TUUNGANISHWE NA NINI? NYUMBA YA IBADA YA KIJIJI? Ningeweza kusema Nyumba ya ibada ya Kijiji, kusema kanisa, si upendeleo wa kidini, ila ni kutaka kuwa mwaminifu kwa yule niliyeongea naye. Hivyo basi pale nitakapotaja Kanisa la kijiji, wewe soma “ Nyumba ya Ibada ya Kijiji”, au “Hekalu la Kijiji” au “Msikiti wa kijiji”. Unaweza kusema chochote kinacholenga kuwaunganisha watu wa kijiji, kitu kinachojenga umoja wa Kijiji. Mwaka 2006 kwenye Jiji la Dar-es-Salaam, nilikutana na kijana kutoka Marekani. Kijana huyu aitwaye Ben Yanda, alikuwa akifanya utafiti kwenye bonde la Rukwa. Yeye ni mfugaji, na utafiti wake ulielekea upande wa ufugaji. Si lengo la makala hii kuelezea mengi tuliyoyaongea. Kusema kweli niliongea mengi na kijana huyu, mfano, alishangaa sana kukuta watu kule Rukwa, wenye uwezo wa kuuza zaidi ya Ng’ombe 50 kila mwezi, na bado watu hawa walijiita masikini. Aliushangaa utajiri mkubwa wa watanzania, wanaotembea kifua mbele wakiutangazia Ulimwengu mzima kwamba wao ni masikini. Baba yake ni mfugaji, lakini hawezi kuota hata siku moja kuwa na ng’ombe zaidi ya mia mbili, ambavyo kwenye bonde la Rukwa, kuna wafugaji wana ng’ombe zaidi ya elfu tatu! Hawa ni masikini Hawa wanahitaji kusaidiwa? Hata hivyo kwa nini wasaidiwe na wanasaidiwa na nani kwa msingi upi? Kwanini mtu wa Amerika, Ulaya au Japan na China, awe na huruma kwa mtu wa Sumbawanga? Kwani wao kule Amerika, hawana watu wa kusaidia? Kwanini watusaidie? Kama wana upendo, kwa nini wasitoe nafasi ya masomo, vijana wetu wakaenda kusona na kurudi kuendeleza taifa letu? Je, si kwamba wanatusaidia ili waweze kutunyonya vizuri? Si kwamba wanatusaidia ili watupumbaze tulale usingizi, ili watuibie vizuri? Kule nyuma walitutawala, walitununua kama samaki na kutupeleka utumwani – mapenzi ya kutusaidia yametoka wapi? Ni mtu gani anaweza kusimama na kuelezea mapenzi ya MISAADA kutoka nchi za nje? Ni nani anaweza kusimama na kuelezea mapenzi ya makampuni ya kigeni? Makampuni ya simu yanayomnyonya maskini na tajiri? Viwango vya kununua muda wa kuongea vinalingana, tajiri na masikini wanalipa sawa. Kama wanatupenda kwa nini wasitofautishe maskini na tajiri katika uwekezaji wao? Wanatupenda kutusaidia au wanatupumbaza watunyonye? Hayo tuyaache! Tuangalie Kanisa la Kijiji. Nilipokutana na huyu kijana Ben Yanda, kwa vile alionekana mcha Mungu, kwa kupenda kusali na kuongelea maadili ya kidini, nilitaka kujua yeye ni dini gani. Alikubali kwamba yeye ni Mkristu. Lakini kwangu hilo halikutosha. Nilitaka kujua ni Mkristu wa dhehebu gani na je ni padri, mchungaji, Askofu au mlei. Hapo ndio maajabu yakaanza. Yeye hakuwa na habari ya dhehebu na wala hakuwa na ile kasumba ya kuwatenga watu katika makundi ya walei na wapakwa mafuta, hakuwa na habari na cheo cha Askofu! Alijua kundi la waumini wenye kiongozi wa ibada anayejulikana kama mchungaji. Na mchungaji huyu ni kiongozi wa ibada tu na wala si kiongozi wa Kanisa, kanisa linaongozwa na waumini! Alizaliwa akalikuta kanisa la Kijiji! Kwa maneno mengine alizaliwa na kuikuta nyumba ya Ibada. Kwa maelezo yake, ni kwamba kijiji chao kina kanisa moja tu, ambalo linaitwa Kanisa la Kijiji. Ni kanisa la kila mwanakijiji. Ni kanisa ambalo si la Kikatoliki, si la Kilutheri na wala la Sabato. Ni kanisa ninalokumbatia kila mwanakijiji. Sharti la kujiunga na kanisa hilo ni kuwa Mwanakijiji! Ni kanisa ambalo halina Askofu wala uongozi wowote wa juu. Linaongozwa kwa ibada na mchungaji, anayechanguliwa na wanakijiji na kuongozwa na kamati ya kijiji! Ni tofauti na sisi tulivyozoea, unalala na kuamka kukuta tangazo kutoka kwa Baba Mtakatifu, kwamba fulani amechaguliwa kuwa Askofu wa jimbo fulani. Ushiriki unakuwa mdogo, kazi zote anaachiwa Roho Mtakatifu, anayevuma na kuleta “Nguvu” kwa wateule wachache! Ben, alisisitiza kwamba kanisa la kijiji, ni nafasi ya utakaso, ni nafasi ya kuponya na kumtuliza kila mtu, ni nafasi ya kufukuza upweke kwenye nyoyo za watu, nafasi ya kupigana na ubinafsi na kujenga moyo wa mshikamano wa kijiji kizima. Nafasi ya majadiliano na kufundishana, nafasi ya kujuliana hali na kutiana nguvu, ni nafasi ya pekee inayofundisha na kuhimiza kuchukuliana na kukumbushana kwamba wanakijiji wote ni watoto wa Mungu na ni watoto wa kijiji chao. Kanisa la kijiji ni kimbilio la kila mwanakijiji, ni maisha na moyo wa kila mwanakijiji. Ni kanisa lililoanzishwa na hitaji la wanakijiji wote – kulikuwa na hitaji ambalo hakukuwa na mtu wa kulipinga; ni hitaji linalokuwa juu ya akili ya kila mtu, juu ya madaraka ya kila mtu na juu sifa ya kila mtu: Kanisa la kijiji ni nguzo ya maisha ya kila mwanakijiji. Kijiji kinasifiwa, kinatukuzwa na kupata heshima zote ambazo hakuna mtu wa kuzibinafsisha. Kufuatana na maelezo ya Ben Yanda, ni kwamba kanisa hili la aina yake, lilianza mnamo mwaka 1828, na limeendelea hadi leo hii. Kufuatana na maelezo ya Ben, kanisa hili ambalo halina mgawanyiko wa waumini, limesaidia kwa kiasi kikubwa kujenga mshikamano na uzalendo mkubwa wa wanakijijini. Kanisa, limekuwa njia pekee ya kukutanisha watu wenye mawazo mbali mbali na kujadiliana kuhusu maendeleo ya kijiji chao. Maendeleo makubwa waliyonayo katika kijiji chao yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwa na nyumba ya ibada ya kijiji. Ninasikia makanisa kama hayo ni mengi kule Amerika na yanatoa mchango wa aina yake katika jamii yao. Kwanini nilivutiwa na Kanisa la kijiji au nyumba ya Ibada ya kijiji. Nilipokutana na Ben, mjadala ulikuwa unapamba moto kuhusu Serikali ya Kikwete, kwamba inawapendelea Waislamu. Mjadala huu bado unaendelea. Ni mjadala ambao utaendelea siku zote, maana akitawala Mkristu, Waislamu wanalalamika kwamba Mkristu anawapendelea Wakristu. Akitawala Mwislamu, Wakristu wanalalamika, kama wanavyofanya sasa hivi kwamba kwa vile Kikwete ni Mwislamu, basi anapendelea Waislamu. Tuligawanywa na wakoloni kwa ujio wa hizi dini za kigeni, na kwa vile tunafumba macho na kusinzia, tutaendelea kugawanyika hadi ujio mwingine wa wakoloni! Baada ya kusikia Kanisa la kijiji, ni kawa na wazo kwamba, labda na sisi hapa Tanzania, tunahitaji nyumba za ibada za vijiji, kata, tarafa, wilaya, mikoa hadi Taifa. Tunahitaji nyumba za ibada ambazo hazikumbatii dini yoyote ile. Kama lilivyo kanisa la kijiji kule Amerika katika kijiji cha kijana Ben Yanda, ndivyo na sisi tunahitaji nyumba ya ibada isiyokuwa ya dhehebu wala dini. Nyumba ya ibada isiyokuwa ya ukoo wala kabila, Tunahitaji nyumba ya ibada isiyokuwa na chama wala siasa. Nyumba ya Ibada ya kuwakusanya watanzania wote wa CCM, CUF, TLP, vyama vingine na wale wote wasiokuwa na vyama. Tunahitaji nafasi ya utakaso, nafasi ya kuondoa kiburi na majivuno yasiyompendeza Mungu; majivuno ya elimu, majivuno ya pesa na utajiri, majivuno ya sura nzuri nk. Tunahitaji nafasi ya kuwakusanya wasomi na wale ambao si wasomi, nafasi ya kumnyenyekesha kila mwanakijiji, kila mwana mkoa na kila Mtanzania. Kanisa la kijiji, ni chombo kizuri ambacho kinaweza kuwasaidia wanasiasa na serikali zote ziwe za demokrasia au za Kidikteta. Kama watu wamejipanga vizuri katika uzalendo wao na mapenzi yao kwa kijiji chao, kata yao, tarafa yao wilaya yao mkoa wao au taifa lao, inakuwa kazi nyepesi kuwaongoza na kuwaelekeza. Binafsi nilivutiwa na Kanisa la Kijiji au nyumba ya ibada ya kijiji. Ninatamani kuanzisha moja, wewe una maoni gani? Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment