PESA ZA MAWE

UHAKIKI HUU ULICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA 2007

UHAKIKI WA KITABU: PESA ZA MAWE

1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA

Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni Pesa za Mawe na kimetungwa na Oscar Ulomi. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D Limited na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 411 38 X. Kimechapishwa mwaka 2006 kikiwa na kurasa 70. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ya Kisima cha Ujuzi ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. UTANGULIZI
Pesa za Mawe, ni kitabu cha hadithi ya kubuni. Hadithi hii imejikita katika mambo yanayotokea kwenye taifa letu. Malezi mabovu, ulevi na ujambazi, ushirikiano wa polisi na majambazi. Pesa, ngono na starehe ni vitu vinavyojitokeza na kuonyesha vinavyokwamisha maendeeleo. Hadithi inatuchorea barabara ya biashara haramu ya madini inayovuka mipaka ya nchi, kanda na hatimaye kufika katika masoko makubwa ya dunia. Hadithi inaonyesha jinsi maliasili yetu ya madini inavyoweza kuishia katika mikono ya watu wachache, watu wanaoabudu pesa na ufisadi.

Kitabu kinazo sura nane. Katika aya zifuatazo nitaoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.

III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.

Tanzania ni nchi yenye madini mengi. Na madini mengine kama Tanzanite, yanapatikana Tanzania tu. Madini haya yamekuwa kiuzwa kwa njia za magendo na kuzifanya nchi kama Kenya na Afrika ya Kusini, zisizo na madini ya Tanzanite, zihesabiwe miongoni mwa nchi zinazozalisha Tanzanite. Hili limetokea kwasababu Tanzanite inavushwa kwa njia ya magendo.

Jeshi la polisi linalalamikiwa kushirikiana na majambazi na kushiriki kuvusha biashara ya magendo.

Malezi ni kitu kinacholisumbua taifa letu. Kelele zinapigwa kila siku juu ya maadili. Kama wazazi wanalewa na kufanya mambo yanayokwenda kinyume cha maadili, ni lazima watoto watarithi maadili mabovu.

Kwa njia ya hadithi ya Pesa za Mawe, Osca Ulomi, anamtumia mhusika mkuu Rasta Kala Ndezi, kutufunulia ukweli wa mambo matatu yaliyotajwa hapo juu. Kala Ndezi, anakoswa dira akiwa mdogo. Kazaliwa kutokana na mzazi mkatili na mlevi. Uhalifu ukawa kitu cha kawaida kwake, naye akawa mtu muafaka wa kutumika katika uhalifu. Anashiriki mauaji na kuikimbia polisi. Alipoingia katika biashara ya kuuza “Mawe”, alijikuta ndani ya mkondo wa maisha ya kichinichini ya ufisadi uliokithiri. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.

IV. MUHTASARI WA KITABU

Sura ya kwanza na ya pili zinaelezea maisha ya familia ya Kala Ndezi, malezi yake na mazingira yaliyomzuka tangia anazaliwa hadi kuwa mtu mzima:

“..Alipoingia darasa la pili alibadili tabia na kuwa mkaidi hakupenda masomo na alisumbua walimu sana na wanafunzi wenzake… aliendelea hivyo hadi darasa la sita, hali ikawa mbaya zaidi, kwani alishaingilia uvutaji bangi, kunywa pombe, kulala nje ..” (uk 5-6).

Maisha ya Kala, yanakuwa mabaya hadi anakuwa jambazi sugu. Anashiriki mauaji ya Polisi, na kujificha. Maisha yake yanakuwa ya kujificha ficha.

“Kala alikuwa na fedha kiasi mfukoni. Alimfuata Merinyo akamwelezea mkasa mzima, Merinyo akamwongezea nyingine. Alimwendea Mwarabu aliyesaidia kumtorosha hadi Chekereni, nje kidogo ya mji wa Moshi…. Chakachui naye aliposkia mkasa mzima ulivyokuwa alimpeleka kwa rafiki yake mwingine upande wa Kenya” (Uk 11).

Sura ya tatu na ya nne, inatuonyesha safari za Kala, kule Tanga, Dar-es-salaam na Tabora. Kala, anaanza kushirikiana na wafanyabiashara. Anaanza biashara ya dhahabu. Hata tunapata mbinu zinazotumika kununua na kuuza madini kwa magendo.

“Kala hakupinga, kwani alikuwa na hamu ya kufahamu Dar-es-salaam. Walielekea Dar-es-salaam na walienda kuishi kwa jamaa yake Mwarabu aliyekuwa maarufu kwa kuuuza gongo na madawa ya kulenya huko manzese Uzuri” (uk 14).

“Huko machimboni walifika raia wa nchi za nje kulangua dhahabu hasa wakitokea Kenya, Mali, Ivory Coast, Nigeria na Ghana. Maarufu kuliko wote walikuwa raia wa Senegal waliojulikana kama Masenesene”(uk 17)

“Walipokaribia mpakani kiasi cha kilometa moja, Jabiri alisimamisha gari, akawaacha wateja wake wakipumzika garini, akaazima baiskeli ya mkulima mmoja ili akachunguze kulikuwa na maofisa wangapi wa uhamiaji na wangehitaji posho kiasi gani” (Uk 21).

Sura ya tano hadi ya nane, tunaingizwa kwenye biashara yenyewe ya madini. Kala, anavuka mipaka na kwenda Zambia hadi Zaire. Hapa tunachorewa barabara ya biashara ya madini na biasha nyingine inayofanyika kimagendo. Biashara hii inawakusanya watu wa kutoka nchi mbali mbali kama Senegal na nchi nyingine za Afrika. Biashara, inatanuka hadi Mashariki ya Mbali. Tunaelezwa jinsi rushwa inavyotembezwa kwenye mipaka ili kuruhusu magendo kupita. Na jinsi watu wanavyopitia njia za panya kuvusha pesa na vitu vingine:

“ Mousa na Kala walivuka mpaka kupitia njia ya panya kuwakwepa maofisa wa ushuru wa mpaka ni wasizishtukie feha zao nyingi zilizokwa ndani ya mbabegi”( Uk. 22).

V. TATHMINI YA KITABU.

Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Oscar Ulomi.

Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, hadithi yake inasisimua sana. Amefanikiwa kutuchorea barabara ya Pesa za Mawe. Kwa kusoma hadithi, mtu anakuwa na mwanga jinsi madini yetu yanavyopotea na kutajirisha nchi za jirani. Hii ni hadithi ya kubuni, lakini waswahili wanasema lisemwalo lipo, kama halipo liko njiani.

Pili, mwandishi amefanikiwa kuonyesha jinsi familia inavyochangia maisha na maendeleo ya mtoto. Kama wazazi wana maadili mabovu, ni lazima na mtoto atakuwa na maadili mabovu. Familia ni msingi wa malezi ya mtoto na msingi wa maadili ya taifa zima.

Tatu, mwandishi, hakujikita katika kubuni tu. Sehemu nyingi anazoziongelea, kama Moshi, Arusha, Tanga, Tabora,Dar-es-salaam hadi Zambia, zipo na anazielezea jinsi zilivyo. Ukisoma utasema kama hajaishi huko basi amesoma sana juu ya sehemu hizo.Matukio yanayoongelewa na mbinu zinazotumika, ni vitu vinavyotokea katika jamii yetu. Kuwaonga mapolisi ni kitu kinachofanyika kila wakati. Kuonga mpakani ni kitu kinachotokea kila wakati. Hivyo si kubuni tu!

Nne, mwandishi anaonyesha amefanya utafiti juu ya Pesa za Mawe. Mbinu zote anazoziongelea, zinaelekea kuwa za kweli. Mfano anafichua mbinu ya kuuza mafuta kwa magendo. Madreva wa magari ya mizigo wanaweka matanki ya ziada kwenye magari yao. Mpakani wanafikiri ni mafuta ya kutumia kwenye magari, kumbe ni mafuta ya kuuza.

“Siku waliyopanga kuondoka pamoja, gari kama 12 kutoka Tanzania, zote za kampuni moja, zilikuwa na nafasi kwenye matanki yao. Walipanga kuongeza mafuta kwenye gari nane, hivyo jumla ya lita 8,000 za dizeli zilinunuliwa. Waliondoka Ndola asubuhi na saa saba mchana walishafika mji mdogo wa mpakani wa Kasumbalesa, wakiwa wamepitia miji ya Kitwe, Chingola na Chililabombwe..” (Uk 38).


Pia kuna hili analoliongelea uk wa 25, linaelekea kuwa kweli, maana kuna uvumi kwamba Serikali ya Uganda inawapatia wananchi wake pesa za kununulia kahawa za Tanzania kwa magendo:
“ Uvumi ambao labda ulikuwa ukweli ni kwamba fedha nyingi walizokuwa nazo hao wageni, walipewa kama mitaji na serikali zao, wakafanye biashara kokote ulimwenguni na walirudisha sehemu ya faida kwenye benki za kwao” (uk 25).

Tano, kwa bahati mbaya au kwa makusudi mazima mwandishi, hapendekezi mbinu za kuzuia Pesa za Mawe. Labda hili analiacha kwa msomaji. Yeye anachokoza mawazo, ili watu wakisoma wajazie alipoachia. Pia, hakupenda kutuonyesha mtoto aliyepata malezi mazuri tofauti na Kala Ndezi, maisha yake yanachukua mkondo gani. Je, malezi mazuri yanachochea moyo wa kizalendo? Malezi mazuri yanamfanya mtu kulinda madini ya taifa na kuhakikisha yanauzwa kwa njia ambazo zitaleta faida kwa taifa letu. Labda na hili ametuachia sisi wasomaji.

VI. HITIMISHO
Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri watanzania kukisoma kitabu hiki cha Pesa za Mawe, ili wafahamu jinsi madini yetu yanavyopitia njia za panya. Ni imani yangu kwamba hadithi hii haikushuka kutoka mbinguni. Inaongelea yale yanayotendeka katika taifa letu. Hadithi hii inaweza kutusaidia kutafakari na kujadiliana miongoni mwetu ni njia gani inalifaa taifa letu Tanzania.

Lakini, kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya jambo moja zaidi katika uandishi wake siku za usoni. Atuchoree akina Kala Ndezi, wanaopambana kuzuia madini yetu yasipite njia za panya. Pia, tuwaone akina Kala Ndezi, waliolelewa kwenye familia zenye maadili mazuri. Kala Ndezi, ambao si majambazi! Ni imani yangu kwamba nchi yetu ina wazalendo, ina watu wanaokesha usiku na mchana kuhakikisha taifa letu linatembea katika mwanga. Hawa pia ni lazima waonekane katika tungo, nyimbo, hadithi na historia ya taifa letu.

Mwisho, kabisa niwahimize watanzania kusoma na kuandika. Jamii inayosoma vitabu na kuandika vitabu inapiga hatua kubwa katika maendeleo.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment