MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE, AMEFUFUKA! YUKO SUMBAWANGA! Kwa wale wanaofahamu mawazo na msimamo wangu juu ya miujiza, wataishangaa sana makala hii. Kawaida siamini miujiza, naamini vitu vinavyoweza kuhakikishwa kisayansi. Huo ndiyo msimamo wangu na wala sijabadilika! Kisa ninachokisimulia kwenye makala hii ni cha kweli na kimetokea mbele ya macho yangu pamoja na watu wengine niliokuwa nao kwenye gari. Tumekutana na Mwalimu Nyerere! Akiwa mzima, anatembea kwenye vijiji vya Kanyezi, Katazi na Ninga, Kata ya Katazi, wilaya ya Sumbawanga Vijijini. Ilikuwa tarehe 19.4.2012, nikiwa naendesha gari. Ndani ya gari hilo nilikuwa na vijana kumi. Namba hii kumi, ilijitokeza tu kwa bahati na wala hatukuipanga; namba hii ni ishara ya nyuma kumi kumi mfumo wa uliokuwa umebuniwa na Mwalimu Nyerere. Siku hiyo kulikuwa na dalili ya mvua kunyesha na upepo ulivuma kwa kasi na kuleta baridi kali kwa watu tuliokuwa tumetokea Dar-es-salaam. Wengi wetu ilikuwa ni mara ya kwanza kufika Sumbawanga. Kwa upande wangu nimeitembelea mikoa yote ya Tanzania, nilikuwa nimebakiza Sumbawanga. Tulipofika kijiji cha Kanyezi, kijana mmoja alipiga kelele na kusema “ Nimemuona Mwalimu Nyerere”. Sikujali sana, nifikiri labda ameona sanamu ya Mwalimu kwenye kijiji cha Kanyezi, lakini baada ya muda mfupi vijana wote kwenye gari walipiga kelele kwa shangwe na furaha kwamba nao wamemuona Mwalimu. Kwa furaha wote walianza kuimba wimbo wa “ Tanzania, Tanzania nakupenda kwa moyo wote” na kufuatisha wimbo wa vijana wa siku zote wanapokumbana na changamoto za maisha.. “ Kama si juhudi zako Nyerere…”. Sikuelewa kinachoendelea. Nilifikiri vijana hawa wamepagawa? Na wao walishangaa ni kwanini mimi peke yangu simuoni Mwalimu Nyerere? Nilifikiri mambo mawili, mbali na kupagawa au ulevi, labda tulikumbana na uchawi wa Sumbawanga au vijana wangu walikuwa wameshambuliwa na kifafa? Wanasema maana ya neno Sumbawanga ni “Tupa uchawi”. Nimekuwa nikisikia kwamba Sumbawanga kuna wachawi wa kutisha; wengine wanapaa juu kwenye ungo na wengine wana uwezo wa kutengeneza radi na mengine mengi. Dar-es-salaam, nimekuwa nikiona mabango mengi yenye maneno “ Mganga kutoka Sumbawanga, anatibu magonjwa yote, ana dawa za kuleta utajiri, kuongeza nguvu za kiume, mapenzi na mengine mengi”. Moyoni nikasema, labda hapo Kanyezi, tumetupiwa uchawi na sasa vijana wameanza kuona maajabu. Wanamuona Mwalimu akitembea, ameshika kifimbo chake, Azimio la Arusha na biblia. Lakini pia nikafikiri juu ya kifafa. Wataalamu wa ubongo wanasema kuna aina mbili za kifafa. Kuna kifafa kamili ambacho mtu hawezi kukumbuka chochote. Akipatwa na kifafa anapoteza kumbukumbu zote. Watu wenye ugonjwa wa kifafa hawakumbuki tukio la kuanguka na asilimia kubwa hawafahamu kama wanaanguka!Aina hii ya kifafa ni mbaya zaidi, maana inapunguza hata uwezo wa mtu kufikiri na utenda. Aina nyingine ya kifafa ni nusu kifafa. Wenye ugonjwa huu, ni kwamba yale yote wanayokuwa wanafikiria kabla ya kuanguka, yanakuwa matukio ya kweli kwenye akili yao. Kama walikuwa wanawaza juu ya Mwalimu Nyerere, wakianguka kifafa, wanamuona Mwalimu kweli. Na kama walikuwa wanaiwaza Amerika, wakiaanguka, wanaiona Amerika kweli. Wakizinduka kutoka kwenye kifafa, watakwambia walishafika Amerika. Huwezi kubishana nao, maana kwenye akili yao wanaona walishafika Amerika. Inaaminika kwamba watu wote wanaojitangazia kutokewa kwa aina yoyote ile, wanakuwa na ugonjwa huu wa nusu kifafa! Hoja hii ya kifafa kamili na nufu kifafa ni ndefu, inahitaji makala inayojitegemea. Kabla ya safari yetu ya Kanyezi, mimi na vijana wangu tulikuwa na mjadala mkali juu ya kufa na kufufuka. Hoja kubwa ikiwa je Yesu alifufuka na mwili wake, au matendo yake kama vile kumegeana mkate ndio ufufuko wake? Tunaambiwa wafuasi wa Yesu waliwatambua kwa kumegeana mkate. Kama matendo ndiyo yanayofufuka, ina maana Tanzania nzima hakuna mtu anayetenda matendo ya Mwalimu Nyerere? Hakuna viongozi waadilifu kama Mwalimu? Hakuna watanzania wazalendo wenye kupenda haki na kuitetea kama alivyofanya Mwalimu? Mbona hatujasikia mtu akitangaza kufufuka kwa Mwalimu? Tulisikia mchakato wa kumtangaza Mwalimu Nyerere Mtakatifu, lakini nayo imefifia! Lakini pia tulikuwa tumeshuhudia kwenye TV mambo yanayotukia sasa hivi katika taifa letu, kama hoja ya Mheshimiwa Kabwe Zitto, ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu; Mawaziri kushindwa kuwajibika pamoja na ukweli ulioonyeshwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwamba fedha nyingi za serikali zimepotea na inawezekana ziko kwenye mifuko ya watu binafsi. Pia tuliona marudio ya Mjadala wa Kigoda cha Mwalimu, wasomi wakimbana Rais Mstaafu Benjamin Mkapa juu ya sera zake za Ubinafshaji. Haya yote yaliwasukuma vijana kujisema kila wakati “ Mwalimu angerudi leo angesema nini”? Hivyo walipoanza kuimba kwa shangwe na kusema wanamuona Mwalimu Nyerere, akitembea kwenye kijiji cha Kanyezi, nilifikiri wote wameshambuliwa na ugonjwa wa nusu kifafa, hivyo yale yote tuliyoyajadili na kuyashuhudia Sumbawanga mjini, yanakuwa ni matukio ya kweli? Kwa vile walikuwa wakijisemea “Angerudi Mwalimu..” Sasa baada ya kifafa, wanamuona Mwalimu? Wakati niko katika hali ya kuchanganyikiwa, niliisikia sauti ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere “ Karugendo, Karugendo, Karugendo, una imani haba..”. Nilitetemeka mwili mzima. Nilisimamisha gari na kutoka nje. Watu wa kijiji cha Kanyezi walikuwa wamejiunga na vijana wangu kwa kuimba wimbo wa “Tanzania, Tanzania, nakupenda kwa moyo wote…”. Sauti ya Mwalimu Nyerere ikarudi tena “ Karugendo, umeviona vijiji vya Itekesha,Mwazye, Kifone, Katazi, Ninga, Sandulula,Songambele, Malolwa na Kalole?” Kwa kutetemeka, nikajibu “Ndiyo Baba wa Taifa”. Sauti ya Mwalimu ikarudi tena “ Unafikiri mpangilio wa vijiji hivyo ulifanywa na Mwinyi, Mkapa au Kikwete?”. Nikawa bubu! Nikafumba macho! Nikabaki kusikia sauti za vijana wangu na wanakijiji wa Kanyezi, wakiimba “Kama si juhudi zako Nyerere…” Ilipita nusu saa nikiwa nimefumba macho na huku nikitetemeka. Nilipofumbua macho Mwalimu Nyerere, alikuwa amesimama mbele yangu! Ameshika kifimbo chake, Azimio la Arusha na biblia mkononi! Nikafikiri na mimi nimeanguka nusu kifafa? Mwalimu, akacheka sana! Akaniambia “Karugendo, uone ukweli mbele ya macho yako”. Nilipotaka kumkumbatia, Mwalimu, alitoweka! Mbele yangu nilikiona kijiji cha Kanyezi, mpangilio mzuri wa kijiji kile, mashamba makubwa ya mahindi, alizeti na mazao mengine. Nikaingia ndani ya gari na kuendelea na safari. Kila tulipopita vijana walishangilia na kusisitiza kwamba wanamuona Mwalimu Nyerere, akitembea kwenye vijiji vya Sumbawanga. Tukaviona vijiji vya Matai, Kasungamile, Mtowisa, Zimba, na Mkamba. Ni mpagilio wa vijiji vya ujamaa. Tuliambiwa mfumo wa vijiji vya ujamaa ulishindikana. Tuliambiwa Mwalimu, alikuwa na ndoto zisizowezekana za kuwakusanya watu sehemu mmoja. Tukashangaa kuona mfumo wa vijiji vya Sumbawanga ni tofauti kabisa na mfumo wa vijiji vingine vya Tanzania. Kila baada ya kilomita kuanzia nane hadi kumi na tano, unakutana na kijiji; ni aina ya miji midogo midogo; watu wanakaa pamoja kwenye sehemu mmoja, wanatoka pale wanakwenda kwenye mashamba na kurudi kwenye “Centre” zao. Mfumo huu, kama alivyokuwa amewaza mwalimu Nyerere, ni rahisi kuwasambazia watu huduma, ni rahisi kuwasiliana na watu wa kijiji kwa muda mfupi, ni rahisi watu kushirikiana na kusaidiana, na riahisi kujenga shule ya kijiji na watoto wasitembee mwendo mrefu, ni rahisi kujenga zahanati ya kijiji na kuwapunguzia mama wajawazito safari ndefu za kuifuata zahanati. Kama serikali inashidwa kuwasambazia huduma watu hawa wanaoishi kwenye vijiji hivi vya ujamaa,ni tatizo la Mwalimu? Tumeambiwa zahanati hazina dawa, wakati kwenye vyombo vya habari tunasikia dawa zilizopitwa na wakati zinateketezwa kule Dar-es-salaam. Serikali inashindwa vipi kusambaza dawa kwa watu wanaoishi kwenye “Centers?” hizi za vijiji vya Sumbawanga. Kama serikali inashindwa kuwasambazi watu hawa maji ni tatizo la Mwalimu? Tulipofika kijiji cha Malolwa, tuliwakuta wananchi wakitengeneza barabara yao. Mwenyekiti wa kijiji alitueleza “ Tumeamua kuitengeneza wenyewe, maana tumesikia fedha zilizotengwa kwa matengenezo ya barabara zimetafunwa na mchwa kwenye Halmashauri ya wilaya” Kilichotushangaza zaidi, na ndiyo maana tumeamua kutangaza Ufufuko wa Mwalimu Nyerere kwa nguvu zetu zote, ni kwamba hatujasikia popote pale, hatujasoma kwenye magazeti wala kwenye radio juu ya mafanikio ya vijiji vya ujamaa vya Sumbawanga. Mbona hatujasikia viongozi wakitolea mfano mafanikio ya Mwalimu ya kufanikiwa kuwakusanya watu sehemu mmoja, ili iwe rahisi kuwasambazia huduma? Hata Mheshimiwa Mzindakaya, anayetoka Sumbawanga, ambaye kwa miaka ya nyumba alikuwa mtoa hoja mzuri sana Bungeni na nje ya Bunge, hajasikika akielezea mafanikio haya ya Sumbawanga ya vijiji vya ujamaa. Inashangaza hakuna anayesema juu ya hili. Hata waandishi wa habari wamekaa kimya. Ni mpaka mtu kusafiri hadi Sumbawanga, kujionea maajabu haya? Tumeambiwa mkoa mzima wa Rukwa na ule mpya wa Katavi, mpangilio wa vijiji ni ule ule! Mbona hatujamsikia mtoto wa Mkulima, Mheshimiwa waziri Mkuu Mizengo Pinda, akijivuna juu ya mafanikio haya ya vijiji vya Ujamaa. Tukaelezwa ukweli huu kwamba hata kama Mwalimu alishindwa mikoa mingine kuunda vijiji vya ujamaa alifanikiwa Rukwa na Katavi na ni mfano wa kuigwa? Kwa nini tunashindwa kutangaza mafanikio yetu wenyewe? Nyumba za vijiji hivi zote zimejengwa ka matofari ya kuchomwa. Hata ambaye hakufanikiwa kuezeka kwa mabati, kuta za nyumba ni za matofari ya kuchomwa. Huo ni uamuzi wa wananchi wenyewe, mtu akijenga kwa matofari mabichi, nyumba yake inavunjwa! Wanapanga pamoja na kusikilizana kwa vile wanaishi karibu. Hatukusikia malalamiko juu ya vijiji hivi, isipokuwa kwamba vijiji hivi vimeleta “Utandawazi”. Kabla ya vijiji wakati watu wakiishi mbali mbali, waliweza kutunza mila zao, sasa hivi kuna mwingiliano wa makabila; watu kutoka mikoa mingine na nchi za jirani. Kuna watu kutoka DRC, Malawi na Zambia, ukiachia mbali wakimbizi wa Burundi na Rwanda. Pamoja na utandawazi huu, watu wanaishi kwa amani. Hatukusikia msamiati wa “Wahamiaji haramu”. Baada ya kazi za siku, wananchi wanajikusanya sehemu mmoja, kwa makundi. Vijana peke yao, wanawake peke yao na wanaume peke yao. Kwenye makundi hayo wanachangishana fedha ya kununua pombe. Wanaweka pombe kwenye chombo kimoja na kunywa kwa kupokezana. Mzee mmoja alitwambiwa: “ Mwalimu Nyerere, alitufundisha kuishi pamoja, kushirikiana katika shida na raha…. tunakunywa pamoja na kufurahi. Eti huko kwenu Dar-es-salaam, mnasema Mwalimu alikufa? Sisi hapa bado yuko hai na hakuna anayeweza kututoa kwenye misingi yake”. Na kweli ukiviona vijiji vya ujamaa vya Sumbawanga, ni vigumu kuamini kifo cha Mwalimu. Aliona mbali, aliona ukweli wa Watanzania wengi kuishi vijijini. Mfumo bora wa makazi ya vijijini, unaweza kusukuma maendeleo ya haraka katika taifa letu. Tusione aibu kutangaza mafanikio yetu wenyewe! Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment