UHAKIKI WA KITABU: MWENDO.
1.REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA.
Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Mwendo na kimetungwa na Elieshi Lema. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D Limited na amekipa namba ifuatayo katika sekwenzi ya vitabu duniani (ISBN): 9987 622 03 8. Kimechapishwa chapa ya kwanza 1998 na chapa ya pili 2004. Kina kurasa 71. Ni miongoni mwa vitabu vilivyokuwa kwenye Mradi wa Vitabu vya watoto. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ya Kisima cha ujuzi ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. UTANGULIZI.
Utangulizi wa kitabu hiki unapatikana kwenye barua ya Felisia akimwandikia rafiki yake Hamiata:
“Rafiki Mpenzi Hamiata.
Je hujambo? Mambo ya huku Mtwara ni mengi mno. Siwezi kueleza yote kwenye barua hii. Halafu tena naiandika kwa haraka shangazi asije akanikamata. Karatasi yenyewe nimeichomoa kwenye daftari la watu.
Sasa sikiliza kwanza. Usiwe na wasiwasi. Yale madhara yaliyomtokea msichana wa Moshi Vijijini hayatanitokea mimi, kwa hiyo tuliza roho mpenzi. Shangazi kaniambia kwamba kutahiri mtoto wa kike ni kama kuteka nyara haki yake ya kuwa mtu wa kike! Hamiata, sisi wasichana wanawake wote kumbe tuna nguvu za uhai ndani mwetu! Sasa kutahiri mtoto wa kike ni kuvunja nguvu hizo na kuzinyima uhuru.Kwa hiyo shangazi kasema kwamba ni lazima sisi wasichana tukatae katu kufanyiwa hivyo……
Mwandishi, anapinga ukeketaji. Ni kitabu kilichoandikwa katika mtindo wa vitabu vya watoto, lakini kikiwa kinailenga jamii nzima. Kitabu hiki kinazo sehemu tatu na ukrasa mmoja wa faharasa. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.
III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU
Ukeketaji unapingwa. Imeelezewa kwamba ni ukatili mkubwa dhidi ya wanawake. Wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakipiga kelele juu ya utamaduni huu. Zamani ukeketaji ilikuwa ni sehemu ya Jando na unyago. Ingawa Ukeketaji ni ukatili, si kila kitu kilichokuwa kikifanyika kwenye Jando na unyago ni kibaya.
Dini zimekuwa zikipiga vita utamaduni wa Jando na Unyago. Kwa vile dini hizi ni za kigeni, zilileta utamaduni mpya, na kuzika utamaduni wa kiaafrika, bila kufanya utafiti wa kutosha, ili kutoa mabaya na kuacha mazuri.
Hadi leo hii shule zetu hazina mfumo wa kumfundisha mtoto wa kike ni nini la kufanya pindi anapovunja uongo.
Wanaharakati wengi wamekuwa wakipinga ukeketaji, bila kuingia kwa ndani kuelezea ubaya ukeketaji na bila kuwa mbinu za kufundisha, ile mtoto wa kike mwenyewe, achukie ukatili huu.
Lakini pia tatizo la maadili kwa vijana wetu limekuwa likiisumbua jamii yetu. Watu wengi wanalalamika kwamba vijana wetu wanaachiwa waogelee jinsi wanavyopenda. Hakuna mwongozo kama ule uliokuwa ukitolewa kwenye mafundisho ya Jando na Unyango. Siku za nyumba hata vitabu vilivyokuwa vikielezea juu ya jando na unyago vilipigwa marufuku!
Akiwa na vitu vitatu kichwani mwake, chuki juu ya ukeketaji, baadhi ya mambo mazuri ndani ya Unyago na hitaji la mwongozo wa maadili kwa vijana, mwandishi aliamua kufanya utafiti kwa kuongea na watu mbali mbali kama Bi. Anastazia Jamdini wa Msibati; Bibi Yosefina Manuel, Berta Pangani, Martin Pundi na Habiba Badru, wote wa Dar-es-salaam; Bibi Rukia Nnete Ntanga na Bwana Athumani Likunda wa Lindi. Pia Mzee Jonas Lepe, alimsaidia mwanidshi kuchimba mila na desturi za Wamakonde.
Elieshi Lema, ni msomi, mwandishi na mchapishaji, mwanaharakati wa haki za Binadamu na mtetezi wa haki za wanawake. Kwa namna ya pekee, ameandika vitabu vingi juu ya maadili katika jamii. Ametumia njia nyepesi ya kutumia hadithi za watoto kuelezea mambo magumu na muhimu katika jamii yetu. Kwa kuangalia kwa haraka utafikiri anawaandikia watoto, lakini ukweli ni kwamba anawaandikia wazazi, ili wao wawasimulie watoto – ili katika utamaduni wa kusoma vitabu tuweze kujenga jamii yenye maadili mema. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.
IV. MUTASARI WA KITABU.
Kitabu kimegawanywa katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza inaelezea maisha ya muhusika mkuu Felisia, shuleni kwake. Felisia, anavunja uongo akiwa shuleni. Hapati msaada wowote. Jibu, si shuleni bali ni nyumbani. Na jibu la nyumbani si kingine zaidi ya Unyago. Sehemu ya pili inaelezea safari ya Felisia kwenda Mtwara, kuchezwa ngoma. Sehemu hii tunakutana na shangazi wa Felisia, ambaye ni mwanaharakati. Huyu anapinga ukeketaji, lakini anaunga mkono baadhi ya mafundiso ya unyango: “Nyago ni daraja.. na huu ni mwanzo tu. Unyago upo wa aina nyingi katika maisha. Aina nyingi, we utakuja uone. Huu unakutayarisha kwa hizo nyingine zitakazokuja baadaye utakapokuwa peke yako bila mama, bila shangazi au aba wa kukuongoza” (Uk 45) Sehemu ya tatu ni juu ya Felisia, anaporudi shuleni baada ya kuchezwa ngoma. Walimu hawana imani na unyago. Wanataka kumfukuza Felisia shule kwa vile alitoroka shule kwenda kuchezwa ngoma:
“… unajua wazi kwamba mambo ya unyago yameshapitwa na wakati. Ni kweli yalikuwepo, lakini hayo mambo sasa hayawezekani tena. Watoto hawawezi kuwa wnaacha shule kwa sababu ya mila tu. Eti mila, mila, hata kama hazima maana yoyote…”( Uk.61)
Lakini shangazi mtu anasimama kidete:
“… Mila ni sheria ambazo jamii imekubaliana nazo. Zilizo mbovu tutupilie mbali, zilizo bora tuweke, tuboreshe. Sheria hizi haziko katika maandishi lakini tunaziheshimu. Sasa wewe mwalimu, mtoto wa kike akivunja ungo darasani unamuambia nini?” (uk 62)
Muhtasari wa kitabu hiki umelala kwenye fundisho tunalolipata kwenye kitabu hiki kwamba ukeketaji ni ukatili lakini baadhi ya mafundisho ya unyago ni muhimu katika jamii. Haya tunayaona Felisia, anaporudi shuleni baada ya kutoroka kwenda kwenye sherehe za unyango kule Mtwara. Walimu, walitaka kumfukuza Felisia, maana aliondoka bila kuaga. Shangazi wa Felistia, anatoa changamoto :
“Sasa basi, tafuteni njia hawa watoto wafundishwe mambo haya. Mtoto wa kike asitupwe tu na kuambiwa ‘nenda nyumbani’. Tangu asubuhi mpaka jioni yuko na mwalimu. Nyie ni walezi vilevile, hamuwezi kumtupa barabarani tu na kusema, ‘ nenda nyumbani.’ Mtoto aelezwe linalotokea, maana yake, umuhimu wake. Mtoto aambiwe yeye ni mtu wa kike ambaye kibayolojia ana tofauti na mtu wa kiume. Halafu aelezwe la kufanya. Apewe tahadhari zake ajue jinsi ya kuishi kama mtu kike. Hiyo ndiyo kazi ya Unyago. Hayo ndiyo mambo niliyomfanyia Felisia. Hayo ndiyo ninayotaka mfanye”. (64).
Pia muhtasari wa kitabu tunaupata katika fundisho jingine kwamba Unyango ni daraja:
“ Unyago ni jadi. Unyago ni daraja. Linakutoa katika dunia ya utoto, linakuvusha na kukufikisha katika dunia ya utu uzima. Usipovuka hilo daraja unabaki umetekwa nyara katika dunia ya watoto. Wote tutakucheka. Wote. Mimi, mama yako, baba yako, ndugu zako, rafiki wanafunzi wenzako wote tutakucheka… Unyago ni daraja, kutahiri sio daraja. Huvuki kwa kutahiriwa. Unalemaa,unakauka, unakufa. Unakuwa kikagarosi-mtu maisha yako yote! Kutahiri ni ishara ya woga unaozidi kifani. Woga wa binadamu anayeogopa maisha. Kutahiri mtoto wa kike ni woga wa kuona jua la mchana linalostawisha viumbe hai. Jua linalokuza vilivyo vichanga hadi vinachanua na kujaza rangi na matunda aina kwa aiana duniani…..Wote hao ni wachawi waliotawaliwa na nguvu za giza la woga” (uk 44).
Muthasari unakamilika pale tunapopata yale yafundishwayo katika unyango. Mafundisho mengi yanakuwa kwenye nyimbo:
“ Naanza kukuambia
Yanayohusu mzazi,
Mwali, nakutajia mzazi,
Ujuwe waziwazi,
Mzazi wako ndo mwanzo
Wa yote asilani
Ukisikia mzazi
Ujuwe maanake ni nini
Heshima yake i wapi
Umuhimu wake ni upi….
Usihau heshima
Ili upate hekima
Mwali, nakutajia heshima
Isiyoachana na haki
Isiyokuwa kisima
Cha maji yasioyoenda.
Nasema pia usafi
Wa mwili
Usafi ndio sabuni
Ya mengi haya maisha.. (Uk 49).
Mwali, nakutajia mapenzi
Jama nakutajia mapenzi
Chukua mbawa uruke
Kwenye haki na uhuru
Mwali, nakuambia mapenzi
Yasiwe kamba shingoni
Yasiwe jiwe rohoni
Nakuambia mapenzi
Na yote mahusiano
Yasiwe kamba shingoni
Kukuvutia pabaya.
Tena nakuambia mapenzi
Yenye maana maishani
Kiini chake kiko kwako
Nafsi yako ndiyo chumvi
Ndiyo kiungo maalum
Nafsi yako ndiyo penzi
La kwanza, pia la mwisho
Halafu litachanua
Kama ua alfajiri
Kuwafikia wengine…(Uk 50-51)
Lakini fundisho muhimu linapatikana uk wa 45-46:
“Binadamu yeyote yule ana unyago. Asikudanganye mtu. Soma usisome, kila mara utapitia kwenye unyago katika maisha. Si nimekwambia kwamba unyago ni daraja. Haya madaraja tunayajenga sisi binadamu. Mengine tunayabomoa na kujenga tena ya ina nyingine. Wazungu wana unyago kama sisi, unyago unaoendana na maisha yao. Usidanganywe nao ukiwa huko shuleni kwamba wao hawana. Wajanja wale, walikuja wakutuambia sisi waafrika kwamba madaraja yetu ni mabovu, tuchuke yao ya dini. Tulipokataa wakatulazimisha, wakatufunga, wakaatuuwa, wakachoma nyumba zetu na vitu vyetu vya sala. Tukanyooka, tukaacha madaraja yetu tukachukua yao. Tukadharau yetu, tukajidharau wenyewe na maisha yetu na mila zetu na njia zetu za kuishi. Tukapenda kuwa kama wao bila kuwajua wao wala dunia yao.”
V. TATHMINI YA KITABU
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathimini ya kazi hii aliofanya Mheshimiwa mama Elieshi Lema.
Kwanza kabisa lazima niseme kwamba mwandishi amefanikiwa kuonyesha ukatili wa kumkeketa mtoto wa kike kwa upande mmoja, na upande mwingine kuonyesha baadhi ya faida ya Unyago. Ingawa ukeketaji ni sehemu ya Unyago, yeye anahoji: “ Ni watu gani hao wanaotahiri watoto wao kama washenzi? Ni nani hao wanaotaka watoto wao wakauke, walemae, wawe vikaragosi maisha yao yote? Ni nani hao washenzi wasiokuwa na ustaarabu?” (uk 44). Anaonyesha ubaya wa ukeketaji, lakini anaonyesha faida ya kuzingatia utamaduni wa Unyago!
Pili, ni ile changamoto kwamba hadi sasa hivi hakuna mfumo katika elimu yetu wa kufundisha mambo muhimu yanayojitokeza kwenye miili ya vijana wanapokuwa na kuingia katia hali ya utu uzima. Felisia, anapovunja ungo, hapati msaada shuleni – hadi anakimbilia nyumbani!
Tatu, ni kwamba mwandishi amefanikiwa kutumia lugha nyepesi kuelezea mambo ambayo ni mazito na yanaleta kelele nyingi katika jamii. Viongozi wa dini wanapinga utamaduni wa Jando na Unyango. Wanaharakai wanapinga ukeketaji. Lakini hakuna njia za kuwafunulia watu kwanini jando na unyango ni mbaya au kwa nini ukeketaji ni ukatili. Kupitia hadithi ya Mwendo, mtu anaona ukweli yeye mwenyewe. Hivyo mwandishi, anafundisha, anaonya,nakemea, analaani na wakati huohuo anaingia uwanja wa mapambano!
Nne mwandishi, anafanikiwa kutufundisha kuacha kusema kwa maneno, bali tufanye matendo. Kama yeye ameonyesha kimatendo kwa kuandika kitabu kinachoelekeweka kwa watu wote, wakubwa kwa wadogo.
V. HITIMISHO.
Kwa kuhitimisha, ninawasharui wazazi kukisoma kitabu hiki cha Mwendo. Ni kitabu cha watoto, lakini umuhimu wake ni wa jamii nzima. Hata hivyo yale yanayoongelewa katika kitabu hiki ni jukumu la wazazi kuwafundisha watoto. Ni jukumu la wazazi kusisitiza umuhimu wa unyago. Ni jukumu la wazazi wakishirikiana na serikali kuunda mifumo ya Jando na Unyago ili ifundishwe mashuleni.
Kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya jambo moja zaidi la kutengeneza filamu ya kitabu hiki. Filamu au mchezo wa kuingiza kwa kutengeneza mikanda, unaweza kusambaza ujumbe kwa haraka. Jamii yetu inaonyesha uvivu wa kusoma vitabu , lakini inaonyesha kasi ya kupenda kuangalia filamu na mikanda. Kitabu hiki na vingine vingi alivyoviandika akiviweka kwenye filamu na mikanda, atakuwa ameongezea kwenye mchangao ambao mekweisha utoa katika jamii yetu.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment