SIKU YA WANAWAKE DUNIANI ITUKUMBUSHE KWAMBA WANAWAKE WANAWEZA. Kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani inatukumbusha ukweli wa kichwa cha habari kwenye makala hii, kwamba wanawake wanaweza, maana inasema: Ushiriki wa mtoto wa kike ni chachu ya maendeleo. Chuma ni kitu kigumu, lakini mbele ya moto hubweteka. Moto ni kitu kinachotisha, lakini huzimwa na maji. Maji yana Nguvu husababisha mafuriko na madhara makubwa, lakini hukaushwa na jua. Jua ni tishio, lakini dhoruba na mawingu hulifunika. Dhoruba hulipuka kwa nguvu, lakini hutulizwa na kumezwa na dunia. Dunia ni kitu cha fahari kubwa, lakini hutishwa na hutawaliwa na mwanadamu. Mwanadamu ana uwezo mkubwa, lakini huzuni na majonzi humlainisha. Huzuni na majonzi ni aina ya ubabe, lakini hulainishwa na divai. Ubabe wa divai kiboko chake ni usingizi! Lakini upole, huruma, unyenyekevu, upendo, kusamehe, heshima na nguvu ya Mwanamke, inazidi kila kitu!( Kutoka kwenye historia ya Ethiopia 1681, tafsiri ni yangu). Sifa hizi anazopewa mwanamke katika historia hii Ethiopia ( 1681) zinaweza kulinganishwa na maneno ya Yesu: “ Heri Wanaojiona kuwa na masikini mbele ya Mungu, maana Utawala wa Mbinguni ni wao… Heri wapole, maana watapewa nchi. Heri walio na njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana watashibishwa. Heri wenye huruma, maana watahurumiwa. Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu. Heri wenye kushughulikia amani, maana wataitwa watoto wa Mungu.” (Matayo 5: 3, 5-9). Ni sifa kama hizi anazopambwa nazo mama Maria: Mama mpole, mwenye huruma, mpatanishi, mama mnyenyekevu, mama wa shauri jema, mama wa ukombozi, mama wa Mungu nk. Tunaposema kwamba wanawake wanaweza, hatuna maana kwamba wapendelewe kupewa nafasi za uongozi. Kwamba wapate nafasi hata kama hawana uwezo, hata kama hawana sifa! Tunazingatia ukweli kwamba wanawake wanaweza. Hata hivyo tuna wanaume wengi ambao hawana uwezo na wamejazana kwenye uongozi; tunaoa wanaume wengi kwenye uongozi wanaochochea vurugu na vita badala ya kuleta amani na utulivu, tunao wanaume wengi kwenye uongozi wanaochochea umaskini na maisha duni ya wananchi. Hili tuliachie mjadala mwingine. Ikiwekwa mbali Elimu ya kusoma na kupata shahada mbali mbali, shahada ambazo hazijawasaidia wengi kuwa viongozi bora au watu bora, sifa muhimu za uongozi ni: Upole, huruma, unyenyekevu, upendo, kusamehe na heshima kwa watu. Mama au mwanamke ni mtu anayemjua vizuri mtoto wake. Kuanzia tumboni, kumnyonyesha, kumlea na kufahamu udhaifu wote wa mtoto wake – pamoja na yote hayo mama ndiye anayemthamini na kumheshimu mtoto wake kuliko mtu mwingine. Ule udhaifu wa utoto haumfanyi mama amdharau na kumnyanyasa mtoto wake. Hekima na kipaji hiki cha akina mama kinahitajika kwa uongozi wote, uwe wa kidini au wa nchi. Hekima hii ya huruma, unyenyekevu na upendo katika uongozi ilipotea kabisa kutoka katika Kanisa Katoliki na kwa vile kanisa hili lilikuwa na ushawishi mkubwa duniani, mfumo huu dume ulizagaa na kuenea dunia nzima. Kanisa na dunia wakatawala akina Petro na funguo zao za kufunga na kufungua kufuatana na mapenzi yao. Badala ya huruma, unyenyekevu na upole kutawala, dunia ikaongozwa na sheria, madaraka, kiburi, majivuno, vita na ubabe wa kila aina – vipaji ambavyo kwa kiasi kikubwa ni vya wanaume. Hekima, huruma, unyenyekevu na uongozi wa akina mama ulipenyeza katika kanisa la mwanzo na kulifanya kanisa hilo liwe la amani, utulivu na upendo uliozagaa na kuziambukiza jumuiya mbali mbali zilizokuwa zimelizunguka: “ Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu…” (Matendo 2: 47…). Wanawake walitoa mchango wao na kuambukiza karama na vipaji vyao moja kwa moja. Si kwa bahati mbaya kwamba hadi leo hii pamoja na ukweli wa kanisa kutekwa nyara na kutawaliwa na wanaume peke yao, bado linaitwa “Mama Kanisa”! Hii inatokana na mchango mkubwa wa kimama na karama na vipaji vya akina mama. Kanisa linatarajiwa kuwa chombo cha huruma, upole, unyenyekevu, upatanishi, upendo – sifa zote za kimama – Hivyo kanisa hadi leo hii linaitwa “Mama Kanisa” watawala wa Kanisa na kiasi kikubwa watawala wa nchi zote ni wanaume, lakini hawaoni aibu kutamka neno “Mama Kanisa”. Ninatoa mfano wa kanisa maana ni njia nzuri na yenye mfano hai wa kuonyesha kwamba wanawake wanaweza na waliweza huko nyuma. Lakini pia Kanisa limekuwa na ushawishi mkubwa kuonyesha kwamba wanawake hawawezi. Kanisa lilipotekwa nyara na wanaume na kuwaweka wanawake pembeni, dunia nzima ilifuata nyayo, hadi leo hii kasumba ni kwamba wanawake hawawezi! Mchango huu wa akina mama ulilifanya kanisa la mwanzo hadi 313 AD liishi kwa amani na utulivu. Na kusema kweli dunia ya wakati ule iliishi kwa amani na utulivu. Hakukuwa na kugombania madaraka, hakukuwa na kanisa kushiriki katika vita. Hakuna Mkristu aliyeruhusiwa kushiriki katika jeshi. Walisisitiza kwamba ujumbe wa Kristo ulikuwa ni wa amani na wa kutotumia nguvu. Hakuna aliyeruhusiwa kueneza habari njema kwa kutumia nguvu na kwa upanga. Walihimiza kumpenda jirani na adui kama alivyofundisha Kristu wa Nazareti. Tamko lao lilikuwa hili: “ Siwezi kuwa mwanajeshi, siwezi kwenda kinyume na haki, mimi ni Mkristu.” Ndiyo maana jumuiya ya Wakristu wa Mwanzo ilihama kama kundi kubwa kutoka Jerusalem na kuishi Pella ( Chirbet Fahil) maeneo ya Transjordan, mwaka wa 66/67 AD, muda mfupi kabla ya Jerusalem, kushambuliwa na Warumi. Msimamo huu wa kanisa la mwanzo wa kueneza neno la Mungu, kwa upole, huruma, kuvumiliana na unyenyekevu ambao uliongozwa na wanawake unaelezwa vizuri na wazee wa kanisa kama vile Athenagoras, Hyppolyt na Lactantius ambaye muda mfupi kabla ya 313 AD, alisema: “Kweli, hakuna kitu cha muhimu duniani kama dini. Hivyo ni lazima kuilinda dini kwa kujitoa muhanga na si kwa mauaji na mateso, si kwa upanga na kumwaga damu. Dini ilindwe kwa uvumilivu, upole na huruma. Dini ilindwe kwa imani na si kwa vitendo vya ujambazi. Unapoilinda dini kwa kuitetea kwa kumwaga damu na mateso, unakuwa huitetei bali unakuwa unaharibu kila kitu. Mtu hawezi kuwa mwenye haki kwa kueneza chuki, mauaji, mateso….”. Mambo yote yalibadilika mwaka wa 313, Mfalme Constatine ( Emperor Constatine the Great) alipobatizwa na kuwa Mkristu. Yeye alikuwa na malengo ya kuutumia Ukristu kupanua utawala wake. Alichanganya uongozi wa dini na serikali. Viongozi wa kanisa walipewa nafasi ya kutawala kama wafalme, walivikwa nguo za kifalme na kupewa ishara za utawala kama vile fimbo na pete (Mpaka leo hii tunawaona viongozi wa kanisa wakivaa kofia, wakishika fimbo na kuvaa pete, vitu hivi havina uhusiano wowote na Ukristu – ni ishara za utawala wa kidunia, ishara za mfumo dume uliotukuzwa na Constantine). Watawala wa Kanisa (wanaume) walianza kuunga mkono vita na kueneza imani kwa kumwaga damu. Msalaba ulitangulizwa vitani kama ngao na alama ya ushindi. Wanawake walitupwa nje ya mfumo huu mpya. Huruma, upole, unyenyekevu na kuvumiliana na lugha ya kutomwaga damu wakati wa kueneza neno la Mungu vilitoweka kabisa katika kanisa na katika duni yetu hii. Kanisa alilolitaka bwana Yesu wa Nazareti lilipotea tangia wakati huo hadi leo hii! Mfumo dume ulianza kuitawala dunia na kuzuka kwa ugonjwa mbaya sana duniani wa kugombania madaraka. Huruma, upole, uvumilivu, upendo, kuchukuliana, kusameheana – karama ambazo kwa kiasi kikubwa ni za wanawake zilitoweka kwenye uso wa dunia. Wapo wanawake waliojitahidi kukosoa mfumo dume na kulitaka kanisa kurudia misingi yake ya zamani. Wanawake hawa walipuuzwa na kutupwa pembeni. Mfano mzuri ni wa Catherine wa Siena na Teresa wa Avila ( 1515-1582). Wanawake hao walionyesha ushupavu wa pekee kwa kuongea na maaskofu na mapapa – kuwataka walirudishe Kanisa njia yake iliyo sahihi. Walitaka kurudisha karama ya huruma, upole, nyenyekevu, uvumilivu na upendo. Juhudi hizo zilileta matunda kidogo – lakini Kanisa liliendelea kuwa mikononi mwa wanaume na mfumo dume ulishika kasi ya kutisha duniani. Juhudi za wanawake wengine zilieleweka vibaya – walisingiziwa uchawi na walitendewa mambo mabaya. Magret Jones, alinyongwa mwaka 1648, Joan Peterson, alinyongwa mwaka 1618, mama Lakeland, aliyekuwa na kipaji cha kuponya na kutenda miujiza alichomwa moto 1645, Isobel Insch Taylor, aliyekuwa na kipaji cha kutibu kwa kutumia miti shamba alichomwa moto na viongozi wa Kanisa mwaka 1618. Mwanamke mwingine mwenye vipaji na aliyeheshimika sana mjini Wurzburg, Ujerumani, alichomwa moto na viongozi wa Kanisa mnamo mwaka 1645. Msichana mdogo Anna Rausch, aliyeonyesha vipaji vya hali ya juu katika Kanisa, alichomwa moto mwaka wa 1628 akiwa na umri wa miaka 12 tu. Ipo mifano mingine mingi ya kuonyesha jinsi wanawake walivyonyamazishwa na watawala wa kanisa (wanaume). Mfumo dume ulijengeka kwa njia hii na kusimika mizizi hadi leo hii. Hivyo tunaposema kwamba wanawake wanaweza hatuna maana ya kuwapendelea kwenye uongozi hata kama hawana uwezo, bali ni wito wa kutaka kuvunjilia mbali mfumo dume na kuingiza ndani ya uongozi karama ya akina mama ya huruma, upole, unyenyekevu, kusamehe, uvumilivu na kuchukuliana. Hata hivyo dunia yetu ni ya binadamu wote, ni dunia ya wanawake na wanaume! Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment