MANGULA ANA MAANA GAZNI?

MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

MANGULA ANA MAANA GANI?

Kwa vile hakukuwa na ushahidi, na kwa vile tumekuwa tukiamini kwamba CCM ni chama cha watu makini, chama chenye uzoefu wa uongozi wa muda mrefu, chama kilichoasisiwa na mababa wa taifa letu, chama cha wazalendo, wapenda demokrasia, wapenda utandawazi, watu wenye hekima na busara na wachamungu, tumekuwa tukipuuzia “uzushi” uliokuwa ukienezwa kwamba CCM inajua “Kuwakolimba” wapinzani wake, na kwamba inajua kuwashutulikia waasi wa chama hicho kiasi cha kuwafilisi na kuwalazimisha kurudi kwenye chama hicho wakiwa wamepiga magoti na kuwalisha matapishi yao. Imekuwa ikitolewa mifano mingi. Utasikia wanasema mtu Fulani biashara yake imekwenda vibaya kwa vile alihama Chama Cha Mapinduzi, anabambikizwa kodi nyingi hadi anachanganyikiwa na kufilisika. Kuna watu tunaowajua si wana CCM, moyoni mwao hawaipendi kabisa CCM, lakini wanapeperusha bendera za CCM kwenye biashara zao ili mambo yawanyookee, ili wakwepe ushuru bila kuguswa. Imekuwa ikisemwa kwamba serikali inawafahamu walarushwa wote na ikitaka kuwakamata ni siku moja, lakini wengi wao ni wanaCCM, wapenzi wa CCM, ndugu za wanaCCM au marafiki wa wanaCCM. Imekuwa ikisemwa kwamba ndani ya CCM kuna neema na usalama na nje ya CCM hakuna usalama wala neema! Tumekuwa tukipinga mambo haya kwa nguvu zote maana huwezi kuamini kila lisemwalo vilabuni kwenye pombe, vijiweni, kwenye daladala, kwenye bao na kwenye mikutano mingine isiyokuwa na mwenyekiti wala agenda. Lakini pia tumekuwa tukipuuzia porojo hizi kama tulivyotaja hapo juu kwa kuzingatia heshima na thamani ya chama hiki kikongwe.

Lakini akitamka Mheshimiwa Philip Mangula, Katibu mkuu wa chama tawala. Mangula, tunayemfahamu kwa umakini wake, uzalendo wake, usomi wake, uchapakazi wake. Mangula, ambaye hadi dakika hii tunashindwa kuamini kama aliyatamka kwa kutaka, kwa uhuru na kwa hiari yake mwenyewe au alipata shinikizo la aina Fulani. Shinikizo la kuogopa “Kukolimbiwa”. Kutamka wazi kwenye vyombo vya habari ambavyo vinasikilizwa na watu wa nje na ndani ya nchi. Akasema kwa majivuno na majigambo kwamba wamekuwa wakiwashughulikia watu waliokihama chama. Na kuendelea kutoa ruhusa kwa yeyote anayetaka kuwahoji watu hawa walioshughulikiwa na chama kufanya hivyo, inatulazimisha kuyaamini yote ya “giza” yaliyokuwa yakisemwa juu ya chama hiki kigongwe katika taifa letu. Tusipokubali, tutakuwa tuna matatizo akilini mwetu. Inashangaza, inatisha, inavunja moyo, inaleta wasiwasi na mashaka makubwa, lakini huo ndio ukweli. Hatuwezi kuyaita maongezi ya walevi, porojo na michapo ya kupitisha wakati. Katibu mkuu ni mtu mzito katika chama, akitamka ni chama kimetamka. Vinginevyo chama kingekuwa kimetoa tamko la kumkana Mangula!

Ingawa vichwa vya habari katika magazeti vilikuwa vinaogopesha: “Mangula awaonya wagombea urais,..
Awataka wasilogwe kuhamia upinzani,… Ahoji waliohama 1995 wako wapi?… Asema asiyejua kufa na aangalie kaburi,… Asema waulizeni waliorejea CCM.” Haina tofauti na yale aliyoyaongea katika kipindi cha Je, Tutafika, kinachorushwa kupitia televisheni ya CTN ya jijini Dar-es-Salaam. Aliyoyasema ndio yaliyoandikwa bila kuwekewa chumvi.

Wameyasikia watanzania. Wameyasikia viongozi wetu wadini. Viongozi hawa wamekuwa wakituhimiza kutowachagua viongozi wanaotoa rushwa na wale tuliowachagua miaka mitano iliyopita lakini hawajatimiza ahadi zao. Sasa wanasema nini juu ya Mangula. Wanasema nini juu ya kiongozi huyu wa juu wa chama cha mapinduzi anayesema waziwazi kwamba wamekuwa wakiwashughulikia watu waliokihama chama chao. Na wataendelea kuwashughulikia wale watakaologwa kukimbia mwaka huu. Wanasema nini juu ya hali hii inayotaka kuwalazimisha watanzania wote kuwa wana CCM. Maana nje ya CCM, hakuna usalama. Ni kweli kwamba nje ya CCM, hakuna usalama? Na kama ni kweli, ni nani mtetezi wa Katiba yetu? Ni nani mtetezi wa wanyonge? Viongozi wa dini wanajiweka upande gani? Upande wa usalama? Ndani ya CCM? Nao pia wanaogopa kushughulikiwa?

Siku za nyuma Kanisa Katoliki lilikuwa na theolojia mbovu iliyofundisha kwamba nje ya Kanisa Katoliki hakuna wokovu. Ni sawa na kusema kwamba nje ya Kanisa katoliki hakuna usalama. Theolojia hii imetupiliwa mbali baada ya kuona hali halisi ya dunia hii kuwa na watu wanaomcha Mungu kupitia imani mbalimbali na dini mbali mbali. Ukweli kwamba haiwezekani mamilioni ya watu ambao si Wakatoliki wawe nje ya wokovu. Wanateolojia wenye busara na hekima, walifutilia mbali theolojia hii ya kiwendawazimu.

Kama chama kinachotawala nchi yenye watu zaidi ya milioni 35, na bado kinaamini kwamba watu wenye usalama ni wale walio ndani ya CCM, ni hatari kubwa. Hii ni mitazamo ya Kinazi! Ni fikra potovu ya kuamini kwamba kuna wateule wachache. Mungu, anawaumba wengi, anawaita wengi kumfuata, lakini wateule ni wachache. Fikra za Kinazi, ni sumu kubwa katika maisha mwanadamu. Dhambi hii ni lazima ikemewe kwa nguvu zote. Viongozi wetu wa dini wana wajibu wa kukemea matamshi kama haya. Kama wanaogopa kukemea kwa kuogopa usalama wao, basi hawana maana yoyote kwa taifa letu. Hawatufai! Wameyasikia aliyoyasema Mangula, wamechukua hatua gani? Wanabembeleza upendeleo wa serikali? Huo ni usaliti mkubwa kwa waumini wanaowasikiliza, kuwaheshimu na kuwafuata.

Mtu kuhama kutoka chama kimoja cha siasa kuiingia kingine ni jambo la kawaida. Inatokea duniani kote. Hii ndiyo demokrasia! Vyama vyote ni vya watanzania na viko chini ya katiba. Ni vyama ambavyo ni lazima vilinde masilahi ya nchi na masilahi ya kila Mtanzania. Hivi ndivyo walio wengi tunavyoviangalia vyama vya siasa. Sera, zinaweza kutofautiana, lakini uzalendo uko palepale. Pamoja na katiba ni lazima tuwe na mambo ambayo hata kama kikiingia madarakani chama cha namna gani hakiwezi kuyabadilisha jinsi kinavyotaka.

Mangula, anataka kuturudisha nyuma. Tumeshatoka kwenye enzi za chama kimoja. Dunia nzima sasa hivi inaimba wimbo wa vyama vingi na demokrasia. Matamshi yake kwamba aliye ndani ya CCM asilogwe kuhama na akihama atashughulikiwa kama walivyoshughulikiwa waliokihama chama hicho 1995, ni kinyume kabisa cha demokrasia. Haya ni matamshi ya utawala kiimla, kidikteta na kifashisti. Kwanini mtu asiwe na uhuru wa kukihama chama kama anaona akiendani na matakwa yake, akizingatia matakwa na masilahi ya wananchi walio wengi.

Vitisho anavyovitoa Mangula, havina tofauti na vitisho na vitendo vya kigaidi. Misemo kama: Asiyejua kufa na aangalie kaburi. Ni ugaidi mtupu! Kama dunia nzima inaupigia kelele ugaidi, basi na huu wa CCM, usitupwe kando. Ugaidi hauna rangi wala kabila.

Mwenyekiti wa CCM, akisema atatumia nguvu zake zote na nguvu za dola ili CCM ishinde, katibu akasema hakuna usalama nje ya CCM. Inatisha na kuleta maswali mengi. Tunaelekea wapi? Kuna njia ipi ya kukwepa machafuko? Je, ni watu wote wataogopa dola na kuogopa kushughulikiwa na Mangula, watakaa kimya? Rushwa izagaae, ufisadi utawale, nchi iuzwe na chama kiendelee kushika utamu? Tunalazimika kuamini kwamba kuna watanzania watakao sema hapana. Na watanzania hawa baadhi yao ni wanaCCM na wengine ni watanzania wasiokuwa na vyama. Tanzania ya 1995 ni tofauti na Tanzania ya leo ya karne mpya. Tukumbuke pia kwamba Tanzania ina wananchi zaidi milioni 35, wanaCCM si zaidi ya milioni 4. Hii ina maanga gani?

Labda ndio maana mambo mengi hayaendi vizuri sehemu nyingi. Nje ya CCM, hakuna usalama, hakuna neema. Tumekuwa tukiitetea CCM dhidi ya malalamiko kwamba majimbo yaliyowachagua wapinzani yalipuuzwa makusudi kusudi wakome na kushika adabu na kurudi ndani ya CCM, ndani ya usalama, ndani ya neema. Sasa tumepata jibu. Kama CCM, inaweza kuwashughulikia wanachama wake waliohama na kuingia upinzani, itashindwaje kuyashughulikia majimbo makorofi yanayowachagua wapinzani? Tunaweza kuyataja majimbo yaliyowachagua wapinzani na jinsi yalivyowekwa pembeni, huduma za muhimu ni za wasiwasi. Barabara hazitengenezwi, shule hazishughulikiwi nk.
Chama cha siasa kilicho bora, kinachofuata mfumo wa demokrasia na ambacho kimepata bahati ya kuiongoza serikali kwa muda mrefu, kinajitahidi kuboresha huduma zake kwa wananchi ili kiwavutie na ili kipate wanachama zaidi. Lakini chama cha siasa kinachotumia vitisho kama vya Mangula, kinakuwa na kasoro kubwa. Kitakuwa kinaogopa kuondolewa madarakani ili kiendelee kutunza mambo yasiyokubalika katika jamii. Viongozi wake wanaogopa usalama wao utakuwa matatani ikiwa chama kitashindwa kuendelea kushika utamu. Kinalazimika kuendelea kutawala kwa mabavu, udanganyifu na mbinu nyingine chafu.

Kwanini Mangula, awe na wasiwasi kwamba kuna wanaCCM, watakaokikimbia chama. Kama kuna haki, uwazi na demokrasia ya kweli, hakuna mizengwe ya kuzibiana njia na kunyimana nafasi za uongozi, kwani awe na wasiwasi? Kama kuna dalili hizo basi kutakuwa na tatizo kubwa ndani ya CCM . Na watu wakibaki ndani ya chama bila kukimbia si kwamba watakuwa wanakipenda chama, bali wanayapenda maisha yao. Watakuwa wanaogopa “kukolimbiwa”. Watakuwa wanaogopa kufanana na akina Stephen Wassira, Stephen Nyakyoma na Mzee Barongo “ Chakula Bora Shambani”. Ni nani anaweza kuamini Mzee Barongo, kwa mchango wake katika nchi hii, hivi leo anasukumana na vijana kwenye daladala za Dar-es-Salaam? Kosa lake kubwa - kukihama chama cha mapinduzi. Hali ya kubaki kwenye chama kama mfungwa, si kwa mapenzi bali kwa kulazimika kuyalinda maisha na masilahi ni hatari kubwa. Tanzania, haiwezi kuwa nje ya Historia ya kawaida. Mpasuko utakaotokea kwenye chama hiki si wa kawaida, ni lazima uwaguse waliomo na wasiokuwemo. Ndio maana kila Mtanzania analazimika kumkemea Mheshimiwa Mangula , kwa matamshi yake.


Kufuatana na matamshi ya Mangula, Katibu mkuu wa Chama tawala, chama chenye kushika utamu ni watanzania wangapi watapiga kura kwa uhuru. Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, ambaye naye anawania kuchaguliwa kama mgombea wa Urais, aliwaonya wakuu wa wilaya, kwamba yeyote atakayefanya uzembe na kuachia majimbo ya uchaguzi katika wilaya yake yachukuliwe na wapinzani atakuwa amejifukuza kazi. Uko wapi uhuru wa Mtanzania katika zoezi zima la kupiga kura? Iko wapi demokrasi?

Vitisho hivi vinapoanzia kwa wakubwa na wale walio ndani ya chungu, itakuwaje kwa wananchi wa kawaida wa kule vijijini? Wananchi wasiokuwa na habari za kutosha. Wananchi wanaolishwa kasumba kwamba kuvichagua vyama vya upinzani ni kuleta vita. Wananchi wanaozungukwa na vitisho vya kila aina, ukianzia na magonjwa, umasikini na ujinga. Mtu ambaye kipato chake si zaidi ya shilingi elfu tano kwa mwaka. Shilingi elfu kumi kwa mkupuo ni kitisho cha nguvu. Inatosha kumwambia chagua fulani, hawezi kuwa na swali. Je, atakuwa amechagua kwa uhuru?

Ni lazima tuseme hapana kwa Mangula. Tanzania si mali ya Mangula, si mali ya Mkapa wala CCM. Tanzania ni ya watanzania wote. Kila Mtanzania ana haki ya kufanya analotaka, kwenda anakotaka, kujiunga na chama chochote, kuhama chama au kuishi bila chama chochote cha kisiasa mradi asivunje sheria. Katiba yetu inataja hivyo na ipo kulinda uhuru wa kila Mtanzania.

Tunamshauri Mheshimiwa Mangula, awaombe msamaha wale wote walioshughulikiwa na CCM kwa vile walikihama chama mwaka wa 1995. Watu hawa warejeshewe heshima zao na taifa liwathamini si kwa vile walilazimishwa kurudi CCM, bali kwa mchango wao katika taifa letu. Pili aombe msamaha kwa watanzania wote kwa matamshi yake ya kulenga kutawanyang’anya watu uhuru wao. Matamshi ya vitisho. Matamshi ya kuvunja amani. Matamshi ya kutaka kutulazimisha sote kuwa wanaCCM, maana nje ya CCM hakuna usalama, hakuna neema. Kinyume na hapo tutaishikia CCM bango, nakutangaza kuwa ni chama cha kigaidi.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment