TUTAFAKARI JUU YA YESU KRISTU NA UKRISTU


Nianze makala hii kwa kuwatakia wasomaji wangu heri ya Christmas na mwaka mpya wenye baraka tele. Ni miaka miwili sasa nimeachana na utamaduni wa kutumiana salaam za Christmas na mwaka mpya kwa ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani; msimamo wangu ni kukwepa kuyatajirisha makampuni haya ya simu wakati wa sikukuu hizi za mwisho wa mwaka. Wale wote watakao ni tumia ujumbe wa sms, nitaupokea lakini sitaujibu, badala yake najibu kupitia makala hii: Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturuhusu kuendelea kuwepo; si kwa ubora wetu bali kwa neema zake. Hivyo basi kwa vile tumejaliwa bure bila hata kustahili, tuelekeze nguvu zetu zote katika upendo, amani na kuwahudumia jirani zetu.

Nitakayoyaandika leo, inawezekana nilikwisha yaandika miaka iliyopitia. Nitakuwa ninayarudia kama ilivyo kawaida yetu ya kurudia mambo yale yale kila mwaka. Mfano tukio hili la Christmas tunalirudia kila mwaka na bila kuwa waangalifu tunaweza kujikuta tunatumbukia kwenye mnyororo wa kufuata ratiba bila kuwa na tafakuri. Hatari ya kujenga utamaduni huu ni siku moja kujikuta hatuna majibu ya maswali mengi yanayoweza kujitokeza kutokana na matukio haya tunayoyarudia kila mwaka. Hivyo katika makala hii kama nitakuwa nimejirudia, si kwa bahati mbaya bali ni kutaka kujenga utamaduni wa kuyatafakari matukio haya ambayo yamegeuka kuwa ni sehemu ya maisha yetu.

Tunatumiana salaam wakati wa sikukuu hii ya Christmas, tunatumiana zawadi, tunakula pamoja na kunywa pamoja, tunafurahi, tunavaa nguo nzuri na wengine tunasafiri kwenda kupumzika au kuwatembelea ndugu na jamaa; lakini je, tunatafakari tukio hili la Mungu, kuzaliwa miongoni mwetu, akaishi na sisi? Tuna tafakari juu ya misamiati tunayoitumia kila siku ya Yesu Kristu na Ukristu? Je ni kweli kwamba kuna Yesu wa Nazareti na Yesu Mkristu? Basi nakukaribisha katika makala hii tutafakari pamoja kwa lengo la kuvunja utamaduni huu wa kuyachukulia matukio haya kama ratiba, bali matuko ya kuyajenga na kuyaendeleza maisha yetu hapa duniani.

 Yesu wa Nazareti au Yesu Mkristu? Lengo la tafakuri  hii si la kiimani wala kihistoria. Kila mtu anakaribishwa kutafakari pamoja na mimi. Kila mtu anakaribishwa kutafakari juu ya mtu huyu Yesu Kristo aliyeishi karne ya kwanza kule Palestina, na kujaribu kumwangalia kwa macho ya karne ya leo katika mazingira ya Mtanzania. Shauku yangu kubwa ni kumwangalia mtu huyu kabla ya kutekwa nyara na kutumiwa kama chombo na imani ya Kikristu.

Tafakuri yetu haitaanza na imani katika Kristo, ingawa nafikiri hitimisho litakuwa hilo. Wala tafakuri yangu haina lengo la kuutetea Ukristu, hii ni dini kongwe ambayo inaweza kujitetea yenyewe. Pia sina lengo la kumtetea na kumlinda Kristo, maana yeye ana uwezo wa kujitetea mwenyewe. Hata hivyo tunaambiwa na wanafalsafa wa zamani kwamba ukweli hujisimamia wenyewe. Yesu, alipobanwa juu ya Ukweli ni nini, alikaa kimya ikimaanisha kwamba ukweli ni yeye mwenyewe! Lakini ikitokea baada ya tafakuri yetu mtu akaamua kumfuata Kristo, nitakuwa sikumshawishi, bali atakuwa amegundua  mwenyewe kwamba Kristo ni njia ya wokovu. Maana tunasikia katika Injili ya Yohana kwamba Ukweli utatuweka huru: Yohana 8:32.

Katika tafakuri yetu tutajikita zaidi juu ya Yesu wa Kihistoria. Lakini pia lengo letu kubwa si huyu Yesu wa Kihistoria. Hatutafakari kutuliza kiu ya tafiti nyingi za kisomi zilizofanyika juu ya Yesu Kristo. Lengo kubwa la tafakuri hii ni hitaji muhimu na la haraka. Ni hitaji la kutafuta mfumo wa kupambana na matatizo yanayomzunguka mwanadamu wa leo. Mamilioni ya watu wanaishi kwenye mateso kila siku ya Mungu. Kuna njaa, vita, umasikini, upweke, magonjwa, uonevu, ubaguzi nk. Hapa Tanzania, watu wanakufa kwa UKIMWI, malaria na magonjwa mengine yanayotibika. Ujambazi, ufisadi, rushwa na kutowajibika vinasambaratisha uchumi wetu. Namba ya wajane na wagane inaongeza kwa kasi, watoto yatima, watoto wa mitaani na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi inaongezeka kwa kasi ya kutisha. Lengo na tafakuri hii ni  tufanye nini kuondokana na mateso na mambo mengine yanayotishia uhai wa mwanadamu na hasa Mtanzania.

Mamilioni ya watu kwa miaka mingi wamekuwa wakilitaja jina la Yesu na kumwabudu, lakini wachache kati ya mamilioni ndiyo waliomwelewa Kristo na namba chache kabisa ndiyo waliofuasa kile alichokitaka kitendeke. Maneno ya Yesu Kristo, yamebadilishwa na kupindishwa ili yatekeleze kile watu wanachokitaka, na wakati mwingine maneno yake yamebadilishwa na kupindishwa yasimaanishe kitu chochote! Jina la Yesu, limetumiwa kubariki maovu ya kila aina, kama wale waliokuwa wakiongoza vita na kuuwa watu huku wakitanguliza msalaba na Biblia. Latini Amerika, mamilioni ya watu walipoteza maisha yao na sehemu nyingine kizazi kilifutika kabisa katika harakati za kueneza neno na mafundisho ya Yesu Kristo. Lakini pia jina la Yesu, limetumiwa kuwashawishi na kuwaletea imani kubwa wanaume na wanawake wengi hata kufikia hatua ya kupumbazika na kufanya matendo ya kijinga, kama kujinyima chakula na kuitesa miili yao kufikia kiwango cha uwendawazimu. Yesu amekuwa akitukuzwa na kuabudiwa kwa yale ambayo hakuyalenga, yale aliyo yapinga na kuyakemea kuliko yale aliyoyalenga, aliyoyahubiri, aliyoyatetea na kuyafia. Jambo la kushangaza ni kwamba mambo ambayo Yesu, aliyapinga wakati wa uhai wake, yalifufuliwa, yalihubiriwa na kusambazwa dunia nzima kwa jina lake.

Hatuwezi kumuunganisha moja kwa moja Yesu wa Nazareti na hii dini kubwa ya Kizungu, inayojulikana kama Ukristu. Yeye alikuwa mwanzilishi wa dini kubwa zaidi ya hii tunayoifahamu. Yeye  anasimama juu ya Ukristu na kutoa hukumu juu yale yote dini hii imeyafanya kwa jina lake. Hata hivyo Ukristu, hauwezi kudai mumiliki Yesu Kristo, maana mtu huyu alikuwa ni wa binadamu wote.

Je, hii ina maana kwamba kila binadamu (Mkristu na asiyekuwa Mkristu) ana uhuru wa kumtafsiri Kristo katika maisha yake jinsi anavyotaka? Inawezekana kabisa kila mtu akamtumia Kristo anavyotaka kwa mabaya na mazuri? Lakini yeye alikuwa ni mtu aliyekuwa na imani nzito ambayo alikuwa tayari kuifia. Je, hakuna namna ya watu, wenye imani na wasiokuwa na imani kumpatia nafasi takika maisha yao Yesu huyu wa Nazareti, akazungumza yeye mwenyewe kwenye mioyo yao? Je, hakuna namna ya watu kulinganisha matatizo yao, nyakati zao na zile za Yesu wa Nazareti?

Hivyo tafakuri yetu inaanza na matatizo mengi yanayoisumbua dunia ya leo. Tishio lililopo leo si la mtu binafsi, kabila, taifa au bara. Tishio ni la dunia nzima, ni tishio la ubinadamu. Tumefika mahali tunachanganyikiwa na kufikiri kwamba hakuna mwenye uwezo wa kuzuia tishio la kuumaliza ulimwengu na binadamu. Wapo vichaa kama Kibwetere na wajinga wengine wanaofikiri kwamba mwisho wa dunia na ubinadamu vinashuka kwa miujiza, kwamba tunaweza kulala na kuamka tunakuta dunia imekwisha. Huu ni ujinga mtupu! Mwisho wa dunia, unaletwa na matendo ya binadamu ya muda mrefu. Matendo ya ubinafsi yasiyozingatia umuhimu wa binadamu na viumbe vingine, yanaweza kupelekea mwisho wa dunia. Hili si jambo la kutokea leo ama kesho, lakini mtu anayejali ni lazima kuhakikisha anarithisha dunia hii kwa vizazi vijavyo. Tunakaa tama kwamba hakuna tena mfumo mzuri wa maisha unaowafaa binadamu wote. Mfumo wa kuweza kuangalia na kutengeneza maisha bora ya mwanadamu wa leo na kesho.


Siku za nyuma kidogo tulifikiri labda silaha za nyukilia zingeweza kutumika kuteketeza ulimwengu. Tumeanza kupunguza woga huu, lakini mambo mengine mengi kama vile uharibifu mazingira, uchimbaji ovyo wa madini, upungufu wa chakula na ardhi nzuri ya kustawisha chakula, hatari ya kupungua kwa maji na ongezeko la binadamu, ni matishio mapya kwa uhai wetu na ulimwengu tunamoishi. Ukweli kwamba binadamu wanaongeza kwa kiasi cha milioni 80 kwa mwaka, ni tishio kwamba kwa miaka michache ijayo, matumizi ya maji na chakula yatakuwa katika hali mbaya duniani kote. Ukweli kwamba magazeti, vitabu na utengenezaji wa karatasi za kuandikia unaitafuna misitu ni tishio la uharibifu wa mazingira katika enzi hizi tulizomo.

Kuna uharibifu mkubwa katika kila biashara zinazofanywa kwa lengo la kupata faida. Viwanda vingi vimekuwa vikiharibu mazingira kwa moshi unaotoka viwandani, lakini pia uchafu unaotiririshwa  kutoka viwandani kwenda mitoni na kwenye maziwa na mabahari umechangia uharibifu mkubwa wa viumbe katika maji. Ni wazi ili tupone, panahitajika mabadiliko makubwa. Swali ni je ni nani atakubali  hasara ya kusimamisha viwanda vyake?

Inakuwa ngumu kuwashawishi watu kubadili mtindo wa maisha, ili kurefusha maisha yao wenyewe, inakuwa ngumu zaidi kuwashawishi kufanya hivyo ili kuyarefusha maisha ya watu wengine. Inakuwa ngumu zaidi na zaidi kuwaambia kufanya hivyo kwa lengo la kunusuru maisha ya mabilioni ambao bado hawajazaliwa.

Kuna ukweli kwamba dunia hii ina  baadhi ya watu, wake kwa waume wenye nia njema, na wanayaona matatizo yote hayo na wangependa kufanya chochote kuleta mabadiliko. Lakini wanaweza  kufanya nini? Mtu mmoja, au kikundi cha watu wachache kinaweza kufanya nini kwenye matatizo haya ya Ulimwengu wa kisasa? Kilicho mbele yetu ni kitu kikubwa, ni mifumo ya dunia hii iliyojikita na kustawi! Ni mifumo ya ubepari, soko huria na utandawazi. Mara ngapi tunasikia kilio cha watu kwamba mtu hawezi kupambana na  mifumo?

Hili ndilo tatizo kubwa. Tumejijengea mifumo ya siasa na kiuchumi kwa kuzingatia mambo fulanifulani, ambapo sasa tunaanza kutambua kwamba mifumo hii italeta maafa kwa dunia nzima. Ni kama tumefugwa mikono na miguu, kiasi tunashindwa kubadilisha mifumo na inafika mahali hakuna kinara kwa kuisimamia na kuiendesha. Na la kushangaza ni kwamba uharibifu wa mifumo hii, hautambagua mtu yeyote. Mfano uharibifu wa mazingira unaoendelea kuongeza joto duniani, hautabagua matajiri na maskini, mataifa makubwa na madogo. Utatuangamiza sote!

Tunaposherehekea sikukuu ya Christmas, ni lazima kutafakari na kujiuliza maswali: Tunamkumbuka Yesu wa Nazareti au Yesu Mkristu. Kama tulivyoona kwenye tafakuri yetu ni kwamba Yesu wa Nazareti, alijenga mifumo ya kupambana na matatizo ya dunia ya wakati wake, matatizo yanayofanana na matatizo ya dunia ya leo. Baadaye Ukristu ulijenga mfumo unaopingana na ule wa Yesu wa Nazareti! Hapa ndipo mjadala unakuja; tunataka tusitake ni lazima tuyajadili haya maana yanagusa maisha yetu. Tuendelee kutafakari wakati tunakula na kunywa!

Na,
Padri Privatus Karugendo.


0 comments:

Post a Comment