DALADALA NI MIONGONI MWA MAJUKWAA YA MAJADILIANO. Ingawa Tanzania tuna majukwaa rasmi machache ya majadiliano, tuna majukwaa mengi ya majadiliano yasiyokuwa rasmi. Miongoni mwa majukwaa haya yasiyokuwa rasmi ni daladala. Ni imani yangu kwamba hata wale walioanzisha kipindi cha Dala dala kilichoanza kwa kurushwa na TBC na sasa kinarushwa na ITV, walisukumwa na umuhimu wa jukwaa hili lisilokuwa rasmi. Tofauti ya mijadala ya dala dala ya kipindi dala dala na ile ya dala dala za kawaida ni kwamba ile ya kipindi hoja za kuongelewa zinapangwa na kuandaliwa na waongozaji wa kipindi hicho, lakini ndani ya dala dala za kawaida hoja zinaibuliwa na wasafiri wenyewe. Ukipanda dala dala, ni vigumu kutoka kituo kimoja hadi kingine bila kuibuka mjadala wa aina yoyote ile ndani ya daladala. Juzi nilipanda dala dala kutoka Posta hadi Tabata. Mjadala juu ya mgomo wa madaktari ulitawala kwenye dala dala hii niliyoipanda. Watu wengi walichangia mjadala huu juu ya mgomo, na la kushangaza ni kwamba karibia dala dala yote, ambayo watu walijazana kupita kiasi, waliwaunga mkono madaktari kugoma na kusisitiza waendelee kugoma hadi watimiziwe madai yao. “Tunajua tutateseka kwa kipindi hiki cha mgomo, lakini potelea mbali, serikali yetu bila mgomo haisikilizi, waache wagome hadi watekelezewe madai yao” Alichangia mtu ambaye alionyesha kuguswa kwa namna ya pekee na mgomo wa madaktari. Mtu mmoja tu aliyeelekea kuwa mkereketwa wa chama tawala ndiye aliupinga mgomo wa Madaktari. Mawazo yote yalikuwa mazuri. Wale wengi waliokuwa wakiunga mkono mgomo wa madaktari na huyu aliyepinga mgomo huu walijielezea vizuri. Inaonyesha jinsi watanzania wanavyofuatilia kwa makini yale yanayoendelea katika Taifa lao. Bahati mbaya ni kwamba mawazo hayo mazuri yaliishia kwenye dala dala, na kila mtu alipofika kwenye kituo chake alitelemka na kuwaacha wengine wakijadili. Hata na mimi sikufahamu mwisho wa mjadala huo, maana dala dala ilikuwa inaelekea Segerea na mimi nilitelemka pale Tabata Bima. Mijadala ya namna hii ni mingi, lakini haina chombo cha kuiratibu na kuiwezesha kusikilizwa nchi nzima. Kama tungekuwa na fumo wa kuratibu mijadala hii ambayo inaendelea kwenye majukwaa mengi yasiyokuwa rasmi ungekuwa ni mchango mkubwa wa mawazo katika taifa letu. Bahati ya mjadala wa juzi kwenye dala dala ni kwamba nilikuwemo kwenye dala dala hiyo na sasa ninaandika, ili ujumbe uwafikie na wengine. Hivyo katika makala hii nitaeleza hoja zilizotolewa na pande mbili. Upande wa aliyekuwa akipinga mgomo wa madaktari na upande wa wale waliokuwa wakiunga mkono mgomo huu madaktari. Aliyekuwa anapinga mgomo huu, alikuwa na sababu mbili kubwa; Kwanza kwamba madaktari wana kiapo chao cha kulinda uhai wa mwanadamu, hivyo kugoma ni kwenda kinyume na kiapo chao, pili kwamba serikali yetu ni masikini haina fedha za kulipa fedha wanazozidai madaktari. Akasisitiza kwamba serikali haiwezi kuwabembeleza madaktari, wakiwa wakorofi watafukuzwa na serikali itawaleta wanajeshi kuendelea kutoa huduma kwenye hospitali za umma. Wale waliokuwa wakiunga mkono mgomo wa madaktari walikuwa na sababu nyingi: kwamba madaktari ni watu wanaofanya kazi kubwa kwa dakitari mmoja kuhudumia zaidi ya watu elfu kumi; kwamba mishahara yao midogo ukilinganisha na mishahara ya wafanyakazi wengine kama wale wa Mamlaka ya Mapato; kwamba serikali yetu si masikini, ina fedha nyingi: Ukiangalia magari ya kifahari yanayonunuliwa na serikali, matumizi makubwa yanayotumiwa na serikali mfano mamilioni yaliyotumika kusherehekea miaka hamsini ya uhuru wetu, mamilioni ya fedha yanayotumika kulipia matibabu ya viongozi wetu nje ya nchi, mamilioni ya fedha yanayotumika kulipia misafara mikubwa ya viongozi wetu na mengine mengi, ni ushahidi wa kutosha kwamba serikali yetu ina fedha. Kama nilivyoeleza ni kwamba upande wa wanaounga mkono mgomo ulikuwa na watu wengi, karibia wote. Aliyekuwa anapinga alikuwa mmoja. Hata hivyo kuna mambo ambayo wote kwa pamoja walikuwa wanakubaliana. Mfano, wote waliokuwa wakijadili walishangazwa na Bunge, kuendelea wiki nzima bila kutoa tamko au kujadili mgomo huu wa madaktari. Walihoji ni kwa nini Spika wa Bunge, alikataa hoja ya Mheshimiwa Zitto, aliyoitoa siku ya kwanza ya kufungua Bunge, kwamba Mgomo wa Madaktari ujadiliwe. Pia wote walishangazwa na ukimya wa Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Walihoji ni kwa nini ameamua kukaa kimya? Mgomo hu ni jambo kubwa na wala si dogo kiasi cha Rais wa nchi kunyamaza bila kutoa mwongozo au kulishughulikia wazi wazi. “Kwa nini rais wetu hayuko wazi? Tuelewe tuna kiongozi wa aina gani? Hatujasikia neno lake juu ya mgomo wa mawaziri. Tulisikia kwamba alibariki wabunge kuongezewa posho, na Spika akatamka kwamba Rais ndo alitoa kibali. Sasa tunasikia kwamba raisi hakutoa kibali hicho? Kwa nini serikali ile ile, Rais wa nchi atofautiane na Spika na waziri mkuu wake?” Alichangia mama ambaye kwa muda mwingi alikaa kimya na kusikiliza lakini baada ya muda uvumilivu wa kukaa kimya na kusikiliza ulimshinda. Ni wazi kwa vile hakukuwepo na mwenyekiti, kila mtu alikuwa akisema bila mpangilio, sauti ya mtu ndicho kilikuwa kigezo cha kusikilizwa, aliyeweza kutoa sauti kubwa, dala dala nzima ilikaa kimya kumsikiliza. Kati ya wachangiaji, alikuwepo mtoto mdogo, nafikiri yuko kidato cha kwanza alichangia “ Nimewasikiliza kwa makini. Kuunga mkono au kutounga mkono haina maana yoyote ile. Ukweli ni kwamba mgomo upo na unaendelea. Nisichokielewa mimi ni uongo unaotangazwa na viongozi wa serikali kwamba huduma kwenye hospitali zimerejea na hali ni shwari wakati tumeshuhudia kwa macho yetu wagonjwa wanakufa na madaktari hawapo kazini. Ninatoka Muhimbili, baba yangu ni mgonjwa na hajahudumiwa leo siku ya saba..” Hoja ya kijana huyu ilizua mjadala mkubwa. Watu walihoji ni kwa nini serikali yetu inajenga utamaduni wa kusema uongo? Walitoa mifano mingi ya serikali kusema uongo,, mfano wakati wa mtikisiko wa uchumi, serikali ilisema sisi hatutaguswa na mtikisiko huo. Lakini leo hii maisha yakiwa magumu, utasikia wanasema ni athari za mtikisiko wa uchumi. Walisema tuna chakula cha kutosha na hakuna atakaye kufa kwa njaa; lakini habari tunazosikia kuna watu hawana chakula katika wilaya mbali mbali . Wanasema uchumi wetu unakua kwa kasi, lakini shilingi yetu inaendelea kudidimia. Kama uchumi unakuwa ni kwa nini shilingi yetu ididimie. Kwa nini waseme mgomo umekwisha wakati ndo mgomo unaanza? Nilichojifunza kwenye mjadala ndani ya dala dala ni kwamba watanzania wanafuatilia kila tukio na wana mchango mzuri wa mawazo. Ni bahati mbaya kwamba hakuna mtu wa kusikiliza hoja zao na wala hadi leo hii hakuna jitihada yoyote ya kuwafikia wananchi ili kusikiliza matatizo yao na mchango wao wa mawazo. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment