TEOLOJIA YA UKOMBOZI IMEPATA PIGO!

MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

TEOLOJIA YA UKOMBOZI IMEPATA PIGO!

“ Et multi ante nos vitam istam agentes,praestruxerunt aerumnosas vias, per quas transire congebamur multiplicato labore et dolore filiis Adam.”

Tafsiri isiyokuwa rasmi: “Na wengi waliotutangulia walioyaishi maisha haya, walitembea juu ya njia zilizopinda pinda, tulizolazimishwa kupitia kwa uchovu na mateso yaliyowekwa juu ya watoto wa Adamu.”

Maneno haya ni mawazo ya Mtakatifu Augustine, na baadaye yalipigiwa debe na kusambazwa na mwanafalsafa Ludwig Wittgenstein.

Ukifungua kitabu cha Leonardo Boff, mwanateolojia ya ukombozi kutoka Brazil, utakutana na maneno hayo niliyoyanukuu hapo juu.

Mwaka 1984, kitabu cha Leonardo Boff: “Church Charism & Power”, kilileta kelele nyingi na woga katika kanisa katoliki. Tarehe 15 Mei 1984, Kadinali Joseph Ratzinger, alimwandikia barua Leonardo Boff, kwenda Roma, kuhojiwa juu ya kitabu chake. Na tarehe 3 Septemba, Kadinali Ratzinger, alitoa barua kali yenye kurasa 36, akionya juu ya upotoshwaji na dalili za kuvunja imani ya waumini wa Latin Amerika, zilizokuwa zikijitokeza kwenye kitabu cha Leonardo Boff na teolojia ya ukombozi. Hii ni barua ya kwanza katika kanisa katoliki iliyopinga teolojia ya ukombozi wazi wazi.

Tarehe 7 Septemba 1984, Leonardo Boff, alijitetea mbele ya Kadinali Ratzinger, kwa muda wa masaa manne na kutoa majibu yenye kurasa 50. Boff, alikataa kuiacha Theolojia ya ukombozi kama alivyoelekezwa na Ratzinger. Na Kadinali Ratzinger, aliendelea na msimamo wake wa kuiona Theolojia ya ukombozi kama tishio la kuingiza mawazo ya Karl Marx na ukomunisti katika kanisa. Leonardo Boff, alirudi kwao Brazil, akaamua kuuweka upadre pembeni na kubaki na Ukristu na kuendelea kujenga jumuiya ndogo ndogo katika mtizamo wa theolojia ya ukombozi. Naye Kadinali Ratzinger, aliendelea na msimamo wake wa kuilaani Theolojia ya ukombozi. Kwa vile ndiye aliyekuwa msimamizi wa imani ya kanisa katoliki na mshauri wa karibu wa Marehemu Papa Yohana Paulo wa Pili, Theolojia ya ukombozi iliendelea kukandamizwa.

Msemo wa Waswahili kwamba ng’ombe wa masikini hazai, sasa kadinali Ratzinger, ni papa Benedict wa 16! Ni pigo kubwa kwa theolojia ya ukombozi. Ni pigo kubwa kwa wanyonge, masikini na wanaonewa. Ni wakati wa kusema maneno ya Mtakatifu Augustine: “ Et multi ante nos vitam istam agentes,praestruxerunt aerumnosas vias, per quas transire congebamur multiplicato labore et dolore filiis Adam.”

Ninapoandika makala hii nimeshika kitabu cha Leonardo Boff, mikononi mwangu. Pembeni mwangu ni makala yangu ya Jumapili iliyopita yenye kichwa cha habari “ Kuwa na Papa mweusi sasa ni ndoto za mchana”. Ninatafakari yale niliyoyaandika. Ninatafakari maoni ya Leonardo Boff, mawazo ya Mtakatifu Augustine. Je Papa Benedict wa 16, anayepinga Theolojia ya Ukombozi, ataweza kutamka maneno ya Yesu:
“ Roho wa Bwana yu pamoja nami, kwani ameniteua rasmi niwaletee masikini habari njema. Amenituma niwatangazie wafungwa kwamba watapata uhuru, vipofu wapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, na niutangaze mwaka ambao Mungu atawakomboa watu wake.” (Luka 4:18-19).

Hoja ya Leonardo Boff, katika kitabu chake ni kwamba kwa sasa asilimia kubwa ya waumini wa kanisa katoliki ni masikini na wanyonge, ni watu wanaoonewa na kunyanyaswa, ni watu wanaoongozwa tu kama vipofu bila kuwa na sauti ya kuhoji na kujitetea. Na kwamba mfumo wa kanisa tulionao sasa hivi, si wa masikini, ni wa matajiri na wenye madaraka. Anatoa wito wa kanisa kubadilisha mfumo kichwa chini miguu juu, uongozi wa kanisa utoke chini kwenye jumuiya ndogo ndogo. Kwa maoni yake Jumuiya ndogo ndogo ndizo zenye nguvu na ndilo kanisa. Kwa mtindo wa jumuiya ndogo ndogo hata mtu wa chini anaweza kutoa mawazo yake na mchango wake wa kulijenga kanisa. Anaukataa ule mtindo wa neno la Mungu kupitia kwa Baba Mtakatifu, kwenda kwa maaskofu, kwenda kwa mapadri, kwenda kwa katekista na mwisho kuwafikia waumini. Anasema neno la Mungu linaletwa na Mungu kupitia Roho Mtakatifu kwenda kwa jumuiya ya waumini ndipo inafuata milolongo mingine, ikiwa ni lazima kuwepo.

Uchumi wa nchi ya Brazil, uko mikononi mwa watu wachache. Inasemekana kwamba asilimia 95 ya uchumi wa Brazil, inamilikiwa na asilimia 5 ya wananchi,( Viongozi wa Kanisa Katoliki wanaanguka kwenye asilimia hii ndogo!) na asilimia 95 ya wananchi wanamiliki asilimia 5 tu ya uchumi. Leonardo Boff, anaangalia hali hiyo na kutaka kuibadilisha, kanisa linasema ni ukomunisti.

Bahati mbaya Leonardo Boff, simfahamu binafsi. Ninamsoma kwenye vitabu. Lakini nimepata bahati ya kumfahamu Kadinali Ratzinger, sasa Papa Benedict wa 16, kwa karibu. Nilimfahamu zamani 1978! Ni mtu mwema. Anapenda majadiliano, mcheshi na ni mtu anayesikiliza kwa makini. Ni mwanamapinduzi! Theolojia yake si ya kizamani. Yeye alimfundisha Leonardo Boff na wanateolojia wengi wanaotaka mapinduzi katia kanisa. Ukikutana naye kwa faragha, utashangaa kukutana na mwanateolojia mwanamapinduzi.

Wale wasiomfahamu kwa karibu wanasema Papa Benedict wa 16 ana msimamo mkali na hataki mabadiliko. Si kweli na ni kweli. Labda tuseme, Kadinali Ratzinger, alikuwa na sura mbili. Kuna Ratzinger, mwanateolojia. Huyu ni mwanamapinduzi na mwenye mawazo ya kisasa, unaweza kukaa naye ukabadilishana naye mawazo kwa kitu chochote, kuanzia kuwaparisha wanawake, uzazi wa mpango, matumizi ya kondomu, theolojia ya ukombozi, kupunguza madaraka ya papa nk, atakusikiliza na kuchangia mawazo. Huyu ni Ratzinger, aliyekuwa anafundisha theolojia kwenye miaka ya sabini na Askofu wa jimbo la Munich-Freising.

Kuna Ratzinger, Kadinali na msimamizi wa Imani ya Kanisa katoliki. Huyu ni mfungwa katika Imani. Huyu hana majadiliano, analinda imani kwa nguvu zote. Yeye mwenyewe anajua ugumu wa kazi yake. Ninakumbuka alipochaguliwa kuongoza kitengo cha imani kule Roma, ilimchukua siku nyingi kuhama Munich, hadi vyombo vya habari vikaanza kusema kwamba Kadinali Mbavaria, anakataa kwenda Roma. Huyu ndiye Ratzinger, aliyetumia nyundo ya imani na kumsambaratisha mwanafunzi wake Leonardo Boff, aliyemfundisha yeye mwenyewe!

Ndio maana nimesema kwamba Theolojia ya ukombozi imepata pigo kubwa, Kama Ratzinger, aliipiga nyundo akiwa kadinali msimamizi wa imani, itakuwaje sasa alipopanda na kuwa Papa Benedict wa 16?

Papa Benedict wa 16 ana kibarua kigumu. Itafika mahali sura zake mbili zitagongana. Siku za nyuma alitaka kujiuzuru kazi ya ukardinali ili akae chini na kuandika vitabu. Ni nani anajua alitaka kuandika nini? Ni wazi akiandika, ataandika kama Ratzinger mwanateolojia. Nafasi hii hana tena. Sasa ni mfungwa zaidi.

Mtihani wake mkubwa, ambao nina imani utamaliza nguvu zake ni kupiga magoti, yeye kama Papa Mjerumani, kuomba msamaha kwa Waisraeli kwa yale waliyotendewa na Wajerumani wakati kanisa limekaa kimya. Hili litammaliza nguvu na kumfumbua macho kuhusu Theolojia ya ukombozi. Jinsi Waisraeli walivyoteswa na kuuawa ndivyo wanyonge wa wa Latin Amerika wanateswa na kuuawa. Mapadre, Maaskofu na watu wa kawaida wanaotetea haki, usawa, wema, huruma, wanapoteza maisha yao. Waisraeli waliuawa kwa gesi na risasi, lakini katika nchi masikini watu wanakufa kwa njaa na magonjwa. Malaria na UKIMWI vinamaliza watu!

Na,
Padri Privatus Karugendo


0 comments:

Post a Comment