MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005
SASA NURU YA CCM INAANGAZA!
Rejea makala yangu iliyopita yenye kichwa cha habari: “ Kama nimesema uongo, nuru ya CCM, na iangaze”. Kwenye makala hiyo nilitoa nukuu ya Bwana Yesu, ambayo ningeomba niirudie kwa vile bado hatujafika mwisho wa safari:
“Ninyi ni kama chumvi ya dunia. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, itakolezwa na kitu gani? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika. Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa chungu, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote aliomo nyumbani. Vyivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” ( Matayo 5:14-16).
Niliandika makala hiyo kabla ya CCM kufanya uchaguzi wa mgombea wao wa urais kupitia chama hicho. Uchaguzi umefanyika! Wasi wasi wa watu kwamba Chama kitasambaratika, kwamba wanachama ambao kipenzi chao hatapitishwa watakimbia na kujiunga na vyama vingine, kwamba CCM itafanya makosa wakati kumchagua mgombea wake, kwa sasa utabiri wa Baba Taifa, kwamba upinzani wa kweli utatokea CCM, unaelekea kutimia, haikutokea! Kwa mshangao ya wengi mambo yamekwenda shwari. Hata hivyo watu wenye busara na hekima, watu wenye uchungu na taifa letu walitegemea yatokee yale yaliyotokea Chimwanga.
Ingawa mzee wa Dodoma, mwenye umri wa miaka 100, ambaye kama sikosei ni kati ya waasisi wa Chama cha CCM, hakufurahishwa na hotuba ya Rais Mkapa, pale iliposisitiza umuhimu wa vijana. Mzee huyu alikuwa na maoni kwamba ni lazima wazee watangulizwe. Hata hivyo wazee wanatangulizwa, maana bila ushauri wa wazee kama vile Mzee Kawawa, Mzee Mwinyi, Mzee Ngobale na Mzee Malecela, yaliyotokea Chimwanga, yasingetokea kamwe!
Kumbe chumvi bado ni chumvi na mwanga haujafifia, taa imetundikwa juu ya mlima wa Kilimanjaro! Chumvi na mwanga, ni Hekima, Busara na fikra pevu! Kamati kuu ya CCM, halmashauri kuu ya CCM na Mkutano mkuu wa CCM, wametuonyesha kwamba wao bado ni chumvi na hakuna haja ya kuwatupa barabarani ili wakanyagwe na wapita njia!
Hivyo basi ushauri wa kila anayelitakia mema Taifa letu ni kwamba hekima, busara na fikra petu, visiishie kwa uchaguzi wa Jakaya Kikwete. Safari bado ni ndefu sana. Bado kuna uchaguzi mkuu utakaoshirikisha vyama vyote vya siasa. Kuna wagombea wengine wa urais kupitia vyama vingine. Kuna uchaguzi wa wabunge na madiwani. Rushwa isitumike, vitisho visitumike, dola isitumike kukipendelea chama tawala. Chema chajiuza na kibaya chajitembeza. Kama CCM bado ni chumvi na ni mwanga watu wataichagua bila kutumia polisi na kumwaga damu.
Ina maana gani kutumia pesa kununua kura, kutumia vitisho na ubabe na baadaye kujigamba kwamba ni ushindi wa kimbunga? Ushindi wa kweli ni kushinda kwa mvuto, ni kushinda kwa kukubalika, ni kushinda kwa kuwa na sera inayotekelezeka, ni kushinda kwa kuwa na vision, ni kushinda kwa kutaka kutumikia na wala si kutumikiwa!
Hekima, busara na fikra pevu, iliyojionyesha Chimwaga, ijionyeshe kule Zanzibar. Ni upumbavu kuamini kwamba kule Zanzibar, hali ni shwari. Mvuto uonekane kule Zanzibar, kukubalika kuonekane kule Zanzibar, sera, vision na utumishi vionekane kule zanzibar.
Inawezekana Mheshimiwa Mkapa, ana mpango wake mzuri kuhusu Zanzibar, ambao ni siri yake, maana hata uchaguzi wa mgombea wa kiti cha urais kupitia CCM, ilikuwa ni siri kubwa aliyoitunza moyoni mwake. Kama ni hivyo, hicho ndio tunachokiomba. Tunaomba amani, utulivu na haki kule Zanzibar. Hakuna mtu anayetaka kuona vurugu na umwagaji wa damu.
Kabla ya uchaguzi wa Kikwete, yalisemwa mengi juu ya Rais Mkapa. Kuna waliosema kwamba Mkapa, alikuwa na mtu wake ambaye si Kikwete. Wakati wanachama wa CCM wanaendelea kujitokeza kuchukua fomu za kugombea, namba ilipofikia kumi, kuna waliosema kwamba chaguo la Mkapa, alikuwa hajachukua Fomu. Siku za kuchukua fomu zilipokwisha. Wakasema chaguo la Mkapa ni Mheshimiwa Sumaye. Wengine wakasema chaguo lake ni Balozi Dk Salim. Kuna waliovumisha kwamba chaguo lake ni Balozi Chokala. Wengine wakasema ni Mheshimiwa Kigoda na wengine wakasema chaguo lake ni Profesa Mwandosya. Hatukusikia kwamba chaguo la Mkapa ni Kikwete! Kumbe yeye alikuwa na lake moyoni!
Hotuba ya Mheshimiwa Rais Mkapa, wakati wa kufungua mkutano mkuu iliyokuwa imejaa busara, hekima na fikra pevu ilikuwa inamlenga Kikwete!
Rais Mkapa, alisisitiza achaguliwe Kijana. Tukifuata umri wa wagombea, aliyekuwa kijana ni Kikwete. Ingawa hapa Tanzania mtu mwenye umri wa miaka 55 huwezi kumwita kijana maana wastani wa kuishi kwa Mtanzania ni miaka 45! Lakini walivyokuwa Kikwete, ndio alikuwa kijana.
Rais Mkapa, alisisitiza achaguliwe mtu anayekubalika visiwani na Bara. Kutokana na kura za maoni, ambazo ni hakika Rais Mkapa, hakuweza kuzipuuzia, mtu aliyonyesha kukubalika ni Kikwete.
Rais Mkapa, alishauri achaguliwe mtu anayekifahamu chama cha CCM na aliyekulia kwenye chama hicho. Aliyekuwa na sifa hizo si mwingine bali Kikwete!
Ukiichambua hotuba yake yote ni kama yalikuwa maelekezo kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM, kumchagua Kikwete. Hakuna shaka kwamba Mheshimiwa Mkapa, aliitoa hotuba hiyo bila shinikizo la mtu au kikundi cha watu. Ni hotuba aliyoitoa kwa uhuru wake akiwa anasukumwa na hekima, busara na fikra petu, lakini hasa kwa kutanguliza uhai wa chama chake cha CCM na uhai wa Taifa letu la Tanzania.
Ili nuru ya CCM iangaze, ili CCM iendelee kuwa chumvi ya Taifa letu la Tanzania, hekima, busara na fikra pevu iliyomwongoza Rais Mkapa, kule Chimwaga, iendelee kumwongoza kipindi chote cha uchaguzi mkuu. Watanzania tupige kura zetu kwa haki na amani. Vyama vyote vya siasa vipate haki sawa. Wagombea wa CCM na wa vyama vingine vya siasa wapendekezwe na kuchaguliwa kufuatana na sifa zao, si kwa kupendelea au kutumia pesa. Madiwani na wabunge na wagombea wa urais wa vyama vyote wawe na sifa zinazofananafanana na za Mheshimiwa Kikwete. Wawe vijana, watu wanaokubalika, watu wanaovifahamu vyama vyao na wazalendo wa kweli.
Chimwaga ni mfano wa pili unaoonyesha kwamba busara na hekima imeanza kulitawala taifa letu. Mfano wa kwanza ni jitihada za busara zilizotumika kuvishawishi vyama vya upinzani kusitisha maandamano wakati wa mkutano wa amani ya maziwa makuu uliofanyika mjini Dar-es-Salaam. Mifano hii miwili inatofautiana na jinsi tulivyokuwa tumezoea kule nyuma wakati ubabe, na nguvu za dola vilikuwa vikitumika bila busara na hekima na wakati mwingine bila hata sababu za msingi.
Kama anavyosema Mheshimiwa Kikwete, sasa hivi ni wakati wa kuanza na ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. Sote tulenge kuijenga Tanzania yenye maendeleo ,haki, amani na utulivu. Nuru ya Tanzania iendelee kuangaza!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment