KUMBE LISEMWALO LIPO...!

MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.


KUMBE LISEMWALO LIPO……..!


Msemo wa Kiswahili usemao Lisemwalo lipo na kama halipo basi litakuwa njiani linakuja, ni msemo wa busara na hekima. Ndiyo maana ninawashangaa wanaokibeza na kukitelekeza Kiswahili. Lugha yetu imejaa misemo ya kufundisha na kuwagusa wale wanaoishi kwenye utamaduni na mila za Taifa letu la Tanzania. Hapa Tanzania, tumekuwa na tabia ya kuwashambulia waandishi wa habari , tunawaita wazushi, wapika majungu, wachonganishi na watu wa kuvuruga amani ya nchi yetu. Ukweli ni kwamba vyombo vya habari vinatekeleza msemo wa: Lisemwalo lipo na kama halipo litakuwa njiani linakuja.

Kipindi cha mwaka mzima, vyombo vya habari vimekuwa vikitaja majina ya watu wanaopanga kuwania urais ya nchi hii kupitia chama cha CCM. Kumbukumbu zinaonyesha rais Mkapa kukerwa na habari hizo, mbali na kuziita za uzushi, alikanya vyombo vya habari kuacha tabia ya kuishinikiza CCM, kuchagua mgombea anayependwa na vyombo hivyo vya habari. Kwamba si kazi ya vyombo vya habari kuwachaguliwa wanaCCM mgombea.

Wagombea wengine waliokuwa wanatajwa hawakukana wala kukubali. Ingawa kuna wengine walibeza uzushi wa vyombo vya habari. Wanasema watafuata utaratibu wa chama. Lakini, kama ilivyotabiriwa na vyombo vya habari, maana lisemwalo lipo na kama halipo liko njiani linakuja, wengine walianza kujitangaza kugombea kinyume na utaratibu wa chama chao cha CCM!

Majina karibu yote yaliyotajwa kule nyumba, yamejitokeza. Waliochukua fomu za kuwania urais kupitia CCM, walishatajwa – labda Balozi Chokala na wengine ambao wanafanya zoezi zima lionekane kama mchezo wa kuigiza au kitega uchumi. Maana wakijitokeza 20, milioni hizo zitakuwa zimeingia kwenye mfuko wa CCM. Hizi si kidogo, zinatosha kuwahonga wajumbe wa mkutano mkuu ili kumpitisha mtu anayeungwa mkono na “system”.

Ni vigumu sasa hivi mtu kusimama na kusema kwamba vyombo vya habari vya Tanzania vinaandika uzushi. Walisema Sumaye, atagombea, na ni kweli amegombea. Kwamba Shein, akigombea, Sumaye, atakuwa mgombea mwenza. Bado tunalisubiri hili kwa hamu, maana Lisemwalo lipo… Ndio kusema, na yale mengine yaliyoandikwa juu ya Sumaye, mazuri na mabaya ni kweli! Waliandika kwamba Sumaye ni mla rushwa, anafuja pesa za serikali, ana mashamba makubwa, ana majumba mengi kule Arusha na kwingineko. Sumaye kusimama na kukanusha, haifuti ule msemo wetu wa Lisemwalo lipo na kama halipo litakuwa njiani linakuja.

Vyombo vya habari viliandika kwamba Babu yetu mzee Malecela, alibadilisha dini. Aliachana na Ukristu na kuiingia Uislamu. Ingawa si dhambi kubadilisha dini, lakini pia si busara kubadilisha dini kwa lengo la kutafuta utumishi wa Umma. Mtumishi wa umma, huchaguliwa kwa sifa zake za kutenda kazi, uzalendo na upeo wake wa kuona mambo muhimu ya kitaifa na kimataifa, bila kuegemea kwenye dini, kabila, umbo na hali yake kiuchumi. Kwa maneno laini, si busara kubadilisha dini kwa kutafuta pesa. Dini, ni imani, ni kutafuta kuwa na mahusiano mazuri na Mungu na watu wake. Dini si kutafuta utajiri, cheo na madaraka. Dini ikitumiwa katika misingi ya kutafuta cheo na madaraka, inazaa vurugu na umwagaji wa damu. Historia ni mwalimu mzuri wa jambo hili. Mzee Malecela, alikanusha. Lakini hii haiondoi ukweli wa msemo wa Kiswahili wa Lisemwalo lipo na kama halipo litakuwa njiani linakuja.

Waandishi wakorofi wameandika kwamba baadhi ya wagombea waliojitokeza wamechota pesa NSSF. Kuna aliyechota bilioni 45 na mwingine 60. Kuna aliyepata dola milioni mia mbili kutoka Uarabuni. Pesa za kampeni. Pesa hizi ndio zinawanunua wajumbe wa mkutano mkuu. Pesa hizi ndio zinamwagwa hovyo na nyingine zinatumika kuwanunua baadhi ya waandishi wa habari. Pesa hizi zinatumika kununua magazeti. Gazeti, likimwandika vibaya mgombea, linanunuliwa lote na kuteketezwa kwa moto au kutupwa baharini na ziwani. Sasa hivi tunaweza kusema kwamba huu ni uzushi wa vyombo vya habari, lakini siku itafika tutakaposema kwa pamoja kwamba: Lisemwalo lipo na kama halipo…

Eti Obasanjo naye katuma pesa, Nyingine zimetoka Libya na nyingine Uarabuni. Yote haya yanaandikwa na kukanushwa. Mengine yanaandikwa lakini hayawafiki wananchi. Yanazimwa kwa nguvu za pesa! Lakini hayaondoi ukweli wa msemo ya Kiswahili usemao Lisemwalo lipo na kama halipo litakuwa njiani linakuja.

Jingine linalosemwa sana na limeandikwa ni UKIMWI. Kwamba baadhi ya wagombea wana virusi vya UKIMWI. Kelele zinapigwa kwamba wagombea wa urais wapimwe afya zao. Lisemwalo lipo na kama halipo liko njiani linakuja.

Inavyoelekea na inavyosemwa, watu wako tayari kumkubali mlarushwa, mporaji na fisadi na kumkataa mwenye virusi vya UKIMWI! Kila siku tunaimba wimbo wa kuacha tabia ya kuwanyanyapaa watu walioathirika, wakati bado tunauweka UKIMWI, kama kigezo kikubwa cha urais. Kwamba rais asiwe na virusi vya UKIMWI. Watu wanaishi na virusi vya UKIMWI, miaka zaidi ya 20. UKIMWI ni ugonjwa kama ugonjwa mwingine. Mbona hatuzungumzii wenye magonjwa ya kisukari, magonjwa ya moyo, ugonjwa wa kusahau? Kama mtu amekuwa na virusi vya UKIMWI, kwa muda wote na anafanya kazi kama kawaida, atashindwa vipi kufanya kazi ya urais akiwa na hali hiyo hiyo. Na kwa upande mwingine labda Rais, mwenye virusi, anaweza kuliponya taifa hili na janga la ugonjwa huu. Huyu kwa vile anaguswa anaweza kusukuma kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Sasa hivi tunaendesha mapambano haya kwa mzaa kubwa.

Tunajidanganya kwa kutoangalia mbali kwamba mtu asiyekuwa na virusi vya UKIMWI, leo anaweza kuwa navyo kesho. Akiwa rais, si kwamba atasita kuwa mwanadamu, si kwamba ataacha tabia ya kufukuzana na dogodogo. Wote wanaogombea wanafahamika vizuri na vyombo vya habari vimekuwa vikiandika vituko vyao. Ingawa inakanushwa.

Hata hivyo hoja kubwa ni je, mtu mwenye virusi vya UKIMWI, hawezi kufanya kazi? Hawezi kufikiri? Hawezi kutoa huduma kwa watu wengine? Ni nani wa hatari zaidi, mlarushwa na fisadi au mtu mwenye UKIMWI. Ni kigezo gani kinatumika kuona kuwa mtu wa UKIMWI, hafai kulionoza taifa?

Jambo linalosikitika katika zoezi zima la kumtafuta Rais wa nne wa Tanzania, ni kwamba watu wanahoji mambo yasiyokuwa ya msingi. Hatusikii watu wakiuliza sifa binafsi za wagombea. Sifa kama mtu kuwa na vision, kuwa na uzalendo, kuwa na msimamo. Haitoshi mtu kusema kwamba ataendeleza yale ya Rais Mkapa. Labda kama mtu huyu ni roboti. Maana roboti inategemea kufanya yale iliyoelekezwa. Bila kuiwekea programu haiwezi kujimudu kufanya lolote! Mtu ambaye ana utashi, akili na uhuru wa kuona na kuchagua mema na mabaya ni lazima awe mbunifu. Pamoja na kuendeleza mazuri yaliyotendwa na wale waliomtangulia ni lazima na yeye awe ana mchango wake ambao ana uwezo wa kuuelezea na kuwashawishi watu. Labda ingekuwa ni lazima kila yule anayetaka kugombea Urais wa taifa letu kutandika kitabu, akielezea mkakati wake na maono yake ya kuliendeleza taifa letu la Tanzania.

Mbona hatusikii watu wakihoji yale yanayosemwa kwamba mtu atakayepitishwa kugombea Urais, ni lazima awe anaungwa mkono na usalama wa taifa, jeshi na Rais, aliyemadarakani. Kwani Rais ni wa kuliongoza usalama wa taifa, ni wa kuliongoza jeshi au ni mtoto mrithi wa rais aliye madarakani? Rais, si ni mtumishi wa wananchi? Usalama wa taifa na jeshi si ni watumishi wa wananchi? Jeshi letu linaitwa Jeshi La Wananchi wa Tanzania. Hili si jina la bahati mbaya! Ni jina lenye lengo na mtazamo wa mbali. Kinyume na hapo ni lazima watu wahoji, Usalama wa taifa unaweza kuundwa upya, Jeshi linaweza kuundwa upya, lakini raia huwezi kuwaunda upya!

Hatusikii watu wakihoji tabia inayofanana na familia ya “ Bwana Nshonzi”. “Nshonzi” ni aina Fulani ya samaki mwenye masharubu. Ni samaki mtamu na anapendwa sana kule Kagera. Kilichotokea kwenye familia hii ni kwamba kila mtu aliota ndevu: Baba mwenye nyumba, mama mwenye nyumba na watoto. Kila mtu katika familia hiyo aliota ndefu, kiasi kwamba hakuna aliyejua anawajibika kwa nani. Kila mtu alikuwa na madaraka. Hayo ndio yanajitokeza kwenye chama cha CCM, chama tawala chenye uzoefu wa kuongoza. Wote wana ndevu na kila kiongozi wa ngazi ya juu anataka kuwa Rais. Wote wana ndevu na hakuna wa kumnyoshea mwenzake kidole. Hakuna wa kumkanya mwingine. Kama ni rushwa wote wameshiriki, kama ni kashfa ya mikataba hewa, wote wameshiriki, kama ni asilimia kumi, wote wameshiriki. Wana majumba, wamenunua nyumba za serikali, watoto wao wanasoma na kufanya kazi nchi za nje. Labda Kikwete, ambaye hakununua nyumba ya serikali na watoto wake wanasoma hapa nchini, hili linawashangaza vigogo wengi na kuwafurahisha walala hoi. Lakini kwa vile CCM inafanana familia ya “Bwana Nshonzi”, Kikwete, anaweza kuonekana adui wa familia! Si chanya kuwa adui wa familia. Hakuna msafi! Mwalimu Nyerere, aliweza kuwanyoshea watu kidole, kwa vile yeye hakuchafua mikono yake. Kwanini uzoefu wa CCM usiisaidie kuwaandaa viongozi? Wakachomoza wawili au hata mmoja. Urais, si kazi ya kila mtu. Anayeipata ni lazima awe na karama ya ziada. Dalili hizi zinazojitokeza za kila mwana-ccm kutaka kuwa rais zinatusukuma kuamini yaliyoandikwa siku za nyuma kwamba amani ya taifa letu itavurugwa na CCM.

Kampenini tunazoziona, makundi yanayojitokeza, kwa majina ya kambi ya Kikwete, Kambi ya Malicela, Kambi ya Sumaye, Kambi ya Simba nk, si makundi ya kuleta amani.

Ndugu Mangula, katibu wa CCM, anataka tuamini kwamba baada ya kumtangaza mgombea, makundi yatakufa. Amesikika akisema hivyo. Ni vigumu kuamini usemi huo. Ni mwendawazimu peke yake anayeweza kuteketeza mabilioni ya pesa kwa hasara. Na akaikubali hasara hiyo na kukaa kimya.

Imesemwa na imeandikwa kwamba wale ambao CCM, itawatema, watakimbilia upande wa vyama vya upinzani. Hili linaweza kuwa jambo zuri, na wala si lengo la makala hii kuonyesha kwamba hilo linaweza kuvunja amani. Swali, ni je CCM, itakubali kuwaona watu hao wakipeta kwenye vyama vya upinzani? Itawafuatilia, itawavua nguo. Wao pia hawatakubali kufuatiliwa, hawatakubali kuvuliwa nguo. Hapo ndipo vurugu zitakapotokea. Unaweza kuuita huu uzushi kama uzushi mwingine. Lakini siku itakapofika, mimi na wewe tutasema: Lisemwalo lipo na kama halipo liko njiani linakuja!

Na.
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment