KISWAHILI LUGHA YA UMOJA, UKOMBOZI NA MVUVUMKO WA AFRIKA. Tarehe 4 hadi 6 mwezi huu Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam kiliandaa kongamano la kimataifa kusherehekea miaka 50 ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya umoja, ukombozi na mvuvumko wa Afrika. Kongamano hili liliwakutanisha wadau wa Kiswahili kutoka nchi mbali mbali za Afrika na kwingineko duniani. Maprofesa waliofundisha Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, miaka ya zamani, kutoka Amerika na Ulaya, walifika pia kusherehekea miaka hamsini ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya umoja, ukombozi na mvuvumko wa Afrika. Nchi ya Kenya ilitia fora kwa kuwa na wajumbe wengi kwenye kongamano hilo na kuonyesha wazi shahuku kubwa ya nchi hiyo kuendeleza na kukitetea Kiswahili. Pia Balozi wa Kenya nchini Tanzania, alizindua kitabu chake alichokiandika kwa lugha ya Kiswahili kwenye Kongamano hilo. Katika Kongamano hilo, Chuo Kikuu chaDar-es-salaam kilitoa tuzo kwa watu mbalimbali waliochangia kukikuza, kukitetea na kukiendeleza Kiswahili. Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,Rais Mstaafu wa Kenya Arap Moi na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ni miongoni mwa waliopata tuzo ya Kiswahili. Mtoa mada mkuu wa kongamano hili alikuwa Profesa Horace Campbell kutoka chuo kiku cha Syracuse nchini Marekani. Profesa huyu alifundisha pia Chuo kikuu cha Dar-es-salaam miaka ya zamani. Katika hotuba yake alisisitiza Utu au Ubuntu kama nguzo kubwa ya Bara la Afrika kuendelea na kujiamini, wakati wazungu wanakazania kutengeneza roboti, sisi tukazanie Utu maana Afrika iko kwenye nafasi nzuri ya kuendelea na kutoa changamoto kwa mataifa ya Amerika,Ulaya na Asia. Afrika bado ina rasilimali nyingi, ina vijana wengi kuliko nchi zote duniani. Afrika ina vijana zaidi milioni 200 ambao wana miaka 15 hadi 24, ukilinganisha na China, ambayo zaidi ya asilimia 60 ya watu wake wana miaka 65 na kuendelea. Hivyo Afrika bado ina nguvu kazi. Hitaji la pekee ni kuwa na lugha kama Kiswahili na kuachana na lugha za kigeni. Kwa maoni ya Profesa Horace Campbell, lugha zetu ndizo zenye uwezo wa kuelezea Utu-ubuntu na ujuzi mwingine ulio kwenye utajiri mkubwa wa mila na tamaduni za mwafrika. Alikumbusha kwamba hata na wanafalsafa wa zamani akina Plato na Aristotle, walipata maarifa hayo kutoka Afrika. Mada nyingi zilitolewa na kujadiliwa katika Kongamano hilo. Pamoja na mambo mengi yaliyojadiliwa kwenye kongamano hilo, jambo kubwa lilojitokeza ni umuhimu wa lugha katika maisha ya mwandamu. Lugha ni sehemu ya mwanadamu kama ilivyo mkono, kichwa na miguu. Lugha inajenga utu wa mtu na kuulinda, lugha inajenga utamaduni na kuulinda na lugha ni chombo cha maendeleo na ukombozi wa mwanadamu kifikra Kwa kusisitiza hoja hii ya lugha na maendeleo ya mwanadamu, mtoa mada mkuu Profesa Horace Campbell, alitoa siri ya maendeleo ya haraka ya nchi ya Malaysia. Wakati Tanganyika inapata uhuru, ilikuwa sawa na Malyasia, lakini leo hii Malaysia iko sambamba na nchi zilizoendelea na Tanzania imebaki nyuma. Profesa Horace Campbell, anasema kwamba siri ambayo hawataki kuisema ni kwamba Malaysia, ilipiga hatu ya haraka ya maendeleo pale walipoamua kutumia lugya yao ya Malay kufundishia. Waliachana na lugha za kigeni na kuanza kutumia lugha yao kufundishia kuanzia elimu ya awali, ya msingi hadi vyuo vikuu. Na matokeo yake ni maendeleo makubwa yanayoonekana Malaysia. Pamoja na ukweli kwamba Kiswahili, imekuwa lugha ya kuleta umoja, mfano umoja wa kuiunganisha Tanzania, ambayo ina makabila zaidi 126, kuiunganisha Afrika ya Mashariki na kuwa lugha ya ukombozi wa kisiasa Afrika, bado haijaleta ukombozi wa kifikra. Nchi kamaTanzania, imeendelea kutumia lugha ya kigeni kufundishia. Kufuatana na hoja ya Profesa Horace Campbell kuendelea kutumia kingereza kufundishia kumechelewesha maendeleo ya Tanzania. Kwa maoni yake, kama Tanzania ingefuata mfano wa Malaysia, leo hii ingekuwa mbali katika maendeleo. Utafiti uliofanywa hapa Tanzania, ni kielelezo cha kutosha kwa hoja ya Profesa Horace Campbell, maana watoto waliofundishwa kwa Kiswahili walionyesha kufahamu zaidi walichojifunza kuliko wale waliofundishwa kwa kiingereza. Wale wanaofundishwa kwa kiingereza wanaweza kushinda kwa alama za juu sana, kwa vile wanakariri kila kitu. Lakini ukipima uelewa, wale wanaliojifunza kwa kiswahili wanakuwa na uelewa wa juu zaidi. Na ukweli ni kwamba watu wakiwa na uelewa wa juu, wanajikomboa kifikra na hii ni hatari kwa mataifa yanayotaka kuendelea kuyatawala mataifa mengine kiuchumi na kifikra na pia ni hatari kwa viongozi wanaotaka kuendelea kuwatawala watu waliogizani. Mwalimu Nyerere, alilihutubia bunge kwa Kiswahili mnamo mwaka wa 1962, na ndiyo maana ya kusherehekea miaka 50 ya Kiswahili. La kushangaza ni kwamba moto moto huo ulioanzishwa na Mwalimu Nyerere, wa kujitambua na kuipenda lugha yetu ya Kiswahili ulipotea! Baadhi ya watoa mada katika kongamano hilo walionyesha jinsi Tanzania ilivyotunga sera za kutumia Kiswahili kufundishia, lakini sera hizo hazikutekelezwa. Viongozi ambao ndo walikuwa na wajibu mkubwa wa kutekeleza sera hizo walianza kuwatafutia watoto wao shule za binafsi zinazofundisha kwa kiingereza na baadaye kuwapeleka watoto wao nje ya nchi kusoma vyuo vikuu vya nje. Lakini pia watafiti wengi waliotafiti juu ya sababu za Tanzania kushindwa kutekeleza sera ya kutumia Kiswahili kufundishia, waligundua kwamba wazazi wengi wa Tanzania wanapendelea watoto wao wafundishwe kwa kiingereza maana hicho ndo “Kiswahili cha dunia” kama alivyopata kusema Marehemu Mwalimu Nyerere. Wazazi wanafikiri watoto wao wakijifunza kiingereza ndipo watapata kazi. Ingawa kuna ukweli kwamba wale wanaomaliza vyuo na kuanza kazi hawapati nafasi ya kutumia lugha hiyo ya kiingereza. Madaktari wanapohitimu na kupangiwa vijijini wanaishia kujifunza lugha za kienyeji. Mbali na kutopata fursa ya kuongea kiingereza hata Kiswahili inakuwa shida maana kuna sehemu za Tanzania ambako watu bado wanaogea lugha zao za kienyeji. Chuo Kikuu Cha Dar-es-salaam, kimepiga hatua kubwa kukiendeleza Kiswahili hadi sasa kuna taasisi ya Kiswahili chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, na shaha ya kwanza hadi uzamifu zinatolewa. Ule ukoloni wa kuandika tasinifu ya shahada ya Kiswahili kwa kiingereza imekoma!Sasa mtu anaweza kuandika tasinifu yake kwa Kiswahili. Hata hivyo mapambano ya kufikia hatua hiyo yalikuwa makubwa. Profesa Mulokozi, wa chuo Kikuu cha Dar-es-salam, alielezea mapambano hayo “ Wakati tunajadili kuanzisha taasi ya Kiswahili, kuna waliopendekeza kwamba taasisi hiyo isiwe kwenye mazingira ya chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, ihamie Kariakoo, maana huko ndiko waliko waswahili!”. Maelezo hayo ya Profesa Mulokozi, yanaonyesha wazi jinsi wasomi wanavyokidharau Kiswahili. Wanaibeza lugha yao na kuzitukuza lugha za kigeni. Wakati duniani kote watu wanazipenda na kuzitukuza lugha zao sisi tunachukia lugha yetu. Profesa. Brigit Brock-Utne, kutoka Sweden, ambaye naye aliishi Tanzania na kufundisha Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, ambaye anaongea Kiswahili, Kijerumani, lugha yake ya Sweden na lugha nyingine za Afrika, alijikuta ni mtu ambaye hajaelimika alipokwenda Japan, maana alishindwa kuwasiliana! Hivyo wanaofikiria kwamba kujifunza kiingereza au kifaransa ni kuelimika wanajidanganya. Ufunguo wa elimu na maarifa ni lugha asili ya mtu, kinachofuata ni kujifunza lugha nyingine jinsi mtu anavyojaliwa kutembea sehemu mbali mbali za dunia, maana lugha duniani ni nyingi. Chuo Kikuu chaDar-es-salaam, kimefanya kazi nzuri ya kuandaa Kongamao hili ambalo kwa kiasi kikubwa wameshiliana na mashirika ya ACALAN na UNESCO(BREDA). Kupitia Kongamano hili wameweza kuonyesha hatua kubwa iliyofikiwa kwa kukiendeleza Kiswahili. Mfano shahada za Kiswahili, machapisho mabi mbali na vitabu vya kufundishia masomo ya sayansi kwa Kiswahili; mfano vitabu vya fisikia, kemia, bioloji na jiografia. Ndalo au changamoto iliyojitokeza ni kogamano kuwa la kisomi zaidi. Mijadala yote ilikuwa ya kisomi na kubaki kule juu hewani bila kushuka chini kwa wadau wa Kiswahili wale wa “Kariakoo”. Labda wasomi waliokuwa wakipendekeza taasisi ya Kiswahili ihamie Kariakoo, walikuwa na maana hiyo? Kongamano hili halikuwa na makundi mbali mbali kutoka kwa watu wa kawaida; makundi ya ngoma, wanamuziki, makundi ya sanaa za maonyesho na wedau wengine wanaokitumia Kiswahili katika shughuli za kila siku kama biashara na mengine. Wadau wengi kwenye kongamano hili la kiswahili walipendekeza kwamba mapambano ya kukitetea Kiswahili na kukiendeleza sasa yatoke kwenye vyuo vikuu na kwenda kwa wananchi. Lugha hii sasa iwe silaha ya mvuvumko wa Afrika, silaha ya kupigania ukombozi wa fikra. Lugha ni ufunguo wa maarifa, na lugha ni nyenzo ya kuleta mabadiliko makubwa. Biblia, ilipotsfsiriwa kwa lugha Kijerumani, palitokea mabadiliko makubwa ya kiimani nchini ujerumani. Hivyo na sisi Tanzania tukianza kukitumia Kiswahili kufundishia, tutegemee mabadiliko makubwa ya maendeleo na ukombozi wa kifikra. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 633122 www.karugendo.com

0 comments:

Post a Comment