PAPA BEBEDICT WA 16, NI RAFIKI WA TANZANIA

MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

PAPA BENEDICT WA 16, NI RAFIKI WA TANZANIA!

Yamesemwa mengi juu ya Papa Benedict wa 16; wengine wanasema ni mzee, mgonjwa, amepitwa na wakati na hapendi mabadiliko katika Kanisa katoliki. Kuna waliokwenda mbali zaidi na kusema kwamba ana sura nzuri na sauti yake ni nyororo! Mtu mwenye akili timamu, msomi na kiongozi wa kanisa, anakoswa sifa za kumpatia Papa, anabaki kusema
“ Papa Benedict wa 16, ana sauti nyororo”. Kwani kazi ya Papa ni ya kuimba kama Michael Jackson? Sauti nyororo inahusiana vipi na mchango wa Papa wa kujenga dunia yenye amani na haki? Sauti nyororo inahusiana vipi na mchango wa Papa wa kuwatetea wanyonge, masikini na wanaoonewa. Sauti nyororo inahusiana vipi na mchango wa Papa wa kuzuia wimbi kubwa la ubepari linalotishia kuifunika dunia hii kupitia mifumo ya utandawazi na soko huria?

Sifa zinazotajwa juu ya Papa Benedict wa 16, ni kumbukumbu ya yale yaliyompata Papa John XXIII, alipotoka kwenye Conclave, kijana mmoja alisema kwa mshangao: “ Huyu Papa, ana sura mbaya”. Na Papa alijibu kwa unyenyekevu mkubwa: “ Ulifikiri Conclave ni Beauty Contest?”

Hadi leo kuna watu wanaofikiri Conclave ni Beauty Contest, Medical Laboratory,Chuo cha teolojia, uwanja wa siasa nk., wanasahau kwamba Conclave ni uwanja wa roho mtakatifu hadi kuna chumba kinachoitwa “Chumba cha machozi”!

Watanzania wanaojidai kumfahamu Papa Benedict wa 16, sijasikia wakitaja sifa ambayo ni ya muhimu kwetu, kwamba yeye ni rafiki wa Tanzania. Ninafikiri hii ndiyo sifa inayotufaa sisi. Sifa hii haigusi imani ya kanisa katoliki, sifa hii haimtaki Papa, kufanya mabadiliko yoyote yale katika kanisa katoliki. Kama wanavyosema wengine, yeye ni mtu asiyetaka mabadiliko, lakini si kweli kwamba amepitwa na wakati. Ni mtu mwenye mawazo ya kisasa na theolojia yake ni ya kisasa. Ukikutana naye kwa faragha, unaweza kujadiliana naye juu ya uzazi wa mpango, kutoa mimba, kuwaparisha wanawake, kupunguza madaraka ya Roma nk., atakusikiliza, atachangia, lakini akisimama kama “mfungwa wa imani”, kama alivyokuwa Kadinali msimamizi wa imani ya Kanisa Katoliki, hana huruma kutumia nyundo yake kwa nguvu zote kuwasambaratisha wenye mawazo ya kutishia uhai wa imani ya kanisa katoliki, hata kama mawazo hayo alikuwa akiyakubali faraghani! Mwaka 1985, alimnyamazisha bila huruma mwanafunzi wake Padri Leonardo Boff, kutoka Brazil. Padri huyu ambaye ni miongoni mwa wanateolojia ya Ukombozi walionyamazishwa na Kadinali Ratzinger, alikuwa na mawazo kwamba kanisa ni lazima lifanane na ujumbe wake wa kuwakomboa masikini, wanyonge na wanaonewa. Na kwamba madaraka ya Kanisa katoliki ni lazima yatoke chini kwenda juu, si kutoja juu kwenda chini. Maana yake ni kwamba madaraka yaanzie kwenye jumuiya ndogo ndogo, mapadre, maaskofu, wachaguliwe kutoka kwenye jumuiya ndogo ndogo na wapate madaraka yao kutoka kwenye jumuiya ndogo ndogo na wala si kutoka Roma!

Hivyo ukiigusa imani au madaraka ya Roma, huwezi kuelewana na Ratzinger, ambaye ndiye sasa Papa Benedict wa 16. Uongozi wake uwe mrefu au mfupi, hakuna mabadiliko yoyote yatakayotokea.

Mwaka 1963, Kadinali Ratzinger, alipokuwa na umri wa miaka 36, alimwandalia hotuba Kadinali Joseph Frings, Askofu Mkuu wa Cologne, kupinga msimamo mkali wa “ Congregation for the Doctrine of Faith” kwa kifupi C.D.F. Miaka kuminatisa baadaye, Ratzinger, ndiye alikuwa kiongozi wa C.D.F, na kuwa na msimamo mkali zaidi ya waliomtangulia.

Kwenye miaka ya sabini, Ratzinger, alikuwa kati ya wanateolojia wanamapinduzi wa Ujerumani. Alipoanza kuonyesha dalili za kutofautiana nao, Hans Küng, alimtania: “ Ukitaka kuwa Kadinali katika nchi ya Ujerumani, ni lazima kuanza mapema kufanya mazoezi ya kuwa mfungwa wa imani”. Alipochaguliwa kuwa Kadinali, mwaka 1977, Hans Küng, alimkumbusha maneno hayo. Na leo hii akiwa Papa Benedict wa 16, maneno ya Hans Küng, yana maana zaidi, sasa ni mfungwa wa wafungwa katika imani.

Lakini kama nilivyosema hapo juu, sisi watanzania tunaweza kunufaika kutokana na urafiki wake kwetu.
Urafiki huu ulianza mnamo mwaka 1978! Ni zamani kidogo. Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, mkowa wa Kagera, alikuwa akihangaika huku na kule dunia nzima akitafuta Jumuiya ya Wakristu wanaoishi maisha ya mitume. Wanaoishi kama jumuiya za mwanzo. Jumuiya isiyoongozwa na mtu mmoja au kikundi cha watu, bali mkutano wa jumuiya. Jumuiya ya watu wanaoishi pamoja, wanasali pamoja, wanatafuta mali kwa pamoja, wanashirikiana furaha, matatizo, mateso na kuishi kwa matumaini. Mwaka 1978, Askofu Mwoleka, alifanikiwa kuivumbua Jumuiya hii nchini Ujerumani katika Diosece ya Munich na Freising. Jumuiya hii inajulikana kama “Ingetrated community”, inaongozwa na mwanamke Frau Wallbrecher, mama mwenye vipaji visivyokuwa vya kawaida na mwenye upendo mkubwa kwa kanisa katoliki. Mwaka huo huo Kadinali Ratzinger, alichaguliwa kuwa Askofu mkuu wa Diocese ya Munich na Freising. Kwa mshangao wa Mwoleka, Kadinali Ratzinger, hakuifahamu jumuiya hii na mbaya zaidi Kanisa Katoliki la Ujerumani halikuikubali jumuia hii maana ilikuwa na theolojia yenye mtizamo wa kimapinduzi. Mwoleka alichukua jukumu la kuitambulisha Jumuiya hii kwa Kadinali Ratzinger.

Kadinali Ratzinger, alishangaa sana. Alimshangaa Askofu kutoka Afrika akavumbua kitu kizuri kwenye Diocese yake, kitu ambacho yeye binafsi hakukifahamu. Yeye alikuwa amezoa kuwaona Maaskofu wa Afrika, wakienda Ulaya kuomba misaada ya pesa, magari, vifaa vya hospitali na mashule. Alikuwa hajakutana na Askofu, anayetafuta Jumuiya ya watu wanaoishi imani. Jambo hili lilimfurahisha na kumpatia Mwoleka heshima ya pekee. Kadinali Ratzinger, alishangaa zaidi alipotaka kujua Mwoleka, alikuwa na mpango gani na Jumuiya hiyo, Mwoleka, alijibu: “Ninataka kwenda na baadhi yao ili wanisaidie kujenga jumuiya kama hii kule nyumbani Rulenge-Tanzania”. Urafiki wao ulianzia hapo na kuendelea hadi mwisho wa Maisha ya Mwoleka. Kadinali Ratzinger, akaitambua jumuiya ya Integrated na kuipenda. Hadi leo hii jumuiya hii iko karibu sana na Ratzinger. Alipotimiza miaka 75,ya kuzaliwa, jumuia hii ilimfanyia sherehe kubwa, Mwoleka na baadhi ya watanzania walikuwa kati ya wageni waalikwa. Kwa tabia ya Ratzinger, uhusiano wake na jumuiya hii umebaki ni wa faragha. Anawatembelea, wanamtembelea, anabadilishana nao mawazo na kujadili mambo mbali mbali ya kiimani na wanateolojia wa jumuiya hii. Kwake jumuiya hii ni kama kivuli cha kupumzikia baada ya kazi ngumu kwenye jua kali.

Ingawa uhusiano wa Ratzinger na Integrated community, umebaki kuwa ni wa faragha, kwa vile sasa amechaguliwa kuwa Papa, jumuiya hii itamsaidia kutibu majeraha ya Waisraeli. Papa Mjerumani, ana wajibu wa kuomba msamaha kwa vifo vya Waisraeli vilivyotokea Ujerumani nyakati za uongozi wa Hitler. Wakati ule kanisa lilikaa kimya! Sasa ni changamoto kwa Papa kutoka Ujerumani. Kiongozi wa jumuiya ya Integrated, Mama Wallbrecher, ameanzisha jitihada za pekee kuelekea kujenga uhusiano mzuri kati ya Wajerumani na Waisraeli. Ameanzisha tawi la jumuiya yake Israeli. Pia kuna majadiliano ya kitheolojia na mambo ya kijamii yanayoendelea kati ya Integrated na vikundi vya Israeli na kwa kumshirikisha pia Kadinali Ratzinger. Jitihada hizi zinaonekana kama tone dogo kwenye bahari kubwa, lakini pia ni kama mshumaa unaowaka kwenye chumba chenye giza nene!

Jumuiya hii iliyo karibu na Papa Benedict wa 16, ina matawi yake Morogoro na Dar-es-Salaam! Kwa maneno mengine tuna watanzania wanaomfahamu kwa karibu Papa wetu mpya! Hili ni jambo la kujivunia. Ingekuwa nchi nyingine jambo hili ndilo lingetawala vichwa vya habari katika magazeti. Bahati mbaya viongozi wetu wa kanisa ambao ndio wangelipigia debe jambo hili wanabaki kusifia sauti ya Papa Benedict wa 16, kwamba ni nyororo!

Sipendi kuwajengea matumaini makubwa watanzania, lakini ninakubaliana na maoni ya Padre mmoja wa Jimbo Katoliki la Rulenge, niliyeongea naye kwenye simu baada ya uteuzi wa Papa Benedict wa 16, kwamba: “Zimwi likujualo…”.

Badala ya kusifia sauti ya Papa, ni bora tukajipanga na kuweka maombi yetu mbele ya Papa aliye rafiki yetu. Ombi letu liwe ni lile lililo kwenye uwezo wake na haligusi imani. Baada ya miaka miamoja ya imani katika Taifa letu, tuna haki ya kuwapata watakatifu. Kuna watanzania wengi waliotutangulia kule mbinguni wenye hadhi ya utakatifu. Baba yetu wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akitangazwa mtakatifu tutamshukuru sana Papa Benedict wa 16. Mwalimu, alikuwa Mkatoliki hodari. Alikuwa mtetezi wa haki na amani, aliutukuza uhai na kuupigania. Bahati mbaya hatuna watu wakulisukuma jambo hili. Nchi kuwapata watakatifu inategemea juhudi, uelewa na uzalendo wa viongozi wa kanisa katika nchi husika.

Papa Benedict wa 16,alimfahamu Marehemu Bishop Christopher Mwoleka, kwa karibu sana. Anafahamu jinsi alivyokuwa ameyatoa maisha yake yote kulijenga kanisa, kuzijenga jumuiya za watu wanaoishi pamoja kama familia kwa kushirikiana taabu na raha, kushirikiana kutafuta mali, kusomesha watoto, kuwashughulikia wagonjwa na wasiojiweza na kuwatunza wazee, anaufahamu nyenyekevu wake, huruma, wema, imani na upendo wake kwa kanisa. Anafahamu jinsi Mwoleka, alivyokuwa mtu wa watu, anakumbuka jinsi alivyokutana naye mwaka 1978, akitafuta jumuiya za watu badala ya kutafuta pesa, magari na misaada mingine ya dunia hii. Anamfahamu Mwoleka, alivyokuwa mtu wa sala na alivyoubeba msalaba wake hadi siku ya mwisho. Ingawa siku za mwisho wa maisha yake watu wenye uchu wa madaraka walijaribu kuharibu jina lake, mbele ya Ratzinger, alibaki Mwoleka yule yule! Akimtaja Mwoleka, mwenye heri na baadaye mtakatifu, tutamshukuru sana Papa Benedict wa 16, hili liko kwenye uwezo wake na wala haligusi imani wala mabadiliko!

Marehemu Mwadhama Laurian Kadinali Rugambwa, alikuwa Kadinali wa kwanza wa Afrika. Aliishi maisha ya unyofu, imani na kuwatumikia watu wote bila ya ubaguzi. Papa Benedict wa 16, alimfahamu Marehemu Laurian Kadinali Rugambwa, kwa karibu. Akimtangaza mwenye heri na baadaye mtakatifu, atakuwa ametufanyia jambo la maana.

Watakatifu, na hasa wale wanaotoka miongoni mwetu, ni wa muhimu katika kukuza imani na kuchangia katika pato la kitaifa. Tukipata watakatifu, watu watatoka sehemu mbali mbali za dunia kuja kuhiji na kukomaza imani yao, lakini pia watakuja na pesa zao! Ziko nchi ambazo uchumi wake unategemea sana pesa za mahujaji. Inaweza kuwa hivyo kwa Tanzania, tukifanikiwa kuwapata watakatifu.

Ombi letu la mwisho, kwa vile Tanzania ni jirani na Rwanda, na ni kati ya nchi zilizoguswa kwa karibu kwa yale yaliyotokea Rwanda, mwaka wa 1994, Papa Benedict wa 16, katika ziara zake za kwanza, angeitembelea Rwanda, Burundi na DRC, kuwatuliza watu, kuponya makovu, kuwatia moyo wa imani watu hawa walioishi kwenye vita muda wote huu na hasa kulisafisha jina la kanisa katoliki lililopakwa matope na damu.

Binafsi nimekuwa nikitetea matumizi ya kondomu, lakini siwezi kuthubutu kutoa ombi hili mbele ya Papa Benedict wa 16, nilivyobahatika kumfahamu kwa karibu, itakuwa ni kupoteza muda, huyu ni mtu asiyetazama nyuma, ni mtu anayetunza “Ukale”, kama anavyosema Askofu Kilaini, kwamba “Ukale” ndio unalifanya kanisa Katoliki kusimama na kuwepo hadi leo hii. Limesimama na kuwepo kwa faida au kwa hasara, limesimama na kuwepo kuwatetea wanyonge na masikini au linawakumbatia matajiri na wenye madaraka, limesimama na kuwepo kueneza mwanga au giza, limesimama na kuwepo kumtangaza Kristu? Si hoja! La msingi ni kwamba lipo!

Mungu, ambariki Papa Benedict wa 16, rafiki wa watanzania.
Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment