UHAKIKI WA KITABU: USHIRIKA TANZANIA
1. Rekodi za Kibikiogarafia
Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni USHIRIKA TANZANIA na kimetungwa na Pius Ngeze. Mchapishaji wa kitabu ni Tanzania Educational Publishers Limited na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN) 978 9987 07 037 4.Kimechapishwa mwaka 1975 na toleo la pili limechapishwa 2010 kikiwa na kurasa 159. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Ushirika Tanzania: Historia na Hatima ya Vyama vya Ushirika na Bodi za Mazao, 1933 – 2010, ni historia ya taasisi mbili kubwa na muhimu nchini, yaani, vyama vya ushirika na Bodi za Mazao. Kitabu hiki kimepekua safari ndefu ya taasisi hizi kuanzia mwaka 1933-2010. Miaka 77 ya taasisi hizi imekuwa ya misukosuko, migongano baina yao, mafanikio, kufutwa, kuruhusiwa tena matatizo.
Taasisi hivi, hususan, Vyama vya Ushirika, mwanzoni kabisa, 1933, vilianzishwa kuondoa unyonyaji katika sekta ya ununuzi wa kahawa na kuhamasisha kilimo bora cha zao hili. Baadaye vilishughulikia mazao mengine na kuongezewa jukumu la kuhamasisha wananchi kudai Uhuru. Baada ya hapo vikatumika kuendeleza sera ya TANU ya Ujamaa na Kujitegemea.
Katika kitabu hiki Bwana Ngeze ameeleza vizuri historia ya vyama vya ushirika; matatizo na mafanikio yake. Ni jambo la kuridhisha kupata kitabu hiki kilichoandikwa na mwananchi mzalendo juu ya historia ya vyama vya ushirika na Halmashauri za mazao.
Kitabu kinazo sura 13, Marejeo ya vitabu, Tafsiri na Vielelezo vya Takwimu. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
Bwana Ngeze, ameandika vitabu vingi juu ya mazao mbali mbali hapa Tanzania. Baadhi ya vitabu hivyo nimevifanyia uhakiki katika safu hii. Baada ya kuandika vitabu kuwaelimisha wakulima juu ya mazao na umuhimu wa kuwa na elimu ya kuendesha kilimo bora, hapendi kuwaacha wakulima hewani. Yeye anaamini mkulima anaweza kupata mafanikio kwa kujiunga katika vyama vya Ushirika. Ndio maana ameamua kuandika kitabu juu ya Ushirika. Kitabu hiki alikiandika mara ya kwanza mwaka 1975 na mwaka huu amekirudia tena kwa kukiboresha na kuongeza mambo mengine ambayo ametokea katika vyama ushirika kuanzia 1975 hadi 2010.
Kama tulivyodokeza kwenye uchambuzi wa vitabu vyake vingine, Bwana Ngeze, ni msomi aliyeamua kuisambaza elimu aliyonayo kwa wananchi na hasa wananchi wa kawaida. Ndiyo maana kitabu hiki kimeandikwa kwa Kiswahili rahisi ili kiwezi kusomwa na kuwafikia watanzania wote. Pia kitabu kinaweza kuwasaidia watumishi wote wanaohusika na maendeleo ya wananchi; Bodi za mazao na Wizara ya Kilimo; Wanafunzi shuleni na vyuoni; walimu, wakulima na wafanyakazi wengine.
Ingawa kitabu hiki kinahusu Vyama vya Ushirika na Bodi za Mazao katika Tanzania Bara, kinawafaa pia watu wa nchi nyingine, hasa zile zinazoendelea, maana mambo yaliyozungumzwa kitabuni yanafanana na yale ambayo yangeweza kuzungumzwa juu ya vyama vya ushirika za Bodi za Mazao katika nchi zao.
Shabaha kuu ya Vyama vya Ushirika vilipoanzishwa, ilikuwa kuuza mazao ya wanachama kwa bi nzuri na wakati huohuo kuondoa unyonyaji wa wafanyabiashara ambao walikuwa wakinunua mazao hayo kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu. Katika kufanya kazi hiyo, hasa baada ya kupata uhuru wetu, vyama hivyo vimekumbana na matatizo mbalimbali ya kukua. Lakini, kwa ushirikiano baina ya TANU, serikali, wanachama na viongozi wa vyama hivyo matatizo hayo yalipungua.
Kazi mojawapo iliyofanywa na TANU ilipoanishwa ilikuwa kuhimiza uanzishaji na uendelezaji bora wa vyama vya ushirika hasa katika zile sehemu za nchi hii ambazo hazikuwa na vyama hivyo. Vilevile kuimarisha vyama hivyo katika sehemu ambazo zilikuwa navyo tayari. Maendeleo ya vyama vya ushirika tangu mwaka 1954, TANU ilipozaliwa, na hasa baada ya kupata Uhuru, ni uthibitisho maalumu unaonyeshesha jinsi wananchi walivyoitikia wito wa TANU wa kuanzisha, kuendesha vizuri na kuimarisha vyama vya ushirika nchini.
Baada ya Azimio la Arusha kutangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere mwaka 1967, na kukubaliwa na Watanzania, kazi za vyama vya ushirika zilikuwa ni pamoja na kuendeleza Siasa yetu ya Ujamaa na Kujitegemea. Tangu mwaka huo, TANU na Serikali inahimiza kwamba licha ya vyama hivyo kuuza mazao lazima pia vijishughulishe na uzalishaji wa mali.
Lakini, mabadiliko makubwa katika muundo wa vyama vya ushirika yalifanywa mwaka 1972 serkali ilipotangaza kwamba tangu hapo vijiji vya ujamaa vitaanza kuwa vinaandikishwa kama vyama vidogo vya ushirika. Haya yalikuwa mapinduzi makubwa katika vyama vya ushirika.
IV. Muhtasari wa Kitabu
Sura ya kwanza inaelezea biashara ya siku za kale katika Tanzania, ambayo inatuelezea kwamba kuja kwa wageni katika nchi yetu, hasa Waarabu na Wazungu kulifanya wananchi wawe na hamu ya kupata vitu zaidi na vya aina mbalimbali. Kwa mfano, badala ya kuendelea kutumia mavazi yaliyotengenezwa kutokana na ngozi za wanyama au magome ya miti, walivutiwa sana na mavazi ya kisasa yaliyokuwa yameletwa na hao wageni. Basi, kusudi wapate vitu kama hivyo, iliwapasa kubadilisha mavazi yao na vitu walivyokuwa navyo wachuuzi. Huu ndio uliokuwa mwanzo wa biashara kati ya wananchi na wageni.
Lakini, biashara ya maana hasa ilihusiana na mazao makuu ya fedha, hasa kahawa, pamba, tumbaku, chai, nk. Ambayo yaliletwa nchini au yalianza kuhimizwa kulimwa tangu mwishoni mwa karne ya kumi na tisa. Kahawa aina ya Arabika ililetwa kwanza katika Misioni ya Kilema kando ya mlima Kilimanjaro na mapadre wa Roho Mtakatifu mwishoni mwa karne ya kumi na tisa, lakini upandaji wa mibuni katika Mkoa wa Kilimanjaro ulianza kufanyika hasa tangu mwaka 1920.
Katika Wilaya ya Bukoba Kahawa aina ya Arabika ililetwa na Wamisionari wa dini ya Romani Katoliki mwaka 1896. hata hivyo wataalamu wanasema kwamba Bwana Speke na Bwana Grant walipokwenda Bukoba walikuta kahawa aina ya Robusta inalimwa na wenyeji wa Wilaya hiyo na ipo mibuni inayosemekana kwamba ina umri zaidi ya miaka 100. Katika Wilaya ya Bukoba mwaka 1912 tani 1,547 za kahawa zenye thamani ya shilingi 1,903,360 zilisafirishwa kwenda nchi za nje na mpaka kufikia mwaka 1925 kiasi cha kahawa kiliouzwa nchi za ng’ambo kiliongezeka na kuwa tani 6,009 zenye thamani ya shilingi 9,621,100. Wilaya zilizobaki zinazolima kahawa kwa sasa zilipata mbegu kutoka Bukoba au mkoa wa Kilimanjaro. Kuhusu zao la tumbaku, serikali iliingiza na kuhimiza kilimo cha zao hili mwaka 1928 huko Songea, katika mkoa wa Ruvuma. Mazao mengine ya fedha yaliletwa au kuhimizwa katika wilaya nyingine baadaye. Hata hivyo, mwanzoni baadhi ya mazao hayo kama vile pareto, chai na katani yalikuwa yanalimwa na Wazungu tu kwa sababu eti wananchi wasingeweza kuyalima na kuyatunza vizuri kama ipasavyo na kupata soko.
Sura ya pili inaelezea historia, maana na madhumuni ya Vyama vya Ushirika; pia inaelezea kanuni za vyama vya ushirika, mwanzo wa ushirikiano nchini, mwanzo wa vyama ushirika nchini, kazi za mrajisi wa vyama vya ushirika, madhumuni ya chama cha ushirika cha Kilimanjaro, uendeshaji wa shughuli za vyama vya ushirika na uhusiano wa vyama vya ushirika na serikali.
“Shida mbali mbali zilizowakabili wakulima huweza kumalizwa tu na umoja wa watu wenyewe wanaoumia. Haja ya kutaka kumaliza shida hiyo ndiyo iliyokuwa chanzo cha vyama vya ushirika katika nchi yetu. Chama cha Ushirika ni umoja wa watu kadhaa wanaoshughulika na ulimaji na uuzaji wa aina moja au zaidi ya mazao au shughuli nyingine za uchumi au utoaji wa huduma na ambao wameamua kujiunga pamoja kwa hiari yao wenyewe, bila kulazimishwa na mtu yeyote, kikundi cha watu, wala serikali ili kuondoa matatizo fulani ambao huzuia maendeleo yao, na ambayo mtu mmoja binafsi hayawezi kuyatatua peke yake..” (Uk.4-5)”
Tutaambiwa kwamba madhumuni ya Vyama vya Ushirika vya kwanza yalikuwa:
- Kukomesha Ubaguzi na unyonyaji uliokuwa ukifanywa na wakulima -masetla wa Kizungu na wafanyabiashara Wahindi waliokuwa wakinunua mazao kwa jinsi waliyopenda hapo mwanzo na kuwalipa bei ya chini.
- Kutafuta masoko ya mazao ya wanachama kwa lengo la kutafuta bei nzuri
- Kutayarisha mazao kusudi yawe katika hali bora inayotakiwa na wanunuzi.
- Kukusanya mazao kutoka kwa wakulima , na kufanya mipango ya kusafirisha mazao hayo toka kwa wakulima hadi “mikononi” mwa Halmashauri za Mazao au mpaka katika masoko ya dunia( kwa mfano kahawa haikuwa na Halmashauri kwa miaka mingi na kwa hiyo uuzaji katika masoko ya ulimwengu ulifanywa na vyama vya ushirika) (uk 5-6)
Chama cha ushirika, kama chama kingine chochote, kina kanuni zinazopaswa kufuatwa kwa kuendelesha kazi zake. Kani hizi za vyama vya ushirika zilianzishwa na Rochdale Pioneers huko Uingereza mwaka 1884, na mpaka leo vyama vya ushirika vinatemewa vifuate kanu hizo ambazo ni kama zifuatazo;
- Mtu yeyote anaweza kuwa mwanachama, bila kujali dini, hali, kabila wala rangi yake na kuwa mwanachama ni hiari ya mtu.
- Chama cha ushirika kiendeshwe kwa misingi ya kidemokrasia....
- Chama cha ushirika, tofauti na makampuni na ushirika wa ina nyingine hakina madhumuni ya kupata faida kubwa. Madhumuni yake ni kuwatumika wanachama hata kama faida kubwa haitapatikana kutokana na utumishi huo. Faida inayopatikana na kutokana na shughuli za chama ni mali ya wanachama wote, na ni lazima igawanywe kati ya wanachama kiasi sawa pia kila mmoja.
- Vyama vya ushirika vinapaswa kuwatumikia wanachama peke yake. Hata hivyo, tangu kanu hizi ziandikwe kumefanywa mabadiliko fulani (ingawa ni kidogo) kuhusu kanuni zenyewe. Kwa mfano, kanuni mbili zimeongezwa, nazo ni kwamba:
i) Vyama vya ushirika vina wajibu wa kuwaelimisha wanachama wake, watumishi wa chama na wananchi kwa jumla.
ii) Vyama vya ushirika vinapaswa kushirikiana na vyama vingine nchini na katika nchi za nje ili kuweza kuwahudumia vema ziadi wanachama wake na wananchi wengine. (Uk 6-7).
Katika sura hii pia tunaelezwa jinsi ushirika ulivyoanzia Kilimanjaro. Serikali ya Kiingereza ilihimiza ulimaji wa kahawa katika mkoa wa Kilimanjaro. Kuongezeka kwa upandaji wa mibuni oka mwaka 1033 hadi 1925 kulifanya wakulima wenyeji waliokuwa wakiishi kando ya mlima Kilimanjaro kuanzisha kwa kuhimizwa na serikali ya kikoloni, chama cha ushirika walichokiita Chama cha Wakulima Wenyeji wa Kilimanjaro mwaka 1925. Madhumuni ya chama hiki yalikuwa:
a) Kuwanganisha wakulima wa kahawa wa sehemu hiyo
b) Kuzuia upandaji ovyo wa mibuni
c) Kuzuia magonjwa na wadudu waharibifu wa kahawa
d) Kuwapatia wanachama ha bari zote zinazoeleza njia za kustawisha na kuendeleza zao la kahawa.
Sura ya tatu inaelezea juu ya maendeleo ya vyama vya ushirika kuanzia 1933 hadi 1971; Maelezo haya yanaviangalia vyama ushirika baada ya vita kuu ya pili ya dunia mpaka wakati wa Uhuru. Pia tunaelezewa juu ya vyama vya ushirika katika Nyanda za Juu, vyama vya ushirika kandokando ya Ziwa Victoria. Katika sura hii, pia kuna maelezo ya juu ya ongezeko kubwa la vyama vya ushirika kuanzia mwaka 1955 hadi 1960. Baadaye tunaelezewa maendeleo ya ushirika baada ya Uhuru kipindi cha kati ya miaka ya 1961 hadi 1971; na tunapata maelezo juu kuanzishwa kwa benki ya ushirika COSATA na Jumuiya ya Taifa ya Mikopo ya Kilimo. Sura ya tatu inahitimisha na maelezo juu Tume ya Rais juu ya vyama vya ushirika na bodi za Mazao iliyoanzishwa mnamo mwaka 1966.
Huko Songea, ambako kulikuwa na shida ya usafiri, serikali iliagiza na kuhimiza kilimo cha tumbaku mwaka 1928, na chama cha ushirika kilianzishwa mwaka 1936. Zao la Kahawa liliingizwa katika wilaya ya Ngara, mkoa wa Kagera na 1936 Chama cha msingi cha Ushirika cha Kahawa cha Bugufi kikaanzishwa kikiwa na rasilimali ya sh. 12,000. Katika wilaya ya Bukoba, kilianzishwa chama cha kilimo cha Bahaya mwaka 1937.
Kati ya mwaka 1939 hadi 1945 vyama vya ushirika viliendelea kwa mwendo wa kinyonga kwa sababu ya msukosuko mkubwa wa vita kuu ya pili ya dunia. Baada ya vita hivyo 1945, mabadiliko makubwa katika siasa na mwenendo wa vyama vya ushirika yalianza kufanywa na vyama vya vingi vilianza kuandikishwa. Chama cha Ushirika cha kwanza katika Jimbo la Nyanda za Juu za Kusini kilianzishwa baada ya vita kuu ya pili mwaka 1947. Chama hiki ni chama cha Ushirika cha Kahawa cha Mwakaleli.
Mwaka 1955, Muungano wa vyama vikuu vya Ushirika vya Victoria ulianzishwa, wanachama wake wakiwa vyama vikuu vya ushirika tisa. Na hapo vyama vingine vya Ushirika viliendelea kuanzishwa.
Sura ya nne inaelezea aina na kazi za vyama ushirika kuanzia mwaka 1933 – 1971; vyama vya ushirika: Katika nchi hii, kuna aina nyingi za vyama vya ushirika ambazo zimejitokeza tangu aina ya kwanza ilipoandikishwa karibu miaka 40 iliyopita; na kwa hiyo, itakuwa kazi ngumu kutaja aina zote za vyama zilizokuwapo nchini. Kwa kipindi hicho vyama vya ushirika vilivyokuwapo katika nchi hii viliweza kutengwa katika aina kuu tatu:
i) Vyama vya ushirika vya uuzaji
ii) vyama vya ushirika vya uzalishaji
iii) vyama vya ushirika vya Akiba na Utumishi
Kwa vile vyama vya ushirika ambavyo vilijiunga na Chama Kikuu cha Ushirika cha Tanganyika ( itakumbukwa kwamba vilikuwapo vyama vichache vya ushirika ambavyo si wanachama wa chama hiki kikuu), aina za vyama vya ushirika vilikuwa kama ifuatavyo:
- Vyama vya uuzaji wa mazao vilikuwa 1,299
- vyama vya walaji (maduka ya ushirika) vilikuwa vyama 51
- vyama akiba vilikuwa vyama 236
- Vyama vya Uuzaji wa Ng’ombe vilikuwa vyama 40
- Vyama vya uuzaji wa mbao na magogo vilikuwa vyama 25
- Vyama vya maziwa vilikuwa 12
- Vyama vya Uchukuzi na usafirishaji vilikuwa 2
- Vyama vya Uvuvi vilikuwa vyama 9
- Vyama vya Uuzaji wa kuku na mayai vilikuwa vyama 2
- Vyama vya kukuza mazao vilikuwa 12
- Vyama vikuu vya ushirika viliwa 23
- Vyama vya ushirika vingine vilikuwa 33 ( Uk 37).
Sura ya tano inafafanua kazi nyingine za vyama vya ushirika kama vile ueneshaji wa kazi za Biashara, uhimizaji wa kilimo bora, utoaji wa elimu kwa wakulima na kazi nyinginezo nyingi. Baada ya Tanzania kuingia katika mfumo wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, Mwalimu Nyerere, alielezea kazi mpya ya vyama ushirika:
“ Kazi mpya ya vyama vya ushirika ilikuwa kung’oa bepari aliyekuwa akinunua mazao kwa wakulima kwa bei nafuu na kuyauza kwa faida kubwa. Lakini, kazi ya sasa ya vyama vya ushirika lazima iwe pamoja na kulima mashamba ya kutoa mazao, na mashamba ya ujamaa ni mashamba ya ushirika” ( uk. 38).
Sura ya sita inaelezea maendeleo ya utoaji wa Elimu ya Ushirika: juu ya umuhimu wa Elimu ya ushirika kwa wanachama, umuhimu wa Elimu ya ushirika kwa Bodi, Umuhimu wa Elimu ya Ushirika kwa watumishi wa vyama vya Ushirika, Umuhimu wa Elimu ya Ushirika kwa watumishi wa idara ya maendeleo ya Ushirika. Pia kuna maelezo juu ya Elimu ya ushirika iliyoanza nchini, shule ya ushirika ya kwanza, mabadiliko katika mafunzo na elimu na mabadiliko baada ya Azimio la Arusha kutangazwa mwaka 1967. na utaratibu wa utoaji wa Elimu ya Ushirika.
Sura ya saba inajadili juu ya matatizo ya Vyama vya Ushirika na mapendekezo ya namna ya kuyazuia. Matatizo yanayojadiliwa ni kama vile:
- Wanachama kutoelewa kazi za vyama
- Wanachama kutofuata sheria za vyama
- Upungufu wa watumishi wenye ujuzi wa kazi
- Ugomvi kati ya viongozi wa chama na au kati ya viongozi wa chama na bodi.
- Kupanga vibaya Mipango ya Maendeleo
- Udugu katika kazi
- Ubinafsi wa viongozi wa chama.
Kuna mapendekezo ya kumaliza matatizo haya ( Uk 61 – 62).
Sura ya nane inajadili kwa kina historia na maendeleo ya Bodi za Mazao za wilaya na mkoa, kati ya mwaka 1933-1971. Tunaelezwa pia uuzaji wa mazao kabla ya vita kuu ya pili ya Dunia. Mwandishi anaelezea kwa kina kuanzishwa kwa bodi za wenyeji za wilaya za kwanza nchini na shabaha kuu za bodi hizi. Bodi iliyoanza ni Bodi ya kahawa ya wenyeji wa Moshi na baada ya hapo tunaelezewa maendeleo ya Bodi za mazao baada ya vita kuu ya pili. Ndipo tunaelezewa juu ya bodi nyingine kama vile Bodi ya kahawa ya wenyeji wa Bukoba, Bodi za Tumbaku za wenyeji wa Songea na Biharamulo, Bodi za Katani za Mkoa wa Ziwa Magharibi, Bodi ya maziwa ya wenyeji.
Pia katika sura hii ya nane, tunaelezwa juu ya kupunguzwa kazi za Bodi ya mazao ya kwanza, na kwamba baadhi ya Bodi zilianza kufutwa na kazi zake kupunguzwa. Na maelezo ya kazi ya bodi za mazao baada ya uhuru,1961. Na maendeleo mengine ni bodi zilizoanzishwa kati ya 1954 hadi 1962. Maelezo ya ziada ni juu ya bodi za mazao za mikoa kati ya 1962-1964
Sura ya tisa inaelezea juu ya Bodi za Taifa za Mazao, kati ya 1938 hadi 1971. Bodi hizi ni:
- Bodi ya Tanganyika ya Chai
- Bodi ya Tanganyika ya Mbegu
- Bodi ya Tanganyika ya Pareto
- Bodi ya kuuza Pamba na Mbegu za Pamba
- Bodi ya Pamba
- Bodi ya usagishaji
- Bodi ya Tanganyika ya Kahawa
- Bodi ya Taifa ya Mazao
- Bodi ya Tanganyika ya Tumbaku
- Bodi ya Taifa ya sukari
- Bodi ya Taifa ya Maziwa
- Bodi ya Tanganyika ya kuuza katani
- Boi ya Tanganyika ya Ngano
- Bodi ya mapapai ya Tanganyika.
Sura ya kumi inaelezea uhusiano baina ya vyama vya ushirika, Bodi za Mazao, TANU na mashirika ya Umma. Tunaelezwa kwamba historia ya Tanzania ni historia ya kazi na mafanikio ya TANU. Jambo linajionyesha wazi ni kwamba hata imani ya vyama vya ushirika ilifanana na Imani ya TANU. Hivyo katika sura hii tunaelezwa kwa kina uhusiano uliokuwepo kati ya TANU na vyama ushirika, pia uhusiano baina ya TANU, Serikali na vyombo vya umma.
Sura ya kumi na moja inaelezea mabadiliko makubwa ya vya Ushirika baada ya Tanzania kuingia katika mfumo wa siasa ya ujamaa na kujitegemea. Tunaelezwa juu ya vijiji vya ujamaa na muundo mpya wa vyama vya ushirika; maana ya chama cha ushirika na maana ya kijiji cha ujamaa. Pia kuna ufafanuzi wa wajibu wa vyama vya ushirika katika kuleta ujamaa vijijini. Mwandishi anajadili pia mapato makubwa yaliyopatikana kupitia vyama ushirika vilivyokuwa chini ya mfumo wa siasa ya ujamaa na kujitegemea. Hakuna chema kisichokuwa na matatizo, hivyo mwandishi anajaribu kutuelezea matatizo yaliyojitokeza katika kubadilisha mfumo wa vyama ushirika.
Sura ya kumi na mbili tunaelezwa juu ya kufaulu na kushindwa kwa vyama vya ushirika na Bodi ya Mazao. Tunaelezwa katika sura hii juu ya uhusiano kati ya vyama vya ushirika na Bodi za Mazao; kushindwa kwa vyama vya ushirika na bodi za mazao na kazi kubwa iliyo mbele yetu.
Sura ya kumi na tatu inaongelea hali ya baadaye ya vyama vya ushirika vya kuuza mazao na bodi ya mazao, changamoto na mapendekezo
V. Tathmini ya Kitabu
Baada ya kuona muhtasari wa kitabu, sasa tufanye tathimini ya kazi hii aliyoifanya mzee Pius Ngeze.
Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki ni kizuri sana. Kama nilivyosema juu ya vitabu vingine ambavyo ameviandika mzee Ngeze, ni kwamba ametumia muda wake wa kustaafu kuielimisha jamii.
Pili, ni kwamba kitabu hiki ni cha zamani kidogo, ila toleo hili ambalo ninalifanyia uhakiki, limeboreshwa zaidi na kuwekewa vitu vya miaka ya hivi karibuni. Sote tunajua kwamba Vyama vya ushirika vimepita katika nyakati mbali mabali na matatizo mengi. Kwa kitabu cha zamani, mengine hayakuwemo maana kengi yalitukia baada ya kitabu kuchapishwa. Kwa vile mwandishi bado yuko hai na ana nguvu za kufikiri, kusoma na kuandika, ameamua kukifanyika kazi upya kitabu chake.
Tatu, mwandisi ambaye ni mtaalamu wa kilimo na ameandika vitabu vingi juu ya mazao, hapendi kuwaacha wakulima hewani. Baada ya kuwapatia elimu namna ya kulima na kupata mazao mengi, bado anapendekeza vyama vya ushirika kama njia pekee ya kumkomboa mkulima.
Nne, historia ya vyama vya ushirika kama alivyoilezea Mzee Pius Ngeze, ni muhimu kwa watanzania wote na hasa sasa hivi tunapoimba wimbo wa Kilimo kwanza. Naweza kusema kwamba yeye ametekeleza sera ya kilimo kwanza kwa matendo. Maana haitoshi kuimba wimbo wa kilimo kwanza bila kuwaelimisha wakulima namna ya kuuza mazao yao. Ingawa tuna vyama vya ushirika kila sehemu ya Tanzania, lakini vyama hivi vina matatizo mengi sana, na bahati mbaya wale wanaohusika, wakati mwingine hawafahamu chanzo cha matatizo ya vyama vyao vya ushirika na mbinu za kutanzua matatizo hayo.
Tano, kwa vile mwandishi ameorodhesha matatizo yanayovikumba vyama vya ushirika na kupendekeza njia za kuyatanzua, kitabu hiki kinaweza kuwa msaada mkubwa kwa wakulima na wale wote wanaotaka kuendesha ushirika katika maisha yao; kuuza mazao yao au kuuza mifugo.:
Kwa maelezo ya mwandishi ni kwamba matatizo yaliyovikumba vyama vya ushirika kabla ya mwaka 1966 na kusababishwa kuundiwa Kamati maalumu ya Rais ya Uchunguzi Juu ya Vyama vya ushirika na Bodi za Mazao yaliendelea kuvikumba na mengine kuongezeka. Taarifa ya Kamati hiyo iligundua kuwa matatizo ya vyama vya ushirika yalitokana na mambo matano yafuatayo:
a) Wanachama kutoelewa kazi za vyama vyao
b) Upungufu wa watumishi wenye ujuzi wa kazi
c) Ukosefu wa demokrasia katika vyama
d) Ukosefu wa watumishi wenye ujuzi maalumu kwa kazi fulani
e) Uingiliaji wa siasa katika vyama vya ushirika.
Pamoja na matatizo haya kujulikana, vyama vya ushirika viliendelea na matatizo hadi vikafutwa mwaka 1976. Hata vyama hivi viliporuhusiwa kufanya kazi tena, bado vilikuwa na matatizo yale yale.
Sita, ni uwazi na unyofu wa mwandishi, Mzee Ngeze, sasa hivi ni mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania, lakini hatafuni maneno anapoongelea juu ya Bodi ya Kahawa. Hata mapendekezo yake yanaonesha jini alivyo mtu wa pekee katika taifa letu. Ni vigumu kuwapata watu ambao ni wanasiasa kama alivyokuwa Mzee Ngeze, kukubali kutambua kasoro, kuzisema wazi na kutoa mapendekezo ya kusonga mbele.
Kitabu kinapendekeza kwamba:
- Vyama vya Ushirika Vikuu vya kuuza mazao ya kilimo vife.
- Vyama vya Msingi vya Ushirika vya kuuza mazao ya kilimo visife
- Benki ya Taifa ya Ushirika ianzishwe haraka
- Ushirika mpya unaopigiwa debe hapa utahusisha:
a) Kuwafanya wakulima wote katika eneo la chama hicho kuwa wanachama
b) Ofisa Mtendaji mkuu wa chama cha Msingi awe na shahada au stashahada katika fani ya uchumi, biashara na/au uhasibu. Wasaidizi wake wote wasiwe na elimu iliyo chini ya kidato cha 4.
c) Wajumbe wa Bodi au Bodi ya utendaji wawe na umri usiozidi miaka 60 na wawe elimu isiyopungua kidato cha 4.
d) Siasa isiingie katika vyama vya ushirika
VI. Hitimisho.
Kwa kuhitimisha, napenda kumpongeza Mzee Pius Ngeze, kwa kuandika kitabu kizuri na muhimu sana juu ya vyama vya ushirika. Pia ningependa kuwahimiza na kuwashawishi watanzania wenzangu kukinunua kitabu hiki na kukisoma.
Kitabu hiki kimeandikwa kwa Kiswahili rahisi ili kiweze kusomwa na kuwafikia watanzania wote na nina imani kuwa kitakuwa cha manufaa zaidi kwa watumishi wote wanaohusika na maendeleo ya wananchi; Bodi za mazao na Wizara ya Kilimo; wanafunzi shuleni na vyuoni, walimu, wakulima na wafanyakazi wengine.
Ingawa kitabu hiki kinahusu vyama vya ushirika na Bodi za Mazao katika Tanzania Bara, kitawafaa pia watu wa nchi nyingine, hasa zile zinazoendelea, maana mambo yaliyozungumza kitabuni yanafanana na yale ambayo yangeweza kuzungumza juu ya vyama vya Ushirika na Bodi za Mazao katika nchi zao.
Na,
Padri Privatu Karugendo.
0 comments:
Post a Comment