KATEKESI HAI YA KIUMBE KIPYA

UHAKIKI HUU ULICHAPWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA

UHAKIKI WA KITABU: KATEKESI HAI YA KIUMBE KIPYA.

1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA.

Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni: Katekesi Hai ya Kiumbe Kipya na kilitungwa na Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, mkoa wa Kagera. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Marianum Press, Kisubi Uganda. Kilichapishwa mwaka 1997, kikiwa na kurasa 177. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ya ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. UTANGULIZI.

Hiki ni kitabu cha mwisho cha Marehemu Askofu Christopher Mwoleka.Vitabu vilivyotangulia ni “Do This” na “The Church as a Family”. Mbali na vitabu hivi, Askofu huyu aliandika machapisho mengi ambayo kwa bahati mbaya hayajashughulikiwa vizuri ili watu waendelee kuyasoma baada ya kifo chake.

Katekesi Hai, imeandikwa katika mtindo wa Barua ya Kichungaji. Ni barua ambayo Askofu Mwoleka, aliwaandikia wakristu wa Rulenge, wakati wa kusherehekea miaka 100 ya ukristu katika jimbo hilo la Rulenge:
“ Barua hii ndio wosia wangu kwa Jimbo la Rulenge likiwa bado ni jimbo moja: Karagwe, Biharamulo, Ngara na Kimwani.Ni tarehe 1 Julai, 1995 wakati namalizia Barua yangu hii ya Kichungaji.Nisikia furaha nyingi moyoni. Hata hivyo ninaomba barua hii ya KATEKESI HAI itangazwe jimboni kote Rulenge taaarehe 4/10/1995 kwenye Siku Kuu ya Mtakatifu Fransisko wa Asizi ambaye tunamwomba awe Msimamizi wa Uchungaji huu.

“ Ninaomba barua hii itangazwe pengine kote nchini na kwa watu wote wenye mapenzi mema tarehe 25 Januari, 1996 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtume Paulo…” (Uk 165).
Aliandika akiwa mgojwa na akiwa anakaribia kustaafu kazi yake ya Uaskofu. Wakati akiandika kitabu hiki, alikuwa hana nguvu za kusimama. Alikuwa anabebwa na kuwekwa kwenye kompyuta. Aliandika kitabu hiki kwa kujikaza, labda ni kwa vile alikuwa akiandika kwa “moyo” wake, vinginevyo kazi hii asingeweza kuimaliza.

Marehemu Askofu Mwoleka, aliandika barua hii ya kichungaji, kwa kuona kwamba nguvu zake zilikuwa zinaisha na kazi yake ya kuunda na kusimika jumuiya ndogo ndogo ilikuwa haijakamilika. Pia alikuwa na wasiwasi wa mtu atakayemrithi, kama kweli ataweza kuendeleza kazi yake. Kwa kuandika aliamini hata kama mfuasi wake akipuuza kazi yake, vizazi vijavyo vitasoma na kuendeleza kazi ya kujenga jumuiya ndogo ndogo za Kikristu.

Marehemu Askofu Mwoleka, alistaafu Uaskofu mwaka 1996 na kuaga dunia mwaka wa 2002.Kabla ya kifo chake, alishuhudia kazi yake yote ikivurugwa na kuvunjiliwa mbali na Askofu aliyerithi nafasi yake, Askofu Severine NiweMugizi.Hata hivyo kilichoandikwa kimeandikwa. Kitabu hiki kinamfunuliwa msomaji nia na “Vision” aliyokuwa nayo Marehemu Askofu Christopher Mwoleka. Wale ambao wamekuwa wakimsikia tu, wanaweza kujisomea kitabu chake na kuchota kutoka kwenye kisima cha ujuzi.

Kitabu kina picha mbali mbali zinazoonyesha jinsi Askofu Mwoleka, alivyokuwa mtu wa watu na aliishi kati kati ya watu na kuishi maisha yao. Alilima mashambani, alifanya kazi viwandani, alishirikiana na wanasiasa hasa Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye walikubaliana vizuri juu ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Kitabu hiki pia kina michoro inayoonyesha muundo wa Jumuiya ndogo ndogo kuanzia jumuiya ya familia tatu hadi,kigango , parokia na Jimbo zima. Inashangaza jinsi Mzee huyu alivyofanikiwa kutengeneza michoro hii kwenye komputya za kizamani ambazo hasikuwa na progamu nyingi kama za siku hizi. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu hiki cha Katekesi hai, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.

III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.

Tangu miaka ya 1970 Maaskofu Katoliki wa AMECEA waliamua kwamba Jumuiya ndogo ndogo ziwe ndiyo vitovu vya Uenjilishaji ndani ya Kanisa.Askofu Mwoleka, aliuuchukulia uamuzi huu kuwa wa muhimu sana na alianza kuutekeleza mara moja.

Maarehemu Askofu Christopher Mwoleka, aliufananisha mpango huu wa Jumuiya ndogo ndogo na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, hasa mfumo wa nyumba kumi kumi na vijiji vya ujamaa. Ili kutekeleza mpango wa Jumuiya ndogo ndogo, alilazimika kujiunga na vijiji vya ujamaa na kuishi na wana vijiji. Wakati huo huo akiandika miongozo na maelekezo ya kuunda jumuiya ndogo ndogo.

Mwaka 1978, alipotembelea Ujerumani, alikutana na Jumuiya ya Integration, iliyokuwa inaishi mfumo wa Jumuiya ndogo ndogo, lakini kwa kiwango cha Juu.Si jumuiya za kusali na kujuliana hali tu, bali Jumuiya zinazozindikizana katika maisha yote ya kimwili na kiroho; kulea watoto pamoja, kufanya biashara pamoja, kuchukuliana katika udhaifu wa mwanadamu na kuishi historia ya Mungu na watu wake kwa pamoja. Jumuiya hii ya Ujerumani,Iliyoanzishwa na Na Mama Walbrecher, mme wake na wakiwa wamezungukwa na wanafamilia, wanateolojia, mapadri na vijana wanamapinduzi, ilibadilisha mwelekeo wa Marehemu Askofu Mwoleka, badala ya kufikiria Jumuiya ndogo ndogo, alianza kufikiria Jumuiya ya Mkamkilishano.

Mkamilishano, ilikuwa ni hali ya juu ya jumuiya ndogo ndogo. Yaani familia zaidi ya tatu, zinaishi pamoja kwa kushirikiana na kusindikiza katika nyaja zote za maisha; kiuchumi na kiroho. Jumuiya hizi zilikuwa zinaungwa na Mapadri na Masisita.

Jumuiya za Mkamilishano, ni kazi ya mwisho ya Askofu Christopher Mwoleka.Jumuiya hizi zilimchukulia muda wake, nguvu zake na raslimali nyingi. Ilikuwa kazi ngumu kuzifanya familia ziishi pamoja. Ilikuwa kazi ngumu kuwaweka mapadri, masista na walei katika mazingira mamoja.

Wakati Askofu Mwoleka, akikazana kuzijenga jumuiya za Mkamilishano, nguvu za mwili wake zilianza kumsaliti, uzee ulianza kumshambulia. Wakati jumuia zinashika kazi na kuwa na mwelekeo, akalazimika kustaafu.

Kwa upande mwingine Kanisa katoliki la Tanzania, lilikuwa likitilia shaka Jumuiya za mchanganyiko. Kwa maana ya Mapadri, Masista na walei kuishi kwenye mazingira mamoja. Badala ya kuangalia umuhimu wa mfumo na mambo ya msingi katika mfuno huo, wao waliangalia tofauti za kuundwa za maisha ya walei na wapakwa mafuta. Hali hii ilifanya Askofu Mwoleka, kuwa na mashaka ya kumpata mrithi wa kuziunga mkono Jumuiya za Mkamilishano. Hivyo kitabu cha Katekesi Hai, kiliandikwa kwa shinikizo na hofu ya uhai wa Jumuiya za Mkamilishano.

Baada ya kustaafu, hofu yake ilitimia. Askofu aliyemrithi, hakuipenda jumuiya hizi. Alihakikisha anazisambaratisha machoni pa Marehemu Askofu Christopher Mwoleka. Hivyo hata kabla ya kifo chake, aliamini kwamba uhai wa Jumuiya zake, utabaki kwenye maandishi yake na kwenye mioyo ya wachache waliokuwa wameiva. Kwa njia hii cheche zinaweza kusambaa na kuwasha moto mkubwa!

Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, alizaliwa Bukoba mwaka wa 1927.Mwaka 1954 alijiunga na Seminari ya Rubya. Baada ya kufuzu masomo ya falsafa na teolojia katika Seminari Kuu ya Katigondo, Uganda, na baadaye katika Chuo cha Mt,Edward, Totteridge, Uingereza. Alipata upadrisho mwaka 1962 kama padre wa jimbo la Rulenge.Baada ya upadrisho aliendelea na masomo Claver House, Uingereza hadi mwaka 1963 aliporudi nyumbani na kuendelea na kazi. Aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Askofu Alfred Lanctor mwaka 1967 na kufanywa Askofu wa Jimbo la Rulenge 1969,Alistaafu 1996 na kuaga dunia 2002. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.

IV. MUHTASARI WA KITABU.

Muthasari wa Kitabu hiki ni: KIUMBE KIPYA.Maarehemu Askofu Mwoleka, aliamini kwamba baada ya miaka 100 ya Ukristu, ni lazima kanisa liwe jipya na litumie mbinu mpya katika kujenga ufalme wa Mungu.

“ KATEKESI HAI isomwe kwa moyo wa kumtii Baba Mtakatifu ambaye anaomba sana mwaka 2000 Kanisa liwe jipya” (x)

“ Kwa moyo ule ule KATEKESI HAI itekelezwe kuwatii Maaskofu wa Tanzania ambao wameazimia kwamba dhamira ya Kwaresima ya mwaka 1996 iwe YOTE YAWE MAPYA”. (x).

Upya wa Kanisa, ni Kiumbe Kipya.Na kiumbe hiki ni Jumuiya za watu wanaoishi pamoja kama familia moja. Watu wanaosindikizana katika nyaja zote za maisha; kiuchumi na kiroho. Askofu Mwoleka, aliamini kwamba mwanadamu kuishi kwenye Jumuiya,ni mpango wa Mungu:

“ Hakuna mkutano wa Bunge lolote uliopata kufanyika katika Taifa lolote kujadili na kuazimia kwamba jua lingeanza kuchomoza magharibi na kutua mashariki. Hakuna wataalamu wanaojiuliza juu ya maumbile ya mwili wa binadamu na kupendekeza kwamba macho bora yangekuwa kwenye miguu, na bora masikio yangekuwa kifuani, na wakawa na uwezo wa kugeuza maumbile ya binadamu ya kawa jinsi wapendavyo. Kuishi kijumiya ndio Mpango wa Mungu. Kutamani kuishi kwa namna yingine isiyo ya ya kijumuiya ni kama kutamani jua lichomoze magharibi na kutua mashariki. Ni kutamani vitu ambavyo havitakusaidia kumpenda Mungu.Kwa mtu mwenye kiu ya kumpata njia ni moja: kwanza uwakumbatie jirani zake.” (Uk. 5,7,).

Ukrasa wa kumi tunakumbana na swali na jibu lake: “Je, lile JAMBO ambalo Mungu anataka tulishughulikie kwanza, na kulitekeleza tu hilo mengine yote tutapewa kwaziada, tuna hakika lile JAMBO ni jambo gai? Linaitwa UFALME wa Mungu au UTAWALA wa Mungu.Hutuwezi kujenga nyumba bila kuwa na mchoro wake kusudi iwe dira ya kuongoza juhudi zetu. Ni muhimu tufahamu kwanza UFALME wa Mungu una sura gani ndipo tuuendee kwa moyo wetu wote bila ku babaisha” (Uk 10).

“Sura ya Mungu ni sura ya jumuiya. Ufalme wa Mungu ni nyoyo za watu zilizokumbatiana katika upendo. Kati yao Mungu ndiye Mtawala. Huo ndo Utawala wa Mungu au Ufalme wa Mungu” (Uk 12).

“ Tukitaka kushughulika na jambo moja tu, kuujenga UTAWALA WA MUNGU, kila mmoja inampasa kuuvua utu wa zamani na kuvaa utu mpya.Niache kujihangaikia nitakula nini, nitavaa nini, na kuanza kuhangaikia wanajumuiya wenzangu kama wao ndio sasa wamekuwa mimi. Nijifunue kwao; Ningojee uamuzi wao; na Niwahangaikie wao” (Uk 15).

Katika kitabu hiki Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, anatuelezea kwamba mtu kabla ya kubatizwa anajihangaikia yeye mwenyewe. Lakini baada ya kuwa amepokelewa katiya wakriso, anaanza maisha mapya ya kuwahangaikia wanajumuiya wenzake ambao sasa amekuwa KIUMBE KIPYA pamoja nao. Anakuwa ameingia katika Utawala wa Mungu.

Katika kitabu hiki tunaelezwa kwamba, Kiumbe kipya ni kule kushiriki uchumi wa pamoja:
“ Tukishiriki mali zetu na karama zetu bila unafiki ule wa Anania na Safira, bilashaka matokeo yatakuwa na mafanikio kuliko kuishi bila kushiriki” (Uk 62).Na maelezo zaidi ni kwamba “ Uchumi wa pamoja, mgawanyo wa usawa na kuondoa tabaka ndivyo pekee vitakavyoondoa kabisa mashindano na vita ulimwenguni”. (Uk65).

Anaongeza kusema kwamba:
“ Visa vikubwa vya kukosa amani na kuleta vita ulimwenguni ni: kugombania mali; mali kutogawanywa sawa na kwahiyo kunyang’anyana; kugombania mamlaka ya utawala, yaani vyeo serikalini na katika nyanja za viwanda na biashara. Tukiishaweka azimio la kuacha yote tangu mwanzo, tunakuwa tumejitayarisha vizuri kwa kutoingia kwenye mashindano ya kugombania vitu hivi…” (Uk 66)

Katika kitabu hiki Marehemu Askofu Mwoleka, anachora mfumo mzima wa kujenga jumuiya za kuishi kiumbe kipya. Jumuiya za konyesha sura ya Mungu, hapa dunia. Anahimiza wanajumuiya kufanya na kupanga shughuli zote kwa pamoja:
“ Malengo ya huhudi zetu za kushughulika na nyanja zote zishughulishazo wanadamu wote ulimwenguni humu ni kusudi nyanja zote hizo zipangwe kwa namna ya kujenga Ufalme wa Mungu. Ufalme wa haki, amani na upendo. Ukristu hauwezi kuwaUkristu wa kweli bila kujitosa katika mambo haya” (Uk 86).

Tunaelezwa katika kitabu hiki kwamba, Kiumbe kipya na ujenzi wa Jumuiya ndogo ndogo, utaleta Ustaarabu mpya. Hii ni hatua ya kutakatifuza shughuli zote na vitu vyote:
“ Yapo mapokeo ya kubagua shughuli mbali mbali kwamba hizi ni shughuli takatifu, na nyingine ni najisi. Lakini Maandiko Matakatifu yanasema ‘ Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa’; Kufua nguo za kanisani ni kazi takatifu, lakini kufua nguo za kitandani ni kazi najisi.Kikombe cha kusomea Misa ni kitakatifu, lakini kikombe cha kunywea chai ni najisi.Hali ya kuwa mtawa ni hali takatifu, lakini hali ya kufunga ndoa ni hali najisi.Kazi ya kupika hostia za kutumika kwenye ibada Kanisani ni kazi takatifu, lakini kazi ya kupika chakula jikoni ni kazi najisi.Hata kama haitamkwi kuwa shughuli hizi nyingine ni “najisi” kuna mazoea ya kuzitofautisha sana na zile zingine” (Uk 102).

Maelezo zaidi ni kwamba: “ Ustaarabu Mpya unadai kuwa kazi yoyote inayotendwa kwa kuwapenda ndugu zetu na kuwafanya watu wapendane ni kazi takatifu. Watu watendao kazi hiyo wana wito kutoka kwa Mungu” (Uk 103).

Ustaarabu mpya ni kuzikumbatia karama zote. Ni kuachana na tabia ya kuwakumbatia na kuwaheshimu wasomi peke yao: “ Kuna karama za watu ambao hawana kisomo lakini hawa watu hawaangaliwi wala hakuna anayewajali. Karibu wote ni wale wanaoishi maisha duni kwa mfano, walio na tabi ya kujituma, walio na tabi ya upatanishi n.k…” (Uk 106).

Ustaarabu mpya unapingana na hali ile ya watu kutawaliwa na fedha, kwamba mwenye fedha ndiye Mtawala.Mfano wafadhili wetu kutoka nchi zilizoendelea walio tayari kusaidia nchi zinazoendelea wakitoa misaada ya fedha wanasisitiza masharti jinsi gani fedha hizo zitakavyotumika. Serikali za nchi zetu zinazoendelea hazipewi sauti ya kutosha kupendekeza matakwa yake…” (Uk 109).

Ustaarabu mpya unapingana na mifumo yote ya mashirika ya Fedha na Mabenki yanayotumika kuwanyonya watu na kuendeleza maovu duniani:
“ Ustaarabu mpya unajiuliza tufanye nini kukabiliana na uouvu huo ulionea kote ulimwenguni? Je haiwezekani kubuni mtindo wetu wa kutunziana fedha kusudi fedha zetu zisitumike kutendea maovu bali zijenge haki ulimwenguni?” (Uk 111).

Marehemu Askofu Mwoleka, anaendelea kuhoji katika kitabu chake cha Katekesi Hai: “ Sasa hivi Tanzania inaruhusu mabenki ya namna zote yaanzishwe nchini. Je, kwa nini sisi kwa sisi tusianzishe banki yetu ndogo, siyo kwa makusudi ya kufanyia biashara na watu wote, bali tu wanajumuiya halisi kutoka maparokia yote jimboni? Je, hatuwezi kuweka fedha zetu na kuweza kukopeshana sisi wenyewe kwa wenyewe?” (Uk 111).

Ustaarabu mpya unatutaka tujenge viwanda vya usalishaji: “ Nchi haiwezi kuendelea bila kuzalisha mali. Tanzani ina rasilimali ya kutosha kwa upande wa ardhi, madini na wanyama. Inao uwezo wa kujenga viwanda vya aina mbali mbali. Inao uwezo wa kujitajirisha na jitegemea, na ni aibu kuona tunaishi kwa kuomba omba na kuchukua madeni ambayo hatutaweza kulipa baadaye” (Uk 113).

Ustaarabu mpya unahimiza usafi wa Moyo si kwa watawa tu, bali kwa watu wote: Wanaofanya kazi viwandani, viongozi wa serikali, walei, watawa, kila mtu katika nafasi yake anaitwa kuishi usafi wa moyo. Watu wote wakilenga kuishi Kiumbe Kipya, ni lazima waishi usafi wa moyo.

Hivyo wito wa Jumuiya ndogo Ndogo, uwe ni kuwaondolea watu maovu na kuwapatia mema, Kuondoa njaa na kuleta Shibe, Kuondoa umaskini na kuleta utajiri, Kuondoa maradhi na kuleta afya njema, kondoa ujinga na kuleta uelevu, kuondoa mashindano na kuleta ushirikiano, kuondoa utengano na kuleta umoja, kuondoa uchonganishi na kuleta upatanisho, kuondoa unyonyaji na kuleta kukarimu, kuondoa ukandamizaji na kuleta usawa, kuondoa wizi na kuleta kujinyima, kuondoa uchoyo na kuleta ushiriki, kuondoa upweke na kuleta kujumuika, kuondoa wivu na kuleta kutakiana mema, kuondoa hasira na kuleta huruma, kuondoa dhuluma na kuleta haki, kuondoa udhalimu na kuleta kuaminiana, kuondoa ubwanyenye na kuleta unyenyekevu, kuondoa rushwa na kuleta uaminifu, kuondoa uhasama na kuleta upole, kuondoa kulipizana kisasi na kuleta kusameheana, kuondoa chuki na kuleta kusamehe, kuondoa uandui na kuleta urafiki, kuondoa vita na kuleta amani, kuondoa kukata tamaa na kuleta matumaini, kuondoa kifo na kuleta umilele nk.

Mwishoni mwa kitabu kuna maneno mazito ambayo kuyapuuzia kwa kiasi Fulani ni kufanya dhambi: “ Barua hii ndio wosia wangu kwa Jimblo la Rulenge likiwa bado ni Jimbo moja: Karagwe, Biharamulo, Ngara na Kimwani…Katekesi Hai imewapa Wakristu wa Rulenge, hasa Wachungaji wao, Dira, ya kuwaongoza na kuwawezesha kutambua walenge wapi ili kwa juhudi zao Ufalme wa Mungu ufike, Haki, Amani na upendo vitawale katika jimbo la Rulenge na popote ulimwenguni” (Uk 165).

V. TATHMINI YA KITABU
Baada ya kuona muhtasari wa kitabu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Marehemu Askofu Christopher Mwoleka.

Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira aliyoikusudia, kitabu hiki kinatoa mwanga na dira ya kuzijenga na kuzidumisha jumuiya ndogo ndogo.

Pili, Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, amefanikiwa kuonyesha upeo wake wa kanisa na ulimwengu mzima. Kwa mtazamo wake, maisha ya Jumuiya ndogo ndogo, si kwa wakristu peke yao, bali ni mfumo wa kutanzua matatizo ya dunia hii, matatizo ya vita, njaa na maafa mengine yanayoikumbuka dunia ya leo.

Tatu, amefanikiwa kuonyesha kile anachokiita “Ukristu Bandia”. Si kila mkristu anaweza kuwa na ushupavu wa kutamka neno hili, achia mbali Askofu wa kanisa Katoliki.Wako wengi wanaoliona hili, lakini woga na unafiki unawaziba midomo. Wanateolojia wengi wa kiafrika wanaliona hili, lakini wanalisema kwa kuzunguka, na wakati mwingine kwa lugha ngumu zisizoeleweka kwa watu. Lakini Marehemu Askofu Mwoleka, anasema wazi na kwa lugha nyepesi.

Nne, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuyaweka yale aliyokuwa akiyaishi na kuyafundisha katika maandishi. Walatini, wanasema maandishi hayafutiki. Mwoleka, amekufa, jumuiya zake zimefutwa, lakini maandishi yapo. Na kwa bahati nzuri yameandikwa vizuri kiasi kwamba, mtu hata akitaka kuunda jumuiya hizo leo hii anaweza bila matatizo makubwa.

Tano, amefanikiwa kuonyesha imani kubwa aliyokuwa nayo;ucha Mungu wa hali juu, utii wake kwa Baba Matakatifu na kanisa kwa ujumla, lakini pia jinsi ambavyo yeye hakuwa mtu wa kupokea tu, hakuwa mtu wa kufuata kila agizo na sheria za kanisa kama “Roboti”, alitumia akili na yeye kutoa mchango wake kama binadamu.

VI. HITIMISHO

Askofu Mwoleka, ni marehemu na Jumuiya zake zimezikwa. Lakini kwa vile Kanisa katoliki la Tanzania, bado linatamani kujenga jumuiya ndogo ndogo, si dhambi kama waumini na wachungaji wa kiroho wangesoma kitabu hiki na kuona kama dira ya Mwoleka ingewasaidia. Kuzifuta hizi jumuiya kule Rulenge, haina maana kwamba haziwezi kufanya kazi sehemu nyingine za Tanzania au Afrika ya Mashariki.

Leo hii Kanisa Katoliki la Tanzania, lina mpango wa kuanzisha Benki. Wazo hili alikuwa nalo Askofu Mwoleka kwa siku nyingi. Alitoa wazo hili, lakini hakusikilizwa. Kwenye kitabu cha Katekesi hai, anaelezea vizuri mfumo wa Benki ya kanisa.

Leo hii Kansia Katoliki linatafuta mfumo mzuri wa kuwatunza watoto yatima na wagonjwa wa UKIMWI. Kwenye kitabu cha katekesi hai, Marehemu Askofu Mwoleka, anatoa ushuhuda wa mfumo mzuri, tena mfumo aliouanzisha na ukafanya kazi, lakini ukafutwa na Askofu aliyemrithi.

Leo hii kanisa katoliki la Tanzania, linatafuta namna ya kushiriki katika kutanzua matatizo yanabolikabiri taifa letu, mfano matatizo ya ujambazi, rushwa, watoto wa mitaani, ukosefu wa ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa. Mfumo mzuri wa kufanya yote hayo, unaonyeshwa vizuri katika kitabu cha Katekesi Hai.

Askofu wa Rulenge, Mheshmiwa sana Askofu Severine NimweMungizi, ana jukumu kubwa la kusambaza vitabu hivi jimbo zima la Rulenge na Tanzania nzima. Yeye kama mrithi wake, ana jukumu la kuheshmu Wosia wa Askofu aliyemtangulia. Kitabu, hiki ni wosia, hivyo ni jukumu la mrithi kutangaza wosia huo. Yeye kama Askfou wa Jimbo ana uhuru wa kufuta yote ya mtangulizi wake, lakini hana uhuru wa kufuta au kuficha wosia wa Askofu waliyemtagulia.

Na,
Padri Privatus Karugendo.
Blogu: www.karugendo.com

0 comments:

Post a Comment