SIKU NILIPOFIKA SUBAWANGA. Hatimaye nimefika Sumbawanga na kukubali kwamba Tanzania ni nchi kubwa, nchi nzuri yenye ardhi nzuri na utajiri mkubwa kupindukia. Safari yangu ya kwenda Sumbawanga mwezi wa nne mwaka huu ilianzia Mwanza. Nilitoka Mwanza na kulala Morogoro. Nikatoka Morogoro na kulala Mbeya. Nikatoka Mbeya na hatimaye kufika Sumbawanga. Ni siku tatu za safari! Ni siku tatu za uchovu, lakini ni siku tatu za kushuhudia ukubwa na uzuri wa Tanzania. Ukisafiri safari hii, ni lazima ujiulize ni kwa nini Tanzania ni nchi masikini. Si lengo la makala hii kuchambua utajiri na umasikini wa Tanzania, hayo tuyaachie makala nyingine. Leo naandika kuelezea furaha yangu ya kufika Sumbawanga. Nimebahatiwa kuizunguka Tanzania yote, na kuitembelea mikoa yote ya Bara na visiwani, nilikuwa nimebakiza Sumbawanga! Mara yangu ya kwanza kukutana na watu wa Subawanga, tuseme wafipa, ilikuwa ni mwaka 1975, nilipokuwa nasoma falsafa kule Ntungamo Bukoba. Wafipa Walionekana kuwa wapole na kuongea kama wanaimba vile. Hawakupenda kula ndizi, walimsumbua sana aliyekuwa Mkuu wa Seminari ya Ntungamo Padri Damian Kyaruzi. Walitaka kula ugali, wakitania kwamba ndizi ni matunda. Walionekana kuwa watu wa msimamo usioyumba kiasi cha kuilazimisha Seminari kuanzisha ratiba ya kula ugali. Nafikiri leo hii Mheshimiwa Askofu Damian Kyaruzi, anayeliongoza Jimbo Katoliki la Sumbawanga, anazikumbuka enzi za Ntungamo na kucheka na kutambua ni kwanini wanafunzi wake wa kutoka Sumbawanga, walikuwa wanakataa kula ndizi. Watu hawa wanalima mahindi na vyakula vingine vingi. Ardhi yao ni nzuri na ina rutuba. Tatizo lao kubwa ambalo ni sugu na ni la miaka mingi ni kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi kufika kwenye masoko. Barabara zilikuwa na bado ni mbaya. Ujenzi wa barabara ya kutoka Tunduma hadi Mpanda, italeta mabadiliko makubwa. Mkoa wa Rukwa, uliundwa mwaka 1975, kwa kuimega wilaya ya Mpanda kutoka Tabora, na Sumbawanga kutoka Mbeya. Hivyo wilaya hizi kubwa ziliunda Mkoa wa Rukwa. Mkoa huu ulikuwa na wilaya za Sumbawanga mjini, Sumbawanga vijijini, Nkasi, Mpanda mjini na mpanda vijijini. Mkoa huu umegawanywa tena kwa kuimega tena wilaya ya Mpanda kuunda mkoa mpya wa Katavi. Pamoja na furaha ya kufika Sumabawanga kuona wanakatoka marafiki zangu niliosoma nao miaka ya ya sabini, kukutana na Mwalimu wangu wa zamani Mheshimiwa Askofu Damian Kyaruzi na kuona alikozaliwa Mheshimiwa Mwadhama Pengo Kardinal Policalypo, ambaye naye alinifundisha miaka ya sabini, furaha ya kuliona kaburi la Marehemu Askofu Msakila, aliyekuwa Askofu wa Sumbawanga ambaye aliyekuwa na msimamo usioyumba, mwenye madaraka ya kutisha, mtu aliyetoa mchango mkubwa katika kanisa na katika jamii nzima ya Tanzania na kuliweka Kanisa katoliki katika gazi ya kutoa huduma za kijamii katika Mkoa wa Sumbawanga na Katavi, hadi leo hii kanisa ni miongoni mwa mashirika ya kidini yanayotoa mchango chanya katika kuindeleza Sumbawanga; nilikutana na mambo mengine mawili yaliyonifurahisha sana, na ningependa kuwashirikisha wasomaji wangu. Jambo la kwanza ni mfumo wa vijiji vya Sumbawanga. Huu ni mfumo wa vijiji vya ujamaa. Ni mfumo ambao hakuna mtu yeyote anauongelea. Sijasikia hata chombo chohote cha habri kikiuelezea mfumo huu na kuusifia. Sijapata kuona pengine hapa Tanzania, ambapo vijiji vimepangwa vizuri kama vya Sumbawanga. Wenyeji wa kule wanasema mfumo huo ni wa Mwalimu Nyerere, maana kabla ya hapo waliishi mbali mbali na ilikuwa vigumu kuwasambazia hudma za kijamii kama vile hospitali, shule na huduma ya maji. Mwanzoni nilifikiri ni vijiji vichache vilivyopangiliwa vizuri hivyo. Lakini baada ya kutembelea Matai, Mtowisa, Sandulula, Mwazye, Katazi, Sintali, Kabwe, Chala na Wampembe, niligundua kwamba Sumbawanga yote imepangwa kwenye vijiji vya watu kuishi karibu kama familia moja. Hili la vijiji vya Sumbawanga, lilinigusa maana tumekuwa tukiambiwa kwamba Mwalimu Nyerere, alishindwa kutekeleza sera zake na ujamaa ulikufa. Lakini ukiona uhai wa vijiji vya Sumbawanga, unashangaa na kujiuliza ni kwanini tumekuwa tukifichwa ukweli. Na ni kwa nini viongozi hawajivunii mafanikio kama haya ya vijiji vya Sumbawanga. Tunataka kuionyesha dunia mafanikio ya aina gani? Kama tukishindwa kujivunia mafanikio ya watu kuishi pamoja na kuwezesha mambo kama uongozi, huduma za jamii, huduma za kiroho kuwa karibu ya wannachi. Vijiji vyote vina shule, nyumba za ibada, zahanati na maendeleo ya pamoja. Kwa vile watu wanaishi pamoja wanaweza kuamua mambo yao rahisi zaidi. Mfano Sumbawanga, wameamua kujenga nyumba kwa matofali ya kuchomwa. Nyumba zote zimejengwa hivyo. Wana mfumo wa kusimamia maadili kwenye vijiji vyao; tulishuhdia kwenye kijiji kimoja vijana na jamii nzima ikitoa adhabu kwa vijana waliokuwa wamekwenda kinyume na maadili. Vijana hawa ambao hatukufanikiwa kujua walikuwa wamfanya makosa gani, walilazwa chini na kuchalazwa viboko bilaya kujitetea mbele ya jamii nzima. Kuna mifano mingi ya kuonyesha faida na uzuri wa mfumo wa vijiji vya watu kuishi pamoja kama familia moja. Inashangaza ni kwa nini mfumo huu mzuri, ulifanikiwa Sumbawanga na hakufuanikiwa kwingineko Tanzania. Inashangaza zaidi kwamba pamoja na mafanikio haya ya Sumbawanga, hatusikii mtu, hata na wale wanaotoka Sumbawanga kama Mheshiiwa Waziri Mkuu Pinda, Waheshimiwa wabunge wa Sumbawanga na Katavi, hata na Mheshimiwa Pengo Karndinal Polycalypo wakisimama na kuimba mafanikio haya makubwa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Jambo jingine lililonifurahisha kule Sumbawanga ni watu wa makabila mbali mbali, watu wa mataifa mbali mbali kuishi pamoja kwa amani kwenye hivyo vijiji vya ujamaa. Sumabwanga hakuna msamiati wa “Wahamiaji haramu” kama tunavyousikia kule mkoa wa Kagera. Sumbawanga, kuna watu kutoka Malawi, watu kutoka Zambia, watu kutoka DRC, watu kutoka Burundi na watu kutoka Rwanda. Wote hawa wanaishi kwa amani na kuzisifia sera za Mwalimu Nyerere na kukubali kwa sauti moja kwamba Afrika ni moja. Jambo la kushangaza ni kwa nini msamiata wa “Wahamiaji haramu” usikike Kagera na usisikike Sumbawanga? Wahamiaji haramu wa Kagera, wanatoka Burundi na Rwanda. Lakini Sumbawanga, kuna watu wa Burundi na Rwanda, mbona hawa wanaishi bila kusumbuliwa kama wale wa Kagera? Tuna mengi ya kujifunza kutoka Sumbawanga. Kuna haja ya kujifunza mfumo wa vijiji vya ujamaa na kujaribu kuunda tena vijiji hivi sehemu nyingine za Tanzania. Lakini pia kuna haja ya kwenda Sumbawanga kujifunza jinsi watu wa nchi mbali mbali wanavyoweza kuishi pamoja kwa amani bila kuamsha kasumba ya msamiati wa “Wahamiaji haramu” Kumbe Mwalimu Nyerere, hakufa! Ni mzima na anaishi miongoni mwetu. Tatizo ni kwamba tuna macho lakini hatutaki kuona, tuna masikio hatutaki kusikia, tuna midomo na chakula kingi cha kututosha sote, lakini hatutaki kujongea mezani, tuna uwezo mkubwa wa kuhamisha milima, lakini tunakubali unyonge ututawale! Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment