SI UBISHI BALI NI KUELIMISHANA Baada ya kusherehekea sikukuu ya pasaka, watu wanaopenda kujadili juu ya imani hii ya Ukristu na wale wanaoipinga imani hii wanakuwa na maswali mengi ambayo mengi hayapati majibu. Kuna wanaouliza: Kama Maria alizaa watoto wengine baada ya Yesu, kwa nini aitwe bikira? Hivi Maria aliendelea kuwa bikira hata baada ya kumzaa Yesu?Mbona Biblia inasema Yesu alikuwa na ndugu zake wa kiume na wa kike? Ina maana Maria na Yosefu walijuana kimwili na kuzaa watoto wengine? Baada ya kuzaa watoto wengine, Maria anastahili kuitwa bikira? Haya ni baadhi ya maswali yaulizwayo na waamini wa madhehebu ya Kiprotestanti na hata Waislamu juu ya ubikira wa Maria na ndugu zake Yesu. Wakatoliki ndio tu huamini kwamba maria aliendelea kuwa bikira, na kwamba hakuzaa watoto wengine zaidi ya Yesu. Kabla sijatoa mchango wangu wa mawazo juu ya mada hii ningependa kuweka wazi kwanza jambo moja la msingi: Kujadiliana juu ya maswala ya kidini, na hasa hizi dini zetu mbili za kigeni: Ukristu na Uislamu si ubishi bali ni kuelimishana. Ni vigumu mtu kuamini kitu asichokijua vizuri. Mtu anayeifahamu dini yake vizuri, hawezi kuogopa kujadili kitu chochote kile kinachohusiana na imani yake. Ni imani yangu kwamba majadiliano haya hayataishia kwenye mjadala wa Ubikira wa Maria, bali yatagusia mambo mengine mengi yenye utata katika dini hizi za kigeni, mambo kama: Utatu Mtakatifu, Kufa na kufufuka, Kula na kunywa mwili na damu ya Yesu, Useja, Ndoa ya mke mmoja na ndoa ya wake wengi, ndoa za waislamu na wakristu,Kafiri na ni kwanini waislamu tu ndo wanaruhusiwa kuchinja nk. Msingi mwingine unaohitajika ili majadiliano yasiwe ubishi bali kuelimishana ni ukweli kwamba yote tunayoyajua juu ya Yesu, yamesimuliwa na kuandikwa takrban miaka 90 baada ya kuzaliwa kwa Yesu. Na kwamba simulizi zote zinaanzia kwenye ufufuko wa Yesu. Hivyo jambo muhimu si Yesu, aliyezaliwa na nani, aliyezaliwa vipi, aliyekuwa na ndugu au ambaye hakuwa na ndugu, aliyeishi kwenye nyumba gani, aliyekula chakula gani - muhimu ni Yesu, aliyekufa na kufufuka. Injili zote nne zinaandika juu ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristu, lakini si Injili zote zinazoongelea kuzaliwa kwa Kristu. Matayo na Luka waliandika juu ya tukio hili, na ni Matayo peke yake anayeingia kwa ndani kidogo. John na Marko, hawaandiki chochote juu ya kuzaliwa kwa Kristu. Baada ya ufufuko ndipo maisha ya Yesu, yanakuwa na maana. Wafuasi walianza kukumbuka mafundisho yake na matendo yake. Walianza kufundisha mafundisho ya Yesu na matendo yake. Umuhimu haukuwekwa kwa Ubikira wa mama aliyemzaa, bali mafundisho yake ya kumpenda jirani kama nafsi yako, ya kutoa uhai wako kwa wengine, ya kupenda, kuponya na kuhurumia, ya kupigwa shavu la kuume ukageuza la kushoto, ya msamalia mwema, ya mtoto mpotevu, ya kutobaguana nk. Yesu, alifundisha kusamehe saba mara sabini. Leo hii tunashuhudia vita inayoongozwa na wale wanaojiita wafuasi wa Kristu. Tunashuhudia ubaguzi wa kijinsia, kanisa na hasa kanisa katoliki linatawaliwa na wanaume tu. Tunashuhudia ubaguzi wa rangi na wa kikabila. Tunashuhudia ufa mkubwa kati ya masikini na matajiri. Tunashuhudia chuki na hasira. Hali ni mbaya kiasi hata na viongozi kama Maaskofu, badala ya kusamehe saba mara sabini wanatunza hasira zaidi ya miaka kumi rohoni mwao. Maaskofu hao hao ndo utawakuta wanatetea na kuendeleza mijadara ya ubikira wa maria. Wanapoteza muda mwingi kwa mambo yasiyokuwa ya msingi na kuacha ya msingi ya: Nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni mkanikaribisha; nilikuwa uchi nanyi mkanivika; nilikuwa mgojwa mkaja kunitazama;nilikuwa gerezani mkaja kunitembelea ( Matayo25:34-36). Matayo, anakwenda mbali zaidi na kusema hicho ndicho kitakuwa kipimo cha hukumu. Kwamba hakuna atakayeulizwa Ubikira, useja, ndoa ya mke mmoja au ndoa ya wake wengi, hakuna atakayeulizwa kama alikuwa Askofu, padri, mlei, mkristu au mwislamu. Hata Bikira Maria mwenyewe angetokea leo hii kama alivyotokea kule Ufaransa na Kibeo-Rwanda, asingesema lolote juu ya ubikira wake zaidi ya kuuimba utenzi wake: “ Moyo wangu wamtukuza Bwana, Roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu. Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mdogo, hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenifanyia makuu, jina lake ni takatifu. Huruma yake kwa watu wanaomcha Hudumu kizazi hata kizazi, Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.......” (Luk 1: 47-53). lililo hai na tusingekuwa na mabishano ya aina yoyote ile! Hata kama Yosefu na Maria, walikutana kimwili na kuendelea kuzaa watoto wengine, haipunguzi chochote kwenye heshima ya Maria kumzaa Yesu, aliyekufa na kufufuka, haipunguzi chochote kwenye mafundisho ya Yesu. Je, ubikira unaoongelewa katika biblia una maana sawa na ubikira tunaoujua sisi wa kutofanya tendo la ngono? Je, Wayahudi wana tatizo kama letu la kuona utata wa mtu kuzaa akabaki bikira au kuendelea kuzaa na kubaki bikira? Je, utata huu unajitokeza kwa vile Biblia imesheheni fasihi ya Kiyahudi? Mtaalam wa Biblia Barbara Thiering, katika kitabu chake: Jesus The Man, anaelezea kwamba ubikira wa Maria, unaoongelewa kwenye Biblia si sawa na ule tunaoufahamu sisi wa kutofanya tendo la ngono na kwamba Bikira Maria hakuwa Bikira peke yake. Ni kwamba kulikuwepo na mabikira wengine na hadi leo hii bado kuna mabikira miongoni mwa jamii ya wayahudi. Barbara Thiering, ni mtaalam na msomi. Amefanya utafiti juu ya jambo hili na wala si ubabaishaji na ubishi usiokuwa na msingi Kufuatana na utamaduni wa wayahudi, utamaduni ambao bado unaendelea hadi sasa, ni kwamba wachumba walikuwa wanaruhusiwa kuishi pamoja kwa kipindi fulani kabla ya ndoa: “Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mja mzito...” (Matayo 1:18). Maneno: “Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke”, yanatujulisha kwamba walishakaa pamoja kwa kipindi fulani, lakini walikuwa hawajafunga ndoa. Lugha ya kiyahudi haina umasikini wa maneno, kiasi cha kutumia maneno mengi “kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke” badala ya kufipisha “kabla ya kuona, au kabla ya kufunga ndoa”. Kurefusha maneno ni kutaka kutoa ujumbe kwamba walishakaa pamoja kabla ya kufunga ndoa. Baada ya kuwaruhusu wachumba kuishi pamoja kwa muda fulani, walitenganishwa tena kwa muda mrefu ili kupima uaminifu na upendo kwa pande zote mbili. Kipindi hiki cha wachumba kuishi pamoja na kutenganishwa kabla ya kufunga ndoa kilijulikana na bado kinajulikana miongoni mwa jamii ya wayahudi kama kipindi cha ubikira. Ingetokea mtu akapata mimba katika kipindi hiki kama ilivyotokea kwa Mama wa Yesu, inatajwa kwamba binti amepata mimba akiwa bikira au wakati wa ubikira. Kupata mimba wakati wa kipindi cha ubikira ilikuwa neema kubwa: “ Salamu Maria, uliyejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe.......usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. Ni hivi: Utapata mimba, utamzaa mtoto wa kiune na utampa jina Yesu” ( Luka 1:29-31). Lakini pia kipindi hiki cha ubikira kilileta wasiwasi kwa upande wa wanaume kama Yosefu ambao hawakuamini mimba kutungwa wakati wa kipindi kifupi cha kukaa pamoja: “ Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani;alikusudia kumwacha kwa siri. Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akwamwambia, ‘ Yosefu, mwana wa Daudi, uisogope kuchumkua Maria mke wako, maana amekuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu...” ( Matayo 1:19-20). Malaika ni wazee wenye busara waliozijua mila na desturi za wayahudi, walioujua pia uaminifu wa Maria na uwezekano wa mtu kupata mimba wakati wa ubikira. Kwa mantiki hii Bikira Maria aliendelea kuwa bikira baada ya kumzaa Yesu na ndugu zake. Jambo hili halina utata kwa wayahudi na labda ndiyo maana hadi leo hii bado wanamsubri mkombozi wao. Hawana imani na Yesu wa Nazareti! Kwetu sisi ubikira wa Maria ni utata kwa vile fasihi ya biblia ni ngeni na hakuna juhudi za kutaka kujifunza. Pia imejengeka tabia ya kupenda vitu vyenye mafumbo mafumbo kuliko vitu vilivyo wazi kama kumpenda jirani! Labda makala hii itachokoza mawazo na kutusaidia kujadiliana mambo ya msingi, hasa yale yanayohusu ujumbe wa Yesu Kristu, na kuachana na mambo kama ya Ubikira, yasiyokuwa na maana yoyote katika maisha yetu ya kila siku. Na , Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment