JUMUIYA NDOGONDOGO ZA KIKRISTO

UHAKIKI HUU ULICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA 2009


UHAKIKI WA KITABU: JUMUIYA NDOGONDOGO ZA KIKRISTO.

1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA.

Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Jumuiya Ndogondogo za Kikristo: Changamoto kuelekea Ukomavu na kimetunga na Padri Stephano Kaombe, wa Jimbo Kuu la Dar-es-salaam. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Ecoprint Ltd na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987-474-01-02. Kimechapishwa mwaka 2006 kikiwa na kurasa 196. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. UTANGULIZI

Kitabu hiki kilichozinduliwa siku ya Jumapili ya tarehe 17, Agosti, 2006, katika kituo cha Msimbazi jijini Dar-es-salaam, ni kitabu kwa ajili ya Wakatoliki wa rika zote, na watu wote katika jamii, maana mwandishi anajadili maswali mbali mbali yanayohusu watanzania wote. Mfano anajadili uwezekano wa mkristu kufunga ndoa na mwislamu na mahusiano ya dini mbali mbali na kugusa maisha ya kila siku ya mtanzania. Kitabu hiki kinaelezea hali halisi ya Jumuiya ndogondogo kuanzia zilizo hai, zilizo vuguvugu mpaka zinazodorora katika azima ya Wakristo kuwa chumvi ya ulimwengu. Anaonyesha ukweli kwamba Jumuia zilizo hai, zinaweza kuwa chumvi ya ulimwengu na kuonyesha umuhimu wa Ukristu wa matendo.

Kitabu hiki kimeandikwa katika mtindo unaofanana sana na ule aliotumia Mtakatifu Thomas Aquinas katika kitabu chake maarufu kwa jina la “ A Summary of Thology”. Kitabu hiki kinazo sura 3 na viambatanisho 7. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na thamini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki

III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.

Tangu miaka ya 1970 Maaskofu Katoliki la AMECEA waliamua kwamba Jumuiya Ndogondogo ziwe ndiyo vitovu vya Uenjilishani ndani ya Kanisa. Baadhi ya maaskofu walijitosa kuanza zoezi hili na wengine walibaki kuangalia na kusikiliza wanayofanya wengine. Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, alijitosa kiasi kizima na kuanzisha Jumuiya ndogondgo katika jimbo lake la Rulenge. Jumuiya hizi zilivuka mipaka ya kusali tu na kuingia katia nyanja za maisha yote. Mwoleka, alilenga kukamilisha kile ambacho Paadri Kaombe, ananukuu katika kitabu chake kutoka katika tamko la AMECEA la 1979, juu ya ya jumuiya ndogondogo:
“Ni njia kwayo Kanisa linaletwa chini toka katika mfumo ambao karibu upo mtupu, wa kufikirika, kwenda katika maisha ya kila siku, yanayowagusa waamini, furaha na majonzi ya watu wanapoishi kabisa, wanazaliwa, wanapenda, wanafanya urafiki, kazi, kulalala, wanasherehekea, wanaomboleza na kufa. Ni njia kwayo watu wanawezeshwa kutambua fumbo la Kristo aliyeko katikati yao, anayeonekana kwao kwa njia ya sura ya jirani. Ni Jumuiya ambazo watu wanasaidiana katika kumtafuta kwao Mungu kwa pamoja, katika njia yao ya mateseko ya kufuata njia ya Kirssto, ambayo katika hiyo msamaha, upendo na uaminifu vinawasilishwa katika kina cha maisha ya kila siku” ( Uk.4).

Mbali na Jimbo la Rulenge, Jimbo Kuu la Dar-es-salaam nalo limekuwa mbioni kutekeleza mpango wa Jumuiya Ndogondogo, kufuatana na mfuno anaouelezea Padri kaombe, katika kitabu chake. Aidha mwaka juzi Julai 15, 2005 Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ilizindua kitabu kiitwacho “ Kompendia ya Mafundisho ya Kanisa Kuhusu Haki za Binadamu” pale kurasini makao makuu ya TEC na kuweka mkakati wa kuyafanya mafundisho haya sehemu ya uenjilishaji katika ngazi zote za Parokia na katika Jumuiya ndogondogo

Ni katika muktadha huu, Jimbo Kuu la Dar-es-salaam lilitangaza kuwa toka Sherehe yaMt. Yosef Mei Mosi mwaka 2006 hadi sherehe hiyo tena mwaka 2007 kuwa ni mwaka wa Jumuiya Ndogondogo, lengo likiwa ni kutathmini ubora wake, udhaifu wake, na hatimaye kuamua namna ya kufanya maboresho stahili.

Kwa ajili ya tathimini hii, Padri Kaombe aliamua kutumia Kipindi cha Zingatia katika Redio Tumaini ambapo waamini walialikwa kuuliza maswali na kutoa mapendekezo mintarafu uhai wa Jumuiya Ndogondogo za Kiikrissto, wakifanya hivyo kwa njia ya meseji za simu. Kitabu hiki ni matokeo ya zoezi hili chini ya uratibu wa Padri Kaombe. Inaelekea, amekuwa mwaminifu kuyapokea maswali na mapendekezo ya wachangiaji na kutoa majibu kadri alivyoweza. Ameonyesha ujuzi wake wa hali ya juu katika ufahamu wake wa Jumuiya Ndogongo, ujuzi wake katika teolojia, ujuzi wake wa taalimujamii, imani yake isiyoyumba na hasa moyo wake wa kuwasikiliza watu. Majibu yake yote yana mantiki na kuvutia. Inaonyesha wazi kwamba yeye ni msomi, ni padre mchungaji wa kiroho na wala si padri mtawala ni kijana na ni mtu anayeutambua ulimwengu wa leo. Ni mchungaji anayefaa sana katika ulimwengu wa leo wa utandawazi. Wakati huu anafanya Shahada ya Uzamili katika Taalimujamii (Sociology) kwenye Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam. Masomo haya hayamtengi na kazi zake za kiroho na majukumu mengine ndani ya Jimbo Kuuu la Dar-es-salaam. Ameandika vitabu mbali mbali kikiwemo na kitabu juu ya falsafa kwa Kiswahili jambo linalomfanya abebe sifa nyingi katina nyanja ya uelimishaji. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenywe kwa muthasari.

IV. MUHTASARI WA KITABU

Sura ya kwanza inaongelea Mfumo wa Jumuiya Ndogondogo (Uk.2-29) na inayo majibu kwa maswali 17. Majibu haya yanafafanua maswali kuhusu maana ya Jumuiya Ndogongo za Kikrsto; tamko la uongozi wa Jimbo kwa waamini wasiohudhuria Jumuiya Ndogondogo; mwongozo wa Jumuiya Ndogondogo; faida za Jumuiya ndogondogo; sifa za viongozi wa Jumuiya hizi; na kadhalika.

Ujumbe muhimu katika sura ya kwanza ni: Jumuiya Ndogondogo “ Ni familia ya Mungu inayosali na kubadilisha uzoefu wa imani na kusoma neno la Mungu na kulitafakari kwa pamoja na kujadili mambo mengine ya kijamii ya kiuchumi kulingana na mazingria yao” (Uk 3).

Sura ya pili inaogelea Maisha ya Jumuiya Ndogondogo (Uk, 30-91) na inayo majibu kwa maswali 28. Majibu haya yanafafanua maswali kuhusu umuhimu wa mahudhulio ya baba, mama na watoto katika Jumuiya Ndogondogo; wajibu wa Jumuiya Ndogondogo kwa wagonjwa wa ukimwi; ufafanuzi kuhusu masomo yanayofaa kusomwa katika mikutano ya Jumuiya Ndogondogo; ushiriki wa wanajumuiya katika shughuli za vifo na mazishi; na kadhalika.

Ujumbe muhimu katika sura hii ni: “kutojua maandiko matakatifu ni kutomjua Kristo” (Uk.56) kwani maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundisha ukweli, kuonya, kusahihisha makosa na kuwaongoza watu waishi maisha ya maadili.” (Uk.61).

Sura ya tatu inaongelea Katekesi ya jumuiya Ndogondogo (Uk.92-162) na inayo majibu kwa maswali 36. Majibu haya yanafafanua maswali kuhusu nafasi ya msalaba wakati wa Ibada; umuhimu wa Sala ya Salamu Maria katika Jumuiya Ndogondogo; msimamo wa ki-Biblia kuhusu pombe; kuabudu sanamu; kutoa pepo na kuponya magonjwa kwa njia ya mombezi; nafasi ya maungamo kwa padre; maana ya sakramenti na visakrament; nafasi ya desturi katika Misa; na kadhalika.

Mojawapo ya ujumbe wa kufurahisha katika sura hii ni kupitia swali hili: “ Je, katika nyumba yetu tunaweza kuweka msalaba chooni?” (Uk.122). Ni lazima kusoma kitabu hiki, ili upate jibu la swali hili. Je w ewe unaweka msalaba chooni?

Baada ya sura ya tatu vinafuata viambatanisho saba ambavyo ni: Ibada ya wanajumuiya kwa wagonjwa; mwongozo wa kuadhimisha sakramenti mbalimbali; Nukuu ya Biblia katika kitabu cha Kutoka 18: 13-23; Ishara ya Umoja katila Adhimisho la Misa.
Viambatanisho vingine ni Sala ya kuomba fadhila ya unyenykevu; sala ya mwaka wa Jumuiya Ndogondogo; na hatimaye ni shairi kuhusu Jumuiya Ndogondoo za Kikristo likiwa na kibwagizo cha maneno: “ Wewe ni mwamini hai, au wewe ni goi goi?” ambapo maneno haya yanapishana na maneno “Wewe ni mwamini hai, au wewe ni hoi hoi” ubeti hadi ubeti. Hii inafurahisha na kuvutia sana.

Kwa ufupi, shairi hili murua linawahimiza waamini kuchukua nafazi zetu katika kuitakatifuza nchi, na hasa nchii hii ya Tanzania, kupitia ushiriki wetu katika Jumuiya ndogondogo! Nchi ikitakatifuka, inakuwa salama kwa kila mtu, awe mkristu au asiwe mkristu! Ndo maana kitabu hiki kinawafaa watu wote!

V. TATHMINI YA KITABU

Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Padre Stephano Kaombe.
Awali ya yote lazima niseme kwamba , kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasisimua sana kutokana na mtindo alioutumia mwandishi. Ni mtindo wa maswali na majibu yenye kusheheni utani mwingi, na tena maswali yanayotokana na waamini wenyewe kwenye Jumuiya ndogondogo ambako ndio walengwa wa kitabu hiki wanapatikana.

Pili, ni wazi kwamba mwandishi amefanikiwa kutimiza lengo lake, yaani kubainisha na kaisha kutoa majibu kamilifu kwa changamoto zinazowakabili waamini kuelekea ukomavu wa Jumuiya Ndogongodo za Kikristu.

Tatu, mwandishi ambaye ni mtaalimujamii amefanikiwa, japo kwa njia ya mzunguko inayoambatana na ucheshi na utani mwingi, kufanya tathmini ya Jumuiya Ndogogo kwa mtazamo wa kitaalimungu (teolojia) na pia kwa mtazamo wa kitaalimujamii (Sosholojia). Hapa ninatoa pongezi nyingi kwa mwandishi kwasababu sayansi za jamii kama vile socholojia, uchumi na zingine bado hazijapewa nafasi ya kutosha katika mchakato mzima wa uenjilishaji ndani ya Kanisa. Yeye ametoa mfano hai.

Nne, mwandishi pia, mbali na kujieleza kwa njia ya utani na vichekesho vingi, ameonyesha umahiri wake katika kujieleza kwa njia ya ushairi. Mashairi ni njia mojawapo kati ya njia muhimu za kufundishia kutokana na ukweli kwamba ni sanaa inayoruhusu wazo la msingi kurudiwa mara kadhaa mpaka likashika mizizi akilini. Wazungu husema “ repeation is the mother of learning!” Tunashuhudia kwamba hata na Zaburi, katika Biblia, takatifu zimeandikwa kwa mtindo wa ushairi.

Tano, mwandishi amefanikiwa kukifanya kitabu chake kiwe cha kuaminika kwa kutumia mbinu mbalimbli. Kwa mfano amefanikiwa kuthibisha hoja zake kwa kunukuu mistari ya kutosha kutoka katika maandiko matakatifu (uk 61 nk), maandiko ya mababa wa kanisa (uk 56, nk) na wasomi maarufu katika elimu dunia (uk,nk).

Sita, mwandishi amefanya jambo la maana sana kuweka Maktaba ya Jumuiya ndogondgo za kikristu mwishoni mwa kitabu (uk 190-191). Orodha ya vitabu aliyoitoa ili waumini wajisomee na kujifunza zaidi juu ya Jumuinya ndogo ndogo, ni muhimu. Orodha yake ina upungufu kidogo kwa kutokuwa na vitabu kama: Kanisa Mahalia, cha padri Jordan Nyenyembe, Injili ya Tano, cha padri Joseph Healey; ingawa mwandishi amemtaja Healey, kwenye kitabu chake na kumbatiza “Mwanajumuiya damu” kuelekeza watu kusoma kitabu chake ingekuwa bora zaidi. Vitabu vingine ambavyo havitajwi ni Katekesi Hai, cha marehemu Askofu Christoper Mwoleka, “Do this” nacho cha Marehemu Askofu Christopher Mwoleka na “The Church as a Family” nacho cha Marehemu Askofu Christopher Mwoleka. Ni bahati mbaya kwamba baba huyu wa Jumuiya Ndogongo hapa Tanzania, hatajwi,kabisa katika kitabu cha Padri Kaombe, nina imani ni kwa bahati mbaya au kupitiwa tu, lakini kuelekeza watu kujisomea vitabu vyake ingesaidia kukokamaza Jumuiya ndogodogo. Mfano, mtu akisoma vitabu ya Mwoleka, hawezi tena kuuliza maswali kama vile swali 11 na 12: “Viwawa hawaendi JNNK wanasema ukishaenda VIWAWA JNNK haina haja. Chama cha kitume na JNNK sio vitu tofauti (Swali 11) na “ Naomba tofauti ya JNNK ya vijana na ya wakubwa” (Swali la 12). Mwoleka, anaelezea vizuri idara zaidi 10 katika Jumuiya ndogondogo za Kikristu, idara hizi zinaonyesha vizuri kila mtu anavyoweza kushiriki katika Jumuiya ndogondogo, inaonyesha jinsi vyama mbali mbali vya kilei vinavyoweza kushiriki, jinsi mapadri na watawa wanavyoweza kushiriki. Inaonyesha mfumo unaoeleweka na kutekelezeka.

Saba, kuna sehemu ambazo Mwandishi, amejichaganya. Ukrasa wa 9-10, anasema hivi: “…..Hili ni la muhimu kwasababau JNNK ndio chemchemi ya uhai wa kanisa. Chemchemi ni eneo tete ambalo halipaswi kusumbuliwa na mizigo ya sheria, kwani kuna hatari ya kukausha ubunifu. Ni katika JNNK pekee utambulisho wa kweli waweza kutokea, na ili uweze kutokea zinapswa kuachiwa katika mambo kadhaa, tena ya msingi tu. Tuzingatie kwamba: ‘.. na pale palipo na Roho wa Bwana ndipo ulipo uhuru (2 Kor 3:17). Lakini Uk wa 13, anajipinga kwa maneno haya “…. Hapana mristo mwenye mitala haruhusiwi kuchaguliwa kuwa kiongozi wa Jumuiya…” . Je hapa si ni kuingiza sheria ambazo mwandishi mwenye amesema zinaweza kukausha ubunifu? Na je kama Jumuiya ndogondogo, familia zote ni za watu wenye mitala, inakuwa vipi? Mfano kama Karagwe, si jambo la ajabu kukuta Jumuiya nzima ina ndoa za mitala. Tena hawa wenye ndoa za mitala, wanashiriki vizuri kanisani, wanasali, wanatoa sadaka na kulisaidia kanisa katika shughuli mbalimbali. Na je, mtu anayetaka kuanzisha jumuiya ndogondogo Umasaini, afanye vipi? Ni kweli kwamba sheria zinakausha ubunifu. Upo mfano wa Jimbo Katoliki, la Rulenge, ambalo lilijenga Jumuiya ndogondogo kwa ubunifu mkubwa, lakini sheria zikatumika kukausha ubunifu huo na kuzizika Jumuiya. Katika eneo hili mwandishi hakuwa wazi. Hili ni eneo nyeti ambalo bila kujadiliwa kwa kina juhuzi za kujenga Jumuiya ndogondogo zinaweza kukwama. Kwa vile anaongelea ukomavu, ni lazima kuzichunguza baadhi ya sheria zinazokwamisha ukomavu wa Jumuiya ndogondogo.

Nane, mwandishi amefanya jambo jema kusisitiza jambo la kujisomea, kwamba waumini wafanye bidii kujisomea vitabu:
“ Moja kati ya desturi ambayo nimeipigia debe katika maandiko haya wito wa JNNK kuwa chemchemi ya utamaduni wa kujisomea. Kuwepo katika JNNK zetu au katika kanda, nyumba ya mtu ambaye watoto na watu wazima wanaweza kwenda kuazima vitabu ili kukuza uwezo wao wa kusoma, kujifunza imani yao, maarifa, elimu na stadi nyingine muhimu kwa maisha ya sasa” (Uk 106). Hili ni jambo jema kabisa, lakini pamoja na kupigia debe utamaduni wa watu kujisomea, mwandishi ana nafasi nzuri kupigia debe somo la teolojia kuwa wazi wa waumini wote. Milango ya vyuo vya teolojia ifunguliwe kwa waumini wote. Hadi leo hii elimu hii hapa Tanzania, imebaki kuwa ya mapadri, mabruda na masisita peke yao. Ili Jumuiya ndogo ndogo zipate ukomavu wa kweli, ni lazima teolojia iwe wazi kwa wote! Ukiangalia vizuri maswali yote yaliyoulizwa na wanajumuiya kwenye kitabu hiki cha Padri Kaombe, utakubaliana na mimi kwamba waumini hawa hawana elimu ya teolojia.

Kwa vile Jumuiya Ndogondogo ndicho kitovu cha uenjilishaji, kama anavyotwambia padri Kombe, na kwa kuwa mafundisho ya kanisa kuhusu haki za binadamu ni sehemu ya mchakato huo, kama ilivyotamkwa wakati kuzindua Kompendia ya Kanisa Katoliki Kuhusu haki za Binadamu mwaka juzi, basi ni mawazo yangu kwamba kama kitabu hiki kingeeleza namna elimu ya haki za binadamu inavyoweza kupenyezwa kwenye “mendulla oblongata” za waamini kupitia Jumuiya ndogondogo, basi kitabu hiki kingepata sifa zinazofikia asilimia 101, badala ya asilimia 100 za sasa!

VI. HITIMISHO.

Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri wanajumuiya na watanzania wote wakipate na kukisoma kitabu hiki ili waweze kufahamu basabau za msingi za mafanikio, mapungufu na namna ya kufanya maboresho panapostahili.

Lakini, kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya jambo moja zaidi katika machapisho mengine ya kitabu hiki katika siku za usoni. Waamini tutafaidika sana ikiwa ataeleza namna ambavyo yale mafundisho ya kansia katoliki kuhusu haki za binadamu, kama yanavyopatika katika Kopmpedia ya Kanisa Katoli kuhusu haki za Binadamu, yanavyoweza kupenyezwa na kufundishwa mpaka yakaeleweka kupitia Jumuiya Ndogondogo.

Maelekezo ya AMECEA ya 1979, juu ya Jumuiya ndogondgo, yanagusa nyanja zote za maisha yaani kichumi na kiroho. Kwa kiasi kikubwa ukomavu anaouelezea Padri Kaombe, katika kitabu chake umelalia sana upande wa kiroho: Kusali pamoja, kujuliana hali nk, Hakugusia upande wa kuzalisha mali pamoja na kupambana pamoja kujenga uchumi wa Jumuiya ndogondogo na hatimaye kujenga uchumi wa kanisa na taifa. Mfumo huu wa kiuchumi na kiroho, ulitekelezwa Rulenge, chini ya uongozi wa Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, ingawa Mwoleka ni marehemu na jumuiya zake zimezikwa, bado kuna vitabu na machapisho mbali mbali, watu wanaweza kujisomea na kuchotoka ujuzi, lakini pia bado kuna watu waliofanya kazi kwa karibu na Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, hawa wanaweza kusaidia kutoa ushauri na kushiriki kujenga Jumuiya ndogondogo katijka jimbo Kuuu la Dar-es-salaam na kwingineko ambako Jumuiya hizi zinakubalika.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

2 comments:

Komango Hill said...

Very interesting

Revocatus Paul said...

Very detailed and well analysed comments

Post a Comment