DK SALIM KASEMA UKWELI

Saturday, March 19, 2005


DK SALIM KASEMA UKWELI

Katika mahojiano yaliyofanywa na Balozi Salim na Livingstone Ruhere, wiki iliyopita, na kutolewa kwenye gazeti hili toleo Na 597, ukweli ulijitokeza: “Maendeleo hayaletwi tu na kiongozi wa nchi, itakuwa ni makosa kufikiria kwamba Rais ndiye anayeleta maendeleo. Rais anakuwa mtumishi mkuu wa nchi na kwa maana hiyo ni kiongozi mkuu. Kwa hiyo, uongozi wake unasaidia kuleta maendeleo. Lakini maendeleo kwa ujumla huletwa na wananchi wenyewe na mazingira mbalimbali ndiyo yanayowezesha ama kuleta maendeleo au kudumaa kwa maendeleo”.

Huu ni ukweli mtupu aliousema Dk.Salim. Maendeleo yanaletwa na watu wenyewe, uongozi unasaidia kuonyesha dira, kutoa nyenzo kama elimu, mitaji, usalama na kuwaonyesha watu njia ya kuelekea kwenye maendeleo. Kwa maneno mengine, ni lazima kiongozi awe anaifahamu njia inayoelekea kwenye kitu tunachokiita maendeleo. Pia ni lazima kiongozi awafahamu vizuri watu anawaongoza kuelekea maendeleo. Bila kuwafahamu watu vizuri kuna hatari ya kuwaambia wale keki wakati hawana uwezo wa kununua mkate, au ukawanunulia ndege wakati hakuna viwanja vya ndege, hawana baiskeli wala magari ya kusomba mazao yao kwenda kwenye soko.

Profesa Chachage, anasema watanzania wanapendelea biashara ya kuuza pombe, bar ni nyingi kuliko maktaba na maduka ya vitabu. Maana yake ni kwamba watanzania hawana jadi ya kujisomea vitabu. Bila kulifahamu hili, kiongozi atajenga maktaba na kuanzisha maduka ya vitabu, matokeo yake vitabu vitafunikwa kwa vumbi! Ni watanzania wangapi wanasoma kitabu kimoja kila mwaka? Ni viongozi wangapi wa serikali wana tabia ya kujisomea vitabu? Hawana muda, wana kazi nyingi, lakini muda wa moja baridi, moja moto na wakati mwingine kukesha wakinywa, unapatikana!

Naye Bwana Jenerali Ulimwengu, anatoa ushuhuda kwamba hakuna nchi yoyote ile iliyoendelea bila ya watu wake kusoma vitabu. Anasema mwenye mfano autoe. Kama wewe unao, utoe ili bwana huyu tumpatie jina la mzushi na mwongo!

Bwana Bubelwa Kaiza, mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la ForDia, anasema ukisafiri kwa gari kutoka Dar, kupitia Nairobi – Kampala-Bukoba, utagundua tofauti zilizopo kati ya nchi hizi tatu za Afrika ya Mashariki. Tofauti ya kwanza ni mzunguko ule wa safari ya kwenda Bukoba, mtu akalazimika kupitia miji yote mikuu ya Afrika mashariki, si kwa kutaka, na wala si matanuzi, bali ni kwa kulazimishwa na hali halisi. Barabara zetu mbovu! Hakuna anayelalamika. Hao ndio watanzania. Wanavumilia kila kitu! Jadi yao ni Amani na utulivu!

Lakini tofauti kubwa aliyoiona Bwana Bubelwa Kaiza, ni wingi wa Bar unaojitokeza kuanzia Ubungo, Kibaha, Chalinze, Mombo, Moshi, Arusha hadi Namanga. Anasema ukitupa jicho unakutana na “Utulivu Bar”, “Safari Bar”, “Kivulini Bar” nk. Ukivuka mpaka wa Namanga, hali inaanza kubadilika. Ukitupa macho, utakutana na mashamba makubwa ya mazao na mifugo, hatua chache utakutana vito vikubwa va mafuta vimepangana na utitiri wa viwanda ambavyo karibu bidhaa zake zote zinauzwa Tanzania. Ukivuka Busia kuingia Uganda, hali inabadilika. Inakuwa hali ya biashara iliyoendelea, kila kitu kinauzwa pembezoni mwa barabara kwa hali ya kisasa. Vitu vinafungwa kwa ubora unaokubalika, hata kama ni mguu wa kuku utakuwa umeandaliwa vizuri kiasi cha kumtamanisha mteja. Lakini hasa linalojitokeza zaidi ni shule. Ukitupa jicho utakutana na “St.Mary High School”, “Mbagatuzinde College of Technology”, “Martyrs University”. Kutoka Busia hadi Mutukula utaona shule za misingi, sekondari, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu. Watanzania wanawapeleka watoto wao kusoma Uganda. Elimu sasa kwa Uganda, ni kitegauchumi kizuri. Wanaingiza pesa za kigeni kwa kuiuza elimu. Safari ya Bwana Bubelwa Kaiza, inakamilika anapovuka mpaka wa Mtukula, kuingia tena Tanzania! Hafidhi ni ileile: “Nyegerea waitu, pombe zote kuanzia rubisi hadi bia zinapatikana hapa”, “Bwikizo, bar ya pombe za kienyeji”, “ Garden Bar” “Buhumuliro- poza kiu na kupata nyama choma” nk. Hao ndio watanzania, wana utulivu na amani, moja baridi moja moto na nyama choma, maisha yanaendelea. Hakuna Matata!

Mbali na kutokuwa na jadi ya kujisomea, kujishughulisha na miradi mikubwa ya kujenga uchumi kama kuanzisha mashamba makubwa na viwanda, watanzania hawana utamaduni wa kufuata muda. Huu ni ugonjwa ulioenea karibu kila sekta. Watu wanachelewa kazini na wakifika kazini wanatoka kidogo. Huu msamiati wa “katoka kidogo” ni wa watanzania. Huwezi kuukuta popote pale ambapo nchi imeendelea au inapigana kuendelea. Ugonjwa huu umeota mizizi kuanzia awamu ya kwanza ya uongozi wa taifa letu hadi leo hii. Bwana Mrema, alijitahidi kupambana na ugonjwa huu, lakini aligonga mwamba. Wataalam wa mambo ya uchumi wanatuelezea kwamba bila kufuata muda na kufanya kazi kwa masaa mengi, maendeleo ni ndoto. Mashirika mengi na makampuni tuliyoyakaribisha kuwekeza katika nchi yetu, jambo ambalo tunajivunia kwamba ni hatua ya kuelekea maendeleo, hayawezi kukubali kuwaptaia kazi watu wasiofuata muda. Matokeo yake, Waganda,Wakenya, Wazambia na Wasouth, watapata kazi na kuwaacha watanzania vijiweni. Haya ndiyo maendeleo ambayo Dk Salim, anasema yanaletwa na wananchi wenyewe?

Tunaambiwa kwamba hakuna nchi iliyoendelea bila kutumia lugha yake. Kama ipo ninaomba nipatiwe mfano ili nielimike zaidi. Watanzania hawaipendi lugha yao. Mikutano ya wasomi, hata kama hakuna mtu kutoka nje ya nchi, lugha inayotumika ni Kiingereza. Ili mtu aonekane kasoma na anajua jambo ni lazima atumie lugha ya kuazima kiingereza- bila kujali ni Kiingereza chenyewe au ni cha “ze” na “zati”. Mtu wa maana, aliyeendelea ni yule anayeongea Kiingereza. Uzembe wetu watanzania, hakuna hata jitihada za kuwaandaa walimu wa kufundisha hicho Kiingereza. Pesa zinazotumika kufanya ziara za nje zisizo za lazima zingetumika kuwapeleka vijana Uingereza kujifunza lugha hiyo ili wakija hapa waifundishe vizuri. Hao ndio watanzania wanaotaka kutumia lugha ya kuazima kuleta maendeleo. Watakuwa ni kwanza katika historia!

Sasa hivi kuna ushindani mkubwa. Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni changamoto kwa watanzania. Huwezi kushindana ukiwa kifungoni! Waganda, milango yao ilifunguliwa siku nyingi. Bidhaa tunazozinunua Uganda, zinaletwa na wamachinga kutoka Asia na Uarabuni. Tunazinunua kwa bei ya juu ambavyo kama wamachinga wetu wangekwenda wenyewe Asia, Ulaya na Uarabuni, vitu hivyo tungevipata kwa bei pungufu. Waganda, wanauza ndizi hadi makuti ya migomba Ulaya, watanzania tumelala usingizi! Hakuna nchi inayoweza kuendelea kwa kuwafungia watu wake ndani ya nchi. Je, Dk. Salim, analiona hili? Na wengine wanajitokeza kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi wanaliona hili? Wengine wanasema wataendeleza yale yaliyopo! Kuendeleza kuwafungia watu kutotoka nje ya nchi? Kuendeleza ya kuwadumaza watu?

Ili aweze kujiweka kwenye nafasi ya kukubalika zaidi, Dk.Salim, angejitahidi kuelezea ni kwa kiasi gani kukaa kwake Adis, kama katibu wa OAU, kulijenga mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika. Ni wafanyabiashara wangapi wa Kitanzania walianzisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Ethiopia kwa ushawishi wa Dk.Salim. Je, alipokuwa Balozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Tanzania ilinufaidikaje? Milango ya Tanzania ilifunguka? Watanzania walipata nafasi ya kutoka na kusoma nchi za nje, Watanzania walifanya biashara nchi za nje. Ni watanzania wangapi waliingia kwenye mashirika ya kimataifa au ya Umoja wa Mataifa kupitia nyuma ya mgongo wake? Mchango wake ulikuwa ni upi kwa kipindi hicho? Haya yangemjenga zaidi kuliko kuongelea yale yaliyofanywa na marais waliotangulia.

Mfano Dk.Salim, anasema: “ Awamu ya kwanza ilisaidia sana kuimarisha misingi ya taifa letu, maadili ya taifa letu, umoja wa taifa, mshikamano wa taifa, lakini na pia kujaribu kuwafanya Watanzania wajione kwamba ni taifa huru.” Hili halina upinzani. Ni imani yangu kwamba kila Mtanzania analijua hili. Na wala hatuwezi kumpima Dk.Salim, kwa hili. Tunachotaka ni jinsi yeye anavyowafahamu watanzania na kufahamu njia wanayotaka kupita ili awaongoze vizuri bila kuwatupa shimoni!

Anaendelea kusema kwamba: “..Jambo kubwa sana la Mzee Mwinyi ni kuimarisha demokrasia katika nchi yetu. Chini ya uongozi wake, Tanzania iliingia katika mfumo wa vyama vingi, pamoja na kwamba mpaka hivi sasa hatujafikia kiwango ambacho kila mmoja akatosheka, lakini ukweli ni kwamba misingi madhubuti imeanza kuwekwa na imewekwa chini ya awamu ya pili”.
Pia haya tunayajua. Yako mbele yetu na hakuna ambaye atamnyoshea kidole Dk.Salim, kwa haya. Swali, ni je kutokana na hayo anaweza kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuwafahamu watanzania na kufahamu njia wanayotaka kupita na akawaongoza vizuri bila kuwatupa shimoni.

Kuhusu awamu ya tatu anasema hivi:
“Awamu ya tatu imeshughulikia zaidi mambo ya uchumi na imefanya kazi nzuri. Mambo ya msingi ya kiuchumi yamewekwa”.
Hili ni swala la kitaalam zaidi. Wachumi wetu watatueleza. Uchumi umekwenda mbele au umerudi nyuma. Ukiangalia kwa macho unaona umasikini, kule Ngorongoro watu sasa wanakufa kwa njaa. Iweje taifa tajiri kama la kwetu ambalo uchumi wake unakua watu wafe kwa njaa. Hapo hatujataja watu wanaokufa kutokana na magonjwa yanayotibika. Hatujaongelea ukosefu wa huduma muhimu kama maji, umeme, barabara, mishahara midogo, ukosefu wa madarasa. Kwani kinachoonyesha uchumi mzuri ni nini? Takwimu au maisha bora ya watu? Au Taifa kuwa na ndege ya rais bora kuliko zote katika bara la Afrika? Awamu ya tatu, inaweza kumfanya Dk.Salim kujiona yuko katika hali nzuri ya kuwafahamu watanzania na kufahamu njia wanayotaka kupita na akafanikiwa kuwaongoza vizuri bila kuwatupa shimoni?

Dk.Salim, alilazimika kutaja awamu zote tatu baada ya kuulizwa swali hili: “ Ukiangalia bado watu wengi ambao wametawala ni watu wa umri mzuri na wenye uzoefu mzuri. Lakini maendeleo ya nchi hii bado yamekuwa hayasongi mbele, nini kinaweza kufanyika sasa.”

Labda swali hili lingesema hivi: “ Kwa vile maendeleo ya nchi hii hayasongi mbele, ni kiongozi wa aina gani tunayemhitaji ili aweze kuwaongoza watu kusonga mbele kuyaelekea maendeleo?”.

Kama Dk.Salim, anafikiri yeye ndiye. Ni vizuri. Kazi aliyonayo ni yeye kujihoji na sisi tukamhoji kama kweli anawafahamu watanzania na kufahamu njia wanayotaka kupita? Hili ni jambo la kawaida na wala halina kumpenda mtu au kumchukia mtu, wala si kupiga debe au kumsagia mtu. Watu wote walio makini ni lazima wapitie hatua hii, kuliongoza taifa si mchezo wa pata potea.

Awamu zote tatu zilizopita Dk.Salim, amezishiriki kikamilifu. Kama zimefanikiwa na yeye ni sehemu ya mafanikio hayo. Kama zimevurunda, na yeye hawezi kukwepa lawama. Mtihani wake mkubwa ni kuwaonyesha watanzania mchango wake, yeye kama Salim, alivyoshiriki kufunga ama kufungua milango ya watanzania kuwa na ushirikiano wa kimataifa, kufanya biashara, kusoma, kuendeleza vipaji vya michezo kama mpira wa kulipwa nk. Ukweli uliombele yetu ni kwamba milango ya Taifa letu imeendelea kufungwa kwa awamu zote tatu. Wale wanaofanikiwa kutoroka kwa kupitia dirishani, hawapendi kurudi nyumbani kulitumikia taifa letu.

Tanzania, ina wataalam wengi wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi. Wengi wao wamepitia dirishani! Hawa wakikubali kurudi wanaweza kusukuma maendeleo ya taifa letu. Swali ni je, ile hali iliyowafanya wapitie dirishani imebadilika? Wakirudi watasikilizwa? Watapata mshahara wa kukidhi mahitaji yao au wataendelea kufuga kuku na nguruwe kama wafanyavyo maprofesa wazalendo wa chuo kikuu cha Dar-es-Salaam? Wataendelea na maisha yale yale ya kutimuliwa vumbi na mashangingi ya watu ambao hawakuingia darasani lakini wameshikilia utamu wa Chama?

Anachosema Dk.Salim, ni ukweli mtupu. Maendeleo hayaletwi na Rais, yanaletwa na wananchi wenyewe. Lakini rais, kama kiongozi, ni lazima awe na kipaji cha uongozi, kipaji cha kuwafahamu vizuri watu wake, kipaji cha kujifahamu yeye mwenyewe, udhaifu wake na uimara wake, kipaji cha kufahamu maana ya neno “maendeleo” na afahamu vizuri njia wanayopitia watu wake kiasi hata akifumba macho kwa bahati mbaya, yeye na taifa zima hawezi kutumbukia shimoni!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment