PAMBAZUKO GIZANI

UCHAMBUZI HUU ULICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA 2008

UHAKIKI WA KITABU: PAMBAZUKO GIZANI

1. REDODI ZA KIBIBLIOGRAFIA

Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni
“Pambazuko Gizani” na kimetungwa na Karumuna Mboneko. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D Limited na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 411 04 5. Kimechapishwa mwaka wa 2004 kikiwa na kurasa 77. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. UTANGULIZI.

Mwaka juzi mwezi wa tano, nilikutana na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, aliyeongelea “ A funny little Book”. Alisema naye alisimuliwa na rafiki yake juu ya kitabu hiki kidogo cha kuchekesha lakini kilichojaa ukweli unaochoma. Bahati nzuri alikipata kitabu hiki kidogo wakati akisafiri kutoka Dar, kwenda Morogoro, na njiani aliweza kukisoma kitabu hicho na kukimaliza.Profesa huyu, alinishangaza jinsi alivyoweza kusimulia hadithi ya “A funny little Book”kiasi cha kutilia shaka kwamba labda yeye ndiye aliyeitunga. “ A funny little Book” ni “Pambazuko Gizani”. Baada ya kusimuliwa, nilifaya jitihada za kukitafuta kitabu hiki.Kinapatikana TPH (Tanzania Publishing House) na kwenye duka la wachapishaji wa kitabu hiki E&D Limited. E&D, wanapatikana maeneo ya Afrika Sana, ukisimama Corner Bar, utaona kibao cha E&D. Nimekisoma kitabu hiki, ningependa na wewe msomaji wa safu hii ukisome pia!

Hii ni hadihi ya kubuni. Bwana Klaus Mayhofer kutoka Freising, Ujerumani ni mjukuu wa Padre Klaus wa White Fathers aliyefanyia kazi kanisa katoliki huko Bubako tangu mwaka 1892.Klaus amefika Tanzania kutafuta ndugu zake, watoto wa Padre Klaus kama walivyosoma katika maandishi ya Padre huyo baada ya kifo chake.

Safari ya Klaus inatufunulia mengi kuhusu maana heshima ya Kanisa Katoliki na vitendo vya Mapadre wanaolitumikia.

Hadithi hii imeandikwa kwa mtindo wa kurudi nyuma. Kwa kutumia shajara za padri Klaus, hadithi inaturudisha nyuma kwenye miaka ya 1892. Lakini pia inaunganisha matukio ya zamani na ya sasa kitu kinacholeta mvuto katika kuisoma hadithi hii ambayo inatuonyesha kwamba hakuna jipya chini ya mbingu.Kitabu hiki kina sura tano.Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.

III.MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.

Hadithi hii inaanza na msemo wa Kihaya: Watunza vibuyu ndio hasa wavunja vibuyu. Kwa maneno mengine, unaweza kusema Watunga sheria ndio hasa wavunja sheria.Msemo huu unaelezea vizuri sana mazingira yanayokizunguka kitabu hiki.

Hivi karibuni kumejitokeza kashfa nyingi kuzunguka useja wa mapadri wa Kanisa Katoliki. Mbali na mapadri kushindwa kuishi kiaminifu maisha haya ya useja, yamejitokeza mambo mengine kama mapadri kuwanajisi watoto wadogo wa jinsia zote.Kule Amerika, tatizo hili liliyumbisha kanisa.

Hapa Tanzania, padri wa kanisa katoliki alifungwa miaka 35, kwa kumnajisi mtoto wa kiume, lakini baadaye alikata rufaa na kushinda kesi. Na kelele nyingi zinasikita kila sehemu ya Tanzania kwamba mapadri wanashindwa kuishi maisha ya useja. Kule Kenya, padri mkatoliki ameamua kufunga ndoa na kuendelea kuwahudumia waumini wake.Katika mahojiano yake na BBC, alitoa ushuhuda kwamba asilimia 80 ya mapadri wa kanisa katoliki kule Kenya, wanaishi maisha ya unafiki. Mbele za watu ni waseja, lakini ukweli ni kwamba wanaishi kinyume na useja.

Askofu Mkuu Milingo, amevunja mwiko wa useja na kuunda umoja wa mpadri walio na ndoa ili waendelee kutoa huduma ndani ya kanisa. Kanisa katoliki, imemtenga – lakini yeye anaendelea kwa nguvu zote na kuna dalili za kuungwa mkono. Kwa mtu anayeona mbali ni vigumu kupuuzia maamuzi wa Askofu huyu, ambaye ana uzoefu mkubwa ndani ya kanisa katoliki na mazingira ya Afrika.

Hivi karibuni katika gazeti la RAI kulizuka mjadala mkubwa juu ya useja. Wengine waliupinga useja na wengine waliuunga mkono.Kutokana na na mjadala huo, ilijitokeza wazi wazi kwamba kuna watu wanaofahamu maana ya useja na wako watu wasiofahamu maana ya useja. Ushuhuda huu pia ulionyesha wazi kwamba kuna baadhi ya waseja, wasiofahamu maana ya useja, na kuna wasio waseja wanaofahamu maana ya useja. Ukweli unabaki pale pale kwamba useja umezungukwa na utata mkubwa.

Pamoja na utata huu,Kanisa Katoliki, ninasimama imara kutetea maisha ya useja, na kwamba kamwe halitabadilisha msimamo wake kuhusu jambo hili.

Mtunzi wa Pambazuko Gizani, kwa kuzingatia utata huo, anajaribu kutufanya tutafakari na kujiuliza maswali. Hadithi kama hii ya Pambazuko Gizani, haikuzoeleka hapa Tanzanai, na ninafikiri ni ya kwanza ya aina yake. Kule ulaya ambako imani imekomaa na watu wanatumia haki yao ya kuhoji, kufikiri na kuamua kwa uhuru,hadithi kama hii ya Pambazuko Gizani, zimezoeleka .

Pia mtunzi wa Pambazuko Gizani, anatufumbua macho kuona kwamba kushindwa kwa useja, si jambo la leo.Anatuonyesha ukweli wa kihistoria kwamba hata na wale walioileta dini hapa kwetu, walishindwa kuishi useja.Baadhi yao walizaa watoto. Na hasa hili ndilo swali kubwa la Pambazuko Gizani, kizazi hiki cha wamisionari kiko wapi? Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.

IV.MUHTASARI WA KITABU

Sura ya kwanza ni barua ya tarehe 5.7.1996, kutoka Urfeld-Ujerumani,iliyoandikwa na Klaus Mayhofer, akimwandikia rafiki yake Kalinguliza,anayeishi Bubako-Tanzania. Barua hii ni kama muhtasari wa kitabu kizima.Kwa kusoma barua hii, mtu anapata picha nzima ya hadithi hii na hasa yale maneno ya mwisho wa barua:
“ Nina imani kwamba utafurahi kusikia kuwa kazi yetu imekamilika.Sasa nimebaki na kazi ya kumtafuta mtu wa kuichapa.Habari nzuri nimezingundua katika barua za babu yangu alizokuwa akimwandikia rafiki yake, Martini Hildebrand. Alikuwa anabakiza nakala ya kila barua aliyokuwa anamwandikia na alikuwa anamwandikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya Bubako. Barua hizi na shajara nia msaada mkubwa.” (Uk.6).

Sura ya pili, ni safari ya Klaus Mayhofer, kutoka Dar-es-salaam hadi Bubako. Katika sura hii tunamsikia Klaus, akijitambulisha kwa rafiki yake Kalinguliza:
“ Mimi ni mjukuu wa Padre Klaus Mayhofer, padre mmisionari wa White Fathers ambaye aliishi Bubako kati ya mwaka 1892 na 1912… Babu yangu alikufa miaka mitatu iliyopita.Katika wosia wake mimi ni mrithi wa maandishi yake yote.Katika shajara yake ya mwaka 1894, niligundua kwamba babu alikuwa padre. Kabla ya hapo hakuna aliyejua, hata baba yangu hakujua.Katika shajara hiyo, babu anataja kwamba wakati akiwa padre alizaa watoto wawili msichana Mary Mukekelezia na mvulana, Petero Mjerumani. Hawa ndio jamaa zangu ambao ninawatafuta ama wao, watoto wao au wajukuu zangu.Miaka si mingi sana kiasi cha rangi kufutika kabissa” ( uk 10-11).

Sura ya tatu inahusu Kabanga.Hii ni sehemu ambayo padri mjerumani alifanya kazi kwenye miaka ya 1892.Sura hii inaanza na barua ya padri huyu aliyomwandikia Mungu wake.Ni barua ya tarehe 14.1.1892:
“ Mungu wangu, Nina imani unanisikiliza.Baada ya kazi ngumu ya kulijenga kanisa lako, nimechoka. Nguvu zimeniishia kabisa….. Kinachonimaliza nguvu si kazi kubwa niliyonayo ya kusimamia ujenzi wa kanisa hili; hapana! Ninaumia sana kuwaona watu hawa katika suluba ya kubeba miti ya kujenga kanisa kwa kuitoa umbali wa kilometa sitini kwa miguu na kubeba vichwani mwao, miti yenyewewe ni mikubwa sana…. Juzi tu wamekufa watu kumi kwa kuangukiwa na miti hii.Watu hawa hatuwalipi dahili yao, bali tunawahidi rehema za mbinguni. Wanakujengea nyumba imara na wenyewe wanaendelea kuishi kwenye nyumba mbovu”(Uk 12).

Sura hii ya tatu ina kumbukumbu nyingine ya tarehe 10.1.1895.Pia, hii ni barua ya padri huyu mjerumani kwa Mungu wake:
“ Mungu wangu, unanisikia? Samahani sana, siku nyingi nilikuwa sijakuandikia. Nilikuwa na kazi hii ya kulijenga kanisa lako.Ujenzi wa kanisa sasa unaelekea mwisho.Kuna kitu nimegundua.Watu wako wa hapa hawahitaji kanisa kubwa kama hili tunalolijenga na wala hawahitaji dini yetu.Wanahitaji nguo, nyumba bora na imara, ufundi, dawa na kujua kusoma na kuandika.Furaha wanayoionyesha wakati wakipokea nguo ni tofauti kabisa na furaha yao wakati wakiyasikiliza mafundisho ya dini” ( Uk17).

Kumbukumbu ya mwisho kwenye sura hii ya tatu ni ile ya tarehe 5.5.1895.Hii ni barua ambayo padri huyu mjerumani alimwandikia rafiki yake Martin Hildebrand:
“……Nitahamishiwa sehemu nyingine.Kuna sababu mbili za uhamisho wangu, kwanza ni kwenda kujenga kanisa la Kibona na pili ni kuwa mbali na Mugonzibwa.Nina kumbuka kwamba, katika barua yangu ya mwisho nilikuelezea juu ya Mugonzibwa.Sasa amekwishabatizwa na kuitwa Clementina Mugonzibwa.Mwaka jana mwezi wa kumi alijifungua mtoto wa kike, Mary Mukekelezia.Maana ya Mukekelezia ni mke wa kanisa au zawadi ya kanisa au tunda la kanisa.Mtoto ni mjerumani.Nina imani utafurahi sana utakapomwona” (Uk 23).

Sura ya nne, inahusu Kibona.Hii ni sehemu nyingine ambayo padri huyu mjerumani alifanya kazi.Sura hii inaanza na kumbukumbu ya tarehe 7.7.1895.Hii ni barua ambayo Padri huyu alimwandikia Mungu wake:
“ Mugu wangu,…… Kanisa hili linajengwa juu ya damu za watu. Tumeipata sehemu hii kwa vita.Mfalme Kayoza hakupenda kabisa tuiingize hii dini yako ya kikristu hapa Kibona. Alitufukuza kwa mishale na sisi tukajitetea kwa bunduki. Sisi mapadre wako tukashika bunduki, Askofu wetu akazibariki bunduki na risasi.Tukapigana bega kwa bega na askari wa Kiganda ambao baadaye tuliwafanya kuwa makatekista wa kueneza neno lako…” (Uk 27).

Kumbukumbu nyingine kwenye sura hii ni barua ya tarehe 10.6.1897. Padri huyu mjerumani, alikuwa akimwandika rafiki yake Martin: “…..Kuzaliwa kwa Petero Mjerumani kuliniletea matatizo makubwa sana, Askofu alisikitika sana, hakupenda kunipoteza maana alijua jinsi nilivyofanya kazi kwa nguvu na kwa moyo wangu wote.Shida kubwa ilitokana na Bwana Mkubwa wa hapa. Yeye alikazana nifukuzwe na kurudishwa nyumbani Ulaya..” (Uk 37).

Kuna kumbukumbu nyingi kwenye sura hii zinazoonyesha mapambano ya padri huyu. Mapambano na useja, mapambano na imani; kuingiza imani ya kigeni na kufuta imani za kienyeji,mapambano na utamaduni, madaraka, heshima ya kanisa nk. Huyu ni padri aliyekuwa na imani, mwenye upendo, mwenye kupenda haki na mwenye kuchapa kazi.Kwa vile alishindwa kuzingatia useja, kazi zake zote zilionekana bure! Alinyanyaswa na kuteswa kiasi kikubwa na mwishowe alirudishwa kwao Ujerumani.

Sura ya tano inaelezea maisha ya ma Kokuleba, huyu aliishi 1888 hadi 1996! Huyu ndiye anayefumbua fumbo. Kumbe watoto waliozaliwa na wamisionari, waliuawa ili kutunza heshima ya kanisa! Kwa vile walikuwa mchaganyiko, ilikuwa ni rahisi kutambua kwamba walizaliwa na mapdri wazungu.Ili kulinda imani, ilikuwa ni hekima kuwapoteza, ili watu wasiwe na mashaka kwamba mapadri wanazaa watoto!Katika hadithi hii watoto hawa wanauawa. Ma Kokuleba, alifanikiwa kumficha mmoja!

V. TATHMINI YA KITABU.

Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathimini ya kazi hii aliyoifanya Karumuna Mboneko.

Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, hadithi hii inasisimua sana kutokana na mtindo aliotumia mwandishi.Mtindo huu wa kutumia shajara na barua za zamani, ili kutoa ujumbe kwa maisha ya leo ya kanisa, inavutia sana na kumfanya mtu kuisoma hadithi bila kupumzika!

Pili, mwandishi amefanikiwa kutumia ukweli wa kihistoria, kuunda hadithi ya kubuni.Ukisoma vitabu vya historia ya Ukristu nchini Tanzania, utaona kwamba yale yote ya kubuni ni matukio hai yaliyotokea sehemu mbali mbali hapa Tanzania. Wanahistoria mbali mbali wanataja wazi kwamba baadhi ya mapadri wamisionari walishindwa useja na walizaa.Utata unaojitokeza ni kwamba kizazi hiki kiko wapi?Idadi inayotajwa ni kubwa ukilinganisha na watu mmoja mmoja wanaohisiwa kuwa kizazi cha wamisionari.

Tatu, mwandishi amefanikiwa kuanzisha mjaddala juu ya mambo ambayo wengi wetu tunaogopa kuyagusa. Mambo ya imani.Wengi wetu tunataka kuamini tu bila kutumia akili. Mfano, mwandishi anaweka wazi ukweli kwamba wamisionari walipokuja, watu walipenda maendeleo ya vitu, kama nyumba, madawa, shule nk, kuliko walivyotamani dini hiyo ya kigeni.Ukweli kwamba wamisimonari walitumia vitu hivyo walivyovitamani watu kama chambo, halina ubishi. Mwandishi pia anagusia jambo la useja na athari zake.Athari hizi zinaendelea hadi leo hii.Je hizi ni athari zinazokubalika, je ni athari za kuvumilika? Mfano ni haki kwamba kizazi cha watoto wa wamisionari kilipotezwa? Ni mambo mengi ambayo mwandishi anaibua kwenye hadithi ya Pambazuko Gizani, ambayo tusipoyajadili leo, yatajadiliwa na vizazi vijavyo.

Nne, mwandishi amefanikiwa kuwachora vizuri wahusika. Kwa mtu ambaye ni padri kama mimi au kwa mtu ambaye amezoea maisha ya kanisani, akisoma hadithi hii, ataona kabisa kwamba huyu ni padri fulani, huyu ni Askofu fulani, au huyu ni mkristu fulani.Au unaweza kusema tukio linalosimuliwa, lilitokea sehemu fulani na wahusika ni fulani na fulani. Mwandishi, amefanikiwa kuchora na kuielezea hali halisi.

Tano, ni mapungufu yanayojitokeza katika hadithi hii. Mfano, majina mengi yanayotumika kwenye hadithi yana maana.Kwa mhaya, hadithi inakuwa na ujumbe mzito kwa kuelewa maana inayobebwa kwenye majina. Pia kufahamu maana ya majina, kunaogeza utamu wa hadithi yenyewe. Kama mtu hajui Kihaya, anapata ujumbe nusu.Haya ni kama mapungufu yanayojitokeza kwenye vitabu vya Ngugi. Mtu, anayejua Kikikuyu, anapata ujumbe mzito kwenye vitabu vya Ngugi. Majina anayoyatumia Ngugi, kwenye vitabu vyake yanakuwa na maana Fulani. Hivyo kama Pambazuko Gizani, ingekuwa na maelezo ya majina, ujumbe ungewafikia watanzania wengi. Mfano jina Kama Kalinguliza, lina maana ya mtu anayechunguza chunguza, Bishuba ni uongo,Kabanga ni kilima.Mushenyele ni Askofu nk.

VI.HITIMISHO.

Kwa kuhitimisha basi, ningewashauri watanzania kukisoma kitabu hiki.Ni wazi kina aina Fulani ya uchokozi na uchokonozi, lakini kwa mkristu mwenye imani komavu, hawezi kusoma hadithi kama hii inayosaidia kuonyesha mapungu mbali mbali katika kanisa akaipuuza;Kwa kuona mapungufu na kuyatafari, mkristu mwenye imani komavu, anaweza kupiga hatua. Kufumba macho na kujifanya kwamba hakuna kitu kinachoendelea ni ujinga na hakuna imani inayoweza kujengeka kwa namna hiyo.

Kuna mambo yanayoibuliwa kwenye hadithi ya Pambazuko Gizani.Mambo haya ni kama useja, mauaji ya watoto mchanganyiko (Chotara), upweke wa maisha ya upadri, uchu wa madaraka, upendeleo na kujuana wakati wa kuchagua viongozi wa kanisa katoliki, dini za kigeni kuchukua nafasi ya dini za kienyeji, watu kupendelea maendeleo ya vitu kuliko dini za kigeni, wamisionari kutumia vitu kama chambo kwa kuwapata waumini katika dini yao, maungamo kutumiwa vibaya nk. Mambo haya yapo, yawe kwa kiasi kidogo ama kwa kiasi kikubwa yapo.Ni muhimu mambo haya kujadiliwa au kukanushwa kwa mifano hai!Yote haya yanajadilika na ni muhimu katika uhai wa kanisa na uhai wa jamii kwa ujumla.

Yawezekana mwandishi wa Pambazuko Gizani, akawa amepandwa na shetani na inawezekana wale wasioona ukweli ulioandikwa kwenye Pambazuko Gizani nao wamepandwa na shetani! Dawa pekee ni kujadiliana, kutafakari na kupambana na changamoto zote zinazojitokeza katika maisha ya kila siku.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

4 comments:

www.yusideablogspot.org.com said...

pamoja kiongozi

Unknown said...

Nimeipenda sana ipo vizur

Unknown said...

Liko vizuri saana

dm said...

Asante sana kwa ujumbe huu. Umenisaidia sana sana kujua mengi lazima ntakinunua kitabu hili mda sio mrefu

Post a Comment