KISWAHILI LUGHA YETU!

MAKALA HII ILICHAPWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

KISWAHILI LUGHA YETU!

“Hapana lugha damiri, ana yake kila mtu,
Mimi hasa nafikiri, tunachekwa na wenzetu,
Tumo katika ngururi, yakutupa lugha yetu,
Hima pakutane watu au tahasiri.

Lugha ngeni nakiri, zina manufaa kwetu,
Tujifunze kwa dhamira, tuseme kama upatu,
Walakini tufikiri ubora wa lugha yetu, Hima
Pakutane watu au tutahasiri.” (Shaaban Robert –
Lugha Yetu).



Wakati wa uhuru 1961, Watanganyika wengi walikuwa wanaweza kuzungumza na kukielewa Kiswahili. Hii ilitokana na sababu mbali mbali zilizosaidia kukieneza Kiswahili kutoka pwani hadi bara: Biashara na misafara ya watumwa kutoka Zanzibar hadi DRC, wavumbuzi na wamisionari, lakini hasa serikali ya Wajerumani iliyoshinikiza Kiswahili kutumika kwenye serikali za mitaa na kwenye shule za misingi. Lakini msukumo mkubwa wa kukiendeleza Kiswahili uliletwa na mwalimu Nyerere, alipokitangaza Kiswahili kama lugha ya taifa na kuanza kulihutubia bunge letu kwa lugha ya Kiswahili mnamo mwaka wa 1962. Siasa ya Ujamaa na kujitegemea iliyotangazwa mwaka 1967, iliharakisha matumizi ya Kiswahili maana viwanda, mashirika, mashamba na vijiji vya ujamaa vilivyoanzishwa chini ya mfumo huo viliwakutanisha watu mbalimbali kutoka makabila 120 ya Tanzania, na walilazimika kutumia Kiswahili ili kuwasiliana na kuelewana.
Mwaka wa 1968, Kiswahili kilianza kutumika kama lugha rasmi ya serikali. Elimu ya kujitegemea ilianzishwa mashuleni na Kiswahili kilianza kutumika kama lugha ya kufundishia kwenye shule za msingi.

Vitu vingine vilivyosaidia kukiendeleza Kiswahili ni kama vile kuanzishwa kwa wizara ya utamaduni, Tanzania Publishing house, kwa ajili ya kuchapisha vitabu(1966),BAKITA(1967), Kitivo cha Kiswahili kwenye Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam(1970),TAKILUKI –Zanzibar(1978),Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) (1986),mfuko wa utamaduni Tanzania(1998),Redio Tanzania, Sauti ya Zanzibar , na magazeti ya Kiswahili na shirika la UKUTA, lilioanza kwenye miaka ya 1958. Hivi ni baadhi ya vitu vilivyokisaidia Kiswahili kushika kasi kubwa nchini Tanzania kwenye miaka ya 60 na 70.Kufikia mwaka 1970, Kiswahili kilikuwa kimekubalika kiasi kikubwa kwa watanzania wote kuwa ni lugha ya taifa.

Pamoja na jitihada zote hizo nzuri za kukiendeleza Kiswahili, Tanzania ilishindwa kufanya mambo manne muhimu na ya msingi ambayo ni: 1. Kukisimika Kiswahili kama lugha ya taifa kisheria. Hadi leo hii hakuna sheria yoyote ya kukitaja Kiswahili kama lugha ya taifa. Hata katiba ya nchi iliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili, haitaji kwamba Kiswahili ni lugha ya taifa. Jambo hili limekikwamisha Kiswahili. Watu wanaweza kukipuuzia Kiswahili na kuendelea kutumia lugha nyingine wanavyotaka katika shughuli za serikali na mashuleni maana hakuna sheria inayowabana. Hii ndiyo sababu inayolidekeza bunge letu kuendeleza mijadala kichaa ya kutumia au kutotumia lugha yetu kufundishia. Hakuna anayeweza kufikishwa mbele ya sheria kwa kukataa kukitumia Kiswahili. Hili ni tatizo kubwa katika jitihada za kukikuza na kukiendeleza Kiswahili.

2.Kuchelewa kuzitafsiri sheria za nchi katika lugha ya Kiswahili. Ingawa baadhi ya kesi huendeshwa kwa lugha zote mbili, Kiingereza na Kiswahili, lakini sheria zote bado ziko kwenye Kiingereza na mara nyingi hukumu huandikwa kwa Kiingereza. Kwa vile sheria zinamgusa kila Mtanzania, hili lingekuwa jambo la kwanza kushughulikia na kwa njia hii Kiswahili kingepanuka haraka.
5. Kushindwa kupambana na ile hali ya kutojiamini kwamba Kiswahili hakiwezi kumudu sayansi ya teknolojia. Kama lugha nyingine zimeweza, kwa nini Kiswahili kishindwe?

4. Kuchelewa kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia elimu ya sekondari na vyuo vikuu. Mjadala mkali juu ya kutumia Kiingereza au Kiswahili kufundishia ulianza kufukuta kwenye miaka ya 1965-1980. Ripoti ya tume ya Makweta ya 1982, ilipendekeza kwamba Kiswahili kianze kutumika Kama lugha ya kufundishia kwenye sekondari kuanzia mwaka 1985. Lakini kabla mpango huo haujaanza kutekelezwa serikali ilitoa mwongozo kwamba Kiingereza kiendelee kutumika katika sekondari na vyuo. Tamko hili lilizua mjadala ambao unaendelea hadi leo hii. Rais William Benjamin Mkapa, alipoingia madarakani mnamo mwaka wa 1995, aliogopa kujifunga kwa tamko au ahadi yoyote juu ya majadiliano haya. Alipendekeza mjadala uendelee hadi kufikia muafaka! Bila nia ya kweli, bila kuthubutu, mjadala huu ni ndoto ambayo haitakaa iwe kweli siku moja!

Kuchelewa huku kuanza kukitumia Kiswahili katika elimu ya sekondari na vyuo kumekumbana na kuanguka kwa ukomunisti na kuzaliwa upya ubepari mtakatifu wenye jina la utandawazi. Kasumba mpya imeanza kujengeka, ukoloni mambo leo umeanza kuzagaa, na watu sasa wanakubali kwamba Kiswahili hakiwezi kumudu kasi ya mageuzi haya mapya ya utandawazi, soko huria na uwekezaji. Hivyo lugha za kigeni zinaonekana za maana zaidi! Zinaanza kutolewa sababu kwamba Kiswahili hakiwezi kumudu sayansi na teknolojia, hakina misamiati ya kutosha, hakina vitabu nk. Mambo mengi ya kimagharibi yameanza kuwa na mvuto, kuanzia kwenye magari hadi nguo. Vijana wa kizazi kipya wameanza kuimba nyimbo za Kiswahili wakiigizia zile za Ulaya na Amerika. Mtu aliyeendelea na kuwa wa kisasa ni yule anayevaa, chana nywele na kuongea kama mzungu!

Kama tulivyoona, jitihada zote hizi za kukiendeleza Kiswahili zilikuwa zinaanzia juu kuja chini. Zilikuwa ni jitihada za viongozi kama Mwalimu Nyerere na wengine. Ndiyo maana kwa kiasi Fulani zilifanikiwa na lugha ya Kiswahili ilikuwa ikipiga hatua ya kupendeza. Lakini hitaji la sasa, hitaji la kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia linatoka chini kwenda juu. Ni hitaji la kidemokrasia zaidi. Hitaji la watu wenyewe katika jamii wanaouona ukweli wa mambo kwamba bila lugha yetu tutamezwa. Inashangaza kuona nchi inayojitangaza kufuata demokrasia, hailioni hitaji hili! Kuna haja ya watu wa chini kuendelea kusukuma kwa nguvu hadi serikali ikubali kutunga sheria ya kukitangaza Kiswahili kama lugha ya taifa.

Pamoja na vikwazo nilivyovitaja vinavyochelewesha kuendelea kwa lugha ya Kiswahili hapa Tanzania, dalili za lugha hii kuendelea kukua na kuenea ni kubwa. Sababu za nyuma zilizokisaidia Kiswahili kusambaa ndani ya nchi na je bado ziko pale pale. Watu wanaendelea kuhama kutoka vijijini na kwenda mijini, huko wanakutana na watu wa makabila mbali mbali, hivyo lugha ya kuwaunganisha ni Kiswahili! Kuna ongezeko kubwa la magazeti ya Kiswahili, redio zinazotangaza kwa Kiswahili na luninga zinazorusha matangazo ya Kiswahili. Vyama vingi vya siasa vimeleta changamoto katika siasa, hivyo ni lazima wanasiasa kwenda vijijini kujitangaza na huko lugha inayotumika ni Kiswahili.

Kwa upande wa kimataifa, vita vya maziwa makuu vimekisaidia Kiswahili kuenea zaidi. Wakimbizi wa Rwanda, Burundi na DRC, waliokimbilia Tanzania, wamejifunza Kiswahili. Wanyarwanda waliokuwa hapa zaidi ya miaka 30 na kurudi Rwanda mwaka 1994, Kiswahili ni lugha yao ya kwanza! Kwa vile nchi za Rwanda na Burundi, zinaomba kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kiswahili kilichoanzia kwenye makambi ya wakimbizi kitaendelezwa, kupanuliwa na kusambazwa kwenye kila kona ya nchi hizi. Lakini pia na wakimbizi wa Somalia, Ethiopia na Sudan, waliokuwa Kenya, wamejifunza Kiswahili pia. Marais wa Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC, wanaweza kuzungumza kwa pamoja kwa Kiswahili.
Kufuatana na takwimu za Profesa Mulokozi, watu milioni 15 wa DRC, wanaongea Kiswahili, Burundi ni milioni 2, Kenya ni milioni 20,Rwanda ni milioni 2,Tanzania ni milioni 32, Uganda ni milioni 8 na nchi nyingine zilizobaki ni milioni 21, jumla ni milioni 80, lakini Profesa Mulokozi, anasema dunia nzima inawezekana kuna watu milioni 100 wanaoongea Kiswahili!

Kiswahili kinafundishwa kama lugha kwenye zaidi ya vyuo vikuu 100(Mulokozi) dunia nzima. Idadi hii ni bila kuhesabu vyuo vya Amerika vya Waamerika weusi wanaokifundisha Kiswahili kama lugha yao ya pili! Kwa kifupi ni kwamba Kiswahili ni kati ya lugha zinazofundishwa kwa wingi duniani.

Kiswahili kinatangazwa kwenye zaidi ya redio na luninga 100 duniani. Zaidi ya kumi ziko Tanzania na Kenya. Nchi nyingine za Kiafrika zinazotangaza kwa Kiswahili ni: DRC, Burundi, Rwanda, Mlisiri, Iran, Sudan, Uganda, Afrika ya Kusini. Nchi nyingine kama Uingereza (BBC), Germany (Deutsche Welle), Amerika (Voice of America).

Vitabu vya lugha mbali mbali vimetafsiriwa kwa Kiswahili. Wakati wa Ukomunisti, vitabu vya Kichina, Kikorea na kirusi vilitafsiriwa sana. Siku hizi vinatafsiriwa vya kimagharibi. Lakini pia waandishi wa Kiafrika, wanaoandika kwa Kiingereza na Kifaransa vinatafsiriwa. Mfano Barua ndefu kama hii kilichotafsiriwa kutoka kwenye Kifaransa na Mkuki na Nyota Publishers.

Sasa hivi zinatengenezwa programu za computer za Kiswahili. Hizi ni dalili za wazi kwamba Kiswahili kinaendelea kwa kasi.

Kiswahili, sasa kinakubalika kwenye mikutano ya kimataifa. AU, baada ya changamoto ya Rais mstaafu wa Msumbiji, Chisano, Kiswahili kimeanza kutumika. Miaka michache ijayo mikutano yote itakipokea Kiswahili. Watahitajika watu wa wakutafsiri Kiswahili kwenye mikutano hiyo ya kimataifa. Watahitajika watu wanaokifahamu Kiswahili vizuri na lugha nyingine za kimataifa vizuri. Kwa vile sisi tunaipuuzia lugha yetu ya Kiswahili ambayo ndiyo ingetusaidia kuzifahamu vizuri lugha za kimataifa kama Kiingereza na Kifaransa, tutashtukia nafasi zote za ukalimani wa Kiswahili zinachukuliwa na Wanyarwanda, Warundi, Wakenya, Waganda na watu kutoka Afrika ya Kusini!

Inaweza kuonekana kama matani, lakini jinsi hali inavyo kwenda, tunaweza kujikuta watanzania tunakwenda nchi za nje au za jirani kama Rwanda, Burundi au Kenya, kujifunza Kiswahili! Tumeshindwa kufundisha elimu ya sekondari kwa Kiswahili, watakaotutangulia kufanya hivyo, watatufundisha! Hii itatudhalilisha na kushusha kiburi chetu ambacho tumekuwa nacho siku zote kwamba Tanzania ni mama wa Kiswahili!

Kazi iliyombele yetu, kazi ambayo ni ya kila Mtanzania, ni kuishinikiza serikali kutunga sheria ya kukitangaza Kiswahili kama lugha ya taifa. Shinikizo hili liendelee hadi Kiswahili iwe lugha ya kufundishia elimu ya sekondari na vyuo vikuu. Shinikizo hili liendelee hadi serikali ifanye mpango maalum wa kuwaandaa walimu wa lugha. Vijana wenye vipaji vya lugha, wafundishwe Kiswahili vizuri, maana mtu anayekifahamu Kiswahili vizuri ndiye anayeweza kujifunza kwa haraka lugha za kigeni na kuzifundisha kwa Waswahili, vijana hawa wakihitimu mafunzo ya Kiswahili, watumwe nchi za nje kujifunza lugha za kigeni, kama Kiingereza, Kifaransa, Kijapani, Kichina nk., wakirudi wafundishe lugha hizi kwenye sekondari na vyuo. Hii ndiyo njia peke yake ya kukiendeleza Kiswahili kwa kasi inayokubalika na kuendelea kuilinda Tanzania, kuwa mama wa lugha ya Kiswahili!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

1 comments:

Unknown said...

Kongole!
Umenena kweli juu ya Kiswahili.
Umenikumbusha wavyele walivyotuusia juu ya Lugha hii adhimu pale waliposema:

Kiswahili tukilinde, na fujo za kitatange,
Na nuhusi za washinde, wenye akili mawenge,
Kwa shauku tukipende, kwa dhati tujiviringe,
Kiswahili tukijenge, mjengo ukipasao.

Post a Comment