TUMEBAKI HAI 2012 NA
TUULINDE UHAI WETU!
Kufunga mwaka na
kufungua mwaka ni sikukuu zinazojirudia kila mwaka. Kwa njia moja ama nyingine
hakuna jinsi ya kukwepa kurudia maneno yale yale ya kila mwaka; imani yangu ni
kwamba kwa kuyarudia kila mwaka inaweza kutujengea utamaduni wa kuyatafakari
matukio ya mwaka mzima na kujipanga upya kwa mwaka unaoanza: Mfano kushukuru na
kuomba ni mambo ambayo lazima tuyarudie kila tunapofunga na kufungua mwaka.
Hivyo basi sote kwa pamoja tumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuuanza mwaka mpya wa
2012. Si kwa ubora wetu tumeendelea kuishi, si kwa wema wetu tumeendelea kuishi
na wala si kwa umuhimu wetu tumeendelea kuishi. Tunafahamu kabisa kwamba tuna
watu wakatili miongoni mwetu, lakini bado wanaendelea kuishi; kuna watu
wanatenda maovu, wana chuki na roho ya kujilipiza kisasi, lakini bado
wanaendelea kuishi. Tulikuwa na watu bora wenye wema wa kupindukia na muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu, lakini
hatunao tena! Hawakubarikiwa kuiona 2012! Kuendelea kuwepo, kuendelea kuishi ni
neema na huruma ya Mwenyezi Mungu. Hivyo kwa wale waliobahatiwa kuendelea
kuishi ni lazima kumshukuru Mwenyezi
Mungu. Mimi na wewe, kwa vile tunaishi, tumshukuru Mwenyezi Mungu na
kujitahidi kulijibu swali muhimu ambalo nimekuwa nikilirudia mara kwa mara:-
Swali la msingi la
kujiuliza ni Je, kwa nini Mungu,
ameturuhusu kuendelea kuishi? Tunaishi ili tufanye nini? Tunaishi ili tuendelee
kula na kunywa? Tunaishi kufurahia maisha? Tunaishi ili kuonyeshana ubabe?
Tunaishi ili kuwatesa wengine? Tunaishi ili kuhakikisha tunayatumia madaraka
yetu kiubabe? Tunaishi kuhakikisha kwamba furaha tunayoipata sasa hivi wajaliwe
kuipata na wale wa vizazi vijavyo? Kwanini tuendelee kuwepo? Pamoja na ukatili
wetu na roho mabaya kwa nini Mungu anaendelea kutulinda? Je, Mungu, anataka
nini kutoka kwetu? Uhai tunazawadiwa, hakuna anayeuomba ! Lakini baada ya
kuzawadiwa kila mwenye uhai ana wajibu wa kuulinda . Uhai ukishapotea haurudi
tena! Hivyo ni wajibu wa kila mwenye uhai, kila aliyebahatika kuumaliza mwaka
2011 na kuingia mwaka wa 2012 kuulinda uhai wake, uhai wa wengine na uhai wa
viumbe vingine vyote vinavyomzunguka. Ni wajibu wa kila mwenye uhai kuulinda
uhai wa mazingira yetu ili na mazingira yetu yachangie kuulinda uhai wetu!
Mwanateolojia wa theolojia ya ukombozi Boff,
ameanza kuhubiri theolojia mpya kabisa. Theolojia ya mazingira. Ana wito kwa
viongozi wa dini kuanza kuyaangalia mazingira yetu kwa jicho la kiimani.
Mazingira yanalinda uhai wa binadamu, hivyo binadamu huyu ambaye ni mcha Mungu,
ambaye anaamini kwamba maisha yake yanaongozwa na Mwenyezi Mungu, ni lazima
ayatunze mazingira kwa misingi ya kiimani. Kwa maneno mengine ni kwamba kutunza
mazingira ni wajibu wa kiimani na hakuna mtu wa kukwepa wajibu huu. Anasisitiza
kwamba huu sasa ndo msingi wa mahubiri yanayoendana na wakati.
Boff, alikuwa padri wa Kanisa katoliki na
mwanateolojia wa hali ya juu. Alikosana na Kanisa Katoliki, baada kuhubiri
theolojia ya ukombozi. Baada ya mapambano ya muda mrefu, aliamua kuachana na
upadri na kuendelea kuihubiri injili kwa uhuru zaidi bila vitisho vya watawala.
Yeye ni mwanafunzi wa Baba Mtakatifu Benedicto wa 16, na ndiye alipandikiza
ndani mwake roho ya “Uana mapinduzi”, lakini Boff, akacharuka zaidi, na Baba
Mtakatifu, wakati akisimamia imani ya Kanisa Katoliki, akatumia nyundo ya
utawala kumsambaratisha.
Kanisa Katoliki, nalo limesisitiza umuhimu wa
Mazingira, kwa kutaja kwamba kuharibu mazingira ni dhambi. Inawezekana kabisa
kwamba Ushawishi wa Theolojia ya Boff, umeanza kufanya kazi. Hii inaweza kuwa
ishara nzuri kwamba hata silaha za kinyonge zinafanya kazi. Si lazima mtu kuwa
na madaraka (power) na silaha nzito nzito ili kuleta ushawishi. Sasa hivi
imekubarika katika kanisa katoliki kwamba, mtu anayeharibu mazingira ni lazima
atubu na kusamehewa kama mtu anayetenda dhambi nyingine. Kama tunavyosema
usiibe, usizini nk, sasa imeongezwa na usiharibu mazingira! Hii ni hatua nzuri
na yenye changamoto hasa kwa viongozi wetu wanaopenda kutawala badala ya kuongoza.
Changamoto hii inahitaji majadiliano na ushirikishwaji, kitu ambacho ni kigeni
sana ndani ya Kanisa Katoliki na hasa Afrika.
Kila tarehe moja ni siku ya kupanda miti.
Tumeshuhudia Rais wetu Mheshimiwa Jakaya Kikwete, akipanda miti. Je, ni viongozi
wangapi wamekumbuka kupanda miti? Ni watu wangapi wamekumbuka kupanda miti
katika maeneo yao? Mungu anatuweka hai ili kulinda uhai na mazingira yetu. Kwa
kupanda miti tunalinda uhai wa mazingira yetu. Je, Maaskofu wetu wametuombea tu
makanisani, au wamekumbuka kupanda miti? Ni wangapi wamefanya hivyo? Tumezoea
kuwaona kwenye vyombo vya habari wakiilaumu serikali kwa utendaji mbovu;
ingekuwa vizuri kuwaona wakipanda miti, maana matendo ni muhimu zaidi ya
maneno. Tunajua kabisa kwamba Baadhi ya
Maaskofu wetu hawapendi kukosolewa; ukiwakosoa wanakuona kama adui – lakini kwa
hili na mengine mengi yanayohusu uhai ni lazima tuwakosoe bila kuwaogopa. Hata
wakitumia madaraka yao kiasi cha kutuumiza ni lazima tukubali kuubeba msalaba
kwa faida ya vizazi vijavyo.
Huu wito wa kuyalinda mazingira yetu unakwenda
sambamba na ujenzi wa Tanzania yenye amani na salama si tu kwa wakati wetu sisi
ambao tumefanikiwa kuingia mwaka mpya wa 2012,bali pia na kwa vizazi vijavyo.
Mungu, anaendelea kutuweka hai ili tupambane na hatari zote zinazotishia uhai
wa Mtanzania. Kuna hatari nyingi za magonjwa, ujinga na umasikini na majanga
mbalimbali. Mfano njaa bado ni tishio la uhai wa Mtanzania. Na njaa ni njaa kwa
wote, wawe wa CCM au vyama vya upinzani. Njaa ikija ni tatizo la taifa zima la
Tanzania. Mvua isiponyesha ya kutosha. Baadhi ya maeneo ya Tanzania, yanakumbwa
na uhaba wa chakula na miaka mingine inakuwa mbaya kiasi cha watu kufa. Ni aibu
jambo hili kutokea kwenye nchi yenye maziwa na mito na ardhi ya kutosha. Wakati
mwingine ni uzembe na kutowajibika. Kuna mikoa inakuwa na chakula kingi wakati mikoa mingine watu wanakufa kwa njaa.
Tatizo kubwa likiwa usafiri wa kusafirisha chakula hicho kutoka mkoa hadi
mwingine. Barabara zilikuwa mbaya! Sasa hivi barabara zinatengenezwa. Mheshimiwa
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kwenye
ahadi zake wakati wa uchaguzi mkuu alituhakikishia kwamba barabara zitatengenezwa. Tunaendelea
kuamini kwamba hilo litatendeka.
Umaskini na ujinga
vinatishia pia uhai wa watanzania walio wengi. Pamoja na jitihada za serikali
inayowajibika, kuondoa umaskini na ujinga ni mradi wa pamoja pia! Ni lazima
kila Mtanzania kushiriki katika jitihada za kuutokomeza umaskini na ujinga.
Hatuwezi kuutokomeza umaskini bila kufanya kazi kwa bidii. Watanzania tuna
utamaduni wa uzembe. Kazi iliyofanyika wakati wa Mjerumani, aliyewalazimisha
Watanganyika kufanya kazi kwa viboko, haikufanyika wakati wa utawala wa
Mwingereza. Hivyo basi Mungu, amezikataa roho zetu ili tuweze kuendelea kupamba
na na umasikini na ujinga.
Je, Mungu, ametuacha hai
ili tushuhudie mwaka mwingine wa awamu ya nne ya uongozi wa taifa letu?
Ametuacha hai ili tushiriki kuiandika historia hai ya taifa letu na kushuhudia
demokrasia ikikua na kukomaa? Ametuacha wazi kushangilia tu au kushangilia na
kushiriki kufanya kazi. Mheshimiwa Jakaya Kikwete,hata kama amejaliwa karama
elfu na moja, hawezi kutanzua kila kitu bila ushirikiano wa watanzania wote
waliojaliwa kuuona mwaka mpya wa 2012.
Hata hivyo ukweli
unabaki pale pale kwamba mwanadamu ni yule yule, mwenye tamaa, uchu wa
madaraka, kujipenda, chuki, kulipiza kisasi nk. Na ukweli mwingine ni kwamba
pamoja na ukorofi wa mwanadamu, Mungu,
hachoki kumvumilia. Jinsi Mungu, anavyotuvumilia ndivyo tunapaswa kuvumiliana
sisi kwa sisi. Viongozi wetu watuvumilie, na sisi tuwavumilie. Bila
kuvumiliana, hatuwezi kuendelea kuishi. Ubabe si karama ya Kimungu, bali
kishetani! Ni lazima CCM kuwavumilia wapinzani na wapinzani kuwavumilia CCM,
tukiwa na imani kwamba sote tunajenga kitu kimoja. Huruma ya Mungu, ndiyo
inatufanya tuendee kuishi. Kwa vile bado Mungu bado ametusimamia, tushirikiane
naye kuulinda uhai wetu na uhai wa taifa letu. Lakini hasa jambo la msingi ni
kuijenga Tanzania bora ya vizazi vijavyo. Heri ya mwaka mpya!
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment