WAHAMIAJI HARAMU, TUNA MPANGO WA KUDUMU?

Tanzania inapakana na nchi nyingi, hivyo suala la kuwa na wahamiaji haramu si la kushangaza. Na hapa ni lazima tutofautishe “Uhamiaji haramu” wa kihistoria na ule ulioibuka siku za hivi karibuni wa watu kutoka nchi za Somalia na Ethiopia wanaopitia Tanzania wakielekea Afrika ya Kusini kutafuta kazi. Hili ni wimbi jipya, mipango yao ikikwama wanajikuta wakiishi Tanzania kinyume na sheria. Binafsi nimeandika sana juu ya suala hili la wahamiaji haramu wa kihistoria  na wachambuzi wengine wamelielezea mara kwa mara, lakini kwa vile kuna dalili za suala hili kutoeleweka vizuri miongoni mwa watanzania  na hasa viongozi wetu kama vile wabunge ni vyema kulijadili tena na kutafuta njia ya kuwa na mpango wa kudumu kuhusu suala hili.

Ni muhimu sana kwa wabunge wetu ambao ndio wawakilishi wa wananchi, ambao ndio wanaotunga sheria za nchi kuifahamu vizuri historia ya taifa letu, kufahamu vizuri mazingira ya majimbo yao ya uwakilishi na kuyafahamu vizuri mahitaji ya siku kwa siku ya wapiga kura wao. Inapotokea mbunge akaonyesha dalili za kutofahamu mahitaji muhimu ya watu wake, inatia simanzi na  ni hatari kubwa. Kwa mbunge aliye makini, kinachotangulia si chama chake cha siasa na wala si serikali iliyo madarakani, bali ni wananchi wake waliomchagua na kumtuma awawakilishe Bungeni.

Ukiachia mbali historia ya bara letu la Afrika ya mipaka ya nchi zetu kuibuka 1884? Mwalimu Nyerere, alifungua mipaka ya nchi yetu kwa Waafrika wote. Tanzania, iliwapokea wakimbizi na wapigania uhuru. Kwa miaka mingi Tanzania, ilikuwa ni kimbilio la wengi na msamiati huu wa “Wahamiaji haramu” haukujulikana. Kwa njia hii watu wengi wa nchi jirani walipata uraia wa Tanzania na wengine waliendelea kuishi hivyo hivyo bila hata kujishughulisha kuomba uraia. Kwa maana nyingine, huko nyuma hakukuwa na mpango wa kudumu wa kulishughulikia suala la wahamiaji haramu.. au hakukuwa na umuhimu wa kutengeneza mpango wa kulishughulikia suala hili.

Leo hii tunahitaji mpango huu wa kudumu. Tunahitaji kuwatambua wahamiaji haramu na kuwatungia sheria na mpangilio wa kuendelea kuishi hapa Tanzania. Busara si kuwafukuza, maana kuna wahamiaji haramu wanaoweza kuishi hapa Tanzania kama wawekezaji; wanaweza kutoa kodi na kuchangia  pato la taifa. Inawezekana kabisa kukaa kwao ndani ya nchi bila kibali, ni makosa yetu kama taifa kutokuwa na mpango wa kudumu kuhusu suala zima la wahamiaji haramu. Hivyo badala ya kelele za wabunge juu ya wahamiaji haramu, tunataka kusikia wakijadili mchakato wa kuanzisha mpango wa kudumu juu ya wahamiaji haramu na sheria ya kusimamia mpango huu. Hayo ndiyo mambo ya kujadiliwa na wabunge makini, si kulalamika bali ni kutafuta majibu na kupanga mipango ya kusonga mbele.

Tanzania, tunaelekea kusherehekea miaka 50 ya uhuru wetu bila kuwa na vitambulisho vya uraia. Mchakato wa vitambulisho hivi uko mbioni, lakini hatuwezi kuwa navyo kabla ya sherehe za miaka 50 ya uhuru wetu. Zoezi hili likianza tunaweza kushuhudia idadi kubwa ya watu ambao ni wahamiaji haramu. Hata ikitokea hivyo, zoezi zima liendeshwe kwa misingi ya utu na roho ili aliyoipandikiza Mwalimu Nyerere ya Umajumui wa Afrika. Watu wasiwekwe ndani, wasinyang’anywe mali zao na kurudishwa kwa nguvu kwenye nchi zao za asili.

Kama nilivyosema mwanzoni mwa makala hii, ni kwamba Tanzania inapakana na nchi nyingi, hivyo mikoa mingi ina tatizo hili la wahamiaji haramu, lakini tatizo hili ni kubwa zaidi katika Mkoa wa Kagera. Ni vigumu kuelewa ni kwa nini tatizo hili linasikika sana Kagera, kuliko kwingine. Mfano Mtwara, watu wa Msumbiji wanaingia na kutoka na wengine wanaishi Tanzania bila kelele za “Uhamiaji haramu”. Arusha ndugu zangu Wamasai wanaingia Kenya na kurudi Tanzania na kuishi bila kuitambua mipaka ya nchi hizi mbili, lakini hakuna kelele za “Uhamiaji haramu”. Juzi bungeni suala la wahamiaji haramu katika mkoa wa Kagera, liliibuka tena. Naibu Waziri wa  Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Benedict Ole Nangolo, alionyesha kulifahamu vizuri suala hili na kutoa jibu kwamba suala hili linahitaji “ Ushirikishwaji mkubwa”.

Jibu la Benedict Ole Nangolo, linaonyesha umakini mkubwa, ni aina ya wabunge tunaowahitaji kuliendeleza taifa letu ni aina ya wabunge wanaoguswa na maisha ya wananchi ni kinyume na mawazo ya viongozi wengine wanaofikiri jibu la tatizo la wahamiaji haramu ni kuwafukuza na kuwarudisha makwao. Kama nilimwelewa vizuri Mheshimiwa Benedict Ole Nangolo, ni kwamba suala hili la wahamiaji haramu linahitaji mpango wa kudumu. Mpango ambao chombo pekee cha kuutengeneza ni Bunge letu tukufu.

Kwa faida ya msomaji wa makala hii ni kwamba Mkoa wa Kagera unapakana na nchi tatu. Uganda, Rwanda na Burundi. Na kuna historia ya miaka mingi ya watu wa nchi hizi kuingiliana, kuwa na utamaduni unaofanana na lugha zinazofanana. Mipaka ya nchi hizi haikufanikiwa kuondoa udugu ulioanzishwa na mababu zetu. Nakumbuka kuandika makala Fulani nikisema kwamba mwenyeji wa Mkoa wa Kagera ambaye hana chimbuko Rwanda, Burundi au Uganda si mzaliwa wa mkoa huo! Kwa hiyo mbali na wakimbizi kuna wahamiaji wa aina nyingi mkoani Kagera, kuna wale wanaovuka mpaka kuja kusalimia ndugu na jamaa na wakinogewa wanahamia, kuna wakimbizi wa kisiasa na wakimbizi wa njaa wanaovuka mpaka kutafuta ardhi yenye rutuba lakini wanao lalamikiwa sana ni wale wahamiaji wafugaji. Hata juzi bungeni Mbunge wa Karagwe, alikuwa akiwalalamikia wahamiaji haramu wafugaji.

Hawa wahamiaji haramu wafugaji wanajulikana kama Wahima. Ni wafugaji kama vile Wamasai na wasukuma. Wanahama kutoka sehemu moja hadi nyingine kutafuta malisho ya mifugo. Wahima, kama walivyo Wamasai hawatambui mipaka ya nchi, kwao mifugo ni muhimu zaidi ya kila kitu. Mifugo ni muhimu kuliko mipaka ya nchi na kuliko vitambulisho vya uraia. Na kawaida hawana utamaduni wa kumiliki ardhi, wao wanatafuta malisho ya mifugo. Daima wanahama kutafuta maeneo mazuri ya kulisha mifugo yao. Magonjwa yakishambulia mifugo yao ikafa, ni lazima wahame kwenye maeneo hayo. Hawajengi nyumba za kudumu, na kwa maana hiyo hawana makazi ya kudumu!

Wahima, ni kabila ambalo limeishi miaka mingi katika maeneo ya maziwa makuu. Wamekuwa wakihama kutoka eneo moja hadi jingine wakitafuta malisho ya mifugo yao. Mipaka ya wakoloni ndo iliwatenganisha Wahima wa Burundi, Wahima wa Rwanda, Wahima wa Uganda na Wahima wa Tanzania. Hata hivyo Wahima hawa wamekuwa wakivuka mipaka ya nchi hizi bila kujali vitambulisho wakiwa katika harakati zao za kutafuta malisho.

Kwa maana hii basi, Wahima wamekuwa wakitoka Uganda, Rwanda na Burundi na kuja Tanzania kutafuta malisho ya mifugo yao. Lakini kuna wahima ambao wamekuwa wakiishi Tanzania miaka yote. Wanazunguka wilaya za Mkoa wa Kagera, bila kuvuka mipaka ya nchi. Mkoa wa Kagera unazalisha maziwa mengi na nyama kutokana na wafugaji hawa wahima.

Tanzania ilipoingiliwa na kirusi cha “wahamiaji haramu”, wahima wote bila kujali wale ambao ni watanzania, wamekuwa wakisumbuliwa. Wanakamatwa na kuwekwa ndani, wananyang’anywa mifugo yao na wakati mwingine wanasombwa na kupelekwa Rwanda. Kwa vile hadi leo hii hatuna vitambulisho vya uraia, mkoani Kagera, sura za watu zimekuwa zikitumika kama vitambulisho!
Kwa sura wahima wanafanana na Watutsi. Bila vitambulisho na mpango wa kudumu juu ya wahamiaji haramu, wahima wote watachukuliwa kuwa ni wahamiaji haramu. Wilaya ya Karagwe, ambayo ina wahima wengi, imekuwa ikitajwa kuongoza kwa kuwa na “Wahamiaji haramu”. Ukweli ni kwamba baadhi ya “Wahamiaji haramu” hawa ni wahima na kufuatana na mipaka ya kikoloni ya 1884? Hawa ni watanzania!

Hawa wahima wa Karagwe, wamesumbuliwa sana. Baadhi yao wamefungwa mara nyingi na kutozwa “hongo” ya ng’ombe. Kwa kutotaka usumbufu, wahima hawa wamekuwa wakitoa ng’ombe na fedha kwa viongozi wa serikali na wafanyakazi wa Uhamiaji ili wasikamatwe na kupelekwa Rwanda. Hata hivyo kuna baadhi waliokumbwa na zoezi hili la kupelekwa Rwanda. Walinyang’anywa mifugo yao, kwa maneno mengine walinyang’anywa maisha yao na kupelekwa ugenini Rwanda.

Serikali ya Rwanda, inalitambua tatizo hili la Wahima, na inaamini suluhu si kuwasomba wahima na kuwapeleka Rwanda, bali ni kutunga sera na sheria juu ya watu hawa wafugaji. Wanavyohama hama wakiwa Tanzania, ndivyo watakavyo hama hama wakiwa Rwanda, Burundi au Uganda. Jibu si kuwasomba na kuwapeleka Rwanda nchi inayodhaniwa kuwa ni asili yao, bali ni kuwajengea watu hawa mazingira ya kuishi na kuendesha ufugaji wa kisasa. Kwa vile maisha yao ni mifugo kuna hitaji la kuhakikisha wanaendeleza maisha yao hayo kwa njia za kisasa bila kuvunja sheria za nchi husika. Rwanda, imeanza kuwafundisha wafugaji kwamba kufuga si lazima kuwa na mifugo wengi kiasi cha kulazimika kuhama hama kutafuta malisho, bali ni kuwa na mifugo kiasi na kuitunza vizuri. Mapato yanayotokana na mifugo michache iliyotunzwa vizuri ni makubwa kulinganisha na mifugo mingi isiyotunzwa vizuri. Hili linaweza kuwashawishi wafugaji kuachana na utamaduni wa kuhama hama kutafuta malisho.

Kuna haja kubwa ya kuwa na mpango wa kudumu juu ya jamii hii ya Wahima. Kama ilivyo muhimu pia kuwa na mpango wa kudumu juu ya Wamasai wa Kenya na Tanzania na wasukuma wanaohama kutoka mkoa moja hadi mwingine wakitafuta malisho ya mifugo yao kiasi cha kuvuka hata mipaka ya nchi. Kule Sumbawanga, kuna habari kwamba wasukuma wameanza kuvuka na kuingia nchi jirani.

Nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Tanzania, zikae pamoja na kutunga sheria ya Wahima. Watu hawa waruhusiwe kuzunguka popote kwenye nchi hizi, mradi wasivunje sheria za nchi husika. Watu hawa wajulikane, wapatiwe vitambulisho maalum na kuruhusiwa kuendelea na maisha yao ya ufugaji. Tunapoelekea kwenye ushirikiano wa Jumuiya ya nchi za Afrika ya Mashariki, jambo hili la kuwatambua wahima kama jamii ya watu wanaohama hama kutafuta malisho ya mifugo yao ni muhimu sana. Kuendelea kuwachukulia wahima kuwa ni wahamiaji haramu ni kuwakosea haki yao ya msingi.

Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122

0 comments:

Post a Comment