HIZI PESA ZINATOKA WAPI?

MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

HIZI PESA ZINATOKA WAPI?

Si jambo la kutilia shaka tena kwamba uchaguzi mkuu ujao utatawaliwa na pesa kama chaguzi nyingine zilizopita. Gazeti hili toleo lililopita 593,ukurasa wake wa kwanza kulikuwa na maneno haya:
" Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekubaliana kuhusu ratiba ya uchukuaji fomu za kuwania urais kwamba utaanza rasmi tarehe mosi mwezi ujao, nguvu ya makundi ndani ya chama hicho imefanya Mwenyekiti wake, Rais Benjamin Mkapa atoe karipio kali kutokana na hali inayozidi kuwa ngumu kuhusu siasa za makundi na matumizi ya pesa kutaka urais, Rai imeelezwa."

Baadhi ya wanaCCM wanasema wazi bila woga kwamba mtu anayetaka ubunge kupitia chama hicho ni lazima awe na si chini ya milioni hamsini wakati wa kura za maoni na kwamba wakati wa kampeni za uchaguzi mtu huyo ni lazima awe na pesa zisizopungua milioni miatatu!

Kuna kijana rafiki yangu anaishi nje ya nchi, ana mipango ya kugombea ubunge katika jimbo fulani lenye kigogo wa CCM. Alikuwa ananiuliza kwa njia ya mtandao juu ya mbinu za kutumia ili kupambana na kigogo huyo. Nilimwambia kama ana zaidi ya milioni miatano aje kwenye uwanja wa mapambano maana watanzania hawana kiu ya haki, utawala bora, maendeleo ya nchi, usalama wa rasilimali za taifa, bali wana kiu ya pesa. Ukiwa na pesa unaweza kununua haki, unaweza kutawala, unaweza kupora rasilimali za taifa bila kuguswa, ukiwa na pesa unaweza kununua mitihani, kununua vyeti na kuishi maisha bora. Kijana huyo amesema atazikusanya pesa kutoka huko Ulaya, na kuja kupambana na kigogo wa CCM.

Ni wabunge wangapi wa CCM, wanaoweza kukanusha haya? Wakasema walichaguliwa kwa sifa zao, bila kutumia pesa? Hata wale wanaopita bila kupingwa, wanatumia pesa kwa kuwanunua wanaojitokeza kuwapinga. Mtu asiyekuwa na pesa, hata kama ana kipaji cha kuongoza, hawezi kupata nafasi ya uongozi hadi pale tutakapotengeneza katiba mpya na kuzingatia misingi ya demokrasia. Tanzania, ina watu waadilifu, waaminifu, wenye malengo ya mbali, wenye juhudi ya kazi, wenye kulipenda taifa hili, lakini hawapati nafasi ya kuliongoza taifa letu kwa vile hawana pesa!

Sisumbuliwi na watu kutumia pesa wakati wa uchaguzi. Si busara kusumbuliwa na kitu kilicho wazi. Ni nani asiyejua kwamba bila pesa huwezi kupata uongozi katika taifa letu? Awe ni mwenyekiti wa kijiji, diwani, mbunge, bila pesa hawezi kupita. Kigezo si sifa na uwezo wa kazi, bali ni pesa!

Mimi binafsi kuhusiana na uchaguzi mkuu ninasumbuliwa na mambo mawili, sina hakika wewe unasumbuliwa na mangapi na pengine hakuna linalokusumbua! Yanayonisumbua ni: Hizi pesa za kununua kura wakati wa uchaguzi mkuu zinatoka wapi? La pili, je ni kwa nini watanzania hawajifunzi? ,kwa nini hawagundui uongo wa wanasiasa? 1995, ahadi nyingi zilitolewa, ninashindwa kusema zilitekelezwa maana bado tunapiga kelele ya umasikini. Ahadi hizo zilikuwa zinalenga kushusha neema ifikapo 2000. Sasa ni miaka kumi ya kuendelea kuimba wimbo wa umasikini! Ni imani yangu kwamba mambo haya yanayonisumbua mimi yanawasumbua na watanzania wengine. Pia, siwezi kushangaa kugundua kwamba kuna watanzania wasioguswa na haya. Ukweli ni kwamba tuna watu wanaoishi tu kwa vile wanaishi, hawana malengo, hawahoji kitu, iwe kiangazi, yawe masika yote ni sawa! Kama baadhi ya viongozi wa serikali hawana malengo ya mbali itakuwa kwa wananchi wa kawaida wa vijijini ambao hawakupata hata nafasi ya kuingia darasani? Si lengo la makala hii kujadili watu wanaoishi bila kuhoji kitu na bila kuwa na malengo ya mbali, huu ni mjadala mrefu. Leo nitajadili mambo mawili yanayoisumbua roho yangu juu ya uchaguzi mkuu.

Hizi pesa zinatoka wapi? Mbona hatuzioni wala kuona dalili zozote kabla ya uchaguzi mkuu? Mzee Mengi, akiamua kutumia pesa zake kununua kura, hakuna atakayejiuliza, pesa amezipata wapi. Tunaijua IPP, imetengeneza ajira nyingi kwa watanzania na inaendelea kuzalisha ajira nyingine. Kila mwanzoni mwa mwaka Mzee Mengi, anawafanyia sherehe walemavu, wanakula, wanakunywa, wanacheza na kuburudika, pia anawatolea zawadi mbali mbali walemavu hao, pesa zinatumika kufanya yote hayo. Mzee Mengi, amekuwa mstari wa mbele kuwasaidia watu mbali mbali katika jamii yetu, anawasaidia watoto yatima, watoto wa mitaani, anawasomesha vijana ambao familia zao hazina uwezo. Ni mifano mingi, inayoonyesha dalili za Mzee Mengi, kuwa na pesa na moyo wa kuzitoa, ninachotaka kusema ni kwamba tunajua Mzee Mengi, anatafuta pesa, na pesa hiyo inamsaidia yeye na kuwasaidia watanzania, inachangia kukua kwa uchumi wa taifa letu.

Sasa hawa ambao hawana viwanda, makampuni na shughuli nyingine za kutengeneza pesa, wanazipata wapi pesa za kununua kura? Tunajua wanapata mshahara ambao kwa kiwango cha mishahara ya Tanzania, hawawezi kuwa na pesa ya ziada! Wanapata wapi pesa za kununua kura wakati wa uchaguzi? Hatujasikia wametengeneza ajira kwa ajili ya watanzania, hatujasikia wametoa msaada wa kujenga zahanati, kuwahudumia watoto yatima na wala hawana historia ya kuwa na moyo wa kutoa. Tabia yao ni kupokea kuliko kutoa! Hili nalo ni mjadala unaojitegemea.

Je, pesa hizi zinakuwa hapa nchini kwenye benki zetu zikisubiri kipindi cha uchaguzi mkuu? Au wanakuwa wamezichimbia kwenye mashimo? Kama wanazichimbia kwenye mashimo basi hawa hawafai kuwa viongozi, maana wanazorotesha uchumi. Pesa ikikaa shimoni bila mzunguko haisaidii ukuaji wa uchumi. Kiongozi bora ni yule anayejishughulisha kuimarisha uchumi wa nchi.

Labda pesa hizi zinakuwa zimefichwa kwenye mabenki ya nchi za nje? Kama ni hivyo basi hawa pia hawafai kuwa viongozi wetu, maana kama pesa iko nje ya nchi, ni sawa na kuichimbia shimoni, tofauti ni kwamba inakuwa inazunguka, na kuzalisha faida kwa watu wa nje na si kwa watanzania.

Nchi ya Somalia, ambayo hadi leo hii baada ya miaka zaidi ya kuminamitatu haina serikali, imekuwa ikiendesha uchumi wake kwa kusaidiwa na Wasomali walio nje ya nchi. Wako Amerika, Ulaya na nchi nyingine, wanatafuta pesa na kuituma Somalia. Nchi nyingi duniani zinafuata mfumo huu, zinatoa utajiri nje na kuingiza ndani, si kutoa ndani na kupeleka nje. Sisi tuna watu wanaotafuta pesa( usiniulize kwa njia gani) badala ya kuziwekeza ndani ya nchi, wanachimbia mashimoni au wanaziwekeza nje ya nchi. Wanasubiri wakati wa uchaguzi mkuu ili wazitumie pesa hizo kununulia kura, wakishaingia madarakani, wanazikusanya tena pesa hizo na kwenda kuziwekesha tena nje ya nchi. Ni mzunguko wa wajinga ndio waliwao, au usimwamushe aliyelala.

Katika mzunguko huu( mzunguko wa wajuaji na wajinga) mwenye faida kubwa ni yule anayezitunza pesa. Faida inayotokana na pesa hizo inaendesha viwanda, makampuni na mashirika ya nchi yake. Ajira inaongezeka katika nchi yake. Na uchumi wa nchi yake unaboreka. Wakati viongozi wetu wanaendelea kutuona kama wajinga ndio waliwao, maana wanatudanganya kila chaguzi, nao pia wanaonekana hivyovyo mbele ya nchi tajiri wanakoficha pesa zao. Wanaogopa kuwatoa kwenye usingizi ili waendelee kuweka pesa kwenye benki zao.

Ukiangalia pesa zinazotumika wakati wa uchaguzi mkuu, itakuwa ni dhambi kusema kwamba nchi yetu ni masikini. Itakuwa ni dhambi serikali kushindwa kupandisha mishahara ya watumishi na kuinua kima cha chini kuwa juu ya dola mia. Itakuwa ni dhambi wanawake kupoteza maisha yao wakati wa kujifungua kwa vile wanaishi mbali na hospitali na hakuna usafiri unaoaminika. Itakuwa ni dhambi watu kuendelea kutembea zaidi ya kilomita 10 wakifuata huduma ya maji. Itakuwa ni dhambi kubwa serikali kushindwa kutoa huduma ya umeme kwa watanzania wote. Ni mengi ya kutaja! Ninaposema pesa zinazotumika katika uchaguzi nina maana ya pesa za serikali na pesa za watu binafsi. Maana kama watu wana pesa za kumwaga wakati wa uchaguzi kwa nini wasifanye kama Mzee Mengi, wakawekeza hapa na kutengeneza ajira kwa watanzania?

Mwezi huu mwanzoni kule Mwanza, nimeshuhudia mbunge wa jimbo fulani, akitawanya pesa kwenye kundi la watu. Anachukua mabunda ya noti za 500,1000 na 10000 na kutupa kwenye kundi la watu. Watu walikanyagana kuokota pesa kutoka kwa mbunge wao. Habari nilizozipata ni kwamba pamoja na mbunge huyo kuwa na nafasi ya juu serikalini, hajatengeneza kitu cha maana katika jimbo lake. Kama ana pesa za kutawanya kama karanga, kwa nini basi asijenge kiwanda au mradi mwingine wa kuwaongezea watu kipato? Huyu mtu anayeanza sasa hivi kutawanya pesa kama karanga, ameandaa mamilioni mangapi kwaajili ya uchaguzi mkuu? Na pesa hizi kazipata wapi? Mbona sikusikia kwamba hiyo ndiyo tabia yake? Tabia inayojulikana juu ya mbuge huyu akiwa jimboni kwake ni kufunga vioo vya gari lake na kuwatimulia vumbi wapiga kura wake. Sasa uchaguzi umekaribia ndio anakumbuka kwa namna ya dharau kubwa kuwatupia pesa wapiga kura wake.

Jambo la pili linalonisumbua, ni kwamba ni kwa nini watanzania wasijifunze? Kwanini wasigundue uongo na ujanja wa wanasiasa. Ahadi zinazotolewa wakati wa uchaguzi hazitimizwi. Jambo la kushangaza watu wale wale walioshindwa kutekeleza ahadi wanarudishwa tena katika uongozi. Watu wale wale wanaotorosha utajiri wa taifa letu na kuuwekeza nje ya nchi, ndio wanaochaguliwa tena kuendelea kuliongoza Taifa letu.

Ni nani wa kusimama na kuhoji juu ya pesa za kununua kura? Ni nani wa kuuliza zinakotoka? Ni nani wa kuwashawishi watanzania kukataa kumchagua kiongozi anayetumia pesa zisizoeleweka ziliko toka kununua kura? Ni nani wa kuwafundisha watanzania juu ya uongo wa wanasiasa? Kuwatoa kwenye usingizi na kuwapatia mwanga wa Ukweli? Viongozi wa dini wangeweza kusaidia kufanya kazi hii, na kusema kweli hii ndiyo kazi yao, kazi ya kuiongoza jamii kuwa na kiu ya haki, utawala bora na utaifa lakini kama wanashindwa kuhoji zinakopatikana sadaka nzito zinazotolewa na viongozi wa chama na serikali, wataweza wapi kuuliza zinakopatikana pesa za kununua kura.

Mbali na mambo yanayoisumbua roho yangu, kuna mambo yanayonishangaza kuhusiana na uchaguzi mkuu. Katika kura za uchaguzi wa serikali za mitaa, CCM, ilipata asilimia 96, hii inamaanisha CCM, ni chama kinachopendwa na kukubalika. Ya nini basi kutumia pesa nyingi wakati wa kampeni? Kwanini pesa hizo zisitengwe kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo. Maana kama chama kinakubalika kiasi hicho kitashinda tu hata bila ya kufanya kampeni!

Na je kama CCM ni chama kilichokomaa kisiasa, mbona karibu kila mwanaCCM, anataka kuwa rais? Kwani asijitokeze mmoja au wawili? Mbona chama hiki kinapenda kutumia vyombo vya dola ili kuhakikisha kinashinda. Mbona kinatumia vitisho na mbinu nyingine nyingi za chini chini? Mbona kuna vurugu juu ya kuwania ubunge na udiwani. Kama chama ni kizuri, kwani kisiwe na vigezo vya kupendekeza wagombea, bila mdinde za kutumia pesa na kupakana matope? Vyama vingine vichanga, vinajifunza nini kutoka kwa CCM?

Wakati kila mtu sasa hivi anajiuliza ni viongozi gani wanafaa kuliongoza taifa letu, ni bora pia kila Mtanzania akaanza kuhoji juu ya pesa hizi za kununua kura na ni kwa nini watanzania hatujifunzi. Kila Mtanzania ahoji, je pesa hizi ni za watanzania na zilikuwa zimechimbiwa kwenye shimo kwa miaka mitano, au je zilikuwa benki zikichangia ukuaji wa uchumi wetu, au je zilikuwa zimefichwa nchi za nje, au ni za watu wanaotaka kulinunua taifa letu. Kama sababu ya mwisho ni kweli, basi tunakuwa hatuchagui viongozi wetu bali vibaraka!
Hizi pesa zinazoibuka wakati wa uchaguzi mkuu na baadaye kupotea ni za kutilia mashaka makubwa. Shaka hii ikiota mizizi tunaweza kupata baraka ya kuwachagua viongozi walio bora, vinginevyo tutaendelea kuwachagua vibaraka watakaotusaidia kuliuuza taifa letu. Ee Mungu isaidie Tanzania.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment