UTETEZI WA JINSIA NA UKOMBOZI WA WANAWAKE KIMAPINDUZI NDANI YA MIAKA HAMSINI YA UHURU WETU.


TGNP,FEMACT  na mashirika mengine yanayoshughulika na utetezi wa jinsia na ukombozi wa mwanamke kimapinduzi wanatukaribisha kutafakari pamoja juu ya mchango wao na changamoto walizokumbana nazo ndani ya miaka hamsini ya uhuru wetu. Mashirika mengi ya kutetea Jinsia na ukombozi wa mwanamke kimapinduzi yameanzishwa baada ya Beijing. Hivyo yaliyo mengi yanatekeleza maamuzi ya mkutano huo wa Beijing. Kwa namna moja ama nyingine tunapozunguzia mchango wa mashirika haya ni kutaka kujua mafanikio na changamoto ya kutekeleza maazimio ya Beijing. Kwa upande mmoja mawazo haya ni sahihi kabisa, lakini kwa upande wa historia ya Tanzania, harakati za kijinsia na ukombozi wa mwanamke zinakwenda nyuma hadi kwenye kupigania uhuru wetu.

Tulipigana kwa pamoja kumwondoa mkoloni na kushindwa kufuta kabisa vikaragosi vya ukoloni. Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanajaribu kupambana na vikaragosi vya ukoloni. Mfumo wa Soko huria na nguvu za kutisha za ubeberu vinatufanya kuwa na “Uhuru” wa bendera. Serikali yetu inaelekea kuwa tegemezi mno kwa wale wale waliotutawala, wakiwemo Wajerumani, Waingereza, Wamarekani, Japani na nchi nyingine za “Kundi la nchi nane”. Hivyo serikali yetu inajikuta haina uhuru wa kuamua mambo yake yenyewe, kwa mfano uwezo wetu wa kufanya maamuzi kuhusu mambo ya msingi ya jinsi ya kugawa rasilimali zetu ni mdogo na umefifishwa na hali yetu ya utegemezi.

Mfano mwingine unahusu mapambano yetu kuhusu umilikaji wa ardhi, jambo ambalo ni kati ya yale yaliyowasukuma Watanganyika kusimama kupigania uhuru wao. Muda mfupi baada ya uhuru, Serikali ilipitisha sera ya ardhi ambayo ilitambua umiliki wa ardhi kuwa wa jamii na kuwazuia wageni wasimiliki ardhi. Sera hii ya ardhi imekuwa ikipigwa vita na wawekezaji na watanzania wenye uroho tangu miaka ya 1980, na hatua kwa hatua, Serikali imekuwa ikiruhusu matumizi ya ardhi kwa wageni katika sekta  za kilimo, utalii, uchimbaji wa madini na mabenki yanayowekeza hapa nchi. Hivyo basi, suala la ardhi limeanza kuibuka upya na wanaharakati pamoja na jamii katika sehemu mbali mbali wameanza kujipanga upya ili kulipinga.

Utafiti uliofanywa na Susan Geiger, juu ya Wanawake wa TANU, unaonyesha wazi kabisa kwamba wakati wa kupigania uhuru, wanawake walipambana bega kwa bega na wanaume. Kitabu hiki kilichotafsiriwa na TGNP katika lugha ya Kiswahili kinafichua ukweli kwamba wakati wa kupigania Uhuru, wanawake walikuwa mstari wa mbele; walitembea nchi nzima wakihamasisha watu kujiunga na TANU, walichangisha fedha za kuendesha chama na harakati nyingine za kupigania uhuru, walifanya kazi mbali mbali za kupata kipato ili waweze kupata fedha za kuendesha chama. Hivyo tunapoangalia utetezi wa jinsia na ukombozi wa Mwanamke kimapinduzi ni lazima tuangalie mbele zaidi  ya kabla ya Beijing.

Kitabu cha Susan Geiger, kinatupatia majina mengi ya wanawake waliopigania uhuru. Majina haya hayasikiki tena. Yamezikwa na kufunikwa na mfumo dume. Ingawa jina la Bibi Titi Mohamed linasikika kwa mbali, majina  ya wanawake wengine alioshirikiana nao Dar-es-Salaam, hayasikiki kabisa. Hata mikoani kulikuwa na wanawake walioshiriki harakati za ukombozi wa taifa letu. Kule
Kilimanjaro kulikuwa na Halima Selengia Kinabo, Mwamvita Salim, Zainab Hatibu, Morio Kinabo, Violet Njiro, Elizabeth Gupta, Kanasia Tade Mtenga,Natujwa Daniel Mashamba na Lucy Lameck. Hata kule Mwanza kulikuwa na wanaharakati wanawake waliopigania uhuru wa taifa letu, lakini historia haiwakumbuki  tena. Wanawake hao ni: Agnes Sahani, Aziza Lucas, Tunu Nyembo, Halima Ntungi, Mwajuma Msafiri, Pili Juma, Mwamvua Kibonge, Zuhura Mussa  na  Chausiku Mzee.

Ni wazi wako wanawake wengine wengi walioshiriki harakati za kuleta uhuru wa taifa letu, ni kazi ya Mashirika yanayotetea usawa jinsia na ukombozi wa Mwanamke kuendelea kufanya tafiti na kuibua majina mengine ili kuweka kumbukumbu sahihi ya historia ya taifa yetu.

Kama tutakavyoona wakati wa kutafakari juu ya mchango wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayojishughulisha na masuala ya jinsia na ukombozi wa mwanamke kimapinduzi ni changamoto ya utegemezi. Mashirika mengi au tuseme yote yanategemea fedha kutoka nje ya nchi. Utafiti juu ya Wanawake wa TANU, unatufichulia “siri” kwamba wakati wa kupigania uhuru na miaka michache baada ya uhuru Wanawake wa TANU, walikuwa na uwezo wa kuendesha mambo yao bila msaada wowote kutoka nje au kutoka kwa serikali ya mkoloni. Msimamo huu wa kujitegemea uliwawezesha wanawake kuunda vyama vyao vyenye nguvu kiasi cha kuwatishia “Usalama” wanaume. Uamuzi wa serikali wa kuvivunja vyama hivi vya wanawake mara baada ya uhuru na kutengeneza chama kimoja cha UWT, ambacho kilikuwa chini ya serikali na kupata ruzuku kutoka serikalini ni ishara tosha kwamba vyama hivi vilikuwa na nguvu za kutisha.

Kwenye kitabu cha Susan Geiger, Bibi Titi Mohamed, ananukuliwa akielezea yaliyotokea “ Tarehe 2 Novemba, mwaka 1962, Mheshimiwa Nyerere aliagiza kwamba vyama vyote vya wanawake Tanganyika vivunjwe; yaani, YWCA, Baraza la Wanawake Tanganyika na UMCA, ili viungane kuunda Umoja wa Wanawake wa Tanganyika (UWT)”

Kwa maoni ya Bibi Titi Mohamed, kuvunjwa kwa vyama vya wanawake na kuanzisha chama kimoja cha UWT kilichokuwa chini ya  CHAMA na Serikali kulidhoofisha maendeleo ya kasi ya ukombozi wa wanawake na usawa wa kijinsia katika taifa letu huru. Utegemezi uliminya uhuru wa wanawake kutoa maoni na kufanya mambo yao kwa uhuru. Wanawake wengi wa TANU, hawakuwa na elimu ya juu, waliongozwa na hekima, busara, kuona mbali lakini hasa na uzalendo. Pamoja  na kutokuwa na elimu ya juu wanawake wa TANU waliona wazi tishio la kuwa  tegemezi; walilipinga wazo hilo kwa nguvu zote, lakini walizidiwa nguvu na vijana wasomi. Usomi wao haukuwasaidia kuona tishio kubwa la utegemezi. Kama anavyoelezea Bibi Titi “UWT ilitaka wizara ilipie semina na walimu waliokuwa wakitoa mafunzo kwa wanawake”. Ukaanza ugonjwa wa posho na kutegemea misaada hadi leo hii.

Bibi Titi anaendelea kuelezea makosa yaliyopelekea kudhoofisha nguvu za wanawake wa TANU; “ Wanawake wengi, vijana na wasomi waliokuwa kitovu cha uongozi UWT, waliteuliwa kutoka taasisi na wizara za serikali, kutafuta fedha, kutoa miongozo katika mafunzo na warsha za uongozi, na katika miradi ya lishe…”

Hivyo kwa njia hii ule uwezo wa wanawake wa kujitafutia fedha za kuendesha mambo yao wenyewe ikawekewa kizingiti.

Susan Geiger, katika kitabu chake anasema hivi kuhusu hali hiyo:
Sasa ni dhahiri kwamba UWT haikuwa mwendelezo wa harakati za wawawake wa TANU. Mkutano Mkuu wa Wanawake wa Afrika uliofanyika Dar-es-Salaam mwaka 1962, uliweka wazi katika rasimu ya katiba yao kwamba UWT ni ya kupigania ukombozi wa wanawake ili waweze kushiriki katika shughuli za -kijamii na za kisiasa Afrika. Lakini Nyerere na washauri wake waliamua kwamba wanawake walihitaji kuendelea na kuendelezwa, na kwamba vikundi vilivyokuwa tayari vinafanya kazi hii viungane chini ya chama kimoja kitakachoshirikisha wawawake wote na kudhibitiwa na serikali. Msomi mmoja alipatwa na mshangao kuwa mara baada ya uhuru, wanawake wamekuwa wajinga na walio nyuma kimaendeleo. Suala la namna ya kuhamasisha wanawake likawa tatizo mara baada ya uhuru. Hiyo ilikuwa kejeli”.
                  
La kustaajabisha zaidi ni mfumo dume uliodumaa wakati wa kupigania uhuru na kuibuka tu mara baada ya Uhuru. Katika kitabu cha Susan Geiger,  Bibi Titi, ananukuliwa akieleza mawazo ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii wakati ule juu ya wanawake: “ Akizungumza kwenye mkutano siku ya  pili, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Bwana Mgonja, alizungumza katika njia iliyofifisha ari ya siasa kwa wanawake na kuimarisha mamlaka ya serikali. Wakati kitengo cha Wanawake kilikuwa kinahamasisha wanawake wajiunge katika harakati za kujenga taifa, Mgonja aliwaambia wanawake kwamba wakilea watoto watakuwa wamelea taifa zima. Aliwasifu wanawake wa juhudi zao katika kupigania uhuru, lakini kwa sasa walichotakiwa kufanya ni kulima, kufuga kuku, kuchimba visima na kupanda miti pamoja na  kushiriki katika kisomo cha watu wazima. Mgonja alionya kwamba itabidi utamaduni wa Kiafrika ukuzwe, kwani wakoloni waliudharau”.

Mgonja, alikuwa akiufufua Mfumo Dume, uliokuwa umedumaa wakati wa kupigania uhuru. Kwa maoni yake kuukuza utamaduni wa Mwafrika ni kuendeleza mfumo dume. Inaelekea hapa ndipo tulipoteleza katika suala zima la usawa wa kijinsia. Anavyosimulia Bibi Titi Mohamed, katika kitabu cha Susan Geiger, ni kwamba idadi kubwa ya wanaume waliunga mkono msimamo wa Mgonja, wa wanawake kurudi jikoni baada ya kupigania uhuru. La kushangaza zaidi ni kwamba hata wanawake vijana wasomi waliunga mkono mawazo ya Mgonja, maana wanawake wa TANU waliopigania Uhuru walikuwa tishio.

Bibi Titi Mohamed anaelezea: “ Kati ya viongozi wanaume, aliyeunga mkono wazo la usawa kwa wanawake alikuwa Nyerere. Yeye alikuwa ameshuhudia wanawake. Hata tuliposema huko bungeni kwamba wanaume waadhibiwe kwa kuwapa wasichana mimba, Nyerere alisimama kidete nyuma yetu…. Kati  ya wanawake wachache bungeni (tuliopigania suala hili) tulikuwa mimi, Lucy, Barbara Johansson na mwanamke mwingine aliyekuwa ameolewa na Mgoa huko Amboni, Tanga. Wanaume walitukasirikia, Nyerere alisema ni lazima sheria hiyo ipite, ili wanaume wanaolaghai wasichana na kuwapa mimba walipe faini, wafungwe au watunze hao watoto”

Hivyo wakati wa kutafakari miaka hamsini ya Uhuru wetu, ni lazima tuchunguze kwa makini yale yaliyopelekea kufuta na kufunika historia ya ukombozi iliyoongozwa na wanawake. Kwa nini mfumo dume ulidumaa wakati wa kupigania uhuru na kuibuka mara tu baada ya Uhuru? Harakati za wanawake wa TANU zilisambaa hadi vijijini, je haraka za siku hizi zinakwenda hadi vijijini?

Kama tutakavyoona kwenye tafakuri yetu ni kwamba kati ya changamoto kubwa ya Mashirika mengi yasiyokuwa ya kiserikali ni kujikita mijini na kusahau kabisa kutandaa hadi vijijini. Wakati inaanzishwa UWT, Oscar Kambona alionya umoja huo kutandaa hadi vijijini. Bibi  Titi, anaeleza katika kitabu cha Susan Geiger:

Oscar Kambona, aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa, ndiye pekee aliyezungumza kumuhimu wa Kitengo cha wanawake, ….Alisema kuwa wanawake wanahitaji kufanya kazi kwa bidii, kwani hakuna  taifa linalodhaniwa kuendelea kama wanawake hawajaendelea. Kambona alisisitiza kwamba maendeleo ni lazima yawe ya vijijini na mijini. Viongozi wa UWT walishauriwa kurudi vijijini kuweka mipango ya shughuli na siyo kukazania sehemu za mijini tu”

Ushauri wa Oscar Kambona, haukufuatwa na UWT na hadi leo hii mashirika mengi yanayotetea usawa wa Jinsia na ukombozi wa Mwanamke kimapinduzi yamejikita mijini. Ingawa si kawaida kuanza tafakuri na hitimisho, ni vyema kuzingatia ushauri wa Oscar Kambona, wakati tunajiandaa kuanza safari nyingine ya miaka hamsini ya Uhuru wetu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122


 

0 comments:

Post a Comment