie Mwl Nyerere kwa kuanzisha vijiji vya ujamaa Sumbawanga, hutafaulu kwani atakuwa anaikataa historia yake yeye mwenyewe, na ya babu zake. Alipoenda kusoma Seminari ya Kaengesa Mh. Pinda alitokea kijijini kwao akiwaacha wazazi wake ndani ya kijiji. Pale Kaengesa alipokuwa anasoma ni juu kilimani, karibu na kijiji cha Kaengesa kilichokuwapo na bado kipo, jirani na maporomoko ya maji (Mpona). Hiyo ilikuwa miaka ya sitini (1960’s). Vile vile Mwadhama Kardinali Pengo alipotoka kwao Mwazye aliwaacha wazee wake kijijini, akaenda kusoma hapo hapo Kaengesa. Alitokea kijijini, akapita vijiji vingi tu hadi kufika seminarini. Leo hii akienda Mwazye akawaambia wazee wenzake wanaoelewa kijiji cha ujamaa ni nini, kuwa Mwazye ni kijiji cha ujamaa watamcheka na kujiuliza “Hivi hata Kardinali amekuwa mwongo?” Maana wamevisikia hivyo vijiji, lakini kwao hawaoni tofauti kati ya sasa na enzi za mkoloni hapo kijijini; hakuna maendeleo isipokuwa yaliyoletwa na mapadri na waarabu wawili watatu waliobaki hapo kijijini kwa ajili ya biashara! “…Nimekwishaeleza ujamaa wa jadi wa Kifipa. Ujamaa huu uliwaponza Wafipa wakatawaliwa kirahisi na Watutsi, wakitanguliwa na Wangoni waliotokea Africa ya Kusini. Hii iliendelea hata baada ya Uhuru. Kwa ukarimu huo huo waliwakaribisha hata Wakikuyu toka Kenya; ukienda kijiji cha Kipande utawakuta Wakikuyu waliobakia. Mfipa ameendelea kushirikiana na makabila na mataifa yanayomzunguka hadi leo. Hivi sasa kuna wimbi kubwa la Wasukuma wameingia Ufipa na makundi makubwa ya mifugo. Wameletwa na siasa za CCM na serikali yake za uraia wa Tanzania. Athari na misuguano inayoibuka hapa na pale na makundi hayo, ni tabia ya uvurugaji wa mfumo wa jadi za Kifipa unaoletwa sasa hasa na kabila hilo katika kutafuta malisho. Zamani mtu akiiba ng’ombe, atakamatwa kwa vile watu wanajuana; mfugaji ni nani, na ana ng’mbe wangapi. Leo haiwezekani. Kwa sasa hata mtu akiua hawezi kukamatwa kirahisi, atajichanganya na wageni hao na kupotelea mbali. “…Kwa hiyo, vijiji vya Sumbawanga kimsingi havikutokana na Ujamaa ulioletwa na Mwl. Nyerere miaka ya sabini (1975 onwards). Si vya “ujamaa” kwa maana hiyo. Hivi ni vijiji vya asili ya Mfipa. Ukitoa gamba hilo la Ujamaa wa Nyerere, vitabaki. Ndiyo maana vimedumu hadi leo. “…Nakuomba usiige tabia ya CCM ya kudandia kila kitu na kukifanya chake: majengo, viwanja, hoja n.k. Kuviita vijiji hivyo “vya Ujamaa, vilivyoletwa na Mwl Nyerere” ni kuvipa nembo visiyostahili na kupotosha historia” Nami nikamjibu: “…Ndugu yangu Syxtus, Nashukuru sana kwa maoni. Nilifika Chala, niliongea na wazee, wote walisema vijiji ni mfumo wa Mwalimu Nyerere! Niliongea na Vijana, niliongea na wanawake. Wote walisema ni vijij vya Mwalimu. Tena baadhi ya wanaume wanalaumu mfumo huu wa vijiji. Wanasema umeleta utandawazi! Wanasema wakati wakiishi mbali mbali ,waliweza kutunza utamaduni. Kukaa kampoja kumeleta mila na desturi za kigeni. Mfano walionipatia ni mfano wanawake kuwa na ukaribu na kuanzisha tabia ya kunywa pombe. Na nilishuhudia vikundi vya kina mama wakiwa wanakunywa pombe kupitiliza! “…Bahati nzuri nilikuwa na kinasa sauti, ni vigumu kukanusha! Si kwamba tukiamka tunaandika tu yaliyo kichwani mwetu. Tunafanya utafiti, tena utafiti wa kina! “…Sikwenda kama mtalii, nilitembelea watu na kuongea nao. Nilifika Mkomachindo, Nkana- Kalemasha, Sintali, Kanchui, Mpenge,Kabwe-Mpanga, Kabwe -Katandala kati, Kasu, Kisula-Kasanza, Milundikwa, Chala "A"- Utulivu, Chala "A"Tuwepamoja, Mwiza, Wampembe na Kizumbi. Huko pote walisema vijiji ni mfumo wa Mwalimu. “… Nilitembelea Kisungamile, Matai, Zimba, Mkamba,Mtowisa, Songambele, Sandulula, Malolwa, Kalole, Mwazye, Itekesha, Kifone, Katazi, Kanyezi na Ninga. Huko kote walisema vijiji ni vya Mwalimu. “…Unaweza kuwa na mawazo yako, unaweza kuwa na mtizamo tofauti na Vijiji vya Mwalimu, lakini ukweli nilioupata huko, siwezi kukubali kwamba wewe una historia nzuri kuliko watu wa Sumbawanga, niliokutana nao na kuongea nao. Nilikutana na mapadri Kama Malema Mwanampepo, Sangu, George na wangine vijana kama vile Mhasibu wa jimbo na Katibu wa Askofu. Wote hao walisema vijiji ni vya Mwalimu. Niliongea na Askofu Damian Kyaruzi,Askofu wa Kanisa Katoliki la Sumbawanga, ambaye unaweza kusema hafahamu vizuri historia ya huko kwa vile si mzawa, lakini na yeye ameambiwa kwamba vijiji ni vya Mwalimu. “…Baada ya kuandika makala, waliopiga simu, wote wanasema vijiji ni vya Mwalimu, tena wote wanatoka Sumbawanga. Nakubali mawazo yako, maana kila mtu ana mawazo yake, lakini nakubali mawazo ya wengi, tena watu wa huko Sumbawanga kwamba vijiji ni vya Mwalimu. “Nakutakia maisha mema na endelea kufanya utafiti juu ya Sumabawanga. Fanya hivyo bila kuwa na chuki ya itikadi yoyote” Nina imani kuna ambao wanaunga mkono mawazo ya mwenzangu na kuna ambao wananiunga mkono. Je Ukweli ni upi? Ni vijiji vya Mwaimu au ni vijiji vya mababu? Ni vizuri tukisikia sauti kutoka Sumbawanga. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment