UA LA FARAJA

UCHAMBUZI HUU ULICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA 2009

UCHAMBUZI WA KITABU


1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA

Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Ua la Faraja na kimetungwa na William Mkufya. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Mangrove Publishers na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 698 11 5. Kimechapishwa mwaka 2004 kikiwa na kurasa 423. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii a Ufahamu ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. UTANGULIZI

Ua la Faraja, ni hadithi ya kubuni iliyoandikwa na William Mkufya. Hadithi hii inaelezea mazingira yanayouzunguka ugonjwa hatari wa UKIMWI.

Kitabu kimegawanywa kwenye sehemu nne pamoja na hitimisho. Sehemu hizo ni Hofu, Majuto, Faraja, Buriani na Hitimisho. Kila sehemu imegawanywa kwenye sura mbali mbali. Mazingira ya hadithi ni Jiji la Dar-es-salaam, eneo la Tandika ambako karibia wahusika wote wanaishi na kuyafurahi maisha katika baa ya Malaika, sehemu waliyoizoa na kuipenda sana. Mwandishi anayachora maisha halisi ya wakazi wa Dar-es-salam. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.

III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU

Mwaka 2001, TEPUSA, iliuchagua muswada wa Ua la Faraja, kuwa muswada bora na ukapata tuzo. Muswada, ulichapishwa mwaka 2004. Ua la Faraja, ni sehemu ya “Utatu Mtakatifu” wa William Mkufya, juu ya ugonjwa hatari wa UKIMWI. Vitabu vingine vitakavyofuata baada ya Ua la Faraja, ni Mau Nyikani na Ua Limenyauka. Taarifa tulizonazo ni kwamba mwandishi anazifanyia kazi sehemu hizo mbili zilizobakia.

William Mkufya ni mwandishi wa siku nyingi. Alianza kuandika kwa lugha ya kiingereza. Vitabu vyake vya mwanzoni ni “The Wicked Walk” (1977), alichokitafsiri yeye mwenyewe kwe lugha ya Kiswahili kwa jina la Kizazi Hiki (1980). Kitabu chake kingine ni “The Dilema”(1982).Kitabu chake cha tatu, alikiandika kwa lugha ya Kiswahili Ziraili na Zirani. Muswada wa kitabu hiki ulichaguliwa muswada bora 1999, na ulipata tuzo. Tafsiri ya kitabu hiki katika lugha kiingereza kwa jina la Pilgrims from Hell, imefanywa na mwandishi mwenywe, lakini bado kitabu hakijachapishwa.

William Mkufya, amejifundisha mwenyewe fani ya undishi kwa kuwasoma waandishi mbali mbali wa Amerika, Ufaransa, Ujerumani na Ugiriki. Amewasoma washairi mbali mbali na wanafalsafa wengi. Udadisi wake na umakini katika kuchambua mambo mbali mbali katika maisha, umemfanya kuwa mwandishi mashuhuri wa kuandika riwaya na hadithi za watoto. Hadi sasa ameaandika vitabu zaidi ya kumi vya hadithi za watoto.

William Mkufya, ni msomi aliyesoma Kemia na Botani. Digrii yake ya kwanza aliipata chuo Kiku cha Dar-es-salaam mnamo mwaka 1977. Baadaye aliendelea na masomo yake huo Budapest (Hungary). Alifanya kazi kama mbiokemia, mwalimu, Meneja uzalishaji katika kiwanda cha kioo, mkulima na sasa ni mhariri mkuu wa Magrove Publishers. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.

IV. MUHTASARI WA KITABU

Hadithi hii ina wahusika wengi kiasi mwandishi alilazimika kutoa majina yao mwanzoni mwa kitabu kama ilivyo kwenye michezo ya kuiigiza (Uk VI). Hata hivyo hadithi inaizunguka familia ya Ngoma na jirani yake Omolo. Ngoma, ni mtu aliyekengeuka na mgomvi. Aliambukizwa virusi vy Ukwimi na mmoja wa vimabada vyake na baadaye yeye akamwambukiza mke wake Tabu.

Kwa upendo wa watoto wake, dada yake Grace, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na kujali kwa Daktari Hans, Tabu aliweza kuukubali na kuupokea ugonjwa alioambukizwa na mme wake Ngoma. Kwa upande mwingine Ngoma, anabadilisha sehemu ya maisha yake na kuwa muumini wa dini ya Uislamu, lakini anashindwa kubadilisha tabia yake ya ugomvi. Anafarakana na watoto wake na kummgombeza mke wake wa kuifuata dini ya kikristu. Mwishoe, anajikuta peke yake akisaidiwa na jirani yake Omolo. Mwishoni kabisa, Omolo, lanafanikiwa kuleta upatanisho katika familia ya Ngoma.

Kuna baadhi ya wahusika ambao ni wanawake, lakini wanne tu ndio muhimu katika hadithi nzima. Kuna Asha, mbaye ndiye alikuwa mmiliki wa hoteli na Queen, mwanasheria mahiri. Hawa wote walikuwa vimada wa Ngoma. Maisha yao ya uzinzi yalipelekea kupoteza maisha yao kwa uongonjwa wa UKIMWI. Mwandishi anaonyesha wazi kwamba namna yao ya maisha ndiyo iliyosababisha vifo vyao.

Queen, mwanamke mzuri na mwenye mafanikio katika maisha, ndiye muhisika wa kwanza anayeanza kuugua. Mwanzoni mwa hadithi, Queen, anaanza kuonyesha dalili za ugonjwa, wapenzi wake wote akiwemo ngoma wanaanza kuogopoa. Baada ya miezi minne, anaugua sana. Mwandishi anailelezea hali yake hivi:

“Queen alikuwa amedhoofu sana. Mashavu yalikuwa yamebonyea, kifua kimesinyaa na ngozi yake ilikuwa imepauka na kuwa kavu kama mtu aliyekuwa kwenye mavumbi (Uk 157)… Fizi zilikuwa nyekundu mno, zenye dalili za vidonda. Lile tabasamu la uzuri alilokuwa nalo zamani sasa lilikuwa limegeuka kuwa la kutisha (Uk 158)…Unene wote uliompa umbile zuri ulikwishasinyaa, amekuwa mweusi., weusi usiovutia. Alikuwa kama nuru ya mwili wake imeingia giza. Sehemu zake za siri silitoa harufu kali kutokana na vidonda vilivyoshambulia nje na ndani (Uk.166).”

Queen, anaamua kuyamalizia maisha yake. Mwandishi anatupatia tafakuri ya Queen, kabla ya kujiua:

“Kwani maisha ni nini hasa? Kuishi miaka mia na kuishi miaka hamsini kuna tofauti gani? Au, mimi ninayekufa leo na yule atakayekufa miaka mitano au ishirini baadaye, tuna tofauti gani?... Eti mtu anapotaka kujiua watu wanamkataza, akikamatwa anadhibiwa kifungo gerezani! Si upuuzi tu! Mimi sioni tofauti yoyote kati ya kuwepo na kutokuwepo (Uk 158)”

Baada ya miaka minne, Asha, naye anaugua sana. Huyu mama aliyekuwa mke wa mzungu tajiri, anaacha mali yake yote mikononi mwa watoto yatima ambao wazazi wao wamekufa kwa UKIMWI. Anafanya hivyo ili kuiokoa roho yake mbele ya safari!

“Katika miaka ile ulikuwa msimu wa wanaume kupenda wanawake wanene, wenye matako makubwa na kifua kilichojaa maziwa. Asha alikuwa na kila sifa ya umbile hilo (Uk 16)…Omolo alishtuka sana uona jinsi Asha alivyopwaya na kukonda. Hakuwa Asha yule aliyemzoe, mwenye matako manene, maziwa yaliyofura na mabega yaliyokuwa imara (Uk 314).

Mwanamke wengine wanaotajwa kwenye hadithi ni dada wawili Tabu na Grace. Tabu, anaugua. Kwa maoni ya mwandishi, huyu ni mtu anyeugua bila kuwa na hatia yoyote ile. Analetewa ugonjwa na mme wake. Kama ilivyo kwa baadhi ya wanawake katika jamii yetu.

Grace, ni karani wa Omolo, mhasibu katika kiwanda cha kusindika samaki. Grace, ni mwanamke wa mfano, ni wa kisasa lakini mwenye misimamo isiyoyumba, mkweli, mwenye roho nzuri na mwaminifu. Anampenda Omolo, ingawa Omolo hapendi uhusiano wao ubakie kwenye ngazi ya urafiki.

Omolo, likuwa kijana mkweli, mwenye roho ya kusaidia, lakini mwenye hulka ya uchunguzi wa mambo katika misha, na alikuwa na uwezo kifedha, lakini hakupenda kupoteza pesa zake kwenye pombe na wanawake. Hakuna kitu kilichoingilia ratiba yake ya upole na utu wema.Hakuwa na matatizo. Wasi wasi wake ni kuwa labda alikuwa na virusi vya UKIMWI, baada ya kufanya mapenzi siku moja na Queen. Lakini baadaye aligundua kwamba wasiwasi wake ulikuwa ni wa bure, hakuwa na virusi. Utata unajitokeza katika mawazo yake yenye itakadi ya kidhanishi. Mawazo kwamba maisha hayana maana yoyote. Mtu mwenye mwazo kama haya anaweza kuambukizwa virusi wakati wowote ule:

“Omolo alikerwa mno na mawazo kwamba yambidi ale, anywe, avae, alale, na ili aweze kufanya hivyo vyote, alilazimika kupika, kufua nguo na mashuka na kujiandalia chakula. Mawazo yote yaliyomwekea ulazima wa kutenda jambo yalimuudhi kama lile wazo la mama yake kwamba alilazimika kuwa na mke. “Mke wa nini?” alijiuliza. Hakuona haja ya kuzaa watoto wala haja ya kuishi na mtu, eti kwa makusudi ya kupikiwa na kutunziwa nyumba; au kwa kutoshelezwa haja za kimwili “Haja gani?” Mawazo ya kuwa na watoto yalimwogofya kama wazo la kuwa na mtu aliyeitwa mke” (Uk 26).

Mwandishi, anaendele kumchora Omolo:
“Ndio nini sasa? Alijiuliza. Omolo alipenda sana kujiuliza swali hili akimaanisha: fida ya misha ni nini? Kwa nini mtu ahangaike kufanya kazi ili apate pesa, akishazipata azitumie ziishe;kisha atafute nyingine nazo ziishe? Kuna manufaa gani au raha gani ya ajabu, iliyowafanya watu wayahangaikie maisha? Alishangaa kwa nini hata yule mwenye maisha ya shida anapougu na kukaribia kifo, hafurahi kwisha kwa shida zake akifa, bali anahangaika kujitibu ili apone halafu aendelee na shida zake” (Uk 30).

Mhusika mwingine kwenye hadithi hii aitwaye Dkt Hans, anayachukua maneno “Ndio nini sasa” ili kumpatia changamoto ya maisha Omolo:

“Unakimbilia nini Omolo? Unahangaikia nini katika misha, ikiwa furaha ya maisha yenyewe huitaki. Unasema unakimbilia ofisini. Ukifanya kazi unatafuta nini? Mshahara au kumtumikia mwajiri wako? Bila shaka unatafuta mshahara. Unatafuta pesa! Ukishazipata unazitumiaje? Je, wewe ni hodari wa kula vizuri? Je, wewe ni hodari wa kunywa? Je, wewe ni hodari wa kwenda kuona sinema nzuri na kusikiliza miziki mitamu? Siyo kweli! Grace liniambia habari zako. Unaishi tu almuradi unaishi. Ndiyo nini sasa?” (Uk 349).

Omolo, ni mtu wa kushangaza. Hana shauku na kitu chochote. Hasikiii furaha, mapenzi, chuki wala hasira. Alipoteza hisia zake miaka mingi ya nyuma baada ya kupoteza wazazi wake.

“Hakupenda kuwaona watu wakihuzunika kwa jambo. Kwake huzuni ilikuwa hisia inayokereketa, asiyoitaka imguse tena baada ya kumgusa huko nyuma. Huzuni ilimkumbusha machungu makali ya utotoni ambayo hakupenda kuyaona tena kwake au kwa wengine” (Uk 172).

Ingawa Omolo, alikuwa mtu mwema na mwenye kusaidia, lakini hisia zake hazikuguswa na misaada aliyokuwa akitoa. Alikuwa hawezi kuanzisha urafiki wa kweli na wa kudumu au kuwa na uhusiano wa kimapenzi. Kwa miaka sita alikuwa anashindwa kukubali penzi la karani yake Grace. Lakini baadaye kwa msada wa Dkt Hans, alikubli kuoana na Grace. Jambo la ajabu ni kwamba Grace, alipojifungua mtoto, kitendo hicho badala ya kumletea Omolo furaha kilimletea woga na mkanganyiko.

V. TATHMINI YA KITABU.

Mwandishi amefanikiwa kwa kutoa ujumbe wake juu ya ugonjwa wa UKIMWI. Anaonyesha elimu kubwa aliyonayo juu ya ugonjwa huu. Anazielezea hatua zote za ugonjwa huu vizuri sana. Hata hatua za mwisho za mgonjwa wa UKIMWI, amezielezea. Mfano: harufu mbaya, kutokwa na jasho, kukohoa damu na kuharisha.

Hadithi, imetulia, kiasi cha mtu kufikiria kwamba labda mwandishi alilenga kuueleze UKIMWI, kama magonjwa mengine, tofauti na maoni ya wengi kwamba ni janga la kutisha. Anakwepa misuguano na magomvi, badala yake anaelezea furaha ya watu kukutana na kufurahia maisha, matibabu na shughuli za mazishi. Hata magomvi ya jamaa wa Ngoma, kugombea urithi wa mali yanaelezwa baadaye.

Ugonjwa wa UKIMWI, unaelezewa kwa matumaini makubwa. Mwandishi anaonyesha kwamba mtu akipata matibabu mazuri anaweza kuishi zaidi ya miaka kumi baada ya dalili za mwazoni kujitokeza. Na anasisitiza kwamba wale ambao bado ni wazi waendelee kujikinga na kuwa waangalifu. Dkt Hans, ndiye kama msemaji wa mwandishi kwa kuhimiza kujikinga na kuacha ngono zembe:

“ Nilichelewa kuoa, ila sikuwa mchovu kama wewe, nilipenda kufurahi. Starehe ndizo zimenifanya nichelewe kuchagua mpenzi. Kila mwanamke niliyezoeana naye alivutiwa na mimi kwa sabababu nilipenda kwenda nao kila mahali: sinema, dansi, kwenye sherehe… Mshahara wangu wote niliumaliza kwenye starehe!”
“Ulikuwa mwasherati!” Omolo alimstu.
“Hapana! Wasichana niliowazoea waliheshimu sana miili yao. Wazo la ngono kabla ya ndoa halikuwepo..”
“Usiseme uongo!” Omolo alimkatisha na kuzidi kumsuta, “ Ulikuwa mzinzi”.
“Kweli! Sisemi hayo kwa sababu ya kuwa kwenye hii ofisi ya nasaha kwa wagonjwa wa UKIMWI. Hapana. Ni kweli, ujana wangu niliufurahia sana, lakini siyo katika ngono. Ila tulipenda sana kusimulia habari zake na kusoma vitabu vinavyoihusu, kama hiki..” Dkt Hans akaonyesha kile kitabu alichokuwa anasoma” (Uk 352).

Mwandishi ana ujumbe wa matumaini hata kwa watu wanaokaribia kufa. Imani yake ni kwamba kwa vile wana watoto hawawezi kupotea kabisa. Maisha yataendelea baada ya kifo kupitia kwa kizazi chao. Maisha yanaendelea kwa kurithisha kizazi uzoefu, mila na utamaduni. Mtu aliyepoteza utamaduni wake, anakuwa amepoteza na utu wake pia – anakuwa kama msukule;

“Watu sharti tuzoee kushereheka kifo kama tunavyosherehekea uzazi kwa sababu ni hatua za lazima na za muhimu katika huo mduara wa uhai. Mtu hufa, lakini kizazi kipo daima. La muhimu ni kuhakikisha kwamba yale tunayojifunza katika maisha tuyarithishe kwenye vizazi vyetu katika majando, mafunzo ya maadili na elimu ya watoto. Taifa la wapumbavu wasiokamilisha jando lao ni lile litakaloruhusu washenzi toka nchi za mbali kuingilia na kuvuruga maadili, imani, miiko na elimu ya watoto wao. Utu wa mtu ni ukamilifu wa jadi yake. Mtu asiye na jadi ni ndondocha…au msukule!” (Uk 415).

V. HITIMISHO.

Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri watanzania kukisoma kitabu hiki cha Ua la Faraja ili wapate ujumbe mzito ulio katika hadithi. Nina imani watajifunza mengi ya kuwasaidia kupambana na ugonjwa huu wa hatari. Pia watajichotea hekima juu ya umuhimu wa utamaduni, umuhimu wa kutunza mila, umuhimu wa ndoa na umuhimu wa kuzaa watoto.

Lakini, kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya haraka kukamilisha “Utatu Mtakatifu”, kwa kutuletea vitabu viwili vilivyobakia: Mau nyikani na Ua limenyauka.

Mwisho, lakini si mwisho kabisa, ni pongezi zangu kwa mwandishi. Amefanya kazi nzuri sana. Kwa vile mimi ni kati ya watu walioupitia muswada wake wa Ua la Fraja na kutoa maoni, ninampongeza pia kwa kusikiliza. Ni matumaini yangu na ya wengine pia kwamba Ua likinyauka, ni lazima lichipuke! Tukizingatia hoja ya mwandishi ya maisha kuendelea kupitia vizazi, ni lazima Ua lichipuke baada ya kunyauka!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment