HEKIMA NA UCHAGUZI

MAKALA HII ILICHAPISHWA KATIKA GAZETI LA RAI 2005.

HEKIMA HII ITAENDELEA HADI UCHAGUZI MKUU?

Hapana shaka kwamba vikao vya CCM vilivyomalizika tarehe 4.5.2005, kule Dodoma viliongozwa na hekima, busara na fikra pevu. Watu wengi walitegemea CCM, isambaratike! Hili halikutokea! Wengine walitegemea fujo kwenye vikao hivyo, hata na wanaCCM wenyewe walikuwa na wasiwasi huo hadi Mheshimiwa Mapuri, akatangaza kwenye vyombo vya habari kwamba wamejizatiti ndani ya chama na kwa kutumia vyombo vya dola kukabiliana na fujo zitakazojitokeza. Fujo hizo hazikujitokeza! Hadi leo hii ninapoandika makala hii, fujo hizo hazijajitokeza popote. Tunachokisikia ni sherehe na maandamano ya kumpongeza Kikwete, mgombea mwenza na Rais Karume.

Habari kutoka Mwanza, zilizotolewa na gazeti dada la Mtanzania zinasema: “Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wamewasili Mwanza na kupata mapokezi ya kihistoria kutokana na kuchaguliwa kwa Jakaya Kikwete kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho….. Baada ya kupokewa, wajumbe hao walivishwa mashada ya maua kama ishara ya ushujaa kutokana na uamuzi wao wa kumpigia kura Kikwete ambayo inaaminika kwamba huo ulikuwa ndiyo msimamo wa wakazi wa Kanda ya Ziwa….Baadhi ya watu walisikika wakisema kwa kupaaza sauti kwamba ole wao kama wajumbe hao wangeliwasaliti kwa kuwaletea mgombea asiyekuwa chaguo lao”(Mtanzania, Jumamosi, Mei 7,2005).

Msimamo wa Rais Mkapa, haukujulikana kabla ya hotuba yake ya kuufungua mkutano mkuu. Hakuonyesha kuwa na upande wowote. Ni imani yangu na imani ya watu wengi kwamba hotuba aliyoitoa Rais Mkapa, wakati wa kufungua mkutano mkuu, aliitoa kwa uhuru bila ya shinikizo lolote lile kutoka kwenye kundi la watu na kwenye nafsi ya moyo wake. Chaguo la mtu aliyemtaka alilitunza moyoni mwake. Mtu msiri sana huyu! Ilikuwa siri kubwa ambayo watu wengi hawakuifahamu. Wasi wasi ulitanda ndani na nje ya chama cha CCM, kwamba rais, akimuunga mkono mtu asiyekubalika, basi chama kingemeguka. Wengine wakaanza kusema kwamba utabiri wa Mwalimu Nyerere, kwamba upinzani wa kweli utatoka CCM, ulikuwa unaelekea kutimia. Usiri wa Rais Mkapa juu ya mgombea anayemtaka ulisaidia sana. Hizi ni kati ya sifa anazojizolea anapoelekea mwishoni mwa utawala wake. Hekima, busara na fikra pevu alizozionyesha kwa kumtumza moyoni mwake mtu anayependa arithi kiti chake kwa tiketi ya CCM, bila kukigawa chama ,zichipuke na kukua hadi uchaguzi mkuu.

Hatukusikia fujo kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CCM kule Dodoma, mbali na uvumi kwamba Mzee Malecela, alihoji hapa na pale kuhusu jina lake kutupwa au kuombwa aendelee kuwa tingatinga! Labda hii ni siri za chama! Lakini kwa vile kamati kuu iliweza kuwateua watu watano kati ya kumi na mmoja waliokuwa wameomba kugombea kiti cha urais na kuwapendekeza kwenye mkutano wa Halmashauri kuu bila kelele zozote, tunalazimika kuamini kwamba mambo yalikuwa shwari kwenye kamati kuu. Halmashauri kuu iliwachagua watatu kati ya watano kwa kura tulizotangaziwa. Hatukuzikia malalamiko yoyote. Mkutano mkuu ulirushwa kwenye luninga. Tulijionea wenyewe jinsi utulivu, demokrasia, hekima, busara na fikra pevu vilivyoutawala ukumbi wa Chimwaga.

Hali ya Chimwaga, iliwachagaza wageni kutoka nje ya Tanzania. Mfano Katibu mkuu wa chama kinachotawala kule DRC, alishangaa sana kuona kiongozi aliyemadarakani, Rais Mkapa, anaendelea “kuwachunga” (Kuwatunza) viongozi waliomtangulia. Alishangaa kuuona Mzee Mwinyi, bado anapewa nafasi na heshima kwenye chama na bado “anachungwa” vizuri na Rais Mkapa. Dr. Salimin, naye bado anapewa heshima na “kuchungwa” vizuri na Rais Mkapa. Hata Mama Maria Nyerere, naye “anachungwa” vizuri. Ili aweze kuelezea vizuri ukomavu wa kisiasa wa Tanzania, kule kwao DRC, Katibu huyo kutoka DRC, aliomba ruhusa ya Rais Mkapa, ili “akamate picha” (kupiga picha) na Mama Maria Nyerere, awaonyeshe kule kwao kwamba hata na Mke wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, bado anapata heshima ndani ya chama cha CCM na kwenye taifa zima.

CCM, imeonyesha ukomavu wa kisiasa na demokrasia ya juu si hapa tu bali hadi nchi jirani na za mbali. Pamoja na pongezi hizi zote, wasi wasi ni je, hekima, busara, demokrasia na fikra pevu vilivyojitokeza kule Dodoma, vitaendelea hadi uchaguzi mkuu? Tutegemee kuwa na uchaguzi wa haki, huru na amani? Uchaguzi usiokuwa na vitisho, rushwa, upendeleo, ukabila na udini? Uchaguzi usiokuwa na udanganyifu – kura zipigwe, zihesabiwe bila kupinda? Kwa vile CCM, ndicho Chama tawala, ndicho chama chenye dola na ndicho kinachosimamia uchaguzi mkuu, kitatuvusha salama kwa kuzingatia ukomavu wa kisiasa uliojionyesha Chimwaga na kushuhudiwa na dunia nzima? Majigambo haya ya kushinda kwa kimbunga na tufani la tsunami yana busara na hekima ndani yake?

Majigambo haya yakitamkwa na watu wenye uelewa mkubwa na waliokomaa kisiasa, wazalendo na wenye vision, hayana shida. Lakini yakidondoka mikononi, masikioni na akilini mwa washabiki na wapiga debe wa CCM, bila ya kuchujwa itakuwa tsunami ya kweli ndani na nje ya chama!

Tunaweza kulijadili hili kwa pande zote mbili. Ndani ya chama cha mapinduzi na nje ya chama hicho. Tukianzia ndani ya chama: Hotuba ya Mheshimiwa Rais Mkapa, yenye hekima na busara, wakati wa kufungua mkutano mkuu, iliweka bayana kauli mbiu: Ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya! Hakusita kusema wazi kwamba asilimia kubwa ya wapiga kura ni vijana. Hivyo, ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya ni lazima isukumwe na vijana! Hotuba hii ilimaliza kimya na usiri wa Rais Mkapa, juu ya mtu amtakaye kuichukua nafasi yake ndani ya chama cha mapinduzi.

Je, kigezo hiki cha vijana kitachukua mkondo wake hata kwa kuwasimamisha wabunge na madiwani? Wabunge wakongwe kama Mheshimiwa Sr George Kahama, watakubali kuwa tingatinga kama alivyokubali kufanya Mheshimiwa Mzee Malecela? Watakubali kukaa pembeni na kuwashauri vijana wa CCM?

Je, upepo huu wa vijana kushika hatamu utakiacha salama chama cha mapinduzi? Je vijana na wazee watashirikiana kumsaidia Kikwete na kuisaidia Tanzania? Au sasa ndio siri zote za CCM zitafumuka, kashfa za uongo na za kweli kusambaa kwenye magazeti na kuwa silaha kubwa ya vyama vingine vya siasa kwa lengo si kuimaliza CCM, bali kuwakwamisha vijana na kuleta vurugu katika taifa zima!

Mzee wa Dodoma, mwenye umri wa miaka 100, ambaye ni kati ya waasisi wa CCM, hakuipenda hotuba yote ya Rais Mkapa, ya kufungua Mkutano mkuu. Alipohojiwa na TVT, mzee huyu alisema Rais, alikosea kuwatanguliza vijana. Ni imani yangu na wale wote wanaojali kwamba mzee huyu alikuwa anaongea kutoka moyoni na bila unafiki wowote. Alisema ni lazima wazee watangulie na vijana wafuate nyuma. Wakati anahojiwa matokeo ya uchaguzi yalikuwa hayajatangazwa. Nina mashaka makubwa kama mzee huyu alifurahishwa na uchaguzi wa Kikwete! Inawezekana mzee huyu anawakilisha maoni ya wazee wengi wa nchi yetu ambao ni hazina kubwa. Inawezekana pia mzee huyu anayawakilisha maoni ya wale walioichukulia hotuba ya Mheshimiwa Mkapa, kuwa usaliti mkubwa kwa wazee wa chama wasiopenda mabadiliko na wanafikiri Chama Cha Mapinduzi, ni mali yao! Inawezekana pia kwamba mzee huyu ni sauti ya wale wanafiki ambao hawakupokea uchaguzi wa Kikwete, kwa furaha na wanaendeleza mapambano ya chini kwa chini!

Alichosema mzee wa Dodoma, ni ukweli. Ni lazima wazee wawe mbele. Ndiyo maana CCM, iliwaweka mbele Mzee Mwinyi, Mzee Kawawa, Mzee Kingunge, Mzee Dr Salmin na Mzee Malecela. Bila wazee hawa CCM, ingesambaratika! Kuwa mbele haina maana ya kushika madaraka na kufanya kazi za siku kwa siku. Kuwa mbele ni kushika taa na kuonyesha njia. Kuwa mbele ni kutoa ushauri wa kizalendo, ni kuamsha fikra pevu, ni kuambukiza hekima na busara!

Tukibaki ndani ya chama. Je demokrasia iliyojionyesha pale Chimwaga, itatumika wakati wa kuwapendekeza wabunge na madiwani? Rushwa, upendeleo, ukabila, udini vitathibitiwa? Uongozi wa CCM kwenye ngazi ya Kata, Wilaya na Mkoa, utaweza kuisimamia demokrasia ya kweli? Watu wasiokuwa na pesa, lakini wana vipaji, wana ari mpya, kashi mpya na nguvu mpya, wataweza kupenyeza?

Upande wa pili, nje ya chama cha Mapinduzi. Rais Mkapa, amejijengea jina kwa kuongoza vikao vya CCM, kwa amani na utulivu bila Mwalimu. Je, sifa hii ataibeba hadi mwisho? Atahakikisha vyama vyote vya siasa vinapata nafasi sawa ya kujitangaza na kuwashawishi wapiga kura? Maana kama demokrasia imekomaa ndani ya CCM, ni lazima ikomae ndani ya nchi nzima. Rais wa nchi, si rais wa chama, bali ni rais wa nchi nzima. Sifa zake ni lazima ziliambukize taifa zima!

Zanzibar, si shwari. Upinzani uliochipuka na kufifia dhidi ya Rais Karume, ni fukuto. Hatuwezi kujituliza kwamba Chimwaga, imetibu na kupoza fukuto. CUF, inaongeza nguvu na nia ya kutorudi nyuma! Bila busara na hekima, kuna hatari ya kushuhudia zaidi ya yale yaliyotokea 2001.
Kama nilivyosema hapo juu, watu walitegemea CCM, isambaratike mwaka huu, walitegemea fujo kwenye mkutano wa Chimwaga, lakini hekima, busara na fikra pevu vimekuwa kinga. Sasa hivi kuna watu wanasubiri Tanzania, isambaratike wakati wa uchaguzi mkuu, wanasubiri fujo na umwagaji damu. Mzigo mkubwa vinatupiwa vyama vya upinzani hasa chama cha CUF, kwa upande wa Visiwani. Si kweli kwamba vyama vya upinzani havipendi amani. Si kweli kwamba vyama vya upinzani vinatamani kumwaga damu. Tatizo ni ukomavu wa kisiasa kwa pande zote mbili. Hakuna wa kumlaumu mwingine! Hekima, busara na fikra pevu isiponyauka na kukauka, ikiendelea kuota kwa afya, wenye nia mbaya watashangaa sana kuiona Tanzania, ikipeta!

Mfano mzuri ni uchaguzi wa Kikwete, ingawa vyama vya upinzani vinajipanga kupambana naye vilivyo, vinamkubali na kuipongeza CCM kwa chaguo hilo. Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamesikika wakisema kwamba CCM, ingemchagua mtu mwingine, kinyume na Kikwete, basi upinzani ungeichukua nchi kilaini!

Wazee wetu wa CCM, wazee wetu wa vyama vya siasa kama mzee Mtei, Makani, Mapalala na wengine, wazee wetu wa dini, wazee wetu wasiokuwa na vyama wala dini wakishikamana , wakawa mbele ya vijana wakashika taa na kuonyesha njia, Tanzania, itapeta na kuendelea kuwa kisiwa cha amani. Kinyume na hapo ni hatari kubwa. Wakati huu wa kuelekea uchaguzi ni wa kuomba kwa nguvu zote. Tuombe sote, na kushikamana kwa moyo wa kizalendo, tulijenge taifa letu kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment