UHAKIKI WA KITABU: MKATE MTAMU 1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA. Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni Mkate Mtamu na kimetungwa na Elieshi Lema. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D Limited na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 411 22 3. Kimechapishwa mwaka 2006 kikiwa na kurasa 44. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. UTANGULIZI Mkate Mtamu, ni kitabu cha watoto. Kitabu hiki ni kama vitabu vingine vya watoto viliyoandikwa na Elieshi Lema; Freshi na Maisha 1: Jipende, Freshi na Maisha 2: Jilinde, Fredhi na Maisha 3: Jijue na Freshi na Maisha 4: Jithamini. Nilifanya uhakiki wa vitabu hivi . Ni matumaini yangu kwamba bado kuna kumbukumbu ya uhakiki wa vitabu hivyo. Mkate Mtamu ni hadithi ya stadi za maisha inayowaelezea Maya na Modi wanaoishi kijijini na wanatamani maisha mazuri yenye neema na mafanikio. Maya anatamani kuwa daktari na Modi anatamani kuwa mfanyabiashara. Ili wafanikiwe ni lazima kufanya kazi, ni lazima kusoma na kuwa wabunifu. Kitabu kina michoro mizuri ya kuvutia ambayo inamfanya mtoto akisome bila kukiweka chini na kinazo sura kuminamoja ambazo ni fupi na haziwezi kumchosha mtoto. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na thamini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki. III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU. Siku hizi kumejitokeza haja ya lazima ya kuandika vitabu vya watoto. Niseme, kwa msisitizo, kwamba ni vitabu vilivyoandikwa na watanzania kwa kuzingatia hali na mazingira ya kitanzania. Vitabu hivi vimejikita katika stadi za maisha, hadithi nk. Waandishi wengi wamejitokeza kuandika vitabu vya watoto. Mashirika mbali mbali ya kimataifa yamejitokeza kufadhili uandishi na uchapishaji wa vipabu hivi. Mashirika kama SIDA,CODE NA CIDA, yamekuwa yakisaidia mradi huu wa Vitabu vya Watoto na yamesaidia pia uchapishaji wa kitabu hiki. Pia, mazingira ya kitabu hiki ni uandishi wa Elieshi Lema, unaoelekea kutoa mchango wa kujenga jamii iliyo sawa kijinsia. Jamii inayozingatia haki za watoto wote, wa kike na kiume, jamii inayoambukiza maadili yake kwa kizazi kijacho bila kujali jinsia. Mtindo, unaotumika kwenye vitabu vya Freshi na Maisha, unachomoza pia katika kitabu hiki cha Mkate Mtamu. Wimbo wa usawa wa kijinsia, umezoeleka kiasi cha upoteza maana yake. Mifano hai inayotolewa kwenye vitabu mbali mbali, kama ilivyo kwenye kitabu hiki cha Mkate Mtamu, inasaidia kuleta mabadiliko. Daima tunasema matendo ni bora kuliko maneno. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari. IV. MUHTASARI WA KITABU. Hadithi ya Mkate Mtamu, inaelezea maisha ya Maya na Modi. Maya ni msichana na Modi mvulana. Maya, anatamani awe daktari na Modi, anatamani kuwa mfanya biashara. Wanaishi maisha magumu ya kijijini na wanatamani maisha ya mjini: “ Siku nyingine nyumbani kwetu tunakuwa hatuna hata tone la mafuta ya taa. Mama anapika mapema halafu tunakula chakula tukimulikwa na mbalamwezi. Kama ni viazi vitamu vya kuchemsha, hamna shida, tunakula na kwenda kulala. Lakini kama mama amepika mboga ya utumbo, inakuwa shida kujua tuna vipande vingapi…” (Uk.1-2). Ingawa Maya na Modi, wanaishi kijijini, na maisha yao yanaelekea kuwa magumu,bado hapo kijijini marafiki zao wanatoka kwenye familia zenye uwezo. Ni mfano mzuri wa kuonyesha tabaka za maisha katika jamii yetu. Rafiki zao wanapajua mjini na nyumbani kwao wana uwezo wa kula mkate.: “Rafiki zake Modi, Jerome na Melvin, wameshakwenda mini. Baba yao aliwapeleka huko kuwanunulia nguo na viatu vya Kirsmasi..” (Uk 1)…. “Wazazi wa Jerome na Mlvin ni walimu wa shule ya Sekondari ya Sinde. Wao wanapata mshahara kila mwezi. Wao hawafugi ngo’mbe. Wanakunywa chai yenye maziwa na mkate uliopakwa siagi na jamu ya beri” (Uk 11). Modi, anakwenda kwa jirani kudoea mkate, lakini Maya, hapendi na kwa vile yeye ni mchunguzi na mbunivu, anajaribu kutumia vifaa vya kawaida na vitu anavyoweza kuvipata bila kuvinunua, kutengeneza mkate wake. Matokeo yake anafanikiwa kupika mkate mtamu.: “ Nilianza kazi. Nilichukua unga wa mahindi, nikauchekechecha. Katika mfuko wa gauni langu nilitoa kifurushi kidogo chenye amira. Nilikuwa nimemwomba Mzee Yusto akanipatia kidogo. Nikachukua chumvi kidogo na sukari kdogo, nichanganya vyote kwenye unga. Niliuweka mchanganyiko huo kando, nikapigapiga mayai mawili niliyokuwa nimeyaficha wiki nzima..? (Uk 20-21). Mwandishi anaendelea kuelezea hatua zote za kutengeneza mkate katika mazingira ya kijijini, kwa kutumia vitu vya kawaida vinavyopatikana kwenye mazingira ya kijijini. Hatua zote zinaelezewa kama vile mwalimu akiwa darasani. Njia hii kwa watoto inasaidia ujumbe kuingia kwa haraka zaidi, kuliko ambavyo angefundishwa darasani. Modi, baada ya kuonja mkate alioutengeneza dada yake, anaamini kwamba huo ni mtamu kuliko ule wa marafi zake. Wanapanga kuendelea kupika mikate zaidi, ili wauze na Maya, apate pesa za kusoma na kuwa Daktari. V. TATHMINI YA KITABU Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathimini ya kazi hii aliyoifanya Elieshi Lema. Mwandishi amefanikiwa kuandika kitabu cha watoto. Lakini pia amefanikiwa kufanya mambo mengi kwa wakati mmmoja. Kwa kuisoma hadidhi hii, watoto wanaweza kuanza kutengeneza mikate yao wenyewe. Hatua zote anazozielezea ni zile za kutengeneza mkate. Kule kuziweka hatua hizi kwenye hadithi,kunafikisha ujumbe na utaalam haraka kwa mtoto. Pili, mwandishi amefanikiwa katika kuisaidia jamii yetu kujenga utamaduni mpya. Utamaduni wa kuwashirikisha watoto wote kazi za nyumbani. Msichana akipika, mvulana anaosha vyombo. Mvulana akifua nguo, msichana anafagia. Hadithi kama hii ya Mkate Mtamu, inasaidia kujenga utamaduni wa usawa wa jinsia. Hadidhi, inaonyesha ushirikiano wa hali ya juu kati ya Maya na Modi. Ushirikiano huu, ni mchango mkubwa katika harakati za sasa hivi za kutaka kujenga jumuiya yenye kuheshimu usawa wa kijinsia. Tatu, ni kwamba katika hadithi za zamani, mara nyingi mvulana, ndo aliwekwa sehemu ya mbele au kuonekana ndiye mwenye akili na ubunifu kuliko msichana. Elieshi, anajaribu kusahihisha jambo hili. Hawa watoto wote, wanatamani maisha mazuri. Maya, anatamani kuwa daktari na Mori, anatamani kufanya biashara. Lakini pia, Maya, msichana, anachomoza na kuwa na ubunifu wa kutengeneza mkate mtamu. Kwa njia hii, watoto wa kike, wanaweza kubadilisha ile hali iliyokuwa imejengeka kwamba wavulana wana akili kuliko wasichana. Tatu, ni ile hali anayoichora mwandishi ya Maya, kutaka kuuza mkate mtamu ili ajilipie karo ya shule. Mfano huu unaweza kuwajengea watoto hali ya kutaka kujitegemea au kutunza vizuri kila senti wanayopewa na wazazi wao. Nne, ni picha anayoitoa mwandishi kwamba si kila kitu kizuri au kitamu kinatoka mjini. Inawezekana kabisa, na vitamu vikapatikana vijijini. Maisha bora yanawezekana pia kule vijijini. Jambo la msingi ni jamii kuwa na ubunifu wa kutengeneza Mkate Mtamu! Kwa maana pana ni kwamba, si kila kitu kizuri au kitamu kinatoka nje ya nchi! Tunaweza kutengeneza vitu vyetu vitamu na vizuri hapa ndani ya nchi.Jinsi Mkate wa Maya ulivyo mtamu, ndivyo na Juisi yetu inaweza ku watamu, na tukaachana na Juisi ya Afrika Kusini na Kenya, ndivyo nguzo zetu zinavoweza kupendeza, tukaachana na mtindo wa sasa hivi wa kukimbilia nguo za nje, ndivyo viatu vyetu vinaweza kupendeza nk. Mtoto, anayekuwa akijua kutengeneza Mkate Mtamu, ni lazima atoe mchango mkubwa katika kuboresha uchumi wa taifa lake. Mwandishi amefanikiwa kuelezea mambo makubwa, mambo ambayo mara yingi yanabaki kuwa kitendawili kwa lugha nyepesi. Hadithi ya watoto, inakuwa fundisho la maana sana katika jamii. VI. HITIMISHO. Mkate Mtamu, ni kitabu cha watoto. Lakini kama nilivyosema kwa Freshi na Maisha, kitabu hiki pia ni cha watu wazima. Ni bora kama na watu wazima wangesoma kitabu hiki na baadaye wakajadili na watoto wao. Yale yanayoibuliwa katika hadithi hii, yanaihusu jamii nzima. Tunapojitahidi kujenga utamaduni wa watu kujisomea vitabu, tuanze kwa hatua kama hizi za kujisomea vitabu vya watoto na kujadiliana yale yanayojitokeza katika vitabu hivi. Ninawashauri wazazi wote wenye watoto wadogo, wanunue kitabu na kukisoma wao na watoto wao. Ni imani yangu kwamba baada ya kukisoma, watashirikiana na watoto wao kutengeneza Mkate Mtamu. Taifa letu la Tanzania, linahitaji Mkate Mtamu! Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment