MGOMO WA MADAKTARI USIBEZWE NA WALA TUSIWAHUKUMU!

 Misahafu inatufundisha kutowahukumu wengine. Ujumbe wenyewe ni mzito, kwamba anayehukumu atahukumiwa! Pia tunaonywa kutoa vibanzi kwa wengine wakati sisi tuna boriti. Mbali na misahafu, mafundisho mengine ya hekima yanasema: Nyani haoni kundule! Mafundisho yote haya yanalenga kutufundisha kwamba, kabla ya kuwahukumu na kuwalaumu wengine, ni bora mtu akajichunguza yeye kwanza. Na kwa kufanya hivyo, inawezekana mtu akashindwa kupata nguvu za kuwalaumu na kuwahukumu wengine. Ukweli ni kwamba kila mtu ana dosari zake. Inawezekana dosari hizi zikawa zinatofautiana, lakini ukweli ni kwamba dosari za kila binadamu ni lazima ziguse ustawi wa jamii husika.

Hivyo kila dosari ni muhimu na ni lazima kutafutiwa ufumbuzi! Bahati mbaya kuna tabia iliyozoeleka ya kulaumu na kuhukumu dosari za wengine. Tabia hii iko kwenye jamii nyingi. Mfano mzuri ni hapa kwetu Tanzania. Tunapenda kulaumu, kuhukumu na kulaani, tunapenda kutoa vibanzi wakati sisi wenyewe tuna maboriti. Nina mashaka makubwa kama kuna Mtanzania anayeweza kusimama na kumnyoshea mwenzie kidole cha uzembe, rushwa, kutowajibika, kupenda pesa kuliko kutoa huduma, uzalendo n.k., yaliyo mengi tunafanana! Badala ya kulaumiana na kuhukumiana, ni bora tungekaa chini kama jamii moja na kuzichunguza dosari zinazojitokeza kwenye jamii yetu. Hakuna dosari, iwe ya mtu au kikundi inayosimama hewani peke yake.

Waswahili wanasema: Hakuna msiba usiokuwa na mwenzie! Mgomo wa Madaktari ni dosari kubwa iliyojitokeza katika Taifa letu, badala ya kukaa chini kama Taifa na kujadiliana, mgomo huu umekuwa gumzo, kero, aibu na kwa upande mwingine ushindi wa aina Fulani! Inawezekana Serikali ikajiona mshindi kwa kufanikiwa kupambana na madaktari na kuwashinda kwa kuwafukuza kazi. Serikali inaona vibanzi kwenye macho ya madaktari, lakini inashindwa kuona boriti zake. Serikali inalaumu na kuhukumu madaktari bila kuangalia dosari zake kwanza. Na inawezekana kwa upande mwingine madaktari wakaonekana washindi pale serikali itakapolazimika kuajiri madaktari kutoka nje ya nchi na kuwalipa pesa nyingi mara tatu ya zile walizokuwa wakidai madaktari. Ipo mifano mingi ambapo mtaalam kutoka nje analipwa zaidi kuliko mtaalam wa ndani, hata kama ujuzi wao na kisomo vinalingana. Ushindi wa serikali au ushindi wa madaktari kwa faida ya nani? Ni nani ananufaika na ushindi huu? Serikali imewafukuza madaktari, ni nani anateseka? Ni viongozi wa serikali na jamaa zao? Ni mwananchi wa kawaida au ni taifa zima? Waswahili walisema: mafahali wawili wakipambana ziumiazo ni nyasi, ingawa serikali na madaktari si mafahali wawili wanaolingana, mapambano yao yanawaumiza wanyonge! Wamejitokeza watu mbali mbali kuandika juu ya mgomo huu. Wengine wanawatetea madaktari na wengine wanawalaumu, wanawahukumu na kuwalaani. Wengine wanashika bango kwamba madaktari sheria inawazuia kugoma na wengine wanakwenda mbali zaidi ya kuwaweka madaktari waliogoma kapu moja na wauaji, maana inawezekana vifo vikatokea wakati madaktari wakigoma. Wengine wanasema madaktari waliogoma ni wazalendo, maana badala ya kuikimbia nchi na kwenda kufanya kazi nchi za nje ambako wangepata mishahara mikubwa, wameamua kubaki hapa nchini. Na ili kuonyesha uzalendo wao, wameamua kutumia njia ya amani kudai kile wanachokiita haki yao. Mgomo unachukuliwa kama njia ya amani ya kushinikiza mambo katika serikali inayoelekea kukwepa wajibu wake.

Mbali na wale wanaojitokeza kuandika magazetini majadiliano yanaendelea vijiweni, kwenye daladala, kwenye vikao vya pombe na wakati mwingine kwenye mijadala ya kisomi inayoendeshwa sehemu mbali mbali kama kwenye redio na kwenye luninga. Kama nilivyosema hapo juu, watu wamegawanyika, wengine wanawatetea madaktari na wengine wanawalaani. Binafsi nisingependa kuwatetea wala kuwalaani. Lengo la makala hii ni kuwakumbusha watanzania kwamba mgomo wa madaktari usichukuliwe kama mgomo wa madaktari. Mgomo huu ni kielelezo cha mambo mengi ambayo hayajapata ufumbuzi. Mgomo huu ni kielelezo cha mambo mengi yanayofunikwa funikwa na ni bomu la kesho. Yapo mambo mengi ambayo yanahitaji majadiliano na hasa tukigusa keki ya taifa na ustawi wa jamii. Lakini la msingi ni kwamba tusikimbilie kulaumu na kuhukumu wengine bila kujigeukia sisi wenyewe. Tusiangalie tu dosari za madaktari, bali tuunganishe dosari hizi na nyinginezo ili tupate ufumbuzi wa kudumu kwa mambo mbalimbali yanayokwamisha maendeleo ya taifa letu.

 Inawezekana kabisa kwamba madaktari wetu waliamini kwamba nchi yetu ni masikini, hivyo ilikuwa ni wajibu wao kama watanzania kushikamana na kufanya kazi kwa kujitolea zaidi ya kuangalia mishahara mikubwa. Ninasema walifikiri hivyo maana karibu kila Mtanzania anafikiri na kuamini kwamba nchi yetu ni masikini. Lakini baada ya kuona yale tunayoyaona, pesa zinavyotumiwa kwa mambo ambayo si muhimu, madaktari nao kama binadamu ni lazima waanze kuhoji. Ndo maana ninasema ni jambo la msingi kujiuliza ni kwa nini mgomo huu uje wakati ambapo taifa letu linaonyesha dalili za kuwa na pesa nyingi. Kwanini mtu aendelee kufanya kazi kwa kujitolea wakati taifa lina pesa nyingi na za kumwaga? Kwanini mtu aendelee kujitolea wakati yeye anafanya kazi nyingi hadi kukesha na kutembelea daladala, wakati wale wasiofanya kazi yoyote wanatembelea mashangingi? Wanasomesha watoto wao nje ya nchi na kuishi maisha kifahari? Wana majumba makubwa na wala hawana kitu chochote kinachosumbua akili yao. Jambo la pili ambalo ningependa watanzania wazingatie juu ya mgomo huu wa madaktari ni neno uzalendo. Mtu mzalendo analipenda taifa lake na kulitumikia na taifa linampenda na kumtumikia. Uzalendo ni kutoa na kupokea. Ukitoa bila kupokea, utaishiwa, utakufa! Mzalendo anawajibika kulitumikia taifa lake, na taifa linawajibika kumtunza na kumjali raia wake. Taifa linalojali linajua kwamba madaktari wanashughulikia maisha ya watu, daktari akifanya kosa, maisha yanapotea. Hivyo ni lazima daktari awe kwenye mazingira mazuri ya kumwezesha kutulia kiakili. Kama daktari ana wasiwasi na karo ya mtoto, kama daktari ana wasiwasi na kodi ya nyumba, pesa za chakula, hawezi kutulia kiakili na kufanya kazi zake ipasavyo. Jinsi daktari anavyowajibika kuyatunza maisha ya raia kwa gharama yoyote ile, ndiyo taifa linavyopaswa kuwajibika kuhakikisha daktari anaishi kwenye mazingira yanayomwezesha kufanya kazi vizuri. Na daktari anayejali akishindwa kufanya kazi kwa matatizo yanayosababishwa na taifa, ni lazima atasema. Kwa maana nyingine, kile kinachoonekana kuwa mgomo, hadi wengine wanataja sheria inayozuia mgomo wa madaktari, si mgomo, ni njia ya kufikisha ujumbe kwa wanaohusika kwamba madaktari hawawezi kuendela kufanya kazi katika mazingira yasiyokuwa na utulivu, vinginevyo wanatasababisha vifo badala ya kuokoa maisha. Hii ni kinyume, kwa mfano madaktari wangeamua kufanya mgomo baridi. Wanakwenda kazini, lakini hawafanyi kazi. Mwisho wa mwezi wanapata mshahara.

Tuna mifano mingi ya watanzania ambao, hawajagoma, lakini hawafanyikazi ipasavyo. Wanashinda kazini, lakini hakuna wanachokifanya. Mtu mwenye akili nyingi, anaweza kusema ni bora hao, maana hawakugoma, kitu kibaya ni mgono na sheria inazuia mgomo. La msingi ni kuitii sheria! Madaktari wetu wangefanya hivyo, hakuna ambaye angepiga kelele. Jinsi ilivyo tunatawaliwa na giza la unafiki uliofungamana na ujinga mkubwa! Madaktari ni watu wanaofanya kazi kubwa na kwa kujitolea na kuyaweka maisha yao hatarini. Madaktari walio wengi wanakesha kwa kufanya kazi masaa mengi zaidi ya watanzania wengine. Ni vigumu kuwalipa kwa kile wanachokifanya. Kama wanadai nyongeza ya mshahara, maana yake ni kwamba wanataka wafanye kazi akili yao ikiwa imetulia. Wanataka wafanye kazi wakijua kwamba nyumbani watoto wanakwenda shule, wana chakula cha kutosha na wana nyumba ya kulala. Si vibaya pia wakiwa wanajua kwamba wana usafiri wa kuaminika na wana pesa ya akiba kwa tatizo lolote linaloweza kujitokeza kama mwizi wa usiku! Madaktari wetu wanaishi ndani ya jamii. Wanaona jinsi watu wengine wanavyotesa tena bila ya kuwa na kazi wala biashara inayoonekana. Wanaona jinsi viongozi wa serikali wanayoyafurahia maisha, na wakati mwingine wale wanaofurahia maisha na kuishi maisha ya starehe ni watu ambao hawakusoma sana kama madaktari. Binadamu yeyote ni lazima aguswe na hali kama hii.

 Tusiwalaumu madaktari na wala tusiwatetee. Jambo la msingi ni kuchunguza chazo cha mgomo wao. La muhimu ni serikali kukaa chini na kuzungumza nao na kuyachunguza madai yao. Pesa wanayoidai si nyingi ukilinganisha kazi nzito wanayoifanya. Kule tunakoelekea panahitaji majadiliano zaidi ya kutumia nguvu na mabavu katika maamuzi mbali mbali katika jamii yetu. Panahitaji hekima na busara badala ya kutumia madaraka na majigambo. Ni kweli kwamba si halali madaktari kugoma, lakini pia si halali serikali inayowajali raia wake kuwafukuza madaktari. Kama nilivyotaja mwanzoni, ni lazima kubadilisha mtizamo. Dosari zinazojitokeza katika jamii yetu zitusaidie kupiga hatua ya kwenda mbele. Dosari, ikijitokeza, ni lazima kuna kitu cha kujifunza, kuna kitu cha kufanyia kazi. Ni heri dosari za hapa na pale, kama walivyosema wahenga kwamba kuna kosa lenye heri, kuliko bomu la kusambaratisha kila kitu.

 Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment