MASHTAKA

UHAKIKI HUU ULICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA

UHAKIKI WA KITABU: MASHTAKA


1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA.

Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Mashtaka na kimetungwa na Elieshi Lema. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D Vision Publishing Dar-es-Salaam, na kitatoka hivi karibuni. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni Mimi Padri Privatus Karugendo.

II. UTANGULIZI.

Mashtaka ni kitabu kingine kati ya vitabu vingi ambavyo mwandishi Elieshi Lema, ameandika hadithi za watoto. Mwandishi huyu amejizolea sifa nyingi katika uwanja huu wa hadithi za watoto. Safari ya Prosper, Freshi na Maisha, Mkate Mtamu, Mwendo na vinginevyo vimedhihirisha “umama” wa mwandishi na hasa ujuzi wake wa kueleza mambo makubwa kwa lugha ya kawaida; ujuzi wa kufundisha mambo makubwa kwa watoto wadogo. Mama huyu ni mwanafalsafa wa enzi hizi tulizomo, ni mtetezi wa haki za binadamu na mwanaharakati asiyechoka kuitumia kalamu yake na kipaji chake kuwaelimisha watanzania na ulimwengu mzima.

Daima katika vitabu vyake anatoa mafundisho yasiyokuwa na shaka wala utata, kama tunavyosikia kwenye maneno haya:
“Hivyo basi, fundisho la hadithi ya Katope, ambalo kwa miongo kadhaa watoto wameelezwa kama njia ya kuwalea ili wawe wasikivu na wenye heshima na utii, limejikita katika kifo cha mtoto Katope, kilichosababishwa na mvua. Mwili wake ukamomonyoka, kiungo kwa kiungo. (Ukurasa wa 20)”.

Katika hadithi hii ya Mashtaka tutaelezwa na kufundishwa juu ya ubaya wa kutumia adhabu za kifo kama mafundisho ya kuwalea watoto wetu. Katika hadithi hii tutaelezwa athari mbaya ya kufundisha watoto kwa vitisho badala ya kuwafundisha kwa kuwafafanulia vizuri bila utata na mafumbo. Mwandishi anajitahidi kutushawishi, bila kutumia nguvu nyingi ili tuchukie utamaduni wa kuwanyanyasa wanawake na watoto. Hadithi ya Katope, inajihukumu yenyewe na kutufanya sote kuichukia. Kwa namna hii watu wataanza kutunga hadithi za kumjenga mtoto, hadithi ya kumfanya mtoto kupenda maisha na kuishi kwa kuzingatia heshima kwa jinsia zote.

Kitabu kina sura kumi, Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.

III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.

Enzi tulizomo ni za kutetea Haki. Kuna harakati za kutetea haki za watoto, haki za wanawake, haki za wanaume, haki za walemavu, haki za wazee, haki za yatima, haki za wajane nk. Semina nyingi zinafanyika na fedha nyingi zinatumika katika harakati hizi. Wakati mwingine utetezi huu unakuwa kama upepo uvumao na kupita, maana walengwa wanabaki katika giza, wakati wale wanaojiita watetezi wakinufaika kiasi kikubwa kutokana na mchakato mzima wa kutetea haki za watoto, wanawake, wanaume, wajane, wagane, wazee, yatima na wagonjwa wa UKIMWI.

Mara nyingi wale wanaotetewa hatusikii sauti zao, hatusikii kilio chao, hatupati hali halisi ya mazingira yao; tunasikia tu sauti za wanaharakati. Tunajifunza matatizo yao kupitia sauti za wanaharakati.

Hadithi ya Mashtaka ni tofauti! Mwandishi anatupatia picha tofauti kabisa. Watoto wanazungumza wenyewe, wanauliza maswali na kuelezea hali yao. Wanaharakati wanafanya kazi mmoja tu ya kumtuma Rehema, kwenda kusikiliza mashtaka ya watoto na kuleta mrejesho kwa wanaharakati ili waone la kufanya. Kwa maneno mengine Rehema, anayetumwa kwenda kwa watoto ni mimi na wewe tutakaosoma kitabu hiki. Kazi yetu ni kuwasikiliza watoto, ni kusikiliza mashtaka ya watoto na kuleta mrejesho kwa wanaharakati na jamii nzima.

Tumekuwa tukifanya makosa makubwa, kufikiri kwamba tunafahamu yote wanayoyataka watoto wetu, hatuwapatii nafasi ya kuwasikiliza.
Tunafikri wao hawana uwezo wa kutamani mambo fulani fulani na kuyachukia baadhi ya yale tunayotaka kuwafundisha. Watoto nao wana utashi, wana maonjo na wana namna yao ya kuyaangalia matukio mbalimbali katika jamii. Tukiwapatia nafasi ya kujielezea, tukiwasikiliza, tunaweza kugundua mengi kama yanayojitokeza kwenye hadithi ya Mashtaka.

“Madhumuni ya kazi hii niliyopewa ni kuyasikiliza maswali yao na kuyatafakari na kuyatoa huko pembezoni ambako hayasikiki na kuyaleta hadharani ili kwa pamoja tutafute njia ya kurejesha amani na haki katika maisha ya watoto kama hao katika jamii zetu, ili tuwe na mategemeo ya kuwa na taifa lenye kujivunia watu wake. Watoto hao wanaitwa Lea na Linda. Hao ndio nimeambiwa niwafuatilie, niwasikilize, ili tupate msingi wa kujengea hoja mashtaka yao. ” (Ukurasa wa 5)

“Kundi la wanajamii wanaharakati wa haki za watoto wamenituma kwenda kusikiliza kisa cha Lea na Linda. Kwa pamoja wameona kwamba watoto hao wanalo shitaka kwa jamii hii inayoongozwa na watu wazima. Nimetumwa kusikiliza tu, nikaambiwa kuwa kusikiliza ni stadi adimu inayowezesha mtu kujiweka wazi, kujivua ubinafsi ili ajifunze na aweze kuruhusu akili kupokea maarifa mbadala. Kusikiliza mtu mwingine ni kutambua uwepo wake na kuheshimu nafsi yake.” (Ukurasa wa 6).

Mashtaka haya ni ya kweli. Swali ni je ni nani atatoa hukumu? Tukitafute kitabu cha hadithi ya Katope na kukichoma? Tumtafute aliyetunga hadithi hii na kumfikisha mahakamani? Au tubadilike sote na kujenga utamaduni wa kuwatambia watoto wetu hadithi za matumaini? Maisha ni matumaini. Malezi yenye matumaini yanamjenga mtoto kiakili na kiroho. Kwa malezi yenye matumaini tunaweza kujenga utamaduni wa maadili bora kwa watoto wetu na kwa taifa letu la Tanzania.

Sasa tuangalie kitabu chenyewe kwa muhtasari.


IV. MUHTASARI WA KITABU

Kwa ufupi hadithi ya Mashtaka, inahoji hadithi tuliyoizoea kuisikia ya Katope Mtoto wa ajabu. Mimi niliisikia hadithi hii zaidi ya miaka hamsini iliyopita. Nilifikiri hadithi hii ilikwenda na wakoloni, kumbe bado inachipuka na uendelee kusambaa katika jamii yetu? Binafsi sina uhakika wa hili, lakini kama mwandishi mashuhuri ameamua kuipigia kelele ni lazima itakuwa bado ipo.

Muhtasari wenyewe wa kitabu hiki upo kwenye maneno ya mwandishi mwenyewe:

“Kusema kweli, ( hadithi ya Katope) hii siyo hadithi ya watoto. Ni hadithi inayohusu wanawake. Mimi nadhani, ingawa sina uhakika sana, lakini nafikiri ni hadithi inayoelezea masuala mawili makuu: ajabu ya nguvu aliyonayo mwanamke; na nafasi ya mwanamke huyu katika u-baadaye wa jamii yake. Hadithi hii ya Katope inaakisi migongano iliyopo katika nguvu kuu mbili; nguvu ya asili ya mwanamke kuweza kulea kiumbe katika mwili wake na baadaye kuzaa, nguvu isiyoweza kuchukuliwa au kunyang’anywa na mtu mwingine kwa njia yoyote ile; na nguvu ya Mungu wake mwenye uwezo ulio nje ya upeo wa binadamu yeyote, na ambaye anaweza kuchukua kiumbe hicho kilichozaliwa na mwanamke wakati wowote bila kuhitaji ridhaa ya mwanamke huyo. Katika kuzungumzia nafasi ya mwanamke huyu katika maisha ya jamii yake, hadithi hii inaweza kuwa kielelezo cha mvutano mkali kati ya mwanamke aliye na uwezo huo wa kuzaa watoto, ambao ndio wanaoendeleza uwepo wa binadamu duniani, kwa hiyo ni muhimu mno kwa jamii yoyote; lakini uwezo huo nyeti kiasi hicho haumpi mwanamke nguvu ya kuwa mtenda kijamii akilinganishwa na mwanamme mwenye nguvu hiyo ya kuwa mtenda na ambaye amejimilikisha hao watoto anaozaa mwanamke. Unyeti wa mvutano huu ndio unaolazimisha hadithi za kuimarisha itikadi ya umiliki na utendi wa wanaume ziandikwe na zihadithiwe kizazi kimoja hadi kingine ili watu waaminishwe kuwa hivyo ndivyo mambo yalivyo na ndivyo yatakavyokuwa milele. Jambo lingine linalohusiana na hilo, ni kwamba hadithi inazungumzia juu ya rasilimali mtoto. Rasilimali hiyo ambayo itapatikana kwa njia moja pekee – kwa mwanamke kuzaa. Mimi nafikiri kwamba Katope anapokufa kwa ukatili wa namna ile, hali ya ugumba imeonekana kukosa suluhu kwa njia yoyote ile. Thamani ya mwanamke iko kwenye uwezo wake wa kuzaa tu, basi. Vinginevyo, hana stahili ya furaha, ingawa anaweza kuishi. Mama Katope aliumia sana, tena sana, mtoto wake alipokufa, lakini bado hakuonewa huruma, alirudishwa kwenye ugumba wake - milele.” (113).

Katika sura kumi za hadithi ya Mashtaka, mwandishi Elieshi Lema, amejaribu kuwasilisha maswali ya watoto juu ya hadithi ya Katope: Watoto wanauliza ni kwa nini jamii itunge hadithi za kikatili? Kwanini Katope afe? Kifo ni adhabu ya kumrekebisha mtu au ni adhabu ya kutoa uhai? Sura zote kumi zina majina ya kumwingiza msomaji katika tafakuri na kumwelekeza kwenye shitaka lenyewe. Katika njia ya kuelekea shitaka lenyewe mambo mengi yanaibuka. Kwa mfano:

“Ni nani analea watoto wa kiume kujiona kuwa wao ni miungu midogo na viongozi wateule wenye sauti hata kwa wanawake watu wazima waliowazaa na kuwalea? Nani analea ubabe wao tangu wakiwa kinda? Na hata katika ngazi ya umma, bado wanawake wanatumika kuwaweka sawa wanawake wenzao ili wasidai vitu fulanifulani, wasipaaze sauti zao katika masuala ya utetezi au siasa, wasijitokeze mbele wakidai masilahi yanayohusu mambo yatakayowakomboa kimaisha. Ndio hivyo jamii ilivyolea na inaendelea kulea makundi ya watu fulani, wakiwemo watoto, katika maadili ya mila na desturi za ukandamizaji. Katika hali hii, watoto wanakua na wanapokuwa watu wazima wanakuwa na upofu wa kutambua tofauti kati ya hali ya heshima na haki, na ile ya ukandamizaji na unyanyasaji. Wengine wanaamini kuwa kukandamizwa ni stahili yao, ni njia ya kuonyesha heshima na mapenzi kwa wanaowatawala, au njia ya kuonyesha kujali na kupendwa. Ndivyo maisha yalivyo. Ndivyo Mungu alivyopanga, hata maandiko ya dini yanasema hivyo.”( Ukurasa wa 13-14).



Majina ya sura za hadithi hii kuanzia ya kwanza hadi ya kumi ni: Hatua, Kisa, Njia, Maswali, Somo, Bila Ukomo, Zimwi la Mto, Kitendawili, Ufunuo na Tunguri.

Sura ya kwanza ambayo inaitwa Hatua, mwandishi anaanza hatua kwa hatua kutuingiza kwenye mashitaka ya watoto:
“Yaani, katika kipindi cha miaka 15 hadi 20, taifa hili litaongozwa na kizazi kilichokuwa kinanyanyaswa, kugandamizwa, kisichokuwa na sauti wala nguvu yoyote. Je, uongozi wa watu kama hao utakuwa na ubora wa aina gani? Kwa sababu hiyo pekee, masuala ya watoto na vijana, hasa yale yanayohusu ujenzi wa utu na akili, ni sharti yawe masuala ya msingi kwa taifa, kwani yanaweza kuathiri jamii ya sasa na ya wakati ujao.” (ukurasa 3-4).

Sura ya pili ambayo ni Kisa, tunaendelea kufunuliwa juu ya mashtaka ya watoto:
”Chanzo cha shitaka la hawa watoto wadogo wa miaka minane hivi kinatokea mbali katika historia. Nikaelezwa kuwa hakuna hali yoyote ya kijamii isiyokuwa na historia, isiyokuwa na mwanzo na chanzo. Hiyo ndiyo bahati nzuri, kwamba historia haipotelei angani, hupotea tu kwenye akili zetu wakati tunapoamua kuisahau, wakati haikidhi maslahi au matakwa yetu. Wanaharakati walisema kuwa kisa kinatokana na vitu vingi, vilivyofungamana, kama hali za maisha zinavyofungamana na uchumi, siasa, dini na itikadi. Walinieleza kuwa wakati fulani katika historia ya jamii, wakati watu wanapambana na mazingira na kupimana nguvu yao na ile ya mazingira yao, watoto walikoseshwa nafasi katika harakati hizo. Watu waliona kuwa kulea ni fadhila na sio haki za pande zote mbili, anayelea na anayelelewa. Wakaona kuwa mwenye kupewa fadhila hawezi kuwa na sauti ya maoni au maamuzi. Baada ya kujenga na kuimarisha imani hiyo, ikawa ni mazoea. Watoto wakaonekana kuwa ni viumbe wanyonge, wasiokuwa na maana kubwa katika harakati za kuishi, kwa hiyo wakaonekana na kukubalika kuwa viumbe dhaifu, wasiokuwa na uwezo wa maamuzi. Asiyekuwa na sauti huweza kufanyiwa chochote, kizuri na kibaya. Au, katika michakato ya maisha, tamaa za watu wazima, za makundi fulani zilizidi na kukosa ukomo, haja ya kuwa na mamlaka ikashinda ile ya mapenzi na amani.” (Ukurasa wa 8-9).

Katika sura hii pamoja na mambo mengi yanayoelezwa, tunaendelea kufunuliwa kwamba:
“Watu wakaishi katika raha itokanayo na maisha ya mazoea yanayotishwa na upya. Wanajamii wakawa wanaishi katika giza totoro, lenye usingizi mtamu uliowaaminisha kuwa ni sawa kabisa tabia za ukandamizaji kuitwa mila au desturi. Jamii ikakaa, ikatulia, ikalindwa na imani yao katika nguvu na umuhimu wa mila na desturi. Jamii ikawa kama mtu avaaye kiatu kinachobana vidole, lakini kwa vile ’utamaduni’ umeifanya akili yake kutozingatia adha ya vidole, mvaaji hakuweza kuhisi haja ya kuwa na viatu vingine vitakavyotoa uhuru na nafasi kwa vidole vya miguu yake, kwa hiyo akaendelea kuvaa tu viatu vinavyobana hadi vidole vikaota sugu inayotesa kwa maumivu makali” (Ukurasa wa 15).

Pamoja na yote hayo yanayojifunua katika sura hii, mwandishi anaendelea kutukumbusha kwamba bado haya yote ni muktadha tu wa kisa chenyewe. Chanzo hasa cha shitaka kinapatikana katika maana ya hadithi ya mapokeo inayoitwa Katope.

Sura ya tatu ambayo ni Njia, mwandishi anatuingiza ndani ya shitaka lenyewe na kutufanya tutafakari kwa makini. Ujumbe wake anaupitisha kwenye sauti ya wanaharakati:

“Wanaharakati wanawasihi nyie watu wazima mlioisikiliza hadithi ya Katope mkiwa watoto, au mlioisoma katika vitabu mjiulize: aliyetoa na anayeendelea kutoa hilo fundisho kwa mtoto wake leo, akitumia visa vilivyotokea na kumwathiri Katope hivyo, ana dhamira ya kumbadilisha mtoto wake tabia au ana lengo la kutimiza azma yake mwenyewe? Kisha mkishapata jibu, mjiulize tena, kama hadithi inafaa ama haifai kwa kutolea fundisho linalohitajika, je, azma ya huyo mtu au watu kuitumia katika kuwezesha malezi bora ya mtoto itakuwa ni nini kama mtoto anakufa?” (Ukurasa wa 21).

Mwandishi anaendelea kututaka tutafakari kwa ndani zaidi:

“Wanaharakati walinieleza kuwa mhusika mkuu, aliyebeba pia fundisho la hadithi, ni mama yake Katope. Mama huyo alimpata mtoto kwa sharti moja kuu, kuwa Katope asinyeshewe na mvua hata tone! Akinyeshewa tu, basi, atamomonyoka na kuwa rundo la tope! Kuvunjwa kwa sharti hili ndiyo iliyokuwa sababu ya kifo cha Katope. Sharti lilitolewa kwa mama, kifo kikawa kwa mtoto! Je, tutakosea kusema kwamba kifo cha mtoto, kilikusudiwa kuwa adhabu sahihi kwa mama?!” (Ukurasa wa 21).

Na swali jingine ni hili:

“Katika hadithi ya Katope, kuna swali linaloibuka bila kizuizi: Je, ni jamii yenye kudumisha maadili gani kwa ustawi wake, iliyomnyang’anya mwanamke hadhi yake ya kuwa nguzo ya kudumisha uhai na ustawi wa jamii yake, kwa kumwadhibu mtoto wake kwa kifo cha kikatili, ili kumrudisha tena mwanamke huyo kwenye adhabu ya ugumba?” (Ukurasa wa 29-30)

Na changamoto ni kwamba:
“Ni changamoto ya kila kizazi kupambana na athari za mabadiliko duniani. Kwa hiyo, tamaa na utashi unaweza kutofautiana kati ya kizazi kimoja na kingine. Hali hiyo ya utofauti ikaleta migongano na migogoro na kuchochea harakati za mabadiliko chanya miongoni mwa watu katika jamii. Kwa hiyo, hata pale maswali fulani yanapofifishwa, historia inakuwa imeshayarekodi, na ukweli huo haufunikwi.” ( pg 33)

Sura ya nne ambayo ni Maswali , ndio inafunua kisa chote cha Katope. Mama anaamua kuwahadithia watoto wake hadithi ya Katope. Lengo ni kutaka watoto wawe wasikivu, wasifanye kinyume na matarajio ya wazazi. Swali kubwa hapa ni kwa nini tutumie mifano ya kikatili kuwafundisha watoto wetu? Kwanini tunapendelea mambo ya kikatili katika jamii zetu:

“Nilishurutika kufungua mlango wa kumbukumbu zangu, kisha nikahesabu: vitoto vichanga vilivyozaliwa na kutupwa jalalani na mama vijana wasiokuwa na uwezo, haja wala muda wa kuwalea; vijana kuchomwa moto kwa kuvishwa tairi na kumwagiwa mafuta ya taa; vijana wa kike kuchomwa sehemu za miili yao na waajiri kwa makosa yasiyoeleweka; watoto kupigwa hadi kufa kwa kuiba shilingi mia moja ya kununulia andazi ili aweze kutuliza njaa inayouma bila huruma; vitoto ambavyo hata miili yao haijaumbika kikamilifu kubakwa na wengine hadi kufa; vijana shuleni kupigwa hadi kufa kwa kudai haki kutoka kwa viongozi wao, na wengine kuchomwa moto wakiwa wamelala kama vile mtu huyo alidhamiria kuchoma viazi; wanawake kulemazwa, kukatwa viungo vya miili yao na wengine kupigwa hadi kufa, vijana wanaohangaika kuzikwa ndani ya ardhi wakiwa hai kwa manufaa ya wenye nguvu, wenye chao … Na zaidi, ukatili wa kuteka wengine na kuwafundisha kuua na kushiriki kwenye vita wasizoelewa, wengine kufanywa watumwa wa ngono… Matukio yote hayo na mengine mengi mno yalisikika, yaliongelewa na watu, maneno yakafukuta chinichini na moshi ukaonekana unapaa angani. Na baada ya siku kadhaa, upepo ukapita, ukachukua moshi, huyoo ukapeperushia mbali, maneno yakafifia, mambo yakapita. Jamii ikapoa, ikaendelea na harakati za kutafuta amani na maisha yenye hadhi!” (37-38)

Lakini pia kuna hili swali la:

“Nilijiuliza, iweje sikuona hali hii? Kila siku katika televisheni tunaangalia ukatili wa aina zote, tunaburudishwa nao, tunacheka na kuushangilia. Ni sisi tunaupenda ubabe, tunausifia na tunautazama katika uhalisia mbadala wa sanaa za maonyesho unaotuambia kwamba ubabe, usaliti, mauaji, fitina, udanganyifu, wizi na ufisadi ndiyo maisha ya kutamani, ndiyo maisha yanayotambulika kuwa bora na jamii yetu, ndiyo yenye hadhi na heshima. Tunalea watoto na vijana wetu kwa dozi za ukatili huo.” (38-39).

Sura ya tano ambayo ni Somo, tunaelezwa juu ya wazazi wa Lea na Linda. Mama huyu aliwapata watoto hawa kwa taabu sana. Hana tofauti na Mama Katope. Hivyo hakutaka awapoteze watoto wake. Aliwatambia hadithi ya Katope, ili wasichana wake waongope na kuachia tabia ya kutoroka kwenda kuogelea. Lengo lake la kuwasimulia hadithi ya katope lilikuwa zuri, lakini bila kufahamu kwamba hiki ni kizazi kipya, kina mtazamo tofauti na wa zamani. Badala ya kuogopa, watoto wanaanza kuhoji hadithi nzima ya katope, wanahoji adhabu hii ya kikatili. Dunia imebadilika, mambo yanabadilika; ya jana siyo ya leo. Tulivyolelewa sisi, ni tofauti na malezi ya watoto wa leo. Sisi hatukuhoji, lakini watoto wetu wanahoji:

“Eti mama, kwa nini mama yake Katope hakumchapa tu, badala ya kumwacha Katope abomoke mwili wake, mikono na vidole na miguu?” (uk 50)

“Kwa nini basi huyo mtu alimuua Katope kwenye hadithi? Kwani katika kuuwa mtu kuna maadili? Au kwa nini hadithi iliishia hapo badala ya kuendelea ili imtengeneze tena?” (111)

“Ni vigumu kujua, lakini ukitafsiri hadithi, labda alitaka kuonyesha kwamba wanawake wagumba hawakubaliki, hawapendelewi. Ugumba wao hauna mafao kwa jamii. Yaani, mama waliozaa watoto wao bila nguvu za miujiza, hawakupewa masharti kama hayo. Wao walikubalika.”(112)



Tunaendelea kupata changamoto kwenye sura hii ya Somo:

“Mimi nilitumwa kuwafuatilia hawa pacha, kusikiliza na kutega masikio ili niweze kutambua, je, yupo msomaji au msikilizaji katika jamii hii, wakati huu, ambaye anasimamia hoja kwamba, hata hadithi, yoyote ile, na mifumo mingine yote ya kijamii na hasa ya kiutamaduni inabidi izingatie haki za msingi za watoto na watu wengine wote?”
(Ukurasa wa.53).

Na kwamba:
“Hadithi ni mawazo; injini inayowezesha gari kutembea na ndege kupaa ni mawazo; nyumba tunamoishi na kufanyia kazi, nguo tunazovaa, bidhaa tunazozalisha ni mawazo; mashine zinazozalisha bidhaa za kila aina ni mawazo; mifumo ya kijamii na serikali zake ni mawazo. Ni nini hakitokani na mawazo ya mtu? Hata kiini cha maisha ya watu hapa duniani ni jambo ambalo limesumbua akili za wanasayansi na watu wa dini kwa muda mrefu, wakifikiri na kutoa mapendekezo tofauti kuhusu maisha yalikoanzia. Kila kitu kina chimbuko katika wazo…” (Ukurasa wa 54).

Sura ya sita na ya saba, Bila ukomo na Zimwi la Mto, zinaelezea matuko ya mapacha kwenda kuogelea na matukio yaliyotokea huko. Ni mwendelezo wa kusisitiza simulizi la Katope. Kuna changamoto ya mfumo dume na tishio la wanaharakati kuegemea upande mmoja wakati wakitetea usawa wa kijinsia. Uzito unatoka upande mmoja na kuelemea upande mwingie. Wasichana wanaonekana wanaweza kila kitu na wana busara kuliko wavulana. Hii ni hatari nyingine ambayo itazalisha harakati nyingine ya kutetea haki za wanaume!

Sura ya nane ambayo ni Kitendawili, inazama kwenye tafakuri ya kifo cha Katope. Kwanini katope alikufa? Kwani mtuzi wa hadithi anatoa adhabu ya kifo kwa Katope? Na kwa nini Mama ndio anapata adhabu hiyo ya Katope? Na ni kwa nini akosee mtoto, mama apate adhabu? Alimpata mtoto kwa taabu kubwa, baada ya kumpata masharti yanakuwa makubwa. Mtoto, anakosea, mama anapata adhabu ya kufiwa na mtoto wake:

“Aliendelea kuyatafakari, huku wenzake wakimshangaa alivyonyamaza ghafla. Je, mtoto anaendelea kuwa kielelezo cha itikadi inayomtaka mwanamke kuwa mzazi baridi, mlezi baridi na mdumisha itikadi baridi? “(101).

Sura ya tisa ambayo ni Ufunuo tunasikia hivi:

“Kwa hiyo, inawezekana kabisa kuwa katika hadithi ya Katope, baba hakuhusishwa na ugumba, kwa hiyo, hakuwekwa kwenye hadithi. Na kama ni hivyo, itikadi iliyompa baba nguvu ya kudai watoto kuwa ni wake, na ambayo haiwezi kuvumilia mwanamke mgumba, kwa sababu watoto wanahitajika katika jamii, ni wazi isingemweka baba katika utata huu.” (Ukurasa
wa 103).

Tena kwa kuchombeza mwandishi anaendelea kutueleza:

“Hadithi hutungwa na watu. Mawazo yanayokuwa katika hadithi hutoka katika jamii ambamo mtunzi anaishi. Mtunzi huona mambo fulanifulani yanayotendeka katika jamii na kuyatumia kujenga hali halisi mbadala. Kwa hiyo, hata kama mtoto anayeitwa Katope hakuwepo, lakini katika jamii walimoishi watunzi wa Katope kulikuwa na matukio ya kiasi fulani cha ukatili ambao ulifanyiwa watu fulanifulani. Inawezekana pia kuwa mtu aliyeitwa Mama Katope hakuwepo, lakini kulikuwepo na akina mama waliokuwa hawawezi kupata watoto na jamii ilikuwa na hisia fulani kuhusu mama hao. Katika mantiki hiyo, hadithi zina ukweli mtupu, tena mwingi tu. Jamii haingeweza kutumia matukio ya hadithi ya Katope kufundishia watoto wao maadili ya utii na usikivu kama hakuna ukweli wowote kuhusu masuala hayo, na hivyo kuelezea hadithi isiyokuwa na maana yoyote. Isingewezekana hata kidogo.” (111)

Sura ya mwisho ambayo ni Tunguri, inatufungia kitabu chetu kwa mwanga ambao watoto wanaupata kwa kutambua kwamba hadithi ya Katope si yao, bali ilitungwa kuwanyanyasa akina mama! Kama ukweli ndio huo, kwani mama yao aliwatambia hadithi hiyo? Na kwa nini hadithi kama ya Katope ziendelee kusimuliwa watoto katika jamii yetu?

V. TATHMINI YA KITABU

Nimpongeze mwandishi kwa hadithi ya kuvutia na kufundisha kwa watoto na watu wazima. Kusema kweli hadithi zake mara nyingi ni za watoto, lakini ukiziangalia kwa undani anawalenga watu wazima; wazisome na kuwasimulia watoto wao; wazisome na kutafakari juu ya njia tunazoweza kuzitumia kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu.

Kwa kutumia lugha ya kawaida na hadithi ya kawaida ya Katope, Mwandishi ameweza kuleta mbele yetu utetezi wa haki za wanawake na watoto: hadithi ya Katope, inaonyesha wazi ubabe wa mfumo dume. Mama anapata mtoto kwa masharti magumu; mtoto anakosea masharti – mama anaadhibiwa kwa makosa ya mtoto. Lakini pia adhabu yenyewe ni ya kikatili kwa mtoto. Je si kweli kwamba baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwapatia watoto wao adhabu za kikatili? Watoto wengine wanapigwa hadi kufa, wengine wanapoteza viungo vyao au wanapata kilema cha kudumu.

Kuna kelele nyingi zinapigwa juu ya uswa wa kijinsia. Kuna kongamano na warsha zinaendeshwa ili kuwashawishi watu kusimama na kutetea usawa wa kijinsia. Fedha nyingi zinatumika na muda unapotea katika harakati hizi za usawa wa kijinsia. Mwandishi wa hadithi ya Mashtaka, ametumia maneno ya kawaida, bila kelele nyingi, bila kongamano na warsha, kwa kutumia hadithi ya Katope, kufikisha katika jamii ujumbe mzito sana wa ukiukwaji wa haki za binadamu. Mama Katope, ananyanyaswa kwa ugumba wake kufikia hatua ya kuuchukia uhai: alimpata mtoto kwa njia ya ajabu, baada ya kuteseka kwa muda mrefu na kupuuzwa na jamii; masharti ya kumtunza mtoto yanakuwa makubwa na yako nje ya uwezo wake: Kwamba mtoto asinyeshewe mvua, mama angeweza kuzuia namna gani? Katope, mtoto wa kiume ni lazima angekwenda kuchunga, ni lazima angekwenda kuwinda, ni lazima angekwenda kuchanja kuni, ni lazima angekwenda vitani, ni lazima angekwenda kufanya biashara na kuhangaika huku na kule. Katika hali hiyo ni lazima angekutana na mvua. Ingekuwa vigumu kabisa kwa Mama Katope, kupambana na maumbile ya mvua kunyesha. Hivyo sharti hili lilikuwa la kiunyanyasaji. Mwandishi amefanikiwa kuitumia hadithi ya katope kutufunulia ukatili uliojikita katika jamii yetu.

Maswali yote anayoyaibuka kwenye hadithi ya Mashtaka ni muhimu sana katika jamii yetu: kwa mfano ni kwa nini mtu atunge hadithi kama hii ya Katope? Kwanini mwanamke apate mtoto kwa masharti magumu kama hayo? Kwanini mtoto Katope afe? Kwanini Baba wa Katope, hapati adhabu?

Pamoja na mafanikio makubwa ambayo mwandishi anaonyesha kwenye hadithi ya Mashtaka, kuna baadhi ya matukio yanayozua maswali kadhaa. Mfano ni kweli kwamba jamii yetu imepiga hatua kubwa kwenye utetezi wa haki za binadamu kiasi cha watoto wa miaka 8 kuweza kuhoji hadithi ya Katope? Mimi nilipoisoma hadithi hii miaka 50 iliyopita, sikuwa na upeo wa kuona unyanyasaji uliojikita kwenye hadithi ya Katope. Ni kweli leo hii watoto wamekuwa na upeo mkubwa hivyo? Kama ni kweli hii ni hatua ya kuipongeza jamii yetu au kuwapongeza wanaharakati ambao wamekuwa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu.

Mwandishi, hakusimulia hadithi nzima ya Katope. Alichukulia kwamba wasomaji wake wote wanaifahamu hadithi ya Katope. Je ni kweli kwamba hadithi hii bado inasimuliwa katika jamii yetu? Bado kuna vitabu vya hadithi hii ya Katope? Vinginevyo mwandishi alipaswa kuisimulia kwanza hadithi ya Katope mtoto wa ajabu.

Pamoja na ukweli kwamba bado kuna unyanyasaji wa kijinsia katika jamii yetu, kuna wanaume wanaopambana kuondoa hali hii. Mwandishi anaonyesha wasichana peke yao kuwa wapambanaji wa hali hii. Katika hadithi yake ya Mashtaka, mapacha Lea na Linda, ndio wanapinga hadithi ya Katope. Hata wahusika wengine wanaowaunga mkono na kupanua mjadala mzima wa hadithi ya Katope ni wasichana. Wavulana wanaonekana ni wanyonge. Mfano Feruzi, hafahamu kuogelea – anaokolewa na Lea na Linda. Hata mjadala mzima wa hadithi ya katope, wasichana wanaonekana kuwa na akili nyingi na busara inayozidi umri wao. Wavulana hawasikiki kabisa!

Hatari inayoweza kujitokeza ni kutetea usawa wa kijinsia kwa kuegemea upande mmoja. Tunaandaa jamii ambayo daima itakuwa kwenye harakati za kutetea usawa wa kijinsia. Leo hii wanawake wanatetea haki zao na kesho wanaume wataanza kutetea haki zao. Ukweli ni kwamba hata leo hii kuna wanaume wasiokubaliana na unyanyaswaji wa kijinsia unaoendelea.

Hadithi ya Katope, ni mbaya kwa watoto wote wasichana na wavulana. Kwa vyovyote vile ni hadithi ya kikatili tu! Hata hivyo Katope mwenyewe ni mvulana! Hadithi niliyoisoma mimi na picha iliyokuwa imechorwa ilimwonyesha katope akiwa mvulana. Hivyo katika hadithi ya mashtaka, wahusika wakuu, wale mapacha, mmoja angekuwa mvulana na mwingine msichana. Na wahusika wengine wanaojitokeza kuipinga hadithi ya Katope, wangekuwa wasichana na wavulana. Kwa kutetea haki za mtoto; tusiangalie mtoto msichana na mtoto mvulana – ni lazima tuangalie haki za watoto kama watoto.

Mtu makini, kama alivyo Mama Elieshi Lema, ni lazima aone hatari ya kuegemea upande mmoja. Kuonyesha hali ya upande mmoja kuichukia hadithi ya Katope, ni kuwasaliti wanaume ambao wamekuwa mstari wa mbele kupinga aina yoyote ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika jamii yetu.

VI. HITIMISHO.

Kwa kuhitimisha, nawahimiza watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma pale kitakapotoka. Kuna mafunzo mengi yanayopatikana katika kitabu hiki. Kitabu chote ni hekima tupu, bila uangalifu wa hali ya juu badala ya kufanya uhakiki unaweza kujikuta unanukuu kitabu kizima. Unashindwa uandike lipi uache lipi.

Napendekeza pia kitabu hiki kisomwe katika shule za msingi na sekondari hadi kwenye vyuo vikuu. Pia ni bora hata na wazazi kukisoma kitabu hiki. Kila familia iwe na kitabu hiki ili hadithi ya Katope isomwe upya katika mazingira ya Tanzania ya leo. Kwa njia hii tunaweza kubadilisha utamaduni potofu.

Mwandishi, atakapopanga kuandika toleo la pili la kitabu hiki azingatie mapendekezo ya kulifanya swala zima la kutetea haki za binadamu kuwa la jamii nzima.

Pia, mwandishi afikilie hatua ya kutengeneza filamu kutokana na hadithi ya mashtaka. Mara nyingi wazembe wa kusoma vitabu, wana uwezo wa kukaa chini na kuagalia filamu; hata hivyo kuona matendo – inasaidia sana kulielewa jambo zaidi ya kulisoma tu. Hasira juu ya hadithi ya katope inaweza kuongezeka kama jamii itapata fursa ya kuiangalia kwenye filamu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment