UCHAMBUZI WA KITABU. 1.Rekodi za Kibibliografia. Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Laurean Kardinali Rugambwa (1912-1997)- Mwana Mtukuka wa Afrika. Kimetungwa na Askofu Methodius Kilaini. Kimechapwa na Old East Graphic(T) Services. Kimechapwa mwaka huu wa 2008, kikiwa na kurasa 94. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. Utangulizi. Kitabu hiki kimeandikwa kama kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo cha Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa. Wazo la kuandika kumbukumbu hii lilikuwa la Maaskofu wa Kanisa Katoliki la Tanzania, na kazi ya kuandika alikabidhiwa Askofu Method Kilaini. Tunaweza kusema kitabu kina sura 32, na picha za matukio mbali mbali. Mtindo uliotumika, ni wa wachangiaji wengi. Askofu Method Kilaini, pamoja na kwamba na yeye amechangia anabaki kuwa “Mhariri”. Kama anavyosema kwenye Shukrani: “ Hapa ingelikuwa rahisi kuketi na kuanza kuchunguza kumbukumbu zangu na kufanya utafiti juu yake na kuaandika kijitabuy hiki, lakini nilionelea tupate watu mbali mbali kila mmoja atoe maonjo yake juu yake, alivyoguswa na huyu hayati Laurean Karinali Rugambwa kwa namna moja au nyingine. Yaliyoandikwa nimeyaacha kama yalivyo hata kama mara nyingine mambo yalijirudia, na hata sikusahihisha minthari ya maandishi ili kupata undani na maonjo ya kila mmmoja” (Uk 1). Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu hiki. III. MUTHASARI WA KITABU. Kitabu kinaanza na neno la Shukrani kutoka kwa Askofu Method Kilaini. Baada ya neno la Shukrani inafuata Dibaji, iliyoandikwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Katika Dibaji hii, Mwadhama Pengo, anaelezea kwa kifupi alivyomfahamu Marehemu Mwadhama Kardinali Rugambwa. Anaelezea umaarufu wake katika kanisa na kudokeza yale yanajitokeza sasa hivi baada ya kifo cha Mwadhama Rugambwa: “ Kwa bahati mbaya, wako pia ambao humwenzi Hayati Baba Kardinali Rugambwa kwa malengo ya kujienzi wao wenyewe binafsi.Hutafuta kujijengea umaarufu kwa kudai juu ya nafsi zao upendeleo wa pekee wa Mwadhama Kardinali. Watu kama hao mara kwa mara hawasiti kumpachikia maneno ambayo kihalali hayaendani kabisa na hadhi aliyokuwa nayo Baba Kardinali Rugambwa. Ni jambo la kusikitisha kwamba watu kama hao wanaendelea na mchezo wa ubinafsi miaka kumi baada ya kifo cha Kardinali Rugambwa. Ningewaomba watu hao kutafakari kidogo juu ya mchezo wao wa ubinafsi ambao badala ya kumwenzi Mwadhama Laurean Karinali Rugambwa, unafaulu kumpotezea sifa na umaarufu wake” (uk 3). Baada ya Dibaji, inafuata Historia fupi ya Maisha ya Mwadhama Rugambwa, iliyoandikwa na Askofu Kilaini. Baada ya Historia fupi, yanafuata maoni ya Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa. Naye anaandika jinsi alivyomfahamu Marehemu Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa. Pamoja na mambo mengine mengi anasema: “ Nina kumbukumu moja ya marehemu ambayo haitafifia maisha yangu yote. Nayo ni ile ya sura za maelfu ya waombolezaji waliojawa na majonzi na vilio, walioshiriki katika ibada za mazishi na kumsindidikiza katika safari yake ya mwisho Dar-es-salaam na Bukoba. Ni kielekezo cha upole na upendo wake kwa watu, na lile neno lilioandikwa; ‘ Mauti imemezwa kwa kushinda’” ( Uk 7). Baada ya Maoni ya Rais Mstaafu Mkapa, yanafuata maoni ya Askofu Method Kilaini, jinsi yeye alivyomfahamu. Anamwelezea Marehemu kama: Rugambwa heshima ya watu weusi, Rugambwa kiungo na mpatanishi wa wote, Kiongozi wa Maaskfou wa Aafrika, Rugambwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Rugambwa na umoja wa wakristo na uelewano na waislamu, mtu mwenye upeo mkubwa katika kuelimeisha watu, maendeleo na elimu ya wanawake na jinsi alivyozitumia nguvu zake za mwisho. Ukrasa wa 21 hadi 48, ni maoni ya maaskofu mbali mbali wakieleza jinsi walivyomfahamu Marehemu Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa. Ukrasa wa 50 hadi 68, ni maoni ya mapadri mbali mbali wakieleza jinsi walivyomfahamu Marehemu Laurian Kardinal Rugambwa wakati wa maisha yake. Ukasa wa 72 hadi 85 ni maoni ya masista mbali mbali wakielezea jinsi walivyofahamiana na Marehemu Laurian Kardinali Rugambwa. Ukrasa wa 87, Mama Olive Luena, naye anaelezea jinsi alivyofahamiana na Marehemu Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa. Mwisho, ukrasa wa 91, jamaa yake Dr. Francis Rutaihwa, anatoa maoni yake, pamoja na mambo mengine tunasikia akisema hivi: “ Katika shughuli zake za kusumbukia wengine, mwenyewe Kardinali aliridhika tu kuishi kimaskini. Niliweza kuona hata nyumbani alivyoishi. Ingawa nilikuwa karibu sana na Karidnali Rugambwa na tuliongea mambo ya kila aina, hata ya kutaniana, lakini hata siku moja sikusikia hata neno moja la kulalamikia hali yake ya maisha. Maimi pia sikumuuliza kulikoni; hata nilipoona “furniture” ya chumbani chake imeishachakaa na kuchanika. Nguo kadhaa pia zilikuwa kuukuu, hasa zile za kiraia..” (Uk 91). Dr.Francis Rutahiwa, anaendelea kueleza: “ Pamoja na kumtembelea mara kwa mara, niligundua kuwa kulikuwa na upweke wa ajabu pale nyumbani kwake. Sikuuliza maswali. Lakini hata kwa muda ule alipokuwa hajiwezi, mimi sikuwahi kuona watu wengi wanakuja kumfariji..... Ni jambo la kushangaza kwamba mtu ambaye aliishi kwa upweke wa kutisha siku zake za mwisho, lakini alipofariki idadi ya waombolezaji ilikuwa kubwa sana kiasi cha kutisha pia. Mimi nilisononeka, na ndani nikasukumwa kujifunza kitu mbacho mpaka sasa siwezi kukieleza vizuri....” (Uk 93) IV. TATHMINI YA KITABU Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii nzuri aliyoifanya Askofu Method Kilaini. Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuagalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasiismua sana na kufundisha kutokana na mtindo alioutumia mwandishi wa kushirikisha watu mbali mbali kuandika juu ya maisha ya Marehemu Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa. Pili, napenda nimpongeze sana Askofu Kilaini pamoja na maaskofu kwa kufikiria kuandika kitabu hiki ambacho kimekuwa ni deni kubwa kwao kwa miaka mingi. Nafikiri kwa mtindo huu, wataendelea kuandika maisha ya watu muhimu katika historia ya kanisa, si maaskofu peke yao, bali waumi wote waliotoa mchango wa kutukuka! Tatu, pamoja na pongezi, kuna kasoro za hapa na pale zilizojitokeza katika kitabu hiki: Kasoro kubwa ya kwanza ni kwamba hakuna popote inapotajwa kwenye kitabu hiki kwamba Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa, hajazikwa. Aliwekwa kwa muda kwenye kanisa la Kashozi, na mazishi yake yanasubiri ukarabati wa Kanisa Kuuu la Bukoba ukamilike. Hivyo ni bora kwa wale watakaokisoma kitabu hiki wafahamu kwamba bado kuna kazi ya kumzika mpendwa wao. Kasoro nyingine ni kwamba, maaskofu, mapadri na watawa, wamepewa nafasi kubwa kuandika maoni yao katika kitabu hiki, ukilinganisha na mlei mmoja tu Mama Olive Luena. Kasoro hii inaendeleza ule ufinyo wa mawazo wa kufikiri kwamba kanisa ni la maaskofu, mapadri na watawa. Mawazo mapana, ni kwamba kanisa ni la waumini wote, na Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa, aliwahudumia wahudumia waumini wote. Maaskofu wengi wameandika mawazo karibia yanayofanana. Busara ingekuwa ni kuchukua maoni ya wawili, ili kupata nafasi ya watu wengine. Kufuatana na maelezo ya Askofu Kilaini, kuna watu wengi waliandika maoni yao, lakini nafasi ilikuwa ndogo kuweza kuweka maoni yote. Kuna waumini walei, waliofanya kazi kwa karibu na Marehemu Mwadhama Kardinali Rugambwa, na bado wako hai. Hawa wangeweza kutupatia picha nyingine na Mwadhama. Watu kama Mwalimu Gerase Kamanzi, Mzee Laurenti Ishungisa na Mzee Nicoras Contris, wangeweza kuandika mengi na ya kusisimua juu ya Mwadhama. Mfano mzuri ni ule wa jamaa yake Dr.Fransis Rutahiwa. Dokezo lake la upweke, hakuna Askofu, padri au sisita, aliyelitaja. Hivyo kwa kuaacha mchango wa walei, tunapoteza mengi ya kihistoria juu ya Mwadhama Rugambwa. Kasoro nyingine ni kwamba, wengi walioandika juu ya Mwadhama, wameandika kusifia tu. Hivyo wamebaki kuandika: Alikuwa mtu mzuri, aliwapenda watu, alikuwa mchapakazi nk. Hatusikii mawazo mazito juu ya Mwadhama. Hatusikii chanya na hasi juu ya mwadhama.Hatusikii juu ya Teolojia yake, juu ya maisha yake ya kiroho, juu ya usimamizi wa mali ya kanisa. Inasemekana kwamba alikuwa na mpango mzuri wa utunzaji wa fedha. Hatusikii juu ya msimamo wake kisiasa: Aliupenda ujamaa? Alikuwa na mawazo gani juu ya Utandawazi? Kasoro nyingine kubwa inayojitokeza kwenye kitabu hiki ni makosa mengi ya uchapaji. Inaelekea kitabu hakikuhaririwa. Pia ukrasa wa 71, picha zote haziendani na maelezo. Inashangaza sana kitabu kizuri na muhimu kama hiki kuwa na makosa ambayo si ya lazima. Makosa haya yanaondoa utamu wa kitabu na kushusha hadhi ya mwandishi. Askofu Medhod Kilaini, ni msomi na mtu makini sana, kazi hii yenye makosa kubeba jina lake ni jambo la kusikitisha. V. HITIMISHO Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri watanzania wakipate na kukisoma kitabu hiki ili waweze kumfahamu kwa udani Marehemu Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa. Pia kitabu hiki kiwe kichocheo cha kuandika, kusema na kuelezea mengi juu ya Mwadhama, ili sifa zisikike hadi kufikia hatua ya kumtangaza mwenye Heri na hatimaye Mtakatifu. Lakini, kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa kitabu hiki kuzishughulikia kasoro nilizozitaja na ikiwezekana kitabu hiki kifanyiwe uhariri na kutolewa toleo jingine.Ni vizuri kuzoeza na kuingia kwenye utamaduni wa kuchapisha vitabu. Si kila mtu anaweza kuhariri na kuchapa kitabu. Kuna watu wanaofanya hazi hizi, hivyo ni bora kuwatumia. Pia, kwa kutumia kitabu hiki, inawezekana kuendesha harambee ya kuchangia ukarabati wa Kanisa Kuu la Bukoba, ili Mwadhama Marehemu Laurian Kardinali Rugambwa, apate kuzikwa. Ukarabati wa Kanisa Kuuu la Bukoba, umechukua muda mwingi, zaidi ya miaka kumi sasa. Kama tatizo ni fedha, ni imani yangu na ya wengi kwamba wa kuchangia ni wengi, tatizo hakuna wakuwahamasisha. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment