ANANIA NA SAFIRA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005

ANANIA NA SAFIRA.

Hotuba ya mheshimiwa Rais William Benjamin Mkapa, mwishoni wa mwezi jana, iliongelea juu ya uaminifu. Alijitahidi kuelezea juu ya tatizo hili na kuonyesha jinsi uaminifu unavyopungua miongoni mwa watanzania. Yeye alipenda kusema "watanzania" lakini wachambuzi wa mambo wanasema Serikali yake ndio imepoteza sifa ya uaminifu, au kwa kutaka kupamba lugha, ukarimu na unafiki, tunaweza kusema: " Kwa kiasi kikubwa serikali yake imepoteza sifa ya uaminifu". Sina haja ya kutoa mifano maana kila siku ya Mungu, vyombo vya habari vinaelezea jinsi watumishi wa serikali ya Mkapa, wanavyopata pesa kwa udanganyifu. Kitine, amelalamika, kwamba wale walionunua nyumba za serikali wamezifanyia ukarabati wa mamilioni kwa muda mfupi usiomruhusu mfanyakazi wa serikali kupata pesa nyingi hivyo. Watetezi wa hoja hiyo wanasema watumishi hao walipata mikopo kutoka benki! Tusubiri , historia itasema ukweli!

Ingawa Rais Mkapa, aliamua kuchagua neno Uaminifu, alikuwa analenga kusema rushwa, uwajibikaji na uzalendo. Kwa Mtanzania anayeishi ndani ya nchi hii kwa asilimia miamoja atakubaliana na maoni yangu! Kwa vile Rais Mkapa, ni mzazi wetu, ni baba yetu, ni bora kumkumbusha msemo wa Kiswahili usemao: Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo! Au, ule msemo wa daima utavuna ulichopanda! Usipande mtama ukategemea kuvuna karanga!

Watanzania walio wengi wamekulia katika mazingira ya udanganyifu, rushwa na uzembe. Katika serikali ya awamu wa tatu tabia hizi zimejionyesha wazi na kufumbiwa macho. Watu wachache wamefanya kazi kwa uaminifu na kwa bidii kubwa, lakini asilimia kubwa ni udanganyifu, rushwa na uzembe. Ni kutaka miujiza isiyowezekana watu hawa kuibuka na uaminifu Mitihani inanunuliwa, vyeti vinanunuliwa na watu wanapata mafanikio ya haraka maishani ( wanajenga majumba, wanakuwa na magari, wanakuwa viongozi wa juu serikalini, wana kuwa na viwanda, pesa nyingi hadi mabilioni) bila kusoma, walau kuwa na digrii moja au cheti na wakati mwingine bila hata kumaliza sekondari. Hadi kuna msemo kwamba mafanikio maishani si kusoma!

Hata hivyo uaminifu ni neno pana na linazua maswali kuliko majibu. Mtu mwenye uchokozi anaweza kutoa maoni kwamba hata na majambazi wana uaminifu mkubwa miongoni mwao. Ikiwa na maana kwamba mtu akiongelea uaminifu ni bora kutoa maelezo ya kina. Jambazi akikamatwa, anakubali kuteswa na wakati mwingine kuyapoteza maisha yake bila kuwataja majambazi wengine. Huu ni uaminifu wa kiwango cha juu! Sitaki kuamini kwamba Rais wetu alikuwa akimaanisha uaminifu wa hivi! Mtu anayechota pesa za serikali ili kukiendeleza chama chake cha siasa, anakuwa anakoswa uaminifu katika serikali, lakini ni mwaminifu katika chama chake. Sidhani Rais, anapingana na uaminifu wa aina hii?! Anayechota pesa kwa manufaa ya CCM, atakuwa bazazi mbele ya Rais Mkapa? Mtu anayechota pesa za serikali ili kuwasomesha watoto wake, jamaa zake na kuleta maendeleo katika wilaya yake, anakuwa anakoswa uaminifu serikalini, lakini ni mwaminifu kwa familia yake na kabila lake, inawezekana au inategemea kwamba huyu pia si mwaminifu machoni mbele ya Rais Mkapa.

Uaminifu unahitaji malengo, kipimo na uwajibikaji. Ni lazima mtu ajiulize ni kwa nini anatakiwa kuwa mwaminifu, na kwa nani? Kwa familia yake, kwa kabila lake, kwa dini yake au kwa taifa lake, na je ni kipimo gani kitatumika kuupima uaminifu wake. Na ni lazima uwepo mfumo wa kumsaidia mtu kutekeleza malengo, kukumbushwa malengo na kupimwa mara kwa mara. Mtu akiachwa peke yake ni lazima atangulize uaminifu unaolenga katika kumletea manufaa yake binafsi.

Majambazi, wana mifumo yao ya kulinda na kukuza uaminifu miongoni mwao. Wana viongozi, wana viapo, wana nafasi za kukutania kufanya mikutano na majadiliano na wana waganga wao wa kuwafanyia zindiko na matambiko. Majambazi wana kipimo cha kupima uaminifu wa kila mshirika. Anayeshindwa kipimo hicho anakwenda maji!

Wakati nikitafakari hotuba ya Mheshimiwa Mkapa, juu ya uaminifu nilikumbuka yale tunayoelezwa katika Biblia kuhusu Anania na Safira. Hawa ni mme na mke walioishi kwenye jumuiya za kwanza za Kikristu zilizokuwa zimejiwekea malengo, kipimo na uwajibikaji:
" Jumuiya yote yote ya waamini ilikuwa moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo........ Hakuna mtu ye yote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmmoja kadiri ya mahitaji yake".(Matendo ya Mitume 4:32-35).

Hayo yalikuwa malengo ya jumuiya za mwanzo. Kuuza mali zao zote na kuishi kwa kugawana kwa usawa. Wanajumuiya wote walipimwa kwa kipimo hiki. Walikuwa na mfumo wa kukumbushana na kuhimizana kutekeleza lengo lao hilo. Udanganyifu ilikuwa ni kwenda kinyume na lengo lao hilo. Mfano mzuri ni Udanganyifu wa Anania na Safira:
" Mtu mmoja aitwaye Anania na mkewe Safira waliuza shamba lao vile vile. Lakini, mkewe akiwa anajua, Anania akajiwekea sehemu ya fedha alizozipata na ile sehemu nyingine akawakabidhi mitume. Basi, Petro akamwuliza, "Anania, mbona Shetani ameungia moyo wako na kukufanya umdanganye Roho Mtakatifu kwa kujiwekea sehemu ya fedha ulizopata kutokana na lile shamba? Kabla ya kuliuza lilikuwa mali yako, na baada ya kuliuza, bado hizo fedha zilikuwa zako uzitumie utakavyo, kwa nini ,basi, uliamua moyoni kwako kufanya jambo la namna hii? Hukumdanganya mtu, umemdanganya Mungu". Anania aliposikia hayo, akaaguka chini, akafa. Watu wote waliosikia habari ya tukio hilo waliogopa sana.....Baada ya muda wa saa tatu hivi, mke wake, bila kufahamu mambo yaliyotukia, akaingia mle ndani( neno mle ndani, ni kutaka kumaanisha, mahali pa kukutania, mkutano wa jumuiya, nafasi ya majadiliano, kukumbushana malengo na wajibu) Petro akamwambia," Niambie Je, kiasi hiki cha fedha ndicho mlichopata kwa kuuza lile shamba?" Yeye akamjibu, "Naam, ni kisi hicho". Naye Petro akamwambia, "Mbona umekula njama kumjaribu Roho wa Bwana?........ Mara Safira akaanguka mbele ya miguu ya Petro, akafa...... Kanisa lote pamoja na wote waliosikia habari ya tukio hilo, waliogopa sana" ( Matendo ya Mitume 5:1-11).

Wataalamu wa Biblia wanatuelezea kwamba kifo cha Anania na Safira, hakikuwa kifo kama tunavyojua sisi mtu kufa akazikwa kaburini. Ni kwamba walitengwa na jumuia ya waamini. Ukosefu wa uaminifu katika Jumuiya za Kikristu za mwanzo kulimaanisha kifo. Kutengwa na jumuiya kulilinganishwa na kifo. Woga wa kutengwa na jumuiya kuliwafanya watu kuwa waaminifu wakati wote. Kila mtu aliujua wajibu wake wa kutanguliza jumuiya kabla ya kuyatanguliza maisha yake binafsi. Walisali pamoja, walionyana, walikumbushana, walitiana nguvu.

Kabla ya uaminifu kwa jumuiya nzima, kila mtu alichunguza uaminifu katika moyo wake. Kila mtu alijipima kwa kipimo cha Anania na Safira. Ni kiasi gani mtu alijiamini yeye mwenyewe. Anania na Safira, walitaka watoe nusu ya mali yao, kwa kisingizio cha kutoa kila kitu walichokuwa nacho.

Mfano huu wa Anania na Safira, unaweza kutusaidia sisi watanzania. Je, sisi tuna malengo gani? Kipimo chetu cha uaminifu ni kipi? Anayekoswa uaminifu anafanywa nini? Tunakutania wapi ili kuonyana, kukumbushana malengo na kutiana nguvu? Ni nani anaogopa kutengwa na jamii akifanya mambo ya udanganyifu? Tunaogopa nini? Ni yapi yaliyojaa mioyoni mwetu?

Ni imani yangu kwamba Rais Mkapa, analijua hili kwamba huwezi kujenga uaminifu kwenye majukwaa, kwenye luninga au kwenye magazeti, kwamba huwezi kujenga uaminifu bila ya kuwa na malengo na kipimo.
Huko nyuma lengo letu lilikuwa ni kujenga Ujamaa na Kujitegemea. Kila aliyekwenda kinyume na sera ya ujamaa, alionekana kuwa mtu asiyekuwa mwaminifu. Sasa hivi hatujengi ujamaa, na hakuna mwenye uhakika tunachokijenga ni kitu gani. Wengine wanasema Utandawazi, wengine wanasema kazi yao au malengo yao ni kujenga barabara, wengine wanasema soko hulia, wengine wanasema ubinafsishaji. Sasa hivi ni vurugu!

Mtu, akipora pesa za serikali, akajenga hekalu, watu wanamshangilia. Huyu anaonekana kama shujaa. Kila Mtanzania, anataka awe kama yeye. Mazingira kama haya hayawezi kujenga uaminifu.

Tume ya Warioba, ilifichua watu na mazingira yanayosababisha ukosefu wa uaminifu (rushwa), hakuna kilichofanyika! Kwanini basi " Bongo land" isimaanishe ubazazi? Watu wana macho na akili. Wakiona kiongozi anaanzisha ubazazi, nao wanafuatisha!

Watu kama Waziri Mkuu Frederick Sumaye, wametajwa mara nyingi kuogelea kwenye dimbwi la udanganyifu. Rais Mkapa, amekaa kimya! Kwa kutuonyesha kwamba hii ni "Bongo land", Sumaye, amejitangaza kutaka kugombea nafasi anayoiacha Mkapa. Kama huu si ubazazi ni kitu gani?
Kama Mkapa, anakerwa na udanganyifu, kama anataka kuiona Tanzania, yenye watu waaminifu, ajitahidi kabla ya kumaliza uongozi wake apendekeze malengo ya kitaifa na kutengeneza mifumo ya kutekeleza malengo hayo. Apendekeza katiba mpya itakayokuwa inaelezea wazi hatua za kumchukulia mtu anayevunja uaminifu wa kitaifa. Katiba inayowapatia wananchi uwezo wa kuwakataa viongozi wala rushwa. Katiba inayoruhusu wagombea binafsi, jambo ambalo linaweza kuleta ufanisi wa kisiasa katika Taifa letu maana kuna watu wanapenda kulitumia taifa letu lakini hawapendi ukiritimba wa vyama vya siasa. Apendekeze tume huru ya uchaguzi, ili wananchi wawe na uhuru wa kuichagua serikali yenye sera ya kujenga uaminifu wa kitaifa. Apendekeza uanzishwaji wa chombo katika ngazi zote cha kuweza kukumbusha, kujadiliana, kutiana nguvu na kupima uaminifu wa kila Mtanzania.

Hali ilivyo sasa hivi, mtu anaweza kujiuliza uaminifu maana yake nini? Na je, ni kwa nini mtu awe mwaminifu? Anaogopa nini? Anawajibika kwa nani? Kipimo cha uaminifu wake nini? Je uaminifu ni wa watanzania wote au kuna baadhi ya watu ambao ndio lazima wawe waaminifu. Uaminifu ni wa maskini tu au na matajiri ni lazima wawe waaminifu? Je umasikini unachangia kiasi gani watu kukoswa uaminifu? Je ukosefu wa huduma muhimu katika jamii yetu unachangia kiasi gani watu kutokuwa waaminifu?

Bila kuyaangalia yote haya na kuyafanyia kazi ni ndoto kuongelea uaminifu. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo! Pia tunakumbushwa kwamba: "Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini kutoka miti ya michongoma, wala hawachumi matunda ya mizabibu kutoka mbigili. Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake, na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake" (Luka 6:43-45).

Ningejua huja baadaye. Rais Mkapa, angekumbuka "Uaminifu" mwanzoni mwa uongozi wake, na kuunda mifumo ya kuukomoza, sasa hivi tungekuwa mbali. Kwa vile alishindwa kwa kufumbwa macho na wapambe, asishangae kujua maana halisi ya "Bongo land" na "Utajiju". Asubiri mkondo wa historia, sote tutahukumiwa na historia, kila mtu kwa nafasi yake, wale watakao kuwa bado hai ndipo watakapolijua Jiji na mitaa yake.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment