TUMWOGOPE MUNGU

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

TUMWOGOPE MUNGU KWA MATENDO YETU YOTE, KILA SIKU NA KILA WAKATI!

Wakati tunapoelekea kwenye kipindi cha uchaguzi mkuu na hasa juma hili CCM inapomteua mgombea wake wa kiti cha urais, viongozi wetu wa dini wameanza zao, wameanza kujifanya wanayafumba macho yao na ya kwetu, wanataka tuamini kwamba wao ni wachambuzi wazuri wa mambo ya kisiasa, wanataka tuamini kwamba wao wanawachukia viongozi wabovu, viongozi wasiolipenda taifa letu, viongozi wanaotupokonya uhuru wetu na kuipora nchi yetu.

Wanaogombea tunawajua, hawakuzaliwa leo, wengi wao wametumikia serikali zote zilizopita. Karibia hao hao ndio wanataka kugombea tena! Kama ni kuwatilia mashaka, viongozi wetu wa dini wamechelewa! Wanatukumbusha kumwongopa Mungu, wakati wa uchaguzi. Maana yake ni nini? Kwamba watu wasikubali kununuliwa na kumchagua mtu asiyelifaa taifa letu, kwamba watu wachague kwa uhuru bila ya shinikizo wala vitisho, kwamba watu wafanye uchaguzi wakizingatia amani na utulivu wa taifa letu, kwamba watu wakifanya mchezo mchafu wakati wa uchaguzi wakumbuke Kwamba Mungu, anawaona na anaweza kuwaadhibu!

Viongozi wetu wa dini wanayaona haya vizuri leo, kuliko walivyokuwa wakiyaona jana! Ni nani anajua labda keshokutwa watayaona haya vizuri zaidi ya wanavyoyaona leo! Ikiingia madarakani serikali inayowakumbatia viongozi wa dini wote bila kujali mwenye hoja, mwenye uwezo wa kuona mbali, mwenye mchango wa maana katika jamii au mzalendo, serikali itakayo zaiachia dini zifanye zinavyotaka bila kuhoji kitu chochote, hatutasikia kelele, ushauri wala maonyo!

Ujumbe huu wa viongozi wetu wa dini kwamba tumwogope Mungu wakati wa uchaguzi ni wa muhimu na unakuja kwa wakati wake. Tofauti ni kwamba tusimwogope Mungu, wakati wa uchaguzi na katika siasa tu, tumwogope Mungu, kwa matendo yetu yote, kila siku na kila wakati.
Tumwogope Mungu, kwa matendo yetu mabaya, Tuongope kuwatendea ndugu zetu yale tusiyopenda kutendewa na sisi.
Tumwogope Mungu, tunapopokea sadaka na zaka nzito nzito kutoka mikononi mwa wanasiasa, bila kuuliza wala kuhoji. Tumwogope Mungu, tunapowakumbatia wanasiasa wenye sifa za ufisadi na kuwaalika kuendesha harambee za kujenga misikiti na makanisa. Tumwogope Mungu, tunaposamehewa kutoa ushuru na badala ya kuwahudumia wanyonge na masikini, tunajitenga na jamii na kuishi maisha kifahari. Tumwogope Mungu, tunapokula na kusaza, wakati wengine wanakufa kwa njaa. Tumwogope Mungu, tunapoziingilia familia na kuzisambaratisha. Tumwogope Mungu, tunapozaa watoto na kuwatelekeza kwenye mitaa ya miji. Tumwogope Mungu, pale tunaposhughulikia afya zetu kwenye mahospitali mazuri na kuwaacha wanyonge kufa kwa magonjwa yanayotibika. Tumwoge Mungu, tunapojikinga na ugonjwa wa UKIMWI na kuendelea kuwapumbaza watu kwamba kutumia kondomu ni dhambi. Orodha ni ndefu! Ni lazima kumwogopa Mungu, kwa matendo yetu yote mabaya.

Kwa viongozi wetu wa dini za Kikristu, ujumbe huu unaweza kuwasaidia kutafakari zaidi:
“……. Nendeni katika moto wa milele aliyotayarishiwa Shetani na malaika wake. Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu hamkunipa maji; Nilikuwa mgeni hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama…… Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi” ( Matayo 25: 41- 46).

Yesu, aliongelea mambo yanayotendeka kila siku katika jamii, mambo ambayo yanawatenga watu na Mungu wao. Hivyo orodha hii inaweza kurefushwa: “Mlinibagua kufuatana na rangi yangu ya mwili, kabila langu na dini yangu, mlininyanyasa, hamkunisikiliza, hamkunionea huruma nilipolala mitaani, hamkunipatia ushauri mzuri mme wangu alipoanza kutembea nje ya ndoa na kuambukizwa na virusi vya UKIMWI, mlinizuia kutumia kondomu, sasa na mimi nimeambukizwa, watoto wetu watabaki yatima, hamkunisaidia kuwalea na kuwatunza watoto mlionishauri nizae bila mpango, mlinibagua, mlinibaka, mlinitomasa na kuninyanyasa kijinsia.. nk”.

Orodha ni ndefu. Hoja ni kwamba ni lazima kumwogopa Mungu, kwa matendo yetu yote mabaya. Tusisubiri wakati wa uchaguzi na kwenye siasa!
Mfano: Yule anayewafukuza Wanawaombi Kanisani, ni lazima amwogope Mungu. Yale anayowafanyia wanawaombi, anakuwa anamfanyia Mungu. Jinsi watu walivyo na uhuru wa kumchagua kiongozi wao wa kisiasa, ndivyo walivyo na uhuru wa kumwabudu Mungu wao jinsi wanavyotaka. Uhuru ni uhuru, uwe ni wa kisiasa au wa kidini. Kuusukuma uhuru kwa upande wa siasa na kuunyamazisha kwa upande wa dini, ni dhambi na huku si kumwogopa Mungu! Tunashauriwa kuondoa kwanza vibanzi kwenye macho yetu kabla ya kuangalia yale yaliyo kwenye macho ya wengine!
- Yule anayewanyanyasa wanawake na kuwanyima nafasi ya uongozi katika kanisa na nafasi ya kufanya maamuzi muhimu katika jamii kama vile ndoa na familia, kuzaa watoto wengi au kuzaa kwa mpango, kutoa mimba au kulinda uhai kwa kupoteza uhai ( mfano mwanamke mwenye matatizo kwenye kizazi, ambaye kama angetoa mimba, angeponyesha maisha yake), kuhusu malezi nk., ni lazima amwogope Mungu, maana kuwabagua na kuwanyanyasa wanawake ni Kumbagua Mungu Mwenyewe. Tunafundishwa kwamba sote tumeumwa kwa mfano wa Mungu, na kwamba binadamu wote ni sawa. Bahati nzuri Katiba yetu inakubaliana na kitu hiki.

- Yule anayewabagua walei na kuwaweka katika nafasi ya kusikiliza na kupokea kila kitu bila kushiriki maamuzi yote, ni lazima amwogope Mungu, maana kuwabagua walei, ni kumbagua Mungu mwenyewe.
- Yule anayewabagua watu wa dini nyingine, ni lazima amwogope Mungu, maana sisi sote ni watoto wa Mungu. Ukweli unaotuzunguka sasa hivi ni kwamba Waislamu wanajiona wana haki zaidi ya wengine, Wakristu pia wanajiona wana haki zaidi ya wengine. Wakristu wanagawanyika katika madhehebu ambayo kila dhehebu linajiona kuwa na haki zaidi ya mengine. Dini zinakuwa kikwazo cha ushirikiano, udugu kama vile ndoa nk, wakati mwingine hata viongozi wa serikali wanachaguliwa si kwa sifa bali kwa kufuata dini zao.
- Yule asiyependa majadiliano, ushauri, ushirikishwaji, ni lazima amwogope Mungu, maana Wakristu wanamwamini Mungu, wa ushirikiano, Mungu wa utatu: Mungu baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Hata dini nyingine zinamwamini Mungu, anayesikiliza, Mungu mwenye huruma , upendo na wema.
- Yule asiyekuwa upande wa wanyonge na wanaoonewa, ni lazima amwogope Mungu, maana mbali na hukumu inayotajwa na Matayo katika sura ya 25, mstari wa 31 na kuendelea, Yesu, alisisitiza sana kuwajali wanyonge, wanaoonewa na wafungwa:

““Roho wa Bwana yu pamoja nami, kwani ameniteua rasmi niwaletee maskini habari Njema. Amenituma niwatangazie wafungwa kwamba watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, na niutangaze mwaka ambao Mungu atawakomboa watu wake” ( Luka 4:18-19).

Habari njema inakuja kwa maskini, wafungwa na wanaoonewa, si kwa matajiri na wenye madaraka. Ili ujumbe huu uwe na maana, Yesu, mwenyewe alijitokeza miongoni mwa maskini na wanaoonewa. Alizaliwa katika umaskini na kukulia katika umaskini. Enzi zake kulikuwa na matajiri wenye majumba ya kifahari, lakini hakuyachagua! Aliishi na masikini. Mitume wake wote walikuwa ni watu maskini. Aliwaponya wagonjwa, waliwafufua wafu na kuwapatia uzima mpya, uzima tele. Wenye njaa aliwashibisha chakula cha mwili na roho, wenye kiu aliwapatia maji ya uzima. Alifanya miujiza mingi bure bila kudai ujira.

Ili ujumbe wa viongozi wetu wa dini na hasa Wakristu uwe na maana yoyote ile ni lazima wajiulize wamesimama upande gani? Kama zilivyokuwa enzi za Yesu, leo hii kuna matajiri na maskini, kuna majumba ya kifahari na kuna vibanda ambavyo ni sawa na zizi la ng’ombe aliko zaliwa Yesu. Viongozi wetu wa dini wanaishi kwenye majumba ya kifahari au wanaishi kwenye vibanda? Wanapanda daladala au magari ya kifahari? Je, wako upande wa maskini na wanaoonewa au upande wa matajiri na wenye madaraka. Je, wanaponya wagonjwa? Wenye njaa wanawapatia chakula? Wenye kiu wanawapatia maji ya kunywa? Je wanafanya miujiza bila ya kudai ujira?


Viongozi wetu wa dini na hasa Wakristu, wanapotukumbusha kumwogopa Mungu, wakati wa uchaguzi unaokuja, ni bora wao wakatafakari ujumbe wa Yesu kwanza. Je, wao wanamwogopa Mungu? Je wao wanashiriki kiasi gani kuchangia hali hii ya watu kuishi bila kumwogopa Mungu. Kwanini watu waamue kuuza haki yao ya kupiga kura? Kwanini watu waamue kumchagua kiongozi si kufuata sifa zake bali wafuate kabila, dini, pesa, pilau na kanga wanazozipata wakati wa kampeni? Je, viongozi wetu wa dini wanachangia kiasi gani katika kuujenga uchumi wetu?

Kama bado kuna dalili za watu kufanya mambo bila kumwogopa Mungu, katika jamii yetu, basi viongozi wetu wa dini hawajafanya kazi yao vizuri. Mafundisho yao yatakuwa yanapeperushwa na upepo, hayajikiti katika jamii! Kutukumbusha ni jambo zuri, lakini pia kutengeneza mifumo ya kubadilisha hali hii mbaya ni jambo muhimu zaidi.

Mungu, ametuumba ili tusaidiane na kukumbushana wajibu zetu. Mtu, akisimama peke yake anaanguka haraka Bahati mbaya hatuna mfumo mzuri wa kukutana na kusaidiana. Watu wanaokutana kanisani au msikitini ni wengi kiasi ni vigumu mtu kumkaribia jirani yake na kumsaidia. Tungekuwa na mpango wa familia chache kukutana, kusali pamoja, kujadiliana na kusaidiana kimawazo, kihali na mali, ungekuwa msaada mkubwa. Haya ndio viongozi wetu wa dini wangekuwa wakiyafanyia kazi.
Jumuiya za mwanzo za Wakristu zilikuwa na mfumo huu na ulizisaidia sana jumuia hizi kuishi kwa kufuata mpango wa Mungu. Mfumo huu ukifufuliwa unaweza kusaidia hata leo hii! Ni kazi ya viongozi kugeukia wajibu zao kuliko kuwanyoshea kidole wanasiasa!

Bahati mbaya Kanisa Katoliki, lilitupilia mbali mfumo wa demokrasia tunaousikia kwenye jumuia za mwanzo na kukumbatia uchaguzi unaoongozwa na nguvu za Roho Mtakatifu, anayepitia kwa watu wachache sana. Kwa misingi hii, ushauri wa Kanisa Katoliki kwa demokrasia ya watu wengi, demokrasia inayomtaka kila mwananchi kupiga kura, si wa kuzingatiwa. Maaskofu wanachaguliwa kwa kura ya siri inayoongozwa na Roho Mtakatifu. Makadinali wanachaguliwa kwa kura ya siri inayoongozwa na Roho Mtakatifu, hawa watashauri nini kwenye uchaguzi wa wazi, wa watu wote, wa vyama vingi vya siasa, uliojaa heka heka, rushwa, upendeleo, kupakana matope, kujinadi nk.?

Ile demokrasia tunayoisikia kwenye makanisa ya mwanzo, ikirudi, kanisa litakuwa katika hali nzuri ya kuwashauri viongozi wa nchi na wananchi wanaoamini katika kuwachagua viongozi kwa kura ya demokrasia, vinginevyo kwa vile viongozi wetu wa dini ni wananchi kama wananchi wengine, ni bora wakashiriki kupiga kura kimyakimya bila kupaaza sauti zao ambazo zinageuka kuwa mwiba katika nguzo zao wenyewe! Viongozi wetu wa dini watufundishe kumwogopa Mungu kwa matendo yetu yote mabaya, mambo ya siasa wawaachie wanasiasa na wale wanaoamini katika demokrasia!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment