KUWAFUTIA LESENI MADAKTARI NI KUWAONEA! Sikupenda kuandika makala hii. Nimepambana sana na nafsi yangu; nimesali na kutafakari, nimeandika zaidi ya mara tano na kufuta; lakini nimefika mahali nikasema liwalo na liwe kama tunavyofundishwa na viongozi wetu! Si kwa maana ya kukata tamaa bali nimekuwa na moyo mkuu! Nilitaka haya nitakayoaandika kwenye makala hii, niyaongee ana kwa ana na wahusika. Bahati mbaya hakuna jukwaa lolote la kukutana nao; ofisini kwao utahitaji siku nyingi kuwapata kama si mwaka mzima. Watu muhimu wanaofanya kazi za kulijenga taifa hawapatikani hivi hivi; simu zao zinazimwa au hazipokelewi? Na wakati mwingine hawana hata muda wa kusoma barua pepe, ingawa wakati mwingine tunawaona wako kwenye mambo yasiyokuwa ya kujenga taifa na wala kuwa na muhimu kwa wananchi wa Tanzania. Nimeamua kuandika kwa kuiogopa historia. Kesho na keshokutwa tunaweza kuwekwa sote kwenye kapu moja. Kutakuwa na maswali mengi nyuma yetu: Walikuwa watu wa namna gani? Walikuwa na akili timamu? Walikuwa wanaipenda nchi yao? Waliishi kwa vile walijikuta hapa duniani au waliishi kwa kutafiti na kutafakari kuwepo kwao hapa duniani? Kwa vile nina imani kwamba kilichoandikwa kimeandikwa. Vizazi vijavyo, watasoma na kutuweka kwenye makundi tofauti. Ujumbe wangu ni mfupi: Kuwafutia leseni madaktari waliogoma na kuwafikisha mahakani ni kuwaonea. Najua, kugoma kwao kumesababisha matatizo makubwa na watu wamepoteza uhai; hata hivyo kwa kulinganisha hawajaleta hasara kubwa kama iliyoletwa na “Vigogo” ambao hadi leo hii wanatembea vifua mbele na kuyafurahi maisha wakati mamilioni ya watanzania wanaogolea kwenye umasikini unaonuka. Nisingejali kuonewa kwa madaktari hawa kama si kuogopa kuchokoza nyuki; nisingejali kuonewa kwa madaktari hawa kama si kusoma alama za nyakati. Nisingejali kuonewa kwa madaktari hawa kama si kutamani kuacha nyuma yangu Tanzania yenye amani na utulivu. Nisingejali kuonewa kwa madaktari hawa kama mafisadi na wahujumu uchumi wote wangekamatwa na kufikishwa mbele ya sheria. Nisingejali kuonewa kwa madaktari hawa kama viongozi wetu wangekuwa wanalazwa na kutibiwa kwenye hospitali zetu za serikali. Kuna watu wengi hapa Tanzania wanaonewa, wananyanyaswa, wanateswa, wanabambikizwa kesi, tunawaona na wala hatusemi chochote na maisha yanaendelea. Hivyo kuonewa si kitu kipya na wala si cha kushangaza. Tofauti ni moja, kuonewa kwa madaktari ni kufunika mambo bila kutoa jibu. Tunataka kusikia serikali ikikaa meza moja na madaktari na kujadiliana. Tunataka tusikie serikali ikiongeza mshahara wa madaktari, fedha zipo na serikali ina uwezo huo, tunataka kusikia serikali ikiboresha huduma za Afya, fedha zipo na serikali ina uwezo huo. Serikali kuacha kufanya hayo niliyoyataja na kukimbilia kuwafutia leseni madaktari na kuwaburuza mahakani ni kwenda kinyume, tatizo linabaki pale pale na kesho ni lazima tatizo hili litaribuka. Na wakati ukiwadia, sote tutajuta isipokuwa wachache wanaojua pa kukimbilia. Kwa vile walio wengi hawajui pa kukimbilia ni lazima kusema bila ya kuogopa, ni lazima kusema bila kufuata itifaki yoyote ile. Ni bora kulaumiwa na kupuuzwa kwa kusema ukweli kuliko kukaa kimya hadi taifa likajikuta njia panda: Hivyo hoja kubwa katika makala hii ni: Kuwafuita leseni madaktari waliogoma na kuwafikisha mahakamani ni kuwaonea, ni unyanyasaji na ni kukiuka haki za msingi za mwandamu. Ni lazima ukatili huu kusimama mara moja! Ni kweli madaktari walifanya makosa kugoma na serikali ilifanya makosa kushindwa kushughulikia mgomo huo kwa haraka, kwa busara na kwa moyo wa kizalendo. Kama Madaktari wanafutiwa leseni na kufikishwa mahakamani, ni lazima na serikali iwajibishwe kwa namna moja ama nyingine na ifikishwe mahakamani. Damu ya watu waliokufa wakati wa mgomo wa madaktari iko juu ya madaktari na serikali. Haiwezekani serikali kusimama pembeni, kwa vile ina madaraka, haina maana haiwezi kukosea. Kuna historia ya serikali nyingi duniani zilizokosea na kusababisha kuwajibishwa au kukataliwa na wananchi. Tunaweza kufika hapo, maana watanzania si malaika na tunaishi kwenye dunia ambayo imekuwa kijiji kimoja Ninajua inaelezeka. Serikali yetu inataka kutuonyesha inavyoweza kuchukua hatua kali kwa wakorofi. Serikali inataka tutambue kwamba haijalala usingizi, bali ipo kazini. Inataka tutambue kwamba serikali ni chombo chenye madarka na hakuna mwenye uwezo wa kupambana nayo. Na madaraka haya inayapata kikatiba! Hakuna la kubisha hapa. Labda mjinga peke yake ndiye anaweza kuchukua hatua za kutaka kupamba na serikali. Tunazijua na kuzitambua nguvu za dola: Ndo maana tumekuwa tukishangaa ni kwa nini Serikali inashindwa kuwashughulikia wakorofi ambao wameliingiza taifa letu kwenye umasikini? Kwa nini serikali yenye madaraka na nguvu zote hizo imekuwa kimya kuwawajibisha wezi walioingia kwenye Benki yetu kuu na kujichotea fedha? Kwa nini serikali yenye nguvu zote hizo imeshindwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wezi wa Richmond na Rada? Wanajulikana kwa majina na sura zao, lakini wako huru na kuendelea kufurahi maisha na familiazao. Tumesikia kwamba kwa upande wa Uingereza, wezi wao walikubaliana kutowashitaki? Je sisi Tanzania tunakubali kutowashitaki wezi wa Rada, wezi wa fedha hizo zote ambazo zingeweza kuyaokoa maisha ya watanzaia wengi na badala yake tunafutia leseni madaktari na kuwafikisha mahakamani kwa kosa la kudai haki zao za msingi? Ni kuwaonea vijana wetu ambao hasira yao hatutaweza kuizima! Serikali hii yenye madaraka makubwa, inaongozwa na CCM. Chama hiki tawala kilitwambia kwamba kina mpango wa kujivua magamba. Tulitajiwa hadi na majina ya magamba hayo na kwamba watahakikisha watu hao wanafukuzwa kwenye chama. Hadi leo hii hakuna kilichotokea. Wale wote waliotajwa kama magamba bado tunawaona kwenye chama chao. Wameshindwa kuwafukuza, wameshindwa kuwawajibisha! Maana yake ni nini? Wamewaogopa? Mbona hizo nguvu zinazotumika kuwafutia madaktari leseni na kuwafukuza kazi hazitumiki kuwashughulika “Magamba”? Ina maana nguvu za serikali zinatumika kwa wanyonge? Nguvu za serikali zinatumika kwa vijana wadogo wanaoanza kazi? Nguvu za serikali zinatumika kwa walalahoi? Ina maana hawa madaktari hawaoni ukweli huu? Watakubali kufutiwa leseni, watakubali kufuzwa kazi, maana hawana nguvu za kupamba na serikali katika njia za kawaida ambazo zote zinaipendelea na kuibeba serikali, lakini kamwe hawezi kukaa kimya. Wakishindwa kupata jukwaa ni lazima wataingia barabarani au watajibu kwa hasira zao zote kwenye sanduku la kura. Uchaguzi mkuu hauko mbali, madaktari zaidi ya 300 ni wengi kiasi cha kueneza sumu na kuhakikisha chama tawala kinapata haki yake ya kuwekwa pembeni. Na huu wala si utabiri au uchochezi ni kusoma tu alama za nyakati. Sina ulazima wa kutoa mifano hapa. Sote tunajua jinsi vijana wakibanwa na kunyimwa jukwaa la kujieleza na kutoa kero zao, vijana wasipopata kazi na kupata mtaji wa kuanzisha biashara ili kuweza kuendesha maisha yao wanavyofanya uamuzi wa kutumia njia nyingine ambazo si nzuri. Tumeshuhudia Tunisia na Misri. Tumeshuhudia jinsi watoto wadoto wa Afrika ya kusini walivyokuwa tayari kusimama mbele ya risasi na silaha nzito za makaburu kutetea haki zao. Wengi walipoteza maisha yao, lakini hatimaye waliobaki nyumba wanafurahia matunda ya damu ya vijana wenzao iliyomwangika. Mtu yeyote asiyeona ukweli huu ninashindwa neno la kutumia, maana hata “Mjinga” bado ni neno la heshima kwa mtu wa aina hiyo. Tumeshuhudia wanyama wakitoroshwa mchana kweupe? Ardhi inaporwa na kuuzwa kwa wawekezaji wan je, mikataba mibovu ya madini na uwekezaji hewa ambao wawekezaji wamekuwa wakibadili majina ya biashara zao kila baada ya miaka mitano: Mahoteli makubwa yamekuwa yakibadilisha majina, makampuni ya simu nayo yamekuwa yakibadilisha majina; wanachota fedha na kwenda zao. Serikali yenyen guvu zote hizo inashindwa kuchukua hatua? Hatujasikia mtu akiwajibishwa kwa kutorosha Twiga. Kama serikali yetu inaweza kuwawajibisha wakorofi kama madaktari waliogoma, kwa nini serikali hiyo hiyo ishindwe kuwawajibisha watu wanaohujumu uchumi wetu? Tumesikia kwamba daktari mmoja anahudumia watu elfu 30. Maana yake ni kwamba tuna uhaba wa madaktari. Mungu bariki Baba wa Taifa alianzisha Madaktari wasaidizi, ambao wanafanya kazi kwa ngazi ya daktari na ni wachapa kazi kweli ingawa mara nyingi wanasahaulika katika mchakato mzima wa kuongeza mishahara ya madaktari na huduma ya kupewa malazi. Kwa kifupi ni kwamba tuna uhapa mkubwa wa madaktari. Katika hali hiyo, serikali kufuta liseni na kuwasimamisha madaktari ni ujumbe wa wazi kwamba sasa wakati umefika wa kuiwajibishwa serikali yetu. Tumeambiwa kwamba madaktari wetu ni wazuri na wana ujuzi wa hali ya juu, lakini hawa vifaa; sote tunashuhudia jinsi taifa letu linavyotumia fedha nyingi kuwatuma watu kutibiwa nje ya nchi. Katika hali kama hii, madaktari wakidai kupewa vifaa; badalala yake wakafukuzwa, wakafutiwa leseni na kufikishwa mahakani ni ujumbe kwamba sasa wakati umefika wa kuiwajibisha serikali yetu. Kuwafutia leseni madaktari na kuwaburuza mahakani ni kuwaonea! Maana yake hawawezi kujadili tena juu ya suala hili la madai yao. Wataambiwa kesi iko mahakamani. Tumejenga utamaduni wa kuitumia mahakama kama chombo cha kuziba midomo ya watu na kupunguza uhuru wa watu kujadili mambo yanayogusa maisha yao. Serikali ikitaka kitu kisijadiliwe, inakimbilia mahakamani. Ikishafika huko, tunaambiwa kitu kilicho mahakami hakijadiliwi. Walipouawa wafanyabiashara wa Mahenge, watanzania walichukia sana na baadhi walitaka kuchukua sheria mkononi. Serikali ikawatuliza watanzania kwa kuwakamata “wahusika”. Kesi ikwafunguliwa mahakamani. Baada ya kese kufunguliwa mahakani, mjadala juu ya wafanya biashara wa Mahenge ukafungwa. Watanzania wakatulia. Kesi ikaendeshwa miaka, matokeo yake sote tunayajua. Ametekwa na kuteswa Dakt Ulimboka. Watanzania wamechukia kiasi cha kutaka kujichulia sheria mkononi. Mfano mzuri ni mtu yule aliyepata kipigo pale Muhimbili kwa kutuhumiwa kuwa mpelelezi. Serikali inajua kwamba watanzania wamechukia kwa kitendo cha kutekwa na kupigwa vibaya Dakt Ulimboka. Sasa Tunasikia amekamakwa mshukiwa wa kumtesa Ulimboka. Akifikishwa mahakani, ndo mwisho wa mjadala. Tutakatazwa kujadili juu ya sakata la Ulimboka. Kesi itaendeshwa miaka, na matokeo yake sote tunayajua. Kuna watanzania wengi wamelisabishia taifa letu hasara kubwa, lakini hawajachuliwa hatua yoyote ile, kuwaacha hao na kuwageukia vijana ambao ndio kwanza wanaanza maisha ni kuwaonea, ni kuwanyanyasa na kuwanyima haki yao ya msingi. Kama wamekosea, waonywe na kuelezwa makosa yao na si kuwafutia leseni na kuwaburuza mahakamani. Tanzania ni yetu sote, ni lazima tuilinde na kuhakikisha ni salama kwetu na kwa vizazi vijavyo. Ni muhimu! Na, Padri Privatus Karugendo. pkarugendo@yahoo.com www.karugendo.net +255754 633122

0 comments:

Post a Comment