UKIMYA HUU UNA MAANA GANI?

MAKALA HII LICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005

UKIMYA HUU UNA MAANA GANI?

Mbio za kumtafuta rais wa taifa letu kupitia chama cha mapinduzi, zimezalisha kimya cha kushangaza upande wa vyama vya upinzani. Ni kimya kinachotisha na kuibua maswali mengi yasiyokuwa na majibu. Nini kimetokea? Vyama hivi vimekwenda likizo au ni mbinu? Hatusikii tena habari juu ya vyama hivi kwenye vyombo vya habari. Vyomo vya habari vinapeperusha habari za wagombea wa CCM, hadi inakera, Ukishika gazeti, utakuta imepambwa na habari za Kikwete, apokelewa kwa kishindo Mtwara, Mwandosya, Kilimajaro, Babu, ashangiliwa Ngara, Salim, atembelea Shinyanga, Sumaye, anguruma Karatu nk. Hatusikii tena viongozi wa vyama vya upinzani.! Wako wapi? Wamekwenda safari nchi za nje? Hata kama ni hivyo , basi walao vyombo vya habari vitangaze kule walipo na wanachokifanya.

Ni kwamba CCM, ina nguvu za kuvifunika kiasi hicho vyama vya upinzani? Si kwamba CCM, imevinunua vyombo vya habari? Kwamba visiandike chochote juu ya vyama vya upinzani wakati wa kipindi hiki cha kumtafuta mgombea wa urais kupitia CCM! Au wagombea wenyewe wamevinunua vyombo vya habari? Wagombea wote wanazo pesa za kumwaga. Zimetoka wapi? Ka waulize wenyewe!Ninachojua nchi masikini kama Tanzania, haiwezi kuwa na uwezo wa kutumia pesa ovyo kiasi hicho! Huko nyumba tulikuwa tukisikia vyama vya upinzani vikienda sambamba na CCM. Ghafla tu, tumeaanza kukisikia chama cha mapinduzi peke yake! Ni lazima mtu mwenye uchambuzi wa akina ajiulize maswali mengi. Inawezekana kwamba na vyama vya upinzani vimenunuliwa? Au ni makubaliano ya aina Fulani? Makubaliano kwamba nafasi ya urais waachiwe CCM! Vinginevyo inakuwa vigumu kuelezea ukimya ulijitokeza mara baada ya CCM, kuanzisha harakati za kumtafuta mgombea wake.

Tume ya uchaguzi imekaa kimya! Je, nayo imenunuliwa? Mbona haikemei kampeni hizi zinazoendelea. Hizi ni kampeni za waziwazi na zimeanza kabla ya muda wake. Hili si jambo linalowagusa wanaCCM peke yao. Mbwembwe hizi zinamgusa kila mtanzania na kwa kiasi Fulani zinaathiri uamuzi wake wa Oktoba. Tuamini kwamba Tume ya uchaguzi hailioni hili? Wagombea wanatoa hotuba zilizojaa kampeni, hotuba hizi zinarushwa kwenye luninga na kwenye magazeti.Hii ni sawa? Wengine wanakuwa na mawazo kwamba wana CCM kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi ya urais ni njia ya siri ya chama cha mapinduzi kuweza kusambaza watu nchi nzima wakipiga kampeni, wanakwenda kwa tiketi ya kuwatafuta wanachama wa wakudhamini, kumbe ni njia za kufanya kampeni kimyakimya. Kila mgombea ni lazima kupata wajumbe mikoa zaidi kumi. Kwa njia hii nchi nzima inakuwa imeshambuliwa na wana CCM wa ngazi ya juu kwa kipindi kifupi. Ni njia ya kuwashawishi watu na kupandikiza mbegu ya uCCM! Ni njia ya kuhakikisha watu wanashawishiwa kumchagua rais wa CCM. Ni nchia ya pekee ya kupenyeza rushwa ya kura kabla ya wakati wake. Kwa vile wakati huu wanamulikwa kwa mwanga hafifu wa Tume ya Uchaguzi,wanaweza kupiga siasa bila ya wasiwasi wowote. Inawezekana Chama Cha CCM, kwa vile ni chama tawala kina haki zaidi ya vyama vyingine? Na vyama hivyo vinajua hivyo? Ndo maana hatusikii neno lolote la kulalamika!

Picha inayojitokeza kupitia kwenye vyombo vya habari na katika maongezi ya hapa na pale, ni kwamba mgombea atakayepitishwa na CCM ndiye rais wa nne wa Tanzania. Kila mtu sasa hivi anajadili jambo hili. Profesa Maliyamkono, alihojiwa na BBC, juzi, anakubali kwamba rais wa nchi yetu ni lazima atoke CCM. Eti rais hawezi kuibuka hivi hivi, ni lazima atoke kwenye “system”. Alisema wao wasomi na wachambuzi wa mambo ya kisiasa wana vigezo. Kufuatana na vigezo hivyo inajionyesha wazi kwamba rais atatoka CCM. Bahati mbaya Profesa Maliyamkono, hakutaja vigezo hivyo. Kwa vile tunaishi Tanzania, tunaweza kubuni vigezo hivyo. Vikitofautiana na vile vya Profesa Maliyamkono, basi atatusahihisha na kutusaidia.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazoongoza kwa rushwa na ufisadi. Hiki ni kigezo cha kwanza. Chama Cha Mapinduzi kimetawala muda wote. Kama kuna rushwa na ufisadi katika nchi hii, basi imelelewa na kukumbatiwa na CCM. Hakuna anayewajibishwa kwa tuhuma za rushwa! Kwao, rushwa si kero, ni sifa! Anayeipinga rushwa hawezi kupitishwa! Si kwamba hawezi kupigiwa kura na wananchi wanaoathiriwa na rushwa, jina likiwafikia wanaweza kumchagua, lakini hatapitishwa na CCM. Kigezo cha kwanza hicho! Anayekipinga mkono juu!

Tanzania, ni kati ya nchi zilizoukumbatia Utandawazi, Ubinafsishaji na Soko huria. Mwenye mawazo tofauti na haya, ni adui wa umma? Hapana! Ni adui wa Vigogo! Adui wa Umma, ni yule anayekumbatia Utandawizi na Soko la Kulia! Tumesikia mengi kuhusu mifumo hii. Kwa wale walioushikilia mrija na wana uwezo ku kufyonza na kunyonya, mifumo hii ni mizuri kwao. Kwa wale wanaofyonzwa au kunyonywa, mifumo hii ni sawa na mauti kwao. Dunia ya leo inatawaliwa na vinara wa Utandawazi, Ubinafishaji na Soko huria. Tunajua jinsi CCM, inavyoimba wimbo wa mifumo hii pia ni sera yake. Pia tunaujua msimamo wa vyama vya upinzani unavyopingana na ule wa CCM, kuhusiana na mifumo hii ya unyonyaji. Bila kuungwa mkono na watawala wa dunia, ni vigumu mtu kuwa rais wa taifa letu. Kigezo cha pili hicho. Anayepinga, mkono juu!

Tanzania, ni miongoni mwa nchi zinazofuata masharti yote ya Benki ya Dunia na IMF, bila swali wala kujadiliana. Na wakati mwingine, Tanzania, inayashika masharti hayo kwa uaminifu zaidi ya wale waliyoyatunga! Uaminifu huu unaongozwa na viongozi wa CCM. Ukweli kwamba hakuna nchi ya dunia ya tatu iliyofuata masharti ya mashirika ya ya kifedha duniani ikafanikiwa kuendelea na kuupiga umasikini mgongo, haupingiki! Tunajua bila kuungwa mkono na mashirika haya ya kinyonyaji mtu hawezi kuingia ikulu. Kigezo cha tatu. Anayepinga, mkono juu!

Wawekezaji, wamewekeza. Wanataka usalama wa “mali” zao. Wamelimdwa vizuri wakati wa kipindi cha rais Mkapa. Ni faida kwa taifa au ni hasara, hiyo ni kazi ya historia. Sasa hivi tunaangalia ni mtu gani wa kuendelea kuwalinda ili wavune. Wavune, salama bila kusumbuliwa. Vyama vya upinzani, havina urafiki wa karibu na watu hawa. Kwa nguvu zote, kwa pesa zote… pesa ambazo tumeanza kuziona wakati wa kumtafuta mgombea wa CCM, watahakikisha kipenzi chao anaingia Ikulu. Kigezo cha nne. Anayepinga, mkono juu!

Tanzania, hatuna historia kama ya Zambia. Mwalimu, aliachia kiti akaendelea kuishi vizuri hadi mauti yalipomkuta. Mzee Mwinyi, anaishi vizuri bila kusumbuliwa na mtu yeyote, Mzee Aboud Jumbe, anaishi kwa starehe naye Komando, hana mtu wa kumgusa. Hivyo hivyo na Rais Mkapa, akiachia kiti, aishi vyema kule Lushoto. Kigezo cha tano. Anayepinga, mkono juu!

Sera ya CCM, ni kupambana na umasikini. Sera hii ni maneno kuliko vitendo. Mafanikio yake ni kwamba imepanua ufa mkubwa kati ya walionacho na wasiokuwanacho. Matajiri, ambao wengi wao ni viongozi wa CCM au marafiki zao, wametajirika zaidi: Wana majumba makubwa, magari yakifahari, watoto wao wanasoma nje ya nchi, wakiugua wanatibiwa nje ya nchi, wana hisa kwenye karibu kila kampuni inayowekeza hapa, wana mashamba makubwa, wana mifugo na mali nyingine nyingi. Kwa upande mwingine hospitali hazina madawa,kipato cha watu kinapungua kila kukicha, nauli za dalaladala zinapanda, umeme unakatika ovyo,maji hayapatikani. CCM, inaendelea kushika utamu. Kigezo cha sita! Anayepinga, mkono juu!

Kichwani nilikuwa na vigezo saba. Lakini washirikina wa kizungu, wanasema namba ya saba ina mkosi. Sitaki mkosi uikumbe nchi yetu. Atakaye taka kuongeza vigezo aanze na namba nane! Ingawa katika vigezo vyangu nimesahahu kutaja kitu Fulani: Wale wote waliojitokeza kuwania urais kupitia CCM, vi viongozi wa muda mrefu. Wote wameshiriki kuiandika historia ya Tanzania. Iwe historia mbaya ama nzuri kuna mkono wao. Watakuja na lipi jipya? Yale waliyoshindwa kuyatekeleza kwa kipindi cha miaka 20 – 30, iliyopita wataweza kuyatekeleza kwa kipindi cha miaka 5? Kama Tanzania, inavumilia na kuindekeza rushwa, nao wameshiriki. Kama ufa kati ya walionacho na wasiokuwanacho umeongezeka, nao wameshirki! Watanzania ni wafungwa, hawatoki nje ya nchi yao. Hawa wanaogombea watakuwa wameshiriki wa njia moja ama nyingine kusababisha hali hii ya kifungo cha watanzania. Ukilinganisha na Uganda na Kenya. Kampala, hata machinga anapanda ndege kwenda Ulaya, Uarabuni na Asia, kufanya biashara. Mjini Nairobi, vilevile watu wanatoka na kuingia. Dar-es-salaam, wanaotoka ni wahindi, viongozi wa serilikali na Chama. Kwenye mashirika ya kimataifa ni nadra kumkuta mtanzania. Mahakama ya kimataifa inayosikiliza kesi za mauaji ya halaiki nchini Rwanda, iliyo Arusha, pamoja na kwamba ipo hapa Tanzania, wafanyakazi wengi ni wa kutoka nchi za nje. Kwanini mlango wetu wa mahusiano ya kimataifa umebaki umefungwa? Tanzania iliongoza mapambano ya ukombozi barani Afrika. Dar-es-salaam kilikuwa kituo na kitovu cha mapambano. Milango ilifunguliwa wageni waingie, hadi leo hii milango imefunguliwa kwa wageni, kiasi tumeanza kuingiza hata mibaka uchumi, lakini milango imebaki imefungwa kwa wenyeji wasitoke! Hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea kwa mtindo huu wa kuwafungia watu wake wasitoke nje. Bahati nzuri tulikuwa na katibu wa nchi huru za Afrika kutoka Tanzania. Ameshikilia nafasi hiyo kwa muda mrefu. Bahati mbaya bahati hii haikusaidia kuifungua milango ya Tanzania. Ni kwanini? Je, hiki nacho ni kigezo? Hapana! Sitaki kuitaja namba saba, ni balaa ni mkosi mtupu! Anayepinga, mkono juu!

Ni imani yangu kwamba Profesa Maliyamkono, atakuwa na vigezo vingine vingi vya kuongeza? Au atapunguza hivi nilivyovitaja. Vigezo vyote nilivyovitaja havina lengo la kumsaidia mtanzania. Havina lengo na kuleta maendeleo katika taifa letu. Ni vigezo vya kudumaza fikra za watu na kuendeleza ukoloni mambo leo. Ni vigezo vya kushangilia Uhuru wa Bendera. Vigezo hivi vinadidimiza uhuru wa fikra na dhana nzima ya ukombozi wa Mtanzania.

Baadhi ya vyama vya upinzani wanaouona ukweli huu na wamekuwa wakipiga kelele. Jambo linaloshangaza, tunapofikia hatua ya kuamua wanakuwa bubu na kuingia mitini. Ndo maana mtu unaweza kuwa na kishawishi kusema wamenunuliwa. Kwanini vyama hivi vimenywea wakati wa kipindi hiki CCM, inapomtafuta mgombea?

Mbona vyama hivi havihoji mbwembwe na pesa zinazotumika wakati huu. Wagombea ambao ni wafanyakazi wa serikali na chama wanapata wapi pesa za kukodi ndege, kuwasafirisha waandishi wa habari na wapambe. Vyama vya upinzani visipohoji jambo hili ni nani atalihoji? Kama vimekata tamaa na kukubali kwamba rais ni lazima kutoka CCM, basi havina umaana wowote wa kuendelea kuwepo. Ni bora ijulikane wazi kwamba Tanzania, ni nchi yenye siasa ya chama kimoja. CCM oyee, CCM juu juu zaidi, CCM, ina wenyewe! Atakayepita akumbuke kunipatia Wilaya au mkoa! Mcheza kwao hutuzwa!

Na,
Padri Privatus Karugendo

0 comments:

Post a Comment