UHAKIKI WA KITABU: “ In the belly of Dar-es-salaam” 1. Rekodi za Kibikiogarafia Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni “In the belly of Dar-es-salaam” na kimetungwa na Elieshi Lema. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D Vision Publishing na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN) 978-9987-521-74-6.Kimechapishwa mwaka 2011 kikiwa na kurasa 185. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. Utangulizi Hii ni hadithi ya kubuni .Mwandishi wa hadithi hii Mama Elieshi Lema, ni mwandishi mahiri .Siku chache zilizopita, nilifanya uhakiki wa vitabu vyake vya watoto. Vitabu vya Freshi na Maisha, vinaonyesha ubunifu wa Mama huyu wa kufikisha ujumbe mzito kwa watoto. Kitabu chake cha “Parched Earth”, ambacho nacho nilikifanyia uhakiki ni ushuhuda mwingine wa kuonyesha kwamba mwandishi huyu ana mbinu si za kufikisha ujumbe kwa watoto peke yao bali na kwa wakubwa pia! Hadithi yake ya “ In the belly of Dar-es-salaam” akimaanisha “Ndani mwa tumbo la Dar-es-Salaam” inachokoza mawazo, inamfanya mtu kutafakari na kujiuliza maswali mengi juu ya maisha yake na juu ya uhusiano wake na jamii inayomzunguka. Hii ni hadithi ya watoto kama nyingine ambazo Mama Elishi amekuwa akiwaandikia watoto wa Kitanzania, lakini mfumo wake wa uandishi unabaki ni ule wa kutumia hadithi za watoto kufikishwa ujumbe mzito kwa watu wazima wanaosababisha “Tumbo la Dar-es-Salaam” liwe na vitu vingi; vizuri na vibaya, matajiri na masikini, matabaka ya watu na mengine mengi ya kulijaza tumbo likawa kubwa hadi kuvimbewa. Hadithi yenyewe ina sura 15. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu hiki. III. Mazingira yanayokizunguka kitabu Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, kitu kinachoongeza mvuto wa kitabu na hadithi yenyewe. Ukweli ni kwamba mpaka sasa hapa Tanzania tuna vitabu vichache vya hadithi za Kingereza vilioandikwa na watanzania wenyewe. Inavutia kuona Mtanzania, anavyoweza kuandika hadithi inayohusu maisha ya Kitanzania kwa Kingereza. Huu ni mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza lugha hii ya kingeni ambayo ni lugha ya kimataifa na inaongoza katika kijiji cha Utandawazi. Na wala huku si kupiga vita Kiswahili, bali ni kuiendeleza lugha hii katika jamii ya Kitanzania .Mwandishi wa riwaya hii ya Kingereza, ameandika riwaya nyingi kwa lugha ya Kiswahili. Jambo la msingi ni kuzipatia nafasi lugha zote na hasa lugha kuu, mfano lugha ya taifa na lugha za kimataifa kama kingereza Mfano, mimi nimeisoma riwaya hii kwa Kingereza, lakini sasa ninafanya uhakiki wake kwa Kiswahili. Hata mtu ambaye hafahamu Kingereza, kwa kusoma uhakiki huu, anaweza kupata ujumbe wa riwaya hiyo – ingawa ingekuwa bora zaidi mtu kuisoma riwaya yenyewe kwa lugha iliyoandikwa. Kitabu hiki kimeandikwa chini ya Mradi wa vitabu vya watoto Tanzania (CBP). Tangia mwaka 2008, Mradi huu wa vitabu vya watoto kwa kusaidiwa na “ The Burt Award for African Literature” umekuwa ukisaidia waaandishi wanaoandika hadithi za Kiingereza, kuandika na kuchapisha vitabu vyao. Lengo likiwa ni kukuza lugha hii ya Kiingereza katika shule za msingi na sekondari. Kawaida waandishi wanashindanishwa na kuibuka na washindi watatu. Tuzo inatolewa kwa washindi watatu. Kwa vigezo vya majaji ambavyo hatuna ruhusa ya kuviingilia, hadidhi hii ya “In the belly of Dar-es-Salaam” ilipata tuzo ya mshindi wa tatu. Riwaya hii imesheheni yale yasiyofundishwa popote, imesheheni yale ambayo kwa kawaida kila mtu anaachiwa kuongelea apendavyo. Wale wanaofanikiwa kuongelea vizuri, wanafanikiwa kuvuka – wenye bahati mbaya wanazama au wanaendelea kuogelea bila kufikia mwisho. Bahati mbaya wale wanaoogelea hadi mwisho, hawako tayari kuelezea uzoefu wao na kutoa mbinu walizozitumia kufanikiwa. Walio wengi inakuwa ni kujaribu hili na kuacha lile, ni mchezo wa pata potea. Haitoshi kumwambia mtoto asizini, haitoshi kuwazuia vijana kufanya mapenzi, bila kuwapatia mwongozo na uzoefu wa kupambana na nafsi zao, bila mwongozo wa maisha ya kiroho ya kuweza kuweka kando mvuto wa kimwili na kuangalia ndani ya nafsi ya mtu, heshima ya mtu, furaha ya mtu, mema na mabaya ya mtu. Maana uzuri wa mtu si umbo lake, bali ni yale ya ndani yanayomfanya kuwa mtu, ni matendo yake yanayomtofautisha na wanyama wengine. Riwaya hii inafumua na kuelezea yale yote yanayotendeka ndani ya Jiji kubwa la Dar-es-salaam. Matatizo ya watoto wa mitaani, maisha magumu ya watu wa kipato cha chini. Umoja na mshikamano wa watoto wanaoishi ndani ya Jiji la Dar-es-salaamKijana. Riwaya hii pia inaonyesha wazi umuhimu wa sokoo Kuu la Kariakoo, ambalo mwandishi analiita “Mama”.Ni soko la uhai, vijana wanaendesha maisha yao kwa kufanya biashara kwenye soko ili na wengine soko hili ni nyumba ya kulala na sehemu ya kuleta matumaini katika maisha yao. Mwandishi anaonyesha wazi kwamba watoto wa mitaani wanaofanikiwa kupata kipato kidogo wanapanga vyumba maeneo ya karibu na Kariakoo, kama vile Kigogo na Bonde la Msimbazi. Bahati mbaya au nzuri riwaya iliandikwa kabla ya mfuliko ya mwaka jana. Vinginevyo angeonyesha kwenye riwaya yake jinsi ilivyo dhamb ya mauti kuwahamisha watu kutoka bonde la Msimbazi na kuwapeleka mbali na “Mama” yao. Soko kuu la Kariakoo. Hawa walitegemea kuendesha maisha yao kutegemea Soko kuu la Kariakoo kama tunavyoelezwa maisha ya Sara na wenzeka kwenye riwaya hii, sasa kule Mabwepande wataweza kumpata “Mama” mwingine? Wataweza kusafiri kila siku kuja Kariakoo na kurudi Mabwepande? Riwaya ya “In the Belly of Dar-es-salaam” inaelezea matatizo ya siku kwa siku yanayowakuta vijana wetu. Kwa upande mwingine inavunja tabia ya kuyafunika matatizo na kujenga utamaduni wa unafiki. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari. IV. Muhtasari wa Kitabu. Riwaya hii ya “In the Belly of Dar-es-salaam” ni kama mwendelezo wa Riwaya nyingine ya Mwandishi Elieshi, ya Safari ya Prospa. Hivyo ili mtu aifaidi vizuri riwaya hii ni bora kuanza kusoma kitabu cha Safari ya Prospa, ndipo apate mtiririko wote. Katika riwaya ya Safari ya Pospa, kijana Prospa anajitosa kwenye ulimwengu wa ujasusi na kuamua kwenda Dar-es-Salaam, kumtafuta Merisho, mpwa wake aliyetoweka nyumbani kwa mazingira ya kutatanisha. Katika safari ya Prospa ya kutoka Moshi kwenda Dar, njiani anakutana na Sara. Wanaambatana hadi Dar-es-Salaam, Zanzibar. Prospar, anaamua kurudi nyumbani, lakini Sara anaamua kubaki Dar-es-Salaam ili “kutafuta maisha”. Riwaya hii ya “In the Belly of Dar-es-salaam, inahusu maisha ya mtaani ya Sara na wenzake akina Mansa kutoka Kibaha, Ali kutoka Lushoto na Kaleb kutoka Mtwara. Wote hawa wanakutana kwenye mitaa ya Dar-es-Salaam, wakiwa wanakimbia umasikini wa vijijini. Wakiwa ndani ya jiji, wanakutana na maisha magumu na kutisha, wanalala wengi kwenye chumba kimoja, wanatembea juani na wakati mwingine kulala barazani. Wakati vijana hawa wakipata taabu na mateso, maisha ya anasa na starehe yanaendelea ndani ya jiji la Dar-es-Salaam. Swali kuba linabaki juu ya mgawanyo wa rasilimali za taifa letu. Kwa nini wengine waishi maisha ya peponi wakati wengine wanaishi maisha sawa na ya jehanamu? Mwandishi anatumia riwaya hii kuelezea yale yanayotendeka ndani ya jiji la Dar-es-Salaam; watu kuishi kwenye makundi ya kikabila, Wamakonde wana kikundi chao na biashara zao, Waha wana kikundi chao na biashara zao, wasambaa wana vikundi vyao na biashara zao (uk 47). Hata watoto wa mitaani, wanaokimbia vijijini kuja Dar-es-Salaam kutafuta maisha, wanajikuta kwenye makundi haya ya kikabila. Mwandisi anatumia riwaya kutuchorea vizuri maisha ya watoto wa mitaani; maisha magumu, kulala kwenye baraza, kulala kwenye muziki, kupigana na kulindana na wakati mwingine kujenga mshikamano mkubwa. Kinachojitokeza hapa ni kwamba watoto wa mitaani ndani ya jiji la Dar-es-Salaam ni jamii ya aina yake ni jamii ambayo inaacha maswali magumu juu ya umakini wa serikali kushughulika na huduma za kijamii na kuwajali watoto. Mwandishi anaonyesha jinsi wasichana wanavyojiingiza kwenye biashara ya kujiuza na wakati mwingine kufanya kazi za kudhalilishwa. Baadhi ya wasichana waliojiuza walifanya hivyo ili waweze kupata fedha ya kuwatumia mama zao na bibi zao waliobaki vijiji wakiwalelea watoto wao. Wengi wao wanafanya kazi hii ya kujiuza bila kikomo hadi pale wanapoanza kuugua na kupelekwa nyumbani kwao vijijini ili wafe kwa amani (Uk 84). Mwandishi anaonyesha umahiri wake wa uandishi pale anapoibatiza “Kariakoo” jina la mama. Kwamba Kariakoo, ndo uhai wa watu wenye kipato cha chini ndani ya jiji la Dar-es-Salaam. Kwamba Kariakoo ni mama wa wanyonge. Hapa anamwaga sifa za mama ambazo wengi wetu tunazijua: huruma, kuvumilia na kujali. Kariakoo inamjali kila mtu: Ni kituo cha biashara ambacho kila mtu anapata riziki yake. Kariakoo inamkumbatia na kumlinda kila mtu, hata Wachina wanatoka kule kwao na kuja kutafuta maisha ndani ya Kariakoo; wanauza maua na mambo mengine mengi ambayo hata watanzania wangeweza kuuza. Lakini mama Kariakoo anawalinda na kuwatunza (uk 145 – 149). Kama kawaida ya mwandishi, ya kutoegemea mabaya peke yake , bado anaamini pamoja na ubaya ulio ndani ya tumbo la Dar-es-Salaam, bado kuna watu wazuri wenye kujali, wenye roho kama ya Mama Kariakoo. Mpenzi wa Sara, ambaye ni baba mwenye familia, anaonekana kuwa tofauti. Anampenda Sara, si kwa kumtumia tu bali anampatia hata mtaji wa kuanzisha biashara. Ni bahati mbaya kwamba riwaya hii inakwisha wakati ndo imeanza; wasomaji wangependa kujua kilichotokea baada ya upasuaji anaofanyiwa Sara, ili kurekebisha macho yake. Huyu mpenzi wa Sara, anajitolea kulipa gharama za matibabu bila masharti yoyote yale. Kumbe dunia hii, na Tanzania yetu ina watu wema na wabaya! Wasomaji wangependa kujua uhusiano huu wa Sara na mshikaji wake unaishia wapi? Je Sara, atamkubali Mansa, kijana wanaoishi na kuendesha maisha magumu? Au ataendelea na uhusiano na mshikaji ambaye alimpatia mtaji na kumtibisha, lakini ana mke mwingine. Mwandishi Elieshi, amebobea kwenye ushauri wa mahusiano. Vitabu vyake vyote anajaribu kuwafundisha vijana juu ya mahusiano ya mtu na mtu, na hasa mahusiano ya mwanamke na mwanamume. Tunamsikia Rose, kwenye riwaya hii akisema: “ Mwanaume ninayeishi naye ni mwema kwangu. Ila nina mashaka kama kuna penzi kati yetu. Yeye alihitaji mwanamke na mimi nilihitaji rafiki.....Sina uhakika wa kitakachotokea endapo nitatumbukia kwenye penzi na mwanaume mwingine” (tafsiri ni yangu). (Uk 166). Maana yake ni nini? Kwamba kuna watu wanaoingia kwenye mahusiano kwa kusukumwa na mazingira fulani; upweke, umasikini au makazi. Mazingira yakibadilika, au mtu akakutana mtu anayemvutia na kuwa na penzi zito, basi mahusiano ya mwanzo yanapotea! Haya yanatokea mitaani miongoni mwa watoto wanaoishi maisha hatarishi mitaani, lakini yanatokea kwenye jamii yetu ndani ya tumbo la Dar-es-Salaam. Ni wito wa mwandishi kwetu sote kuwa na utamaduni wa kujenga upendo imara kwenye familia zetu. V. Tathmini ya Kitabu. Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Mama Elieshi Lema. Awali ya yote lazima niseme kwamba , kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasisimua sana na kutoa mafundisho katika jamii yetu na hasa kuhusu uhusiano wa mtu na mtu na maisha ya watoto wanaoishi maisha magumu ndani ya jiji la Dar-es-Salaam. Changamoto anayoitoa Mama Elieshi Lema, katika riwaya hii ni swali la kawaida: Kwa nini tunaendelea kuwa na watoto wa mitaani? Hali hii itakwisha lini? Je serikali inaona ukweli huu wa watoto wa mitaani? Kama anavyosema Kaleb kwenye riwaya kwamba Mawaziri wanaishi kwenye ulimwengu wao na wako juu sawa na ndege inayopaa angani na wakati mwingine inakuwa vigumu kuwaona kwa macho ya kawaida (uk 54) Lengo la riwaya hii kufuatana na matakwa ya Mradi wa vitabu vya watoto, ni kuwasaidia vijana wa shule za msingi na sekondari kusoma riwaya za Kiingereza na kwa njia hii kujifunza kingereza. Tofauti na waandishi wengine walioshiriki zoezi hili ka kuandika riwaya za watoto kwa lugha ya kingereza , Elieshi, hakuandika riwaya ya kufikirika, amejikita kwa mambo yanayotokea kwenye jamii. Hivyo riwaya yake inafanya kazi mbili kwa wakati mmoja. Inawasaidia watoto kujifunza lugha ya Kiingereza, lakini pia inawasaidia watoto kujifunza mambo yanayotokea katika jamii yetu na hasa yale yanayowahusu watoto wenyewe kama vile maisha ya watoto wanaoishi maisha hatarishi. Maisha ya kuishi mitaani, maisha ya kuishi maisha mgumu ya kupanga chumba kimoja watu wengi, ni hali inayoweza kumtokea kila kijana hapa Tanzania. Hivyo kuyasoma kwenye riwaya, hata kama ni ya kubuni, inasaidia, maana mwandishi anatwambia alifanya utafiti kwenye maeneo ya Kigogo na sehemu nyingine ambazo watoto wanaishi kwenye mazingira hatarishi; ni muhimu kuisoma riwaya hii. Mama Elieshi Lema, ameonyesha mfano mzuri wa kutuandikia riwaya ya “In the belly of Dar-es-salaam”. Ni bora kila mzazi angemnunulia mtoto wake kitabu hiki. Kama wazazi hawana nafasi ya kuongea na watoto wao, riwaya hii itaongea badala yao. Si lengo langu kukipigia debe kitabu hiki, bali ni kuupigia debe ujumbe mzito ulio katika riwaya hii iliyotukuka. VI. Hitimisho Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri watanzania kukisoma kitabu hiki ili waweze kujionea wenyewe uhondo uliomo ndani. Lakini kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya jambo moja la ziada, nalo ni kushirikiana na waandishi na wachapishaji wa vitabu na watu wengine wanaojali umuhimu wa vitabu katika jamii, kubuni mbinu za kuwashawishi watanzania kujenga utamaduni wa kujisomea. Bila mbinu hizi, uandishi wa vitabu na ujumbe wake utakuwa sawa na kupigia ngoma kwenye maji! Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment