WANAFALSAFA WA KALE WA MAGHARIBI

UHAKIKI HUU ULICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA

UHAKIKI WA KITABU: WANAFALSAFA WA KALE WA MAGHARIBI.

1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA

Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni “Wanafalsafa wa kale wa Magharibi” na kimetungwa na Padri Stefano Kaombe, wa Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Ecoprint Ltd na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 8874 30. Kimechapishwa mwaka 2004 kikiwa na kurasa 172. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. Utangulizi

Nilipofanya uhakiki wa vitabu viwili vya falsafa vilivyoandikwa na Dkt. Mihanjo:Falsafa na Usanifu wa Hoja – kutoka Wayunani hadi watanzania (Waafrika) na Falsafa na ufunuo wa Maarifa, nilisema kwamba vitabu hivi ndivyo vilikuwa vya kwanza kwenye lugha ya Kiswahili. Baadaye niligundua kosa nililolifanya. Nawaomba wasomaji wanisamehe. Ukweli ni kwamba kitabu cha falsafa kilichotangulia kuandika kwa lugha ya Kiswahili ni hiki ninachokihakiki sasa hivi: Wanafalsafa wa kale wa Magharibi, kilichoandikwa na Padre Stefano Kaombe.

Ili kuunyoosha usemi wangu kwanza, ni kwamba Dkt. Adolf Mihanjo, ni wa kwanza kuchimba zaidi na kuandika kwa kirefu. Labda alisikia wito wa Padre Kaombe, ambaye kwenye utangulizi wa kitabu chake anasema hivi:
“ Kitu kimoja tangu mwanzoni lazima nikiri, Sokratesi alisema tunapoanza kuidadisi nafsi yetu, la kwanza linalofumuka ni umbumbumbu wetu. Katika historia ya falsafa, mimi ni mbumbu kabisa! Kazi hii fupi lengo lake ni uchokozi, ni kutoa changamoto kwa “wakali” wa historia ya falsafa. Wahamaki, “wewe anzali wa falsafa mbona unacheza na mambo yasiyokuelea? Hivyo watuoneshe harakati za kuutafuta ufunguo huu kama alivyosema mwanafalsafa wetu Shaaban Robert katika titi la mama yetu: Kiswahili. Lugha ninayoitumia ni nyepesi mno, si ya kitaalamu. Nyakati nyingine niliingiwa na woga, wa kuharibu hata kile kidogo nilichokiokoteza. Naomba msamaha”.

Si kweli kwamba Padri Stefano Kaombe ni mbumbumbu katika uwanja huu wa falsafa. Anachotaka kusema ni kwamba alifanya alichokifanya kwa kiasi chake. Alichokifanya si kidogo. Ni wachache waliofanya jitihada kama za kwake. Hata na kuchokoza mawazo ni kazi kubwa.

Katika kazi yake ametoa Istilahi isiyozidi maneno 20. Lakini Dkt. Adolf Mihanjo, anatoa Istilahi inayokaribia maneno 300. Hii inaonyesha kwamba kuna hatua kubwa iliyofuata baada ya kazi ya Padri Kaombe. Maana yake ni kwamba, baada ya uchokozi wa Padre Kaombe, lugha ya Kiswahili inashika kasi kuimudu falsafa.

Kitabu hiki kimegawanyika kwenye sehemu kumi na sita. Katika aya zifuatazo nitaoa muhtasari na tathimini yale, lakini baada kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu.

III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.

“Hekima ni dhana inayovutia sana. Sababu za mvuto huu ni nyingi, lakini moja ni wazi zaidi; hekima ni ufunguo katika maisha ya mwanadamu. Binadamu anatafuta ukweli, furaha na mengine. Hekima ndiyo ufunguo wa kufungulia malango ya kasri yeye fadhila hizi. Ndiyo maana elimu ya hekima yaani “falsafa” ni msingi katika maisha binadamu.” (uk 5).

Kwa vile jitihada za kuitafuta falsafa zilianzia Babilonia, Asiria, Misri, China na India na baadaye kusambaa Ulaya. Elimu hii ilifundishwa kwenye lugha za Ulaya, Kingereza, Kifaransa, Kijerumani nk. Miaka mingi, hata hadi leo hii Elimu hii imekuwa ikitolewa kwa lugha za kigeni hapa Tanzania. Wito wa siku hizi wa kutumia lugha yetu kutoa elimu, umegusa pia falsafa. Watu waliojitupa uwanjani kujaribu ni Dkt. Mihanjo na Padri Stefano Kaombe.

Padri Stefano Kaombe, ni msomi, kiongozi wa kiroho, mwandishi na mchambuzi wa mambo mbali mbali katika jamii yetu ya Tanzania. Baada ya kupata daraja la upadri, alifanya kazi kwenye ofisi ya Mwadhama kadinali Pengo, baadaye alisomea shahada ya kwanza kwenye chuo kikuu cha Dar-es-Salaam, na kwa sasa anafanya Shahada ya Uzamili katika Taalimujamii (Sociology) kwenye Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.


IV. MUTHASARI WA KITABU.

Sehemu ya kwanza ya kitabu hiki inaongelea Kambi ya Waionia. Kambi hii inaundwa na Thalesi, Anaksimanda na Anaksimenesi. Hawa waliishi kwenye jiji la Miletusi. Watu hawa waliyasoma maumbile na kutafuta chanzo cha vitu vyote. Kambi hii ilidumu zaidi ya miaka hamsini. Thales alifundisha kwamba viumbe vyote vimekuwepo kutokana na maji. Huyu ndiye anayetambulika kuwa ni mwanafalsafa wa kwanza wa Magharibi. Anaksimanda, alipinga fundisho la Thalesi kwamba chanzoasili cha vitu vyote ni maji. Yeye alifundisha kwamba chanzo cha vitu vyote ni “kisichomwisho” au “Kisichompaka” kwa lugha ya kiyunani ‘apeiron’. Naye Anaksimenesi, aliingia na mafundisho yake kwamba chanzoasili au msingiasili wa vitu vyote ni “HEWA”, akiwa anamaanisha mvuke, upepo na pumzi. Ingawa wote walipingana, chanzo chao cha kufikiri kilikuwa ni kimoja: Chanzoasili cha vyote nini? Hili linawafanya wawe mizizi ya kihistoria ya falsafa. Kuanguka kwa jiji la Miletusi mwaka 494 kutokana na uvamizi wa mfalme Dario wa Uajemi, kulisababisha kudorora kwa kambi ya wanafalsafa wa Ionia.

Sehemu ya pili inajadili Jumuiya ya Pithagorasi:

“Wakati falsafa ya Waionia imeanza kufa katia Asia ndogo, awamu mpya ya falsafa iliibuka katika koloni la Kigiriki la Italia. Mazingira mapya ya kijamii ni kuwa kulikuwepo kudorora kwa dini na maadili. Watu walishapoteza dira ya maisha mema. Falsafa ya kipindi hiki zaidi si utafiti wa chanzoasili, lakini utaratibu wa maisha, njia ya wokovu. Jumuiya ya Pithagorasi iliundwa kwa lengo la kuhuisha dini na maadili, Wafuasi walikuwa wa kike na kiume, iliongozwa kwa karibu na walitambuana kwa alama za siri. Mavazi yao yalikuwa ya kawaida na rahisi. Walisisitiza kujinyima katika chakula na kudumisha ukimya kati yao. Useja na utunzaji wa hali ya juu ya mafundisho yao vilikuwa ni vitu muhimu” (Uk 11).

Jina la jumuiya hii linachukua jina la mwanzilishi wake Pithagorasi. Huyu alikuwa mwenyeji wa jiji la Samosi jiji pinzani la Miletusi katika Ionia. Alitembelea Uajemi na Misri (554-533) alikokwenda kujifunza hisabati na ngano zao. Pithagorasi anasema hivi juu ya mwanafalsafa:

“Maisha ya mwanadamu yanaweza kulinganishwa na michezo ya hadhara, inayovutia aina anuai za watu Baadhi ili kushindana kupata heshima na taji za ushindi, wengine kufanya biashara, wengine wa aina bora zaidi kwa ajili ya kufurahia onesho tu. Vivyo hivyo katika maisha, baadhi wanatenda wapate heshima, wengine faida na wachache kwa ajili ya ukweli tu; ndio wanafalsafa..” (uk 12).

Pithagorasi, alifundisha juu ya uhamajiroho; kwamba mtu akifa roho yake kwa sababu ni ya milele huchukua umbo jingine. Pia alijishughulisha na uwekaji wa sheria za kimaadili, na hasa mtazamo wake wa kimahisabati na kidini. Wanafunzi wa Pithagorasi, kama Filolausi ndio wanaoelezea vizuri mafundisho yake. Wapithagorasi, fundisho lao la kipekee ni muhimili kwamba namba ndicho chanzo cha kila kitu. Wanahitimisha kwa kusema “ yote ni namba”. Mafundisho yao juu ya namba na uhamajiroho yalimuathiri kwa kiwango kikubwa Plato.

Sehemu ya tatu inaongelea juu ya kambi ya Elea. Kambi hii iliundwa katika jiji la Velia, Italia. Velia, kwa kiyunani inatamkwa Elea. Kambi hii iliundwa na wakimbizi waliokimbilia kwenye jiji hili baada ya ushindi wa waajemi dhii ya Ionia. Miongoni mwa wakimbizi hawa walikuwa watu wa jumuiya ya Pithagorasi na makambi mengine ya wanafalsafa. Kilichowaunganisha si makazi bali hasa mwegamo wao wa kifalsafa. Kambi hii ilidumu takribani miaka 250. Kwa Waelea falsafa si hekima ya kidini na maadili bali ni elimu ya kiakili, mwono wa moja kwa moja wa fikra. Kwao falsafa ni ufunuo toka juu kuliko kukamata fikra.Hawa walizama kwenye “Metafizikia”. Washiriki wa kambi hii ni Khenofanesi, huyu alikuwa mtaalimungu, Pamenidesi alikuwa Mmetafizikia, wanafunzi wake wawili Melisusi na Zeno, walikuwa wayakinifu. Na wa mwisho katika kambi hii ni Melisusi aliyefundisha kwamba:

“ Kile ambacho kilikuwepo, wakati wote kilikuwepo na kitakuwepo. Kama kilikuja kuwepo, kwa ulazima hufuata kwamba kabla hakijapata kuwepo, hakuna kilichokuwepo. Hata kama, hakuna kilichokuwepo, kwa jinsi yoyote hakuna chochote ambacho kingeweza kuwepo kutoka katika kutokuwepo. Kwa sababu hakijaja kuwepo, wakati wote kilikuwepo na kitakuwepo na hakina mwanzo wala mwisho, lakini hakuna kisichompaka.. kwani hakiwezekani chochote kuwepo wakati wote, isipokuwa ni kikamilifu” (uk 21).

Kitu cha muhimu katika historia ya falsafa ni kwamba kambi hii ilikuwa ya kwanza kuibua tatizo la kiwa na kuwa. Tatizo ambalo wakati wote limekuwa kiini cha mawazo ya kimetafizikia. Tatizo hili lilikuja kutanzuliwa na Plato na Aristoto. Fundisho la kambi hii ya Elea, liliwaathiri wanafalsafa waliowafuata.

Sehemu ya nne inaongelea kambi ya pili ya Ionia. Hawa ni akina Helaklitusi, Empedoklesi na Anaksagorasi. Heraklitusi ndiye muunganishi wa kambi hizi mbili. Kwa maana ya kushuhudia uhai wa kambi ya kwanza na ya pili. Kilichounganisha kambi hizi mbili ni mji wao. Vinginevyo, waliishi nyakati tofauti na mawazo tofauti. Kambi ya pili ya Ionia ilichukua mtazamo wa ulimwengu wa uwili. Mfano Heraklitus alifundisha juu ya ubadilikovote, moto, mwanzo wa ulimwengu, ukinzani, anthroporjia na maadili. Empedoklesi, alifundisha juu ya Metafizikia, taalimuliwengu, taalimuviumbe na taalimuroho. Anaksagorasi, alifundisha juu ya vianziasili, akili, taalimulimwengu na taalimuroho.

Sehemu ya tano inawajadili Waatomu: “ Hawa wanawakilisha awamu ya mwisho ya mawazo ya Waionia mintarafu maumbile. Walikubali uwili uliofundishwa na kambi ya pili ya Waionia. Kwa kubadilisha nguvu za kiakili kwa ulazima, walikataa falsafa ya kuwili waliorithishwa. Miletus ndipo Waionia waliibuka na ndio Leuchipusi mwanzilishi wa Uatomu alikozaliwa. Juu ya Leuchpus kidogo mno kinajulikana kwa uhakika. Hivyo tukitaka kuujua uatomu, mwakilishi wake mzuri ni Demokritusi” (uk31).

Waatomu walikubali kwamba bila ombwe mwendo hauwezekani. Lakini walishikilia kwamba ombwe lipo na katika lenywe ipo miili isiyo idadi yaaani “Atomi”: “Neno hili kiasili lilimaanisha ambacho hakiwezi kukatwa au kugawanywa. Kwa waatomu ni kitu kisichogawanyika kinachoenea. Sifa yake ni kwamba, hazina idadi kwa uwingi, hazigawanyiki, zinatofautiana kwa umbo, kanuni na nafasi. Aidha zinatofautiana katika kiasi au ukubwa, kwani si nukta za kihesabati tu. Kutogawanyika kwao ni kutokana na ombwe. Zina kani sawa, lakini kutokana na tofauti ya maumbo zinatofautiana katika uzani” (uk 32).

Sehemu ya sita inajadili Wasofia. Hawa ni akina Protagorasi wa Abdera, Jorjiasi wa leontini, Hipiasi wa Elisi na Prodikusi wa Keosi. Wasofia, wanatokana na neno la kiyunani “Sophia”, lenye maana ya hekima, busara. Hivyo Wasofia au msofia ni mtu mwenye hekima. Neno hili pia lilimaanisha fundistadi mahiri, watu waliobobea katika sanaa mbali mbali. Baadaye Wasofia walitumia vibaya mbinu za mabishano katika midahalo na hivyo kusababisha usofia kumaanisha uongo, mkwepa ukweli mwenye ndaire. Falsafa ya kisofia ilishamiri kati ya mwaka 480 KK hadi mwaka 400 KK. Sokratesi alipoanza falsafa yake usofia ulipwaya kiasi cha kutokuwa na maana tena!

Maelezo mafupi juu ya watu wanaowakilisha kikundi hiki yanaweza kutupatia picha ya usofia: Protagorasi wa Abdera, huyu anaitwa “Mbinafsi”, Jorjiasi wa Leontini, anaitwa “Mkanavyote”, Hipiasi wa Elisi naitwa “Mwingi wa elimu” na Prodikusi wa Cheosi anayeitwa “Mmaadili”.

“Kifalsafa, usofia ni matokeo ya hali ya jamii, siasa, falsafa na dini ya Athene. Usofia haukuwa muendelezo wa mawao ya kifalsafa. Ni kweli ulizungumzia vijenzi vya mhusika katika elimu ya binadamu. Ulivichukulia vijenzi vya mhusika kama kitu muhimu katika elimu. Uliushusha ukweli na kuufanya ni maoni na mtu akawa kipimo cha kila kitu. Katika hili ndimo linamolala kosa la usofia na kuudhoofishia hadhi. “ (Uk 42).

Lakini tukumbuke kwamba usofia na mchango wake si hasi tu, kwani ilikuwa nguvu katika kuelimisha jamii hasa katika uzungumzaji. Pia baadhi ya wasofia waliheshimika katika majimbo yao mpaka wakawa mabalozi. Usofia uliwakilisha kipindi cha mwisho kabla ya Sokratesi.

Sehemu ta saba inamjadili Sokratesi. Historia yake, mafundiso yake na umuhimu wake katika historia ya falsafa. Mchango wa Sokratesi katika falsafa unaonekana katika mwanafunzi wake Plato. Zao linalomstahilisha nafasi kati ya waalimu bora duniani. Katika fundisho lake vitu vitatu ni vya muhimu. Kwanza kutengeneza upya njia ya kujifunza kisayansi. Toka kukijua kimoja kimoja hadi ufahamu jumla na kutoa maana ulimwenguni. Pili, utaratibu wa kuchunguza masharti ya elimu, ambao ulijenga msingi wa taaliemulimu.Tatu, uwekaji wa taratibu za kwanza za maadili uliojenga msingi wa sayansi ya maadili.

“ Baada ya kifo cha mwalimu mkuu Sokratesi, wanafunzi wake waligawanyika. Hawa walilishika wazo lake hili na wengine lile. Hii ilichangiwa na kukosekana kwa usikivu wa fundisho lake la maadili. Tunaweza kuwagawa wanafunzi wa Sokratesi katika makundi matatu:

Mosi: Wale waliochukua fundisho la maadili la Sokratesi na kulitumia katia maisha halisi, mfano mzuri ni Chenofoni.

Pili: Plato na Aristoto wao walizama ndani ya fikiriko la Sokratesi na kuliendeleza kwa mapana na mshikamano zaidi.

Tatu: Wanafunzi wake walichukua wazo Fulani la kisokratesi na kuliendeleza katika muungano na wazo la wanafalsafa waliomtangulia, hasa Waelea na Wasofia. Wanafunzi hawa wanajulikana kuwa ni wanafalsafa nusunusu wa kisokratesi.” (51)

Sehemu ya nane, inaelezea wanafalsafa nusunusu wa Kisokratesi. Hawa wanagawanyika katika shule tatu tofauti. Shule ya Megara, Shule ya Kinesi na shule ya Wasirene.
“ Shule za wanafalsafa nusunusu wa kisokratesi ziliibuka pamoja, bila kuwa na undugu kati yao. Kila moja ilijitegemea katika kipengele kimoja cha kisokratesi ilichoamua kukurika nacho. Shule hizi zilitindikiwa ukamilifu kwani falsafa zao zilijikita katika tafsiri isiyosahihi ya moyo wa falsafa ya Sokratesi. Mchango wao kifalsafa ni mkubwa. Wao waliwaathiri wanafalsafa wa kipindi hicho. Visivyoumbo vya Wamegara, vilikuwa ni kivuli vha nadharia ya mawazo a Plato. Urithi wa Antisithenesi na Aristipusi tunauona kwenye fundisho la chema kikuu cha Plato” (Uk 56).

Wastoa walifuata maadili ya Wakinesi. Falsafa ya ushuku ilichipuka katika fundisho la Wamegara, shule ya Epikarusi ilirekebisha upya fundisho la maadili ya Wahedonia. Toka Thalesi hadi Sokratesi, tunaweza kusema kwamba kilikuwa ni kipindi tangulizi, uandalizi wa shamba la falsafa. Wanafalsafa waliopanda na kuvuna falsafa pevu ni Plato na Aristoto.

Sehemu ya tisa inamjadili Plato. Maisha yake, tabia yake, maandishi yake, falsafa yake nk. Mwanafalsafa huyu gwiji, aliathiriwa na wanafalsafa wengi waliomtangulia. Hata hivyo yeye hakuwa mkusanyaji tu. Yeye alifikia hatua hata ya kuyarekebisha mafundisho ya mwalimu wake Sokratesi kabla ya kuyapokea kama yake. Na ndivyo alivyofanya kwa wanafalsafa wengine, aliyanyumbua, akayakarabati na kuyafanya upya kabla hajayaweka mafundisho yao katika himaya yake kubwa ya kifalsafa ambayo msingi wake ni nadharia ya mawazo.

“Nadharia ya mawazo ndicho kitambulisho cha pekee cha Plato. Ni msingi kwayo amejenga kasri yake ya Fizikia, Majadiliano na Maadili. Pia ni kanuni unganishi ya mfumo wa fikra zake. Japo tatizo analozungumzia liwe ni kutokufaroho, hulka ya elimu, mustakabali wa maisha ya baada ya kifo, utume wa serikali au hulka ya uzuri, kituo anachoanzia wakati wote ni wazo.” (Uk 90).

Plato, alileta mwanga mkubwa katika falsafa.
“Plato hatuoneshi kitu chochote, lakini anakuja na nuru, anaweka mwanga katika macho yetu na anatujaza uangavu ambao kwao vitu vyote baadaye vinaangazwa” (Uk 91).

Sehemu ya kumi inajadili akademi za kiplato. Akademi ya kwanza ilistawi kuanzia kifo cha Plato 347 KK. Mpaka alipoteuliwa Archesilausi kuwa gombera takribani mwaka 250 KK. Akademi ya kati iliyokuwa na wahusika wakuu Krantor, Archesilausi na Kaneadesi. Akademi hii ilikuwa na mtizamo wa ushuku. Akademi ya mwisho ni ile mpya. Hii iliacha ushuku na kurudia mafundisho ya Plato.

“ Akademi, japo ndizo zilikuwa wawakilishi rasmi wa falsafa ya kiplato, walishindwa kuelewa maana halisi ya nadharia ya mawazo. Kwa kuingiza mbegu za kipithagorasi na zinginezo waliutoa utamaduni wa shule ya Plato nje ya mkondo wa ukoo wake wa kiasili na wakaishi kukumbatia ushuku au ushupavu wa kung’ang’ania yote. Lolote kati ya haya lipo nje na matokeo ya kimantiki ya mafundisho ya Plato. Akademi za kiplato kwa Plato ni sawa na shule nusunusu za kisokratesi kwa Sokratesi. Muendelezo wa fikra za kiplato, hivyo hatuwezi kuuona katika akademi hizi, isipokuwa kwenye shule iliyoasisiwa na Aristoto.

Sehemu ya kumi n moja inaelezea juu ya jadiliano la Krito. Hii ni kuonyesha jinsi Plato, alivyokuwa akiandika mambo mengi kwa mtindo wa mahojiano Haya ni mahojiano kati ya Socrates na rafiki yake kipenzi Krito. Mahojiano haya yanafanyika gerezani wakati Sokrates, akiwa kifungoni.

Sehemu ya kuminambili inamjadili Aristoto. Maisha yake, tabia yake, maandiko yake, falsafa yake, mantiki ya nadharia ya elimu, falsafa ya kinadharia,metafizikia, mata/Sababishi mata, umbo/sababishi umbo,sababishi uwezo, sababishi hatima, uwepo wa Mungu, fizikia, wakati, mwendo, taalimulimwengu,taalimuviumbe, uhai, taalimuroho Uhisi, akili, hisabati, falsafa tendaji, jamaa kuu, urafiki, fadhila, fadhila ya maadili,fadhila za kiakili, siasa, na falsafa ya kishairi.

“Machache tuliyoyaona juu ya falsafa ya Aristoto, yaweza kutupa picha ya upana wa aliyoyashughulikia. Njia yake pamoja na kuheshimu mawazo ya waliomtangulia na jinsi alivyodumisha mapendeleo ya Plato katika visivyo mata na vya milele. Alisisitiza kwamba elimu dutu ya mata vyaweza kutupatia elimu ya vitu hivyo kama twaweza kusema kwamba ni vigumu kufikiria tawi la elimu ambalo liliepuka uangalifu wake hautakuwa mbali na ukweli. Ni lazima tongeze kwamba kwa kiasi kikubwa ni kutokana naye, matawi mengi ya elimu yamekuwa kutokana na uwezo wake wa kung’amua na kuelezea njia ya mawaidha ya utafiki na uthibitisho wa kifalsafa . Kutokana na hili Aristoto anaitwa baba wa mantiki.” (Uk 38).

Sehemu ya kuminatatu inajadili falsafa baada ya Aristoto. Hapa ndipo tunakutana na wanafalsafa kama Wastoa, Waepikuri, Waeklektiko na kukumbana na mabadiliko ya Sayansi na falsafa ya warumi.

“ Kifo cha Aristoto tunaweza kudiriki kusema kuwa kilichora mpaka wa mwisho wa kipindi cha dhahabu cha falsafa ya kiyunani. Kutoka kwa Thalesi mpaka kwa Sokratesi kilikuwa ni kipindi cha uasisi. Kutoka Sokratesi mpaka Aristoto, kilikuwa kipindi cha ukamilifu mkuu, ukomavu wafalsafa. Baada ya kifo cha Aristoto kilianza kipindi cha kudorora, kuporomoka na kuoza kwa falsafa. Kipindi hiki kinatawaliwa na uabudumiungu wa Wastoa, Uyakinifu waepikuri na mwisho uregevu wa bidii zote katika ukikiriko wa falsafa, uliofikia kilele chake katika ushuku mkamilifu wa Wapirho. Wakati wa ukamilifu mkuu wa falsafa, ulikuwa pia ni wakati wa ukuu wa siasa katika Uyunani. Sababu zilizosababisha mmomonyoko wa kisiasa wa wayunani, kwa sehemu Fulani zilichangia uozo wa falsafa pia.”( Uk 139).

Sehemu ya kuminanne ni Istilahi, Sehemu ya kuminatano ni Faharasa na sehemu ya Kuminasita ni Bibliografia.

V. TATHMINI YA KITABU.

Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye thathimini ya kazi hii kubwa aliyoifanya Padre Stepahano Kaombe.

Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinafundisha na kusisimua na ni changamoto kubwa.

Pili, ni lazima niungame wazi kwamba mwandishi amejitahidi kiasi kikubwa kuelezea mawazo ya falsafa kwa Kiswahili. Hiyo Kiswahili kinaweza kuimudu falsafa!

Tatu, mwandishi amefanikiwa kutuelezea kwamba wazo la falsafa ni sehemu isiyoepukika ya uwepo wa mtu. Takribani kila mmoja wetu ameshawahi kutatizwa na maswali muhimu ya kifalsafa: maisha ni nini? Je nilikuwepo kaba sijazaliwa? Je, kuna maisha baada ya kifo? Wengi wetu tuna aina ya falsafa kwa maana ya mtazamo binafsi juu ya maisha. Hata mtu anayesema kujadili matatizo ya kifalsafa ni kupoteza muda, anabainisha lililo muhimu na la thamani kwake. Hivyo, ukatao wa falsafa kwa wenyewe ni falsafa.

Nne, anafanikiwa pia anapotuelezea na kutufikisha kuona kwamba katika kujifunza falsafa, watu wanaainisha wanachokiamini na wanaweza kuhamasishwa kuwaza juu ya maswali muhimu sana. Mtu aweza kujifunza juu ya wanafalsafa waliopita ili kugundua kwa nini walifikiri kama walivyofikiri, aidha mawazo yao yana thamani gani katika maisha yao ya sasa.

Tano, mwandishi ameweza kutufanya tukubaliane naye kwamba falsafa ina athari isiyosemeka katika maisha ya kila siku. Lugha tunayozungumza inatumia uanishaji kutoka katika falsafa. Mfano tofauti ya jina na kitenzi inahusisha wazo la kifalsafa kwamba kuna tofauti kati ya kitu na tendo. Kwamba tunapouliza tofauti ni ipi, tunakuwa tunaanza tafiti ya kifalsafa.

Sita, pamoja na mafanikio yote, mwandishi amejikita kwenye falsafa ya magharibi, bila kuunganisha falsafa hii na maisha ya Mtanzania. Hakujaribu kuonyesha falsafa ya Mwafrika. Katika vitabu vyake viwili Dkt Mihanjo, anaunganisha falsafa ya kiyunani na falsafa ya Kiafrika. Ni muhimu kuonyesha umuhimu wa falsafa kwa mifano hai. Kama padre Kaombe, angefanya kama Dkt. Mihanjo, alivyofanya kitabu chake kingevutia zaidi.

Saba, Padre Kaombe, ametupatia Istilahi kidogo. Hii inapelekea kitabu kuwa kigumu kusomeka kwa sababu ya ugumu wa kutoa mawazo ya kifalsafa kwenye lugha moja na kupeleka lugha nyingine. Kwa kusoma vitabu vya Dkt. Mihanjo, itamsaidia kulinganisha Istilahi na kuibua majadiliano miongoni mwa wataalamu wa Kiswahili. Watu hawa wawili wanahitajiana kwa kujenga msingi mzuri wa falsafa katika lugha yetu ya Kiswahili.

VI. HTIMISHO

Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja ninampongeza sana Padre Stephano Kaombe, kwa kazi hii kubwa, na kwa upande mwingine ninawashauri watanzania kukisoma kitabu hili ili waweze kuchota elimu ya falsafa. Kitabu, kinaweza kusomwa na watu wote, kuanzia vijiweni hadi sekondari na vyuo vikuu. Elimu iliyojikita hapa ni muhimu kwa kila mtu. Tukumbuke kwamba Sokrates, alikuwa akifundishia vijiweni!

Lakini, kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya jitihada za kukutana na Dkt.Adolf Mihanjo, ili kwa pamoja waweze kuboresha kazi hii ya kuandika falsafa kwa Kiswahili. Ni imani yangu kwamba Padre Kaomba ana la kujifunza kutoka kwa Dkt.Mihanjo na Dkt Mihanjo, ana ya kujifunza kutoka kwa Padre Kaombe. Umoja ni nguvu!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment