TUKUBALI KUKOSOLEWA
Kuna magonjwa mengi yanayolisumbua taifa letu la Tanzania. Bila kutafuta dawa ya kuyaponya magonjwa haya ni vigumu kupiga hatua ya maendeleo. Tumeandika mara nyingi juu ya magonjwa haya, labda kuyarudia tu kwa faida ya msomaji wa makala hii, inawezekana akaisoma asiyekuwa Mtanzania: Tuna magonjwa kama: kutowajibika, rushwa, uchu wa madaraka, kutegemea miujiza, kujilimbikizia mali, kutegemea misaada, kutojiamini na kutojikubali (kutopenda lugha yetu na ngozi yetu nyeusi, baadhi yetu wanajichubua ili wafanane na Wazungu, kutopenda nywele zetu na kushabikia nywele bandia na kuzipaka rangi) na mengine mengi ikiwemo na ugonjwa sugu wa kutokukubali kukosolewa.
Kutokukubali kukosolewa ni ugonjwa wa hatari, maana asiyekubali kukosolewa hawezi kujifunza. Na asiyekubali kujifunza hawezi kupiga hatua ya maendeleo; asiyekubali kujifunza hawezi kupata ujuzi na maarifa. Daima tunasema tunajifunza kutokana na makosa, tukikosea tukakosolewa, tunajifunza na kusonga mbele. Hatari zaidi ni pale ugonjwa huu wa kutokukubali kukosolewa unaporithishwa kwa vizazi vijavyo. Vijana wetu wamerithi ugonjwa huu na wanaushabikia kwa nguvu zote. Vijana wetu wakilishwa kasumba na watu wenye nia zao za kuutafuta uongozi kwa udi na uvumba, piga ua hawako tayari kuangalia ukweli kwa upande wa pili. Vijana wetu na hasa wale wanaovishabikia vyama vya siasa na kujiingiza kwenye siasa kwa malengo ya kupata vyeo na kutoka kimaisha, hawakubali kukosolewa. Kwa mtizamo wa mbali ni kana kwamba wamejiaminishwa kwamba kukubali kukosolewa ni kukubali kushindwa? Kwa maana hiyo ni kama kusema “Hakuna kushindwa, hakuna kujisalimisha”. Huu ni msimamo wa hatari sana katika nchi changa kama yetu ya Tanzania.
Viongozi wa chama cha CHADEMA, walipokwenda Ikulu kujadiliana na Mheshimiwa Rais Kikwete juu ya sheria ya kuandika katiba mpya, ujumbe wao ulikuwa ni wa wanaume watupu. Ni kitu ambacho mtu asingekitegemea kutoka kwa chama makini kama Chadema. Niliandika makala kwa nia njema ni kihoji juu ya tukio hilo la chama ambacho ni cheche ya mapinduzi na utetezi wa haki za binadamu katika taifa letu kutoa picha ya kutokuzingatia jinsia katika ujumbe wao mzito. Nilihoji ni kwa nini CHADEMA inaendeleza mfumo dume katika taifa letu. Baada ya makala hiyo kutoka, nilipokea ujumbe mfupi (sms) kwenye simu yangu ya kiganjani na barua pepe za matusi. Nilitukamwa kwa “kuishambulia” CHADEMA. Maoni yangu yalionekana ni kuishambulia CHADEMA.
Siandiki makala hii kujitetea, maana ninajua sikufanya kosa lolote kustahili matusi hayo niliyoyapata. Nilichokifanya kwenye makala ile ni kuikosoa CHADEMA. Tunajua Chadema ilivyo na wanawake wenye uwezo wa kujenga hoja, uwezo wa kuongoza na uwezo wa kulisimamia jambo lolote la msingi, tumeshuhudia wenyewe jinsi wanawake wa CHADEMA wanavyojenga hoja Bungeni na kuzisimamia, hivyo ilishangaza kuona ujumbe wa kwenda Ikulu ni wanaume watupu. Huko nyuma nimeandika makala nyingi kuisifia CHADEMA; nilikuwa na kila sababu ya kufanya hivyo maana walikuwa wakitoa mchango chanya kwenye taifa letu. Ila imani yangu ni kwamba CHADEMA, pamoja na mema mengi inayoyafanya, inatenda makosa pia. Hivyo ikifanya makosa ni lazima tuikosoe. Na tukifanya hivyo, nao wasikilize, wajadili na kujitetea ama kukubali kukosolewa na wala si kwa matusi na shari.
Ninaamini wale walionitumia ujumbe wa matusi, na mengine matusi ya nguoni ni wanachama wa CHADEMA na labda vijana, maana siamini mtu mzima anaweza kuandika lugha ya matusi kama niliyotumiwa. Hatari ninayoiona na ambayo kila mwenye nia njema na taifa hili ni lazima aione ni kwamba mtu anayeamua kutoa matusi mazito kwa vile amekosolewa au chama chake cha siasa kimekosolewa, mtu ambaye hajali anamtukana nani awe mzee au mtu mzima, awe mtu mwenye madaraka au yule wa barabarani, awe kiongozi wa dini au muumini wa kawaida, anaweza kukupiga, kukukata na panga au kukupiga risasi mkikutana uso kwa uso.
Juzi wakati wa sherehe za miaka 35 ya chama cha Mapinduzi, niliandika kwenye mtandao wa -kijamii wa Facebook juu ya yale yaliyonikwaza kwenye sherehe hizo. Huko nako nikapokea matusi ya nguoni kutoka kwa vijana, nina hakika ni vijana maana Facebook, wanaweka umri. Nilichokifanya kwa CCM ni kama kile nilichokifanya kwa CHADEMA: Kukosoa! Lakini ugonjwa ni ule ule wa kutotaka kukosolewa. Facebook niliandika hivi:
“Sherehe za miaka 35 ya CCM zilinikwaza mambo mawili. La kwanza ni vijana wa Green guard. Kwa maoni yangu hawa ni Interahamwe! Hawa vurugu zikianza watatumaliza. Kwa nini chama cha siasa kiwe na Jeshi? Serikali ina jeshi na vyombo vyote vya ulinzi. Hawa Green Guard wa nini? Gwaride lao litakuwa limeteketeza fedha nyingi; tunasema serikali haina fedha za kuwalipa madaktari! Kuna haja kubwa ya kupiga vita majeshi haya ya vyama vya siasa. Tuachane na Green Guard, Yellow Guard, white Guard, Blue Guard na Red Guard. Iterahamwe, lilikuwa ni jesha la chama cha siasa cha Rwanda. Sote tulishuhudia mauaji yaliyoendeshwa na Interahamwe. Ni bora tujifunze kwa wenzetu, jamani hawa green guard ni jeshi kabisa, wakipata silaha ni hatari!”
“Jambo la pili lililonikwaza kwenye sherehe za miaka 35 ya CCM ni mfumo dume. Rafiki yangu Nape, alisema CCM ni chama Dume. Na Vick Kamata, aliimba wimbo kwamba wapinzani wananuka shombo wasimguse, yeye kaolewa na CCM. Maana yake CCM ni Me? Kwa nini CCM isiwe ke? Mfumo dume huu unasikitisha sana. Nitashangaa kama wanaharakati wa haki za binadamu na usawa kijinsia watakubali wimbo wa Vick Kamata, aliosema uliimbwa na wanawake wa Geita, wataruhusu wimbo huo kuendelea kuimbwa. Ni wimbo wa ubaguzi na kiunyanyasaji. Haiwezekani chama kikongwe kama CCM kinaendeleza mfumo dume, lazima kubadilika. Chama ni chama, haya mawazo kwamba chama kinaoa, yamepitwa na wakati! Ni aibu kubwa kwa mbunge kijana kama Vick Kamata kuimba wimbo huo wa kibaguzi, sawa awe na mapenzi na chama lakini sikufikia hatua ya kwenda kinyume na haki za binadamu.”
Kama nilivyosema hapo juu, siandiki makala hii kujitetea, maana pia sioni nilichowakosea hawa “vijana” wa CCM. Ninajua kabisa CCM nayo imetenda mambo mengi mazuri, lakini pia ina makosa yake. Tunapoyaona makosa haya ni lazima tuyataje na wao wakubali kukosolewa. Wajadili na kuhakikisha wanatumia nguvu ya hoja. Na muhimu zaidi ni vyama hivi vya siasa kuwafundisha vijana wao kukubali kukosolewa.
Green Guard, kama tulivyoonyeshwa Kirumba ni jeshi kamili. Swali, ni kwa nini chama cha siasa kiwe na jeshi? Hakuna historia nzuri inayoonyesha chama cha siasa kuwa na jeshi la vijana, na kikaleta amani. Kwa mtizamo huu majeshi yote ya vyama vya siasa hapa nchini kwetu, kama kweli tuna ndoto za kuishi kwenye kisiwa cha amani yavunjwe. Blue Guard, Yellow Gurard, Black Guard, white Guard na Red Guard yavunjiliwe mbali. Jeshi letu la wananchi, Polisi wetu na vyombo vyote vya ulinzi na usalama, vilinde usalama wa watanzania wote pamoja na wanachama wa vyama vya siasa. Itungwe sheria ya kuzuia majeshi haya ya vijana wa vyama vya siasa.
Pale Kirumba, wakati wa gwaride la Green Guard, viongozi wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wao,Rais Jakaya Kikwete, walionyesha kufurahishwa na jeshi hilo la vijana wa CCM. Walishangilia na kupiga makofi ya furaha. Rais Kikwete alionekana akitabasamu muda wote. Inawezekana hafahamu hatari ya kuunda jeshi kama hilo? Ina maana yeye hasomi historia? Yeye ni Amiri Jeshi mkuu wa Jeshi letu la wananchi. Vyombo vyote vya ulinzi na usalama viko chini yake. Kwa nini amri jeshi mkuu ashabikie jeshi la vijana wa chama? Ni jeshi la kulinda usalama wa nani? Usalama wa nchi au usalama wa wanachama wa CCM. Tuamini kwamba usalama wa watanzania wote ni kipaumbele namba moja, au kipaumbele ni usalama wa wana CCM na usalama wa watanzania wote ni jambo la baadaye?
Hitler, alikuwa na kikundi cha vijana wa chama chake kama vile Green Guard. Matukio yaliyofanywa na kikundi hiki cha vijana wa chama cha Hitler ni chukizo la historia. Interahamwe, kilikuwa ni kikundi cha vijana wa chama cha siasa cha Habyalima. Dunia nzima ilishuhudia jinsi vijana hao wa chama cha Habyalima, kilivyotekeleza mauji ya kimbali. Haiwezekani Green Guard, wakawa tofauti kama wakati ukifika.
Ukisoma matusi wanayoyaandika vijana hawa wa vyama vya siasa kwa kutetea makosa yanayofanywa na vyama vyao, ukisoma namna yao ya kujenga hoja kuulinda uovu, unakuwa na wasiwasi kwamba ikitokea vurugu ikazuka vijana hawa wanaopatiwa mafunzo ya kijeshi kwa lengo la kulinda “Usalama” wa chama chao na “Usalama” wa viongozi wao damu nyingi itamwagika. Mfano mzuri ni pale vijana wa chama cha CUF, walipopambana na wafuasi wa Mheshimiwa Hamad Rashid jijini Dar-es-Salaam.
Nilipohoji wimbo wa Mheshimiwa Vick Kamata, vijana wa CCM, walijibu kwamba mimi ni mjinga, sifahamu hata lugha ya Kiswahili. Hoja ni kwamba Vick, anaposema ameolewa na CCM, hiyo imetumika kama picha na wala si kuushabikia mfumo dume. Kama huo ndo ukweli, kwa nini basi picha hiyo isiwe CCM ni mama? Hata hivyo uongozi wote wa juu wa CCM ni wanaume watupu. Mwenyekiti, Makamu mwenyekiti bara na visiwani, Katibu Mkuu, Katibu Mwenezi na wengine wengi ni wanaume. Kwa mantiki hiyo CCM ni chama dume kama alivyosema Nape na kinaendeleza mfumo dume unaopigwa vita dunia nzima.
Hata na CHADEMA ni chama dume! Ujumbe wao kwenda kuzungumza na Rais Jakaya Kikwete, ulikuwa ni wa wanaume watupu. Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Kiongozi wa upinzani Bungeni na Naibu Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na wanaume.
CUF, pia ni hivyo hivyo ni chama dume, Mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu mkuu, katibu mwenezi na wengine ni wanaume. Wana wanachama wanawake, tena wenye uwezo lakini hawapati nafasi. Hiyo ndiyo hoja yangu, kuukataa ukweli huu na kutoa majibu ya matusi ni dalili za kutokutaka kukosolewa. Na huu ni ugonjwa wa hatari!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment