MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005
UJUMBE KUTOKA MAKABURINI.
Mpendwa msomaji wa Tanzania Daima Jumapili, uliyezoea kuzisoma makala zangu katika safu hii, ninakuomba uniamini. Ni kweli nimepokea ujumbe kutoka makaburini,(Usiwe na mawazo ya Makaburi ya Kinondoni na madhambi yanayoendelea kwenye makaburi hayo) Ujumbe huu ni kitu kilichonifikia kwa wakati wake. Ni ufufuko wa aina yake. Bahati mbaya ni ufufuko unaotokea nyakati za ubishi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Ni ufufuko ambao bila kushuhudiwa na Wazungu tutasema ni porojo. Ufufuko halikuwa jambo geni katika maisha na utamaduni wa Mwafrika, falsafa na theolojia iliyokuwa imeuzunguka ufufuko wa Mwafrika ni kati ya mambo mazuri ya utamaduni wa Mwafrika yaliyofutwa na Wazungu wakati wakileta ukoloni, ustaarabu na dini zao hapa kwetu. Mwafrika akikutwa na mifupa ya wafu, unakuwa ushirikina, mzungu akikutwa na mifupa ya wafu, inakuwa ni masalia ya watakatifu, mifupa hiyo inatunzwa kila sehemu, makanisani, majumbani na kwenye pete za watu wakubwa katika jamii kama vile maaskofu! Mwafrika akiabudu chini ya mti, akajenga vibanda vya kuabudu, akautukuza mti na kuuona kama mwakilishi wa Mungu aliye hai katika jamii, inaitwa kuiabudu miungu na upagani. Mzungu, akiabudu kwenye sanamu ya Bikira Maria na watatifu wengine, hiyo ni imani iliyo sahihi! Si lengo langu kupiga porojo na wala si tabia yangu kuwatania wasomaji wangu. Nimekuwa nikijitahidi kuwaletea wasomaji wangu mada zenye ukweli, zenye kuelimisha, kuburudisha na kuchokoza mawazo. Sijaenda nje ya malengo yangu. Kisa hiki ninachokisimulia leo hii ni cha kweli. Wakati ninatafakari kuhusu ujumbe wa kukupatia wakati wa kipindi hiki cha pasaka, nilipata barua pepe kutoka kwa kijana anayesoma chuo kikuu cha Dar-es-Salaam. Si kati ya barua zinazoingia bila ya anwani ingawa kwa makusudi mazima nimeamua kufuta anwani na jina la kijana huyu. Hata hivyo sifa za mtu na mahali anapoishi vinamtangaza mtu kuliko jina lake. Mfano akina John ni wangapi? Akina Mutembei ni wangapi? Akina Masanja ni wangapi? Akina Nassor ni wangapi? La msingi si jina, ni huyo mwenye jina kafanya nini katika jamii, mchango wake ni upi? Anachangia kukua kwa haki, wema na huruma katika jamii au anachangia kuzalisha dhuluma, ukatili na unyanyasaji? Ni kama kijana huyu wa chuo kikuu cha Dar-es-Salaam aliyasoma mawazo yangu, labda alitumia teknolojia ya Mwafrika, teknolojia isiyoendelezwa kama ile ya kuruka na kupaa juu ya ungo, alijua jinsi nilivyokuwa na wakati mgumu, wa kuandaa ujumbe wa Pasaka. Labda wewe hupati shida, inawezekana Pasaka kwako ni kitu cha kawaida! Mungu,( tunafundishwa ana nafsi tatu, Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, wote ni Mungu mmoja!) muumba Mbingu na dunia, Mungu anayeumba viumbe vyote, akamatwe, apigwe na kuuawa na Binadamu. Mungu afe! Kinyume na mafundisho kwamba yeye yupo leo jana na kesho, yeye hana mwanzo wala mwisho, yeye ni Alfa na Omega. Anakufa wakati wa Pasaka! Lakini kwa kuonyesha Umungu wake,(Kana kwamba anapima nguvu zake na Mungu mwingine!) afufuke siku ya tatu. Akifufuka, ajionyeshe kwa wanawake, lakini ukweli huu uenezwe na wanaume, madaraka yote kuuzunguka ukweli huu ulioshuhudiwa na wanawake, utawaliwe na wanaume! Maana viongozi wa dini za Kikristu na hasa kanisa Katoliki ni wanaume watupu! Mungu au mwana wa Mungu, kama tunavyofundishwa ni kwamba alikufa kufuta dhambi. Sasa ni miaka elfu mbili baada ya kufa na kufufuka kwake, dhambi bado inautawala ulimwengu wetu. Uonevu, dhuluma na ukiukwaji wa haki za binadamu ni maua yaliyoupamba ulimwengu wetu. Tunawashuhudia wenye nguvu hata na wale wanaongozwa na “In God we Trust” wanaendelea kutoa uhai wa watu wasiokuwa na hatia. Irak ni mfano unaochoma na kuuvua Ukristu nguo na kuuacha uchi. Kabla ya kuanzisha vita ya Irak, Rais Bush, aliingia kanisani na kusali, baada ya hapo mabomu yalinyesha kama mvua na maisha wa watu wa Irak, kuteketea. Bush, anaendelea kuingia kanisani kumshukuru Mungu, kwa kumsaidia kuyamaliza maisha ya watu wasiokuwa na hatia. Bush, anapitia kwa Yesu, kujiita “Mlokole”. Yesu, aliyeishinda dhambi kwa kifo na ufufuko wake, anatumiwa kuendeleza dhambi na kuieneza duniani kote. Leo hii Bush, yuko kanisani akisherehekea sikukuu ya Pasaka! Tunashuhudia wenye mali wanaendelea kuneemeka zaidi wakati masikini wanaendelea kunyong’onyea. Chuki, hasira, visasi, ubaguzi wa rangi na jinsia ni vitu vinavyoutawala ulimwengu wetu katika nyanja zote, iwe ni serikali au dini. Ubinadamu unaendelea kuogelea katika dimbwi la madhambi makubwa kiasi kwamba na huyo Yesu anayetajwa kuzifuta dhambi alifanya kazi bure. Nilikuwa katika tafakari hii ndipo barua pepe ya kichwa cha habari: Ujumbe Kutoka Makaburini, ikaingia. Nimeinukuu yote jinsi ilivyo. Uisome, ili tutafakari sote:
“Mpendwa Karugendo, shikamoo Mwezi Januari nilibahatika kutembelea eneo la Mazimbu Morogoro yalipo makaburi ya wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini. Hakika baada ya kutoka huko naona sina raha maishani mwangu. Hata hivyo nimeonelea nikushirikishe sauti hii niliyoisikia hata kama huenda ulishawahi kufika na kushuhudia mwenyewe nakuhakikishia mwangwi wake umebadilika.
“ Baada ya kufika makaburini ambayo yanatunzwa vema kuliko ya ndugu zetu wanaozikwa Kinondoni au Mburahati, niliona kibao chenye ujumbe ambao umeweka alama katika maisha yangu. Maneno haya yalisomeka hivi:
"Ours was not for glory nor personal distinction but it was due for the noble cause of our time and the liberation of humanity of the entire community of South Africa".
“ Wakati bado nimepigwa ganzi na ujumbe huo huku nisijue la kufanya, wenzangu niliokuwa nao yapata kama ishirini hivi wao walikuwa wanashughulika na kupiga picha za ukumbusho. Nilidhani labda mimi ni mjinga kushughulika na kisicho na maana badala ya kuweka kumbukumbu ili nije nikawaonyeshe watu kwamba nani nilishawahi kutembea.
“Hata hivyo nilihitimisha kuwa mtu mwenye akili hawezi kushughulika na mambo mengine na kuacha ujumbe wa kutisha, wa kijasiri wa kizalendo, wa kujitoa mhanga kama huo. Basi nilijua ndio elimu yetu ya siku hizi maana imekaa kiutandawazi.
“Kumbe vifo vyao havikuwa ili waandikwe kwenye majina ya vitabu vya historia na kuimbwa kwenye nyimbo huku wakisifiwa kila mara! Kumbe kufungwa kwa Mandela hakukuwa kukuza jina la ukoo. Bila shaka walijua wazi kuwa wanacho kipigania wanaweza wasikifaidi lakini kwa utu wao na vizazi vijavyo walilala msituni kama wanyama.
“Swali lilinijia kuwa Je ukombozi wa utu wa mwanadamu sasa umekwisha. Uliondoka na kuisha kwa ubaguzi? La hasha bado tu watumwa wa wageni na hata ndugu zetu. Ndipo nikaenda mbali kuwa watu wanalala darasani ili wapate madigrii wawe maprofesa kwa ajili ya kukomboa wenzao au kukuza jina tu. Na rais na wabunge wanataka nafasi hiyo kama ujumbe wa makaburi ulivyo au ni "for glory and personal distinction".
Wasalaam .”
Tukiacha maswali mengine yasiyokuwa na majibu au yale yaliyo juu ya akili zetu, tunaambiwa kwamba Yesu, alikufa ili kuwakomboa wanadamu. Hakufa ili apate heshima au jina lake litukuzwe. Aliwafia wengine. Alijitoa muhanga. Alikufa ili kwa kifo chake wengine wapate uhai tele.
Ndio maana, ujumbe wa kijana huyu ulinigusa sana. Maandishi aliyoyasoma kwenye makaburi hayo ni ya kutufikirisha sisi sote tunaosherehekea kifo na ufufuko wa Bwana Yesu. Wafuasi ni wengi na madhehebu ni mengi pia. Kila mtu anajitahidi kumtangaza Yesu aliyekufa na kufufuka. Je tunakufa na kufufuka na huyo Kristo? Je tunawafia wengine, tunalifia taifa letu la Tanzania? Imani hii ya kufa na kufufuka inasaidia kuujenga uzalendo miongoni mwetu? Ili makaburi yatoe ujumbe, ni lazima waliozikwa kwenye makaburi hayo wafufuke. Ufufuko kama ule alioushuhudia kijana wetu wa chuo kikuu cha Dar-es-Salaam, pale Morogoro. Ukweli kwamba makaburi ya Morogoro ya wapiganaji wa Afrika kusini yaliweza kuugusa moyo wa kijana huyu aliyeyatembelea, yanazungumza: "Ours was not for glory nor personal distinction but it was due for the noble cause of our time and the liberation of humanity of the entire community of South Afrika".
Maneno haya yaliyoandikwa juu ya makaburi ya Morogoro, yanaonyesha kwamba makaburi hayo yako wazi. Ni sawa na ujumbe ule tunaoupata siku ya Pasaka. Wanawake, waliokwenda kaburini walimkuta malaika, akawaambia Yesu, amefufuka na kaburi liko wazi. Wakati wale walioandika Injili wanatusimulia juu ya malaika kwenye kaburi, huyu kijana wa chuo kikuu cha Dar-es-Salaam, anatuelezea maandishi aliyoyasoma kwenye makaburi yakamwingia rohoni mwake hadi anathubutu kusema hivi: “Swali lilinijia kuwa Je ukombozi wa utu wa mwanadamu sasa umekwisha. Uliondoka na kuisha kwa ubaguzi ?La hasha bado tu watumwa wa wageni na hata ndugu zetu. Ndipo nikaenda mbali kuwa watu wanalala darasani ili wapate madigrii wawe maprofesa kwa ajili ya kukomboa wenzao au kukuza jina tu. Na rais na wabunge wanataka nafasi hiyo kama ujumbe wa makaburi ulivyo au ni "for glory and personal distinction".
Pasaka inaweza kuwa na maana kwetu sisi tunaomwamini Kristu na wale wote waliotuzunguka, tukimfuasa yeye. Tukiyatoa maisha yetu kwa ndugu zetu, tukikubali kufa na kufufuka, tukijiweka kwenye hali ya kuyaacha makaburi yetu yakazungumza nyuma yetu.
Ni sherehe kama nyingine, ndiyo tule tunye na kufurahi. Ni sherehe kama nyingine tuvae nguo na kupendeza. Lakini tusiishie hapo, twende zaidi, tutafakari na kujiuliza maswali mengi yenye majibu na yasiyokuwa na majibu. Kila Mtanzania aliyebahatika kuisherehekea Pasaka, ya mwaka huu, ajiulize kama kweli inamsaidia kumpenda jirani yake, inamsaidia kulipenda taifa. Je anaweza kuyatoa maisha yake kwa wengine?
Ujumbe tunaoupata ni kwamba anayetoa maisha yake kwa wengine, anayetoa maisha yake kwa taifa lake, hafi, anaishi milele. Hata akifa anafufuka. Huu ndiyo ujumbe wa Pasaka. Ni ujumbe wa kumgusa kila mtu aliye Mkristu na asiyekuwa Mkristu. Ni ujumbe wa familia nzima ya Kitanzania.
Kitu kilicho muhimu wakati huu, kitu ambacho ni lazima kimguse kila Mtanzania ni kuujenga uzalendo wa taifa letu. Kila mtu kwa nafasi yake. Sherehe zote za dini zetu zilenge katika kuujenga uzalendo wa taifa letu. Iwe ni sikukuu ya Iddi, Christmas, Pasaka, Mavuno, Jando na Unyago nk, zote zilenge katika kuujenga uzalendo wa taifa letu.
Ninawatakia Pasaka njema yenye mwanga mpya. Ufufuko utuletee uhai, matumaini, mshikamano na uzalendo uliotukuka kama ule wa wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment