MAUAJI YA KIMBALI YA RWANDA, NANI WA KUJIFUNZA?

Naandika makala hii kulaani mauaji ya kimbali yaliyotokea Rwanda 1994. Yalikuwa ni mauaji ya kinyama yaliyolenga kuwafuta Watutsi katika uso wa dunia ni “Lazima” yalaaniwe na kila mwanadamu mpenda amani. Ingawa mauaji haya yalipotokea nilikuwa ninaishi Karagwe, jirani kabisa na nchi ya Rwanda; nilishuhudia maiti waliokuwa wakielea kwenye mto Kagera, niliwapokea wakimbizi na kuishi nao, niliyasikiliza yote waliyokuwa wakisimulia wakimbizi hao, nimesoma maandishi mengi na kuangalia filamu juu ya mauaji ya Rwanda; nilikuwa sijapata picha kamili ya mauaji hayo mpaka juzi tarehe 17.10.2011 nilipotembelea makumbusho ya mauaji ya kimbali.

Makala mbili zilizotangulia, nilielezea safari ya Kigali na sherehe za Kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere. Nilielezea maendeleo ya kasi nchini Rwanda chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Paul Kagame. Wanyarwanda wakikuonyesha maendeleo yao; nyumba za kisasa, usafi wa jiji lao la Kigali na miji mingine, huduma ya maji, shule, hospitali na kukuhakikishia kwamba sasa nchi ina amani na utulivu, watahitimisha ziara kwa kupeleka kwenye makumbusho ya mauaji ya kimbali. Hawawezi kusahau tukio hilo, imebaki kuwa kumbukumbu isiofutika. Wanasamehe yaliyotokea, lakini kamwe hawawezi kusahau. Hivyo nahitimisha makala zangu juu ya safari ya Rwanda, kwa kuandika juu ya Makumbusho ya mauaji ya kimbali. Swali langu kubwa likiwa: Mauaji ya Kimbali Rwanda, nani wa kujifunza.

Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Balozi Dkt. Matiko, alitwambia “ Mwezi wa nne, kila mwaka ni juma zima la kukumbuka ya mauaji ya kimbali. Kila kitu hapa kinakufa ganzi. Hakuna shughuli zinazoendelea. Taifa linakuwa kwenye majonzi makubwa ya kukumbuka ndugu zao waliopoteza maisha yao wakati wa mauaji ya kimbali”.

Rwanda ina vituo vingi vya Makumbusho ya mauaji ya kimbali, sisi tulitembelea vituo viwili, kituo cha Nyamata na Ntarama. Vituo hivi viko kwenye eneo la Bugesera, ambako kulikuwa na Watutsi wengi. Historia ni kwamba baada ya ile vita ya 1959, watawala wa Kihutu waliamua Watutsi wapelekwe Bugesera ili wafe kwa kushambuliwa na mbungo. Walikufa wachache wakati ule, maana walipata mbinu za kupambana na mbungo mpaka mauaji ya kimbali yalipowakuta.

Nyamata, ilikuwa ni parokia ya Kanisa katoliki na Ntarama kilikuwa ni kigango cha parokia ya Nyamata. Ndani ya kanisa la Nyamata, waliuawa watu elfu kumi (10000) na miili ya watu hawa imetunzwa kwenye kanisa hili. Kigango cha Ntarama waliuawa watu elfu tano (5000) na miili ya watu hawa na vitu vyao kama vile nguo, viatu, magodoro, vifaa vya maji bado vinatunzwa kwenye kanisa hili dogo.

Vifaa vilivyotumika kwa mauaji, kama mapanga, nyundo na vijiti walivyokuwa wakiwaingizia wanawake sehemu za siri hadi vinatokea mdomoni, bado vimetunzwa. Damu zilizotapakaa kwenye makanisa hayo bado zinaonekana na hasa sehemu ambapo watoto wadogo walikuwa wakibamizwa hadi vichwa vinapasuka, damu iliyokauka inaonekana kwenye ukuta na kuashiria kwamba watoto wengi walikufa kwa kubamizwa kwenye ukuta.

Makanisa haya mawili hayatumiki tena kwa ibada. Yamebaki kama vituo vya makumbusho ya mauaji ya kimbali. Wamejitahidi kuacha kila kitu kilivyokuwa mwaka 1994, ingawa kwenye kanisa la Nyamata, wamejenga kaburi kubwa chini ya kanisa, kutunzia mabaki ya miili ya wahanga wa mauaji ya kimbali. Pia nje ya kanisa la Nyamata, wamejenga kaburi kubwa ambalo mtu unaweza kuingia na kushuhudia mwenyewe mabaki ya miili ya wahanga wa mauaji ya kimbali.

Mwili wa Mwanamke, aliyebakwa na wanaume 20, na baadaye kuteswa ahadi kufa kwa kuwekewa kijiti sehemu za siri na kutokea mdomoni umetunzwa kwenye kanisa la Nyamata. Mauaji na mateso ya kutisha yalitokea kanisani na kuna ushahidi kwamba watu wengi waliuawa juu ya Altare, meza ambayo kila Jumapili padri wao alikuwa akisimama na kugeuza mkate kuwa mwili wa Bwana, na divai kuwa damu ya Yesu; watu wote wa Nyamata, waliouawa na walioua walikuwa kila Jumapili wakikutana kwenye kanisa hilo kusali pamoja.

Watu walikimbilia kanisa kupata ulinzi. Miaka ya nyuma makanisa ndo yalikuwa kimbilio. Waliamini hakuna baya linaweza kutokea kanisani. Wauaji walitumia mbinu hiyo kuwahadaa Watutsi kukimbilia kanisani, ili wapate njia nzuri ya kutekeleza mauaji yao. Baada ya kuhakikisha idadi kubwa imeingia kanisani, walitoa taarifa kwa jeshi. Hivyo kwa kiasi kikubwa mauaji ya Nyamata na Ntarama, yalifanywa na Jeshi. Mabaki ya risasi na mabomu kwenye kanisa la Nyamata, matundu ya risasi kwenye kuta, milango na paa la kanisa hilo ni ushahidi wa kutosha kwamba mauaji hayo hayakutekelezwa kwa mapanga na nyundo tu bali hata kwa risasi na mabomu.

Risasi hazikuangalia Mwili ya Kristu, maana kwenye kanisa hilo la Nyamata, kisanduku(Tabenakulo) kinachotumika kuhifadhi mwili wa Kristu, kilicharazwa risasi, na ni wazi hostia (Mwili wa Kristu) zilimwagika chini. Bwana Yesu, akawaacha watu wake kuchinjana mbele yake! Sanamu ya Bikira Maria, mama wa shauri jema, mama wa huruma na upendo, kwenye kanisa hilo nayo ilicharazwa risasi! Sanamu hiyo bado ipo hapo kanisani na “majeraha” yake! Hapana shaka kwamba ukatili wa kutisha ulifanywa kwenye kanisa hilo.

Binti anayewapokea wageni na kuwaelezea yaliyotokea hapo Nyamata, alikuwa na umri wa miaka 8 mauaji yalipotokea. Ana kumbukumbu ya mauaji hayo yaliyotekelezwa ndani ya siku mbili tu. Baada ya kututembeza, kutuonyesha masalia ya miili na kutuelezea kwa kirefu yaliyotokea Nyamata, alituuliza swali gumu ambalo hatukupata jibu lake: “ Baada ya kutembelea makumbusho haya, mna ushauri gani? Je ni vizuri kuendelea kuonyesha masalia ya miili ya wahanga wa Mauaji ya kimbali, au tuizike na kufunika kabisa na kuisahau historia hii ya uchungu? Mnatushauri nini ndugu zetu kutoka Tanzania?”

Hakuna jibu lililotoka. Tulitizamana sote na kasha kimya kilitawala. Ni wazi kila mtu alikuwa na jibu lake. Tulipokuwa kwenye gari tukirudi hotelini tulikofikia, mjadala ulianza: wengine walisema “ Ni bora kuifunika miili na kuacha kuonyesha, maana kuionyesha kunaweza kuchochea hasira” wengine na hasa wakereketwa wa “amani” walisema “ isifunikwe ili watu waone na kujifunza kutochezea amani”. Ni imani yangu hata wewe msomaji wa makala hii utakuwa na maoni yako kuhusu jambo hili. Unaweza kutoa maoni yako, Wanyarwanda ni wasikifu, watasikia.

Tulikuwa kama watanzania ishirini na tano tuliotembelea makumbusho haya ya Nyamata na Ntarama. Kila mtu alikuwa na la kwake moyoni. Kilichokuwa wazi ni kwamba simanzi, hofu na huzuni vilimgusa kila mmoja wetu. Kila mmoja wetu alionyesha kuchukizwa na unyama uliotendeka kanisani. Mimi binafsi nilikuwa na maswali mengi kichwani mwangu: Kwa nini mauaji haya yalitokea kanisani? Je, leo hii Kanisa Katoliki la Rwanda lina mbinu gani za kutibu majeraha haya na kama kanisa lina msimamo gani juu ya makumbusho ya mauaji ya kimbali ambayo yako kwenye makanisa yao? Wana nguvu za kuweza kusimama na kuhubiri? Je kwa nini roho ya mtu igeuke na kuwa kama ya mnyama? Haingii akilini kwamba vitendo vya Nyamata na Ntarama vilitendwa na binadamu. Kwa nini watu walifikia hatua hiyo? Ni propaganda za kisiasa? Ni siasa mbaya? Ni uongozi na utawala mbovu ni nini?

Tulielezwa kwamba kwenye makanisa mengine yalikotokea mauaji, hata mapadri walishiriki mauaji. Waliwatenga Wanyarwanda kwenye makundi ya Wahutu na Watutsi, na kuwaruhusu wanajeshi kuwaua Watutsi. Baadhi ya mapadri hawa bado wanaishi na kuhubiri neno la Mungu Rwanda. Na la kushangaza ni kwamba makanisa yanajaa waumini, nilipouliza, niliambiwa “ Wanyarwanda wanapenda sana dini”

Wakati mimi nikitafakari ya kwangu na wenzangu walikuwa wakitafakari pia. Huwezi kutembelea Nyamata au vituo vingine vya mauaji ya kimbali ukatoka bila tafakuri nzito. Wenzetu wengine ilibidi wameze vidonge vya kuteremsha shinikizo la damu na wengine niliona wakimeza panadol kutuliza maumivu ya kichwa baada ya kushuhudia unyama unaoweza kutendwa na binadamu. Baadhi ya wenzetu walisikika wakisema kwa masikitiko “ Watanzania wenzetu wasiopenda amani, waje hapa Nyamata na Ntarama wajifunze”.

Swali langu kwao likawa “ Ni watanzania gani wasiopenda amani”. Jibu likawa “ Wale wanaopenda maandamano”.

Nafikiri tusijidanganye. Mauaji ya kimbali ya Rwanda, ni fundisho letu sote. Ni fundisho kwa chama tawala cha CCM na ni fundisho kwa wapinzani pia. Ni lazima kutambua kwamba binadamu ni binadamu, awe CCM au upinzani anabaki kuwa yule yule; mwenye tamaa, mwenye wivu, mwenye kiburi, mwenye ubaguzi, mwenye mashindano, mwenye kutaka madaraka, mwenye kutaka kuwanyanyasa wengine, mwenye kutaka kuwa bora zaidi ya wengine. Hivyo mwanadamu ni lazima aongozwe na vitu kama sheria, katiba, kanuni, utamaduni, mila na desturi. Na haya ni lazima kuyajenga pamoja kama taifa na kila mtu lazima awe na mchango wake na ni lazima kila mtu kuyafuata na kuyaheshimu. Nchi si mali ya mtu au kikundi chochote cha kisiasa. Ni imani yangu kwamba hakuna mtu asiyependa Amani. Sote tunapenda amani, ndo maana ninasema ni jambo muhimu sote kujifunza matokeo ya uvunjifu wa amani kutoka Rwanda.

Matukio ya Igunga, ya wanasiasa kupanda jukwaani na bastola, si kupenda amani! Kununua shahada za watu ili  wasipige kura si kupenda amani, maana watu hawa wakitaka kupiga kura kwa nguvu, amani itapotea. Serikali kuingiza nchi kwenye mikataba mibovu, si kupenda amani, maana kuna siku wananchi watasimama na kuikataa mikataba hii, na hili likitokea hakuna amani. Kupora ardhi kwa visingizio vya uwekezaji si kupenda amani, maana wananchi wakisimama kudai ardhi yao amani itapotea.

Tusipokuwa na chakula cha kutosha, amani itapotea! Mtu mwenye njaa hawezi kuwa na amani. Bidhaa muhimu zinapanda bei usiku na mchana; mafuta ya taa yanapanda bei, sukari inapanda bei na vyakula sasa vinapanda bei. Hatuwezi kuwa na amani , kama wananchi watakuwa hawana bidhaa muhimu katika maisha yao ya kila siku. Amani itavunjika pole pole na hatimaye inaweza kufikia kilele kama kile cha Nyamata.

Tusiwatupie lawama  wale wanaopenda maandamano. Tujiangalie kama taifa tunaelekea wapi? Tunajenga taifa la kuvunja amani siku za mbele au tunaweka misingi imara ya kulinda amani na utulivu? Tumeanza kujenga matabaka ya walionacho na wasiokuwa nacho, ufa unakuwa mkubwa kila kukicha. Tunajenga sekondari za kata na kuacha watoto wa vigogo kusoma shule nzuri na nje ya nchi. Je watoto hawa kesho na keshokutwa watapikika chungu kimoja? Hatuna mpango mzuri wa kuwaingiza kwenye jamii watoto wa mitaani. Tunawaacha wanakulia mitaani, wanaoa na kuolewa na kutengeneza familia wakiwa mitaani. Siku ya siku hawa watakuwa salama yetu?

Tusipoziba ufa tutajenga ukuta! Tusikwepe wajibu wetu, kujenga amani ni kazi yetu sote. Kama kuna la kujifunza juu ya kuilinda amani ni lazima tujifunze wote. Kwa maana hiyo mauaji ya kimbali ya Rwanda ni fundisho kwa watanzania wote.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

+255 754 6331 22.

0 comments:

Post a Comment