INASHANGAZA, JE TATIZO
LIKO WAPI?
Kwa mataifa mengine
sikukuu za mwisho wa mwaka huwa ni za kutafakari yaliyotendeka ndani ya mwaka
mzima na kujipanga upya kwa maka unaofuata. Sina uhakika kama sisi Tanzania
tunafanya hivyo. Katika makala hii najaribu tu kidogo kuangalia mambo
yanayoshangaza ndani ya taifa letu na kujiuliza tatizo nini? Ni wazi kuna mambo
mengi tunayoyafanya vizuri, lakini kama mtu unataka kuendelea mbele ni lazima
kuangalia pale unapojikwaa.
Tumemaliza sherehe za
miaka hamsini ya uhuru wetu. Ni vyema kusherehekea kwa mafanikio ama kwa
kushindwa kufikia malengo: Miaka hamsini bado kuna mapungufu mengi, la
kushangaza hapa ni kwamba tumetumia fedha nyingi kwenye sherehe hizi wakati
taifa linayumba kiuchumi na kuna hatari bajeti isiweze kufikia mwisho wa mwaka
wa fedha. Kwa nini matumizi makubwa ya sherehe, wakati bado kuna hitaji kubwa
la kuboresha huduma za -kijamii? Je tatizo liko wapi hapa? Ni uongozi? Ni
kutokuwa na malengo ya mbali au hatuna wataalam wa uchumi?
Baada ya sherehe za
uhuru tunawasikia viongozi wetu wakisema kwamba hali ya uchumi ni mbaya na maisha ni magumu! Inashangaza baada ya
kutumia fedha zote hizo kwenye sherehe za uhuru tunalia kwamba maisha ni
magumu. Huu ndio utamaduni wetu wa kulalamikia ugumu wa maisha wakati
tunateketeza fedha: tunalalamika maisha magumu wakati barabara zetu zimejaa
magari hadi foleni hazitembei, magari hayo yanakunywa mafuta! Tunalalamika
maisha magumu lakini watu wana simu zaidi ya tatu, simu zote hizo zinakula
fedha na kila ukipita watu wote simu masikioni; tunalalamika ugumu wa maisha,
wakati sehemu za starehe na nyama choma watu wamejazana kibao; wanakula na
kunywa; bei ya bia inapaa na bei ya nyama inatisha; tunalalamika ugumu wa
maisha wakati tunachanga mamilioni ya fedha kufanya sherehe za arusi;
tunalalamika maisha magumu wakati majumba makubwa yanajengwa usiku na mchana!
Inashangaza!
Siku tatu zilizopita
mvua ilinyesha kwa nguvu kubwa ndani ya jiji la Dar-es-Salaam na kuleta mafuriko
na maafa makubwa. Watu wamekufa na wengine hadi sasa hivi hawana makazi. Amini
usiamini, baada ya saa moja mvua hii kubwa kunyesha, nilishuhudia maeneo ya
Tabata Chang’ombe watu wakienda kununua maji ya chumvi na kuilaumu idara ya
maji kwamba siku hizi haitoi maji. Inashangaza kabisa mvua kunyesha siku tatu
mfulizo na watu wakashindwa kuvuna maji ya mvua. Mtu anaweza kujiuliza: Je hapa
tatizo liko wapi? Nyumba nyingi zimeezekwa kwa bati, mvua ikinyesa maji
yanatiririka kwenye bati, yanaingia barabarani, yanaharibu barabara, yanaleta
mafuriko. Tunashindwa kuyatumia maji haya, kupikia, kuoga, kufua na kufanya
shughuli nyingine. Nina imani kama tungeweza kuyavuna maji haya ya mvua hii
iliyoleta maafa makubwa kwenye Jiji la Dar-es-Salaam, yangetusukuma zaidi ya
miezi miwili.
Kule Rwanda, wametunga
sheria ya maji ya mvua. Ni kinyume cha sheria maji ya mvua kutiririka kwenda
kwa jirani au kuingia barabarani na kuleta uharibifu. Kwa mujibu wa sheria kule
Rwanda, kila mtu ni lazima avune maji ya mvua. Sheria hii imesaidia watu kule
Rwanda kupata maji ya kutumia majumbani
mwaka mzima,, pia imesaidia kupunguza uharibifu wa miundo mbinu na mafuriko.
Nina imani kwamba kama nyumba zote za Dar-es-Salaam zingekuwa na mfumo wa
kuvuna maji ya mvua, ni wazi athari ya mvua hizi ingekuwa ndogo.
Lakini jingine
linaloshangaza ni madaraja kusombwa na maji barabara mpya ya Mandela,
iliyofunguliwa juzi kwa mbwembwe kubomoka. Mtu anaweza kujiuliza, madaraja haya
yalijengwa kwa kiwango gani? Na je hii barabara ya Mandela inayobomoka kwa mvua
ya siku tatu, itakuwa na hali gani miaka miwili mitatu ijayo? Ni kweli maji
yana nguvu kubwa, lakini wanaojenga barabara hawalijui hili? Wanatengeneza
mitaro ya kupitisha maji, wakijua kwamba kuna siku maji yanaweza kuja kwa kasi
kubwa, la kushangaza ni kwamba mitaro hii ndiyo iliyobomoka!
Inashangaza pia watu
kujenga kwenye mkondo wa maji. Watanzania wanaamini kwamba maji yanawakimbia
watu! Sasa wametambua kwamba maji hufuata mkondo wake. Maji yamebomoa kuta na
kusomba vitu vingi vya thamani. Mtu anaweza kujiuliza je tatizo liko wapi, watu
kujenga kwenye mkondo wa maji? Mbona Dar-es-Salaam bado ina maeneo makubwa?
Hadi leo idadi ya watu
waliokufa haijulikani. Wengine wanasema ni 20, wengine wanasema ni 50! Serikali
inasema ni 20, lakini watu walioshuhudia mafuriko haya wanasema watu waliokufa
ni wengi kiasi cha kufikia hata 100. Kinachoshangaza hapa ni kwamba anayeweza
kujitokeza kusema ukweli wa jambo hili, ataitwa mchochezi. Gazeti lolote likijitokeza kuandika ukweli wa idadi
ya watu waliokufa inayokinzana na ile ya serikali, litaonekana kuwa ni gazeti
la uchochezi na linaweza kufungiwa!
Tukiachana na hili la
mafuriko, yako mambo mengine yanayoshangaza sana katika taifa letu na bora
kuyatafakari kwa pamoja na kutafuta tatizo lilipo ili tuweze kusonga mbele kama
taifa. Kabla ya mvua hii ya mafuriko tulikuwa na tatizo la mafuta. “Wakubwa”
wanaouza mafuta waliamua kuyaficha na kuacha kutoa huduma hii. Hatujashuhudia
polisi wakiendesha msako wa kuwashika “wakubwa” na kuwapeleka mbele ya sheria;
maana hawa ni wachochezi wakubwa wanataka watu waichukie serikali yao na
matokeo yake ni kuleta vurugu; watu hawa wanahujumu uchumi wa nchi, siku tatu
bila mafuta mambo mengi yanakwama na uzalishaji unazorota. Mtu anaweza
kujiuliza tatizo liko wapi? Kwanini polisi wasiwakamate “wakubwa” hawa? Badala
yake tunasikia waandishi na wahariri wa vyombo vya habari wanakamatwa kwa
uchochezi. Badala ya kuwakamata watu wanaoficha mafuta, wanaopandisha bei ya sukari, wanaoiba wanyamapori na
kuwasafirisha nchi za nje wanamkamata Mwigamba, anayeandika makala katika
gazeti hili. Makala kama hii ninayoiandika inaweza kuleta uchochezi zaidi ya
mtu anayeficha mafuta na kupandisha bei ya sukari? Tatizo liko wapi hapa?
Ni watanzania wangapi
wataisoma makala hii ninayoiandika sasa hivi? Nikikamatwa na kuwekwa ndani kwa
uchochezi, ni imani yangu kwamba idadi kubwa ya watu wataisoma makala hii. Kama
ilivyotokea kwa Mwigamba; sina uhakika kama mapolisi wengi waliisoma makala ile
ilipoandikwa, lakini la uhakika ni kwamba baada ya Mwigamba kushikwa na kuwekwa
ndani, makala hiyo imesomwa na karibia polisi wote. Hivyo yule aliyemkamata
Mwigamba ndiye mchochezi kama kweli
makala ile ina aina yoyote ile ya uchochezi.
Tanzania ina mambo mengi
ya kushangaza. Siku chache kabla ya kamata kamata ya waandishi na wahariri
Jukwaa la wahariri Tanzania lilikutana kujadili amani. Mkutano uliwashangaza
wengi, maana ulionekana kutokuwa na agenda. Waandishi wa habari wanaweza
kudumisha amani kwa kuandika ukweli bila kuongeza chumvi au kuegemea upande
mmoja. Hawawezi kuzuia matukio, hii ni kazi ya watu wengine. Ni wazi wao kama
watanizaia walikuwa na haki ya kujadili amani ,lakini si kujadili hivyo kama
wahariri. Nafasi yao ya kukutana na kujadili ni kama hivi walivyokamatwa
waandishi na wahariri. La kushangaza ni
kwamba hatujasikia Jukwaa la wahariri likikutana na kukemea mbinu hizi mpya za kuwaziba midomo waandishi wa habari.
Nimetaja machache tu
yanayoshangaza kwenye taifa letu, lakini yako mengi mfano chama tawala CCM
kutembea kifua mbele na kujigamba kwamba kina ridhaa ya kutawala kutoka kwa
watanzania; tuko watanzania milioni 40, waliojiandikisha kupiga kura ni milioni
20, waliopiga kura ni milioni 8, na CCM ikawapata kama milioni tano hivi – ni
asilimia ngapi ya watanzania? Mtu unaweza kujigamba kwamba chama kinapendwa?
Nimalizie makala hii kwa
kutaja pia jambo hili linaloshangaza zaidi la huu ugonjwa wa kutotaka
kukosolewa. Huu ni ugonjwa wetu sote watanzania. Ukimkosoa mtu, wewe ni adui!
Hatupendi kuambiwa ukweli! Wenye imani zao wanasema Ukweli, utatufanya Uhuru!
Basi wakati wa sikukuu hizi za mwisho wa mwaka, tukae pamoja kama taifa na
kutafakari na kujifunza kukubali ukweli.
Nawatakia wasomaji wangu
Christmas njema na mwaka mpya wenye baraka na mafanikio.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment