HATA NJAA NI HATARI KULIKO UKIMWI Kuna hoja inayotolewa kwamba hapa Tanzania ugonjwa wa malaria unaua watu wengi kuliko UKIMWI, na wengine wanafikiri kwamba ajali za mabarabani zinaua watu wengi kuliko UKIMWI!! Si lengo la makala haya kupingana na waheshimiwa wanaofikiri kwamba Malaria na ajali za barabarani ni hatari zaidi ya UKIMWI. Lengo ni kuongezea hapo, kwamba hata na baa la njaa ni hatari na linaweza kuua watu wengi kuliko UKIMWI. Kwa maneno mengine ni kwamba bila mpangilio mzuri wa kuihudumia Jamii, kila kitu kinaweza kuwa hatari. Ni jukumu la serikali inayoongoza kutekeleza sera za chama tawala za kuihudumia jamii husika.Serikali yenye utawala bora inaelekeza matumizi ya pato la taifa katika kuhidumia jamii. Ethiopia, ilipokumbwa na baa la njaa, watu wengi na hasa watoto walipoteza maisha yao, ukweli huu haukuizuia serikali ya Ethiopia, iliyokuwa madarakani kwa wakati huo kuendelea kulitumia pato la taifa kwa mambo yasiyokuwa ya msingi! Viongozi wa serikali ya Ethiopia, waliendelea na safari zao za Ulaya za mapumziko na matanuzi, waliendelea kujenga majumba ya kifahari, waliendelea kuwasomesha watoto wao nchi za nje kwa kutumia pato la taifa lao. Mbaya zaidi waliendelea kutumia pesa za taifa lao kununulia silaha za kuwalinda waendelee kukaa madarakani wakati wananchi wanaendelea kufa kwa njaa. Tatizo la njaa la Ethiopia, lilishughulikiwa na mataifa ya nje, kuliko lilivyoshughulikiwa na viongozi wa nchi hiyo! Mungu, apishe mbali ikitokea hapa Tanzania, tukakumbwa na baa la njaa, ni kiasi gani cha watu watakufa? Ni wazi wengi kuliko wale awanaokufa kwa ugonjwa wa UKIMWI, lakini je ukweli huo unaweza kuyazuia mashagingi kuendelea kutembea? Misafara ya RAIS na viongozi wengine wa serikali itapungua? Viongozi wa serikali wataacha kutibiwa nje kwa gharama kubwa? Ajali za barabarani zinatokea kila siku. Ni nani anajali kufuatilia chanzo cha ajali hizo? Magari ya abiria yanapakia kupindukia, ni nani anajali kufutilia? Polisi, wana njaa, wakipewa senti kidogo wanaachia magari yaendelee na safari. Au magari hayo ni mali ya vigogo serikalini ?– ni nani ana uwezo wa kulizuia gari la kigogo hata kama gari hilo ni bovu na halifai kuwapakia abiria? Bila mpangilio mzuri wa huduma za jamii, kila kitu ni hatari. Hoja kwamba malaria inaua watu wengi kuliko UKIMWI inaungwa mkono na tafiti mbali mbali zinazoonyesha kwamba nusu ya vifo vyote barani Afrika husabishwa na magonjwa yanayozuilika na kutibika kama ilivyo malaria.Barani Ulaya ni asilimia 2 tu ya vifo husababishwa na magonjwa hayo. Ni kwanini? Viongozi wa Serikali za nchi za Ulaya, wana mpango mzuri wa kushughulikia huduma za jamii. Tofauti na viongozi wa Afrika. Viongozi wa Afrika, wanaangalia matumbo yao, anasa,majigambo na mashindano ya mtu binafsi.Marehemu Mobutu, alikuwa akitumia ndege ya rais na pesa za watu masikini wa Zaire, kwenda Amerika, kukata nywele!! Ninasikia kinyozi huyo alikuwa akilipwa zaidi ya dola 50,000 kwa safari moja! Katika kichaa kama hiki ni lazima magonjwa yanayotibika yawatafune waafrika maana kiasi kikubwa cha pato la kitaifa kinatumika kumhudumia mtu mmoja. Kiongozi mwingine wa Afrika, alikuwa anatumia ndege ya serikali kuwapeleka watoto wake shuleni Ulaya, asubuhi na kuwarudisha jioni!! Rais, mwingine alitumia pesa nyingi kwa mashindano ya kujenga kanisa kubwa kuliko la mtakatifu Petero la Roma! Juzi tu tumesikia kelele za Waganda, kwamba Rais Museveni, alitumia ndege ya Rais, kumpeleka mtoto wake Ujerumani, kujifungua! Wanasema pesa zilizotumika zingeweza kuwasaidia wanawake zaidi ya 500 kujifungua salama nchini Uganda. Ipo mifano mingi inayoonyesha kwamba watawala wa Afrika, wanafanya vituko vya kusikitisha badala ya kutumia rasmali za nchi zao kushughulikia huduma za jamii. Kama takwimu zinazotolewa na watafiti kama ni za kweli, basi hali ni ya hatari na inaonyesha kuna kasoro kubwa katika uongozi wa taifa: “ Malaria huua wastani wa Watanzania 100,000 kila mwaka, yaani sawa na kuua mtu mmoja katika kila dakika 5” Katika nchi zilizoendelea utafiti kama huu ungezua kelele na kutaka viongozi wa juu serikaini kujiuzulu!! Watu wangehoji ni kwa nini watu 100,000 wanakufa kila mwaka kwa ugonjwa unaotibika? Lazima maswali yangekuwa mengi: Kwani serikali haikupanga mipango ya kupambana na malaria? Kwanini serikali haikusambaza vyandarua na madawa? Kwanini serikali haikuwaelimisha wananchi juu ya hatari ya ugonjwa wa malaria. Kila mtu angechunguza bajeti ya serikali na kuangaalia ni kitu gani kilipewa kipaumbele na kupuuuzia ugonjwa wa hatari.Wangeagalia magari, ndege,posho za viongozi,safari za viongozi na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima sana. Vifo 100,000 kila mwaka ni vingi. Uchunguzi ungefanyika na kuiweka serikali kitimoto- hasa kushinikiza wanaohusika kuwajibika. Sisi tunaelezwa kwamba watu 100,000, kila mwaka wanakufa kwa ugonjwa wa malaria, tunabaki kimya. Serikali yetu ina vyanzo vingi vya mapato: Watalii, wanaingia nchini mwetu kwa maelfu, hawa wanaleta pesa za kigeni. Tuna migodi mingi,tuna viwanda vinauza minofu ya samaki nje ya nchi na kuingiza mamilioni ya dola, makampuni ya wawindaji kutoka nje yanaingiza mamilioni ya dola kila mwaka, tunazalisha mazao mengi nk, si kweli kwamba uwezo wa Serikali ni mdogo. Serikali yenye uwezo mdogo haiwezi kuwa na mpango wa kununua ndege ya Rais, na kuwa na uwezo wa kuwatibisha viongozi wa juu Serikalini kule Ulaya, kuwa na uwezo wa kumuda msafara wa magari zaidi ya kumi mumsindikiza Rais,Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Mawaziri wengine wanaopenda mbwembwe za ukubwa wanapoyatembelea majimbo yao. Ukiangalia bajeti inayotumika kuwatunza viongozi wetu,inakuwa vigumu kuamini kwamba Serikali yetu ina uwezo mdogo. Ni imani yangu kwamba hakuna mtanzania hasiyejua hatari ya malaria. Hata mtoto mdogo anajua kabisa dalili za malaria. Hata bila vipimo atakwambia ana malaria na ukimpima utakuta ana malaria. Mwaka, 1982, karibia nipoteze maisha kule Ujerumani. Nilisikia dalili za malaria, nilikwenda kwa daktari mjerumani na kumwambia anipatie dawa za malaria. Daktari huyo hakuamini, alisistiza kunipima kwanza. Hakuelewa nilijuaje nina malaria bila kunipima. Kupima kulichukua muda mrefu, unaju tena ukiwa mwafrika wanataka wapime kila kitu. Huku mimi nilikuwa hoi, malaria iliendelea kupanda. Wakati wanagundua kuwa nilikuwa namalaria,nilikuwa katika hali ya kutisha! Sisi tunaifahamu malaria – hasa watu wa vijijini wanaifahamu vizuri. Hakuna haja ya kuwaelezea wala kuwakumbusha. Tatizo ni wafanye nini: Zahanati za vijijini hazina madawa, watu wa vijijini hawana uwezo wa kununua vyandarua - wale wenye uwezo wanahitaji kuelimishwa. Ni kazi ya serikali kuwaelimisha watu. Mfano, watu wanapoteza pesa nyingi kwenye pombe. Wanakunywa pombe bila kuzijali afya zao na za familia zao.Pesa wanazozitumia kwenye pombe zinatosha kumnunulia kila mwanafamilia chandarua na kumtibisha. Elimu ni muhimu sana kule vijijini. Siku moja nilikuwa nikiongoza ibada ya jumapili,familia moja ilitoa sadaka ya shilingi 1500. Baada ya ibada, familia hiyo ilinioamba msaada wa usafiri kumpeleka mtoto hospitali. Nilipotaka kujua ni kwanini mtoto hakupelekwa hospitali hadi malaria ikapada hivyo, nilijibiwa kwamba hawaku na pesa. Niliamua kuwarudishia pesa zao walizokuwa wametoa sadaka ili wazitumie kumtibisha mtoto.Ni wazi niliiingia matatani baadaye kwa kulaumiwa kuzitumia pesa za sadaka vibaya; heshima, ni kwamba mtoto alipona! Vijijini watu wanaweza kupata shilingi 1500 kutoa sadaka au kuchangia sherehe za kumkaribisha mkuu wa wilaya kijijini wakashindwa kupata pesa za kununua dawa za kumtibu mtoto! Tunaimba kwamba kilimo ni uti wa mgogo wa uchumi wa taifa letu. Tunajua wazi kwamba kilimo kwa asilimia kubwa kinaendeshwa na watu wa vijijini. Ni watu hawahawa wanaoshambuliwa na malaria, ugonjwa unaotibika na kuna uwezekano wa kujikinga mtu asishambuliwe na mbu. Kwanini basi serikali isiwe na mpango maalumu wa kupambana na malaria? Kwanini serikali isinunue vyandarua na kuvisambaza vijijini, kwanini serikali isihakikishe zahanati zetu zote zina madawa ya kutibu malaria? Takwimu zinaonyesha watoto walio chini ya miaka mitano wanashambuliwa sana na malaraia na wengi wao wanapoteza maisha. Kwanini ugonjwa unaotibika uendelee kutupokonya taifa la kesho? Hawa wanaokufa si watoto wa viongozi, si watoto wa matajiri, ni watoto wa masikini – ni watoto wa vijijini. Hawa ni watoto wanaoishi kwenye nyumba za kimasikini ambazo hata wakipewa vyandarua hawezi kupata mahali pa kuzifunga! Sasa hivi njaa inanyemelea. Kwanini tuwe na uhaba wa chakula wakati tumezungukwa na maziwa makubw matatu? Bila kuitaja bahari ya Indi? Ni bora kuwa macho, bila mpangilio kila kitu ni hatari kubwa. Tusiangalie malaria na ajali za barabarani tu! Kuna njaa,tishio la ukosefu ajira,ujambazi, watoto wa mitaani nk. Hapa ni lazima kukumbuka ushauri wa bure: Adui wakubwa wa nchi hii, adui wakubwa wa serikali na chama tawala, si wengine bali ni wale wanaouona ukweli wa mambo na kukaa kimya. Ni wale wanaokaa kimya kuyalinda maslahi yao; hawa ni hatari kubwa kuliko UKIMWI! Na, Padre Privatus Karugendo

0 comments:

Post a Comment